Ndagullachrles
JF-Expert Member
- Jun 20, 2023
- 256
- 259
Kutoka Dawati la Habari polisi Kilimanjaro
Wananchi wapatao 300 wa Kata ya Manda na maeneo ya Tarafa ya Mengwe, Wilaya ya Rombo, wamepata elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora, matumizi ya vyakula vya asili, uzalendo na wajibu wa kila mwananchi katika kulinda amani na usalama wa nchi.
Elimu hiyo ilitolewa Oktoba 29, 2026, katika kongamano la uzinduzi wa Lishe Bora ngazi ya Wilaya lililofanyika katika Kijiji cha Manda Chini, Wilaya ya Rombo, lililokuwa na kaulimbiu isemayo “Imarisha Afya, Kula Kiasili, Punguza Chumvi, Sukari na Mafuta.”
Katika kongamano hilo, Mkaguzi wa Polisi Kata ya Manda ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Rombo, INSP Stephano Bukwimba, alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa wazalendo na kuendelea kulinda amani iliyopo nchini, akisisitiza kuwa amani ni tunu inayopaswa kulindwa na kila mwananchi.
Aidha, alieleza namna bora ya kujiepusha na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe bora, faida za kupenda na kutumia vyakula vya asili pamoja na umuhimu wa kuzingatia afya na lishe bora katika familia na jamii kwa ujumla.
Sambamba na elimu ya afya, INSP Bukwimba aliwakumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kusalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi mapema wanapoona viashiria vya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama katika maeneo yao.
Akihitimisha ujumbe wake, aliwasisitiza wananchi kuimarisha malezi bora katika familia na kutambua kuwa jukumu la kulea na kusimamia maadili ya watoto ni la kila mmoja katika jamii, si Jeshi la Polisi pekee.
Kongamano hilo lilizinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Mwalimu, Laymond Mangwala, likishirikisha viongozi na wadau mbalimbali wa lishe kutoka ngazi za kijiji, kata na tarafa, wakiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Lishe Wilaya, Kaimu DAS na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya.
Kwa upande wao, wananchi walimshukuru Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Rombo kwa kutenga muda wa kushiriki katika kongamano hilo na kutoa elimu kuhusu masuala ya usalama, wakiahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kulinda amani na usalama wa jamii.
Ushiriki wa Jeshi la Polisi katika shughuli hizo za kijamii unaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi hilo na wananchi, sambamba na kuhamasisha jamii kuchukua wajibu wa pamoja katika kujenga familia bora, jamii yenye afya na mazingira salama