03
Aug 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Habari
Nipashe
Utouh aunga mkono wabunge kukatwa kodi
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh, amesema anaunga mkono hoja ya Mbunge wa Ukonga, Jerry Slaa na Hussein Bashe, kuhusu wabunge kukatwa kodi.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh.
Akizungumza jana katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga, alisema miongoni mwa misingi mikubwa ya kodi ni usawa kwa kuwa kodi yoyote haitakiwi kuwa na matabaka ya watu.
“Tunalipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi sasa hawa wabunge si wana kipato, wanapokea mshahara kwanini wasilipe kodi, mantiki ya hiyo haipo,” alihoji Utouh.
Julai 23, Mbunge wa Ukonga, Slaa, akihutubia wananchi katika jimbo hilo, alisema imefika hatua wabunge waanze kulipa kodi kupitia mishahara yao ili wapate uwezo wa kuwaambia wananchi na wao walipe kodi.
Pia Utouh alizungumzia nafasi ya CAG aliyowahi kuihudumia miaka kadhaa iliyopita kuwa nasafi hiyo ni nyeti na inamtaka mtu kuwa muadilifu ili kutende haki kwa sababu inabeba dhamana ya wananchi.
“Madhumuni ya ukaguzi ni kuleta maboresho, serikali ifanye vizuri zaidi kwahiyo mkaguzi ni mshauri mkuu wa serikali katika kuweka mambo sawa ili fedha na rasilimali za wananchi zitumike vizuri kwa maendeleo jamii.
“Mwaka 2012 baada ya ripoti yangu kutoka mawaziri wanane waliachia ngazi, kwasababu ya ile ripoti ilileta mtafaruku watu wakawa wanamwongelea CAG Utouh, lakini anayoyaripoti sio ya kwakwe ni vitu anavyokwenda kuviona katika ukaguzi wake,” alisisitiza Utouh.
Alisema yeye hakuwatoa mawaziri, lakini kwasababu ripoti yake ilianika yale yaliyokuwa ya ukweli, ndiyo iliwalazimisha kuwajibishwa.
Alibainisha kuwa mwaka 2007-8 vyama vya siasa vilikuwa vinatumia zaidi ripoti ya CAG kuichambua serikali, na ikafika mahali akashauri kuwa chama tawala kiachie vyama vya upinzani vitumie ripoti ya CAG kuikosoa serikali.
“Ilifika kipindi tukasikia mawaziri mizigo, ilikuja baada ya majadiliano, na chama tawala kikaanza kuitumia ripoti ya CAG kuikosoa serikali ambayo ni serikali yake, na hiyo ndiyo imekuwa kama utamaduni sasa,” alisema Utouh.
Pia alisema ripoti ya CAG haiandaliwi kwa ajili ya kumnufaisha mtu, inaandaliwa kwa dhumuni la kuweka bayana hali iliyopo ya utendaji wa serikali.
Alisema chama tawala kina wajibu wa kuisimamia serikali yake na kuhakikisha inatekeleza yale yaliyokisababisha chama kikachaguliwa kuingia madarakani.
“Serikali yoyote inayokumbatia ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma kwa kipindi kirefu haidumu itaanguka kwasababu wananchi hawataikubali.
Katika uchambuzi wa watu wanaopewa nafasi ya kusimamia rasilimali za nchi kuwe na uangalizi zaidi, je hawa tunaowapeleka wana maadili ya kufanya ile kazi, wana uwezo na ujuzi, ili majukumu wanayopatiwa wakayatimize kwa weledi,” alishauri Utouh.
Alisema uteuzi wowote mtu anaopata wa utumishi wa umma, anapaswa kujua kuwa hiyo ni dhamana aliyopewa inayomfanya awe mtumishi wa watu na si vinginevyo, kwa kuwa kuna baadhi ya watu wakishapata nafasi wanajiona wako juu, na hiyo ndiyo inaleta matatizo.
Madarasa ya FEZA SCHOOL, IST, HOPAC, KIDUNGILO, BARBA OHNSON yapo vizuri ambapo ndipo watoto wa kina Mwigulu wanasoma huko , sasa wewe unataka mnaposoma watoto wa maskini nako kukarabatiwe? Subiri ukuta ukiwaangukia watoto ndio ukarabati utafanyika.