Kijana wa Ifoza
JF-Expert Member
- Oct 31, 2025
- 1,180
- 2,302
Wakuu, kalamu yangu leo inamwangazia mmoja wa nguzo imara za jukwaa hili na tasnia ya habari nchini, Wakili Msomi na Mwanahabari Nguli, Pascal Mayalla. Nikiwa kama shabiki wake mkubwa na mdau niliyeandika hadi makala za kiutafiti hapa jukwaani kuelezea jinsi alivyowahi kunyanyaswa na mifumo ya mamlaka kupitia "soft censorship," leo ninalazimika kuweka mezani uchambuzi wa nafsi mbili tofauti za mtu huyu mmoja.
Lengo langu si kumshusha thamani, la hasha! Nia yangu ni kutunza na kulinda heshima ya jina kubwa alilolijenga kwa jasho na damu kabla halijamomonyolewa na watu wasiomfahamu vizuri hapa jukwaani.
Pasco wa Masai Studio: Nguli wa Broadcaster na "Mpishi" vya Kitimoto
Tukirudi nyuma kidogo, jina la Pascal Mayalla lilibeba uzito wa kipekee kupitia Masai Studio, ambapo akishirikiana na wamiliki wenza wa studio hiyo kama Allyoki, walitengeneza historia ya kipekee ya habari nchini. Huyu alikuwa mwanahabari huru, mtayarishaji wa maudhui, na mtangazaji wa kwanza kabisa wa Talk Show ya kwanza ya runinga nchini—kipindi cha "Mada Moto" pale DTV mwaka 1995. Enzi hizo akiwa kijana mbichi asiye na majukumu ya kifamilia, akilipwa mishahara minono ya "six figures" kwa ushupavu wake!
Sisi kama hadhira tulimkubali bila masharti kwa sababu alisimama kama sauti ya kweli ya Muhula wa Nne wa Dola (The 4th Estate). Kilele cha uandishi na utangazaji wake kilionekana kupitia kipindi cha kihistoria cha Kitimoto kilichoruka DTV na Channel 10. Kipindi kile kilikuwa moto haswa, kiasi kwamba hata msemo wa mtaani wa kuitia nyama ya nguruwe jina la "kitimoto" ulizaliwa pale, kutokana na jinsi wanasiasa na mawaziri (kama akina Daniel Yona wa Wizara ya Fedha na Askofu Kakobe) walivyokuwa wanatolewa jasho jukwaani!
Kwenye kiti kile, Pascal alikuwa anawapika na kuwapakua wanasiasa bila uoga, akiongozwa na maswali ya mitego na utafiti mkubwa wa Masai Studio
Mabadiliko: Imekuwaje Mayalla wa Sasa Anatofautiana na Yule wa Masai Studio?
Ukiangalia mwenendo wa sasa wa mzee wetu Pascal ndani ya JamiiForums na kwenye medani za uchambuzi, kuna utofauti mkubwa unaoacha maswali mengi. Yule mwanahabari aliyekuwa anashambulia kwa mbele, leo anaonekana kuwa mtu wa kujihami, kupiga siasa za kimkakati, na wakati mwingine kuandika kwa tahadhari kubwa inayozua hisia za "kusaka teuzi" au kuegemea upande fulani, jambo linalowapa fursa baadhi ya wana-jukwaa wasiomjua vizuri kumshushia heshima yake.
Ninajua vizuri—na sote tunajua—kwamba nyakati tunazoishi sasa kimuktadha si rafiki hata kidogo. Tuko katika mazingira ya kiserikali ambayo mara nyingi yameonyesha sura ya ukatili (ruthless) na isiyothamini utu wala uhuru wa mawazo.
Dhoruba hizi si geni kwake; hata huko nyuma amewahi kukumbana na misukosuko ya kunyang'anywa leseni na kufukuzwa ofisini kisa tu kuuliza swali gumu mbele ya wakuu wa nchi. Hata hivyo, kama mwanahabari anayewakilisha muhula wa nne, Pascal anapaswa kukumbuka kuwa dhoruba hizi ni sehemu tu ya wajibu wa mwanajeshi. Unapoingia vitani, unajua kabisa utakutana na milio ya risasi na dhoruba kali, lakini uaminifu wako unabaki kwenye kupigania ukweli mstari wa mbele.
Ushahidi wa dhoruba hizi ni huu wa hivi karibuni wa Machi 2026, ambapo Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ilimshushia rungu la onyo yeye na Wilberforce Ngoto kule Jambo TV. Kisa kikajulikana? Kisa ni uchambuzi wake wa kiutu na kisiasa juu ya hisia za viongozi na "makofi ya msibani". Mfumo ulimtaka athibitishe hisia za moyoni za kiongozi ndani ya saa 24! Hapa ndipo tunapoona jinsi Pascal wa sasa anavyolazimika "kukiri makosa" na kupiga magoti kidiplomasia kulinda ugali na usalama wa chombo cha habari, jambo ambalo lisingewezekana kwa yule Pasco wa Masai Studio.
Vita Kuu ya Tatu ya Dunia ya Nafsi Mbili
Nikifanya hitimisho la kiweledi, nina amani ya moto kusema kuwa: Ikitokea siku moja Pascal Mayalla wa Masai Studio akakutana uso kwa uso na huyu Pascal wa sasa mwenye kofia mbili (Uanasheria na Uandishi wa Habari), lazima kitazuka vita vikali sana vya kisaikolojia na kifalsafa. Yule wa Masai Studio atamshangaa huyu wa sasa kwa namna anavyozingatia sana kujilinda na mistari ya kijani na "uchawa wa kimamlaka" unaolazimishwa na mifumo, na huyu wa sasa atamcheka yule wa zamani kwa ukosefu wa mbinu za "kisayansi" za kijeshi na kisheria za kujilinda dhidi ya dhoruba za dola.
Mzee wangu Pascal, andiko hili linatokana na mapenzi mazito kwako. Kwa jinsi unavyoshambuliwa sasa na vijana wa kizazi kipya hapa jukwaani wasiojua kabisa historia na mchango wako, ninaamini kabisa ingekuwa heri ungalifanya kazi ya Uanasheria pekee mahakamani tujue kimoja, kuliko kuendelea kuona thamani ya nguli wa habari ikishushwa na kudhihakiwa hapa jukwaani na watu wasiojua ulipotoka.
Nawasilisha, wakuu. Mzee Pascal Mayalla, karibu uwanjani utupe neno lako.