Admin,
Suala la wananchi 200 wa Morogoro kuwashikia kidedea viongozi waliochaguliwa kwa kutumia vigezo vya elimu wasiokuwa nayo linatia moyo. Cha kushangaza ni kuwa viongozi haohao labda wangechaguliwa hata kama wasingeongopa kuhusu viwango vyao vya elimu. Ushauri wangu ni kuwa hili suala la wananchi kuchukuwa jukumu la kuwafikisha Mahakamani hawa waheshimiwa lisiwe la kisiasa kwani litakufa kabla halijaanza.
Raia wa Morogoro wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wasomi wa kujitolea waliobobea katika masuala ya sheria na hata ushirikiano kutoka serikalini. Hili ni jambo linalohusu muafaka wa kitaifa. Inabidi tuwashe Mwenge na tuupitishe sio tu kwenye siasa, bali hata katika fani zote kama alivyosema Mzee Mkandara.
Rejea maneno aliyoyasema na Waziri wa Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia Profesa Peter Msolla alipozungumza kwa mara ya kwanza na wafanyakazi wa wizara yake kwenye makao makuu ya wizara hiyo mjini Dar es Salaam. Nanukuu;
"Kughushi vyeti kwa vijana wanaojiunga na elimu ya juu kumesababishwa na kuimarika kwa teknolojia ya mawasiliano lakini hatua zaidi lazima zichukuliwe kwani kuwaondoa tu chuoni haitoshi, hatua nyingine zitakazochukuliwa ni kuwasaka na kuwagundua watu waliopata vyeti kwa kununua digrii kutoka mataifa ya nje ambako Marekani inaongoza kwa biashara hiyo. "Kuna hili suala la mtu kuwa na fedha na kuuziwa digrii...anatakiwa kusema anahitaji cheti cha aina gani na kwa daraja gani kisha akiwasilisha hundi anatumiwa digrii yake. Watu wa aina hii lazima hatua zichukuliwe ili kuwabaini na tuwachukulie hatua," Mwisho wa kunukuu.
Baada ya tamko la Waziri Msolla, niliwahi kuandika mahala kuwa imefikia wakati wa kuwauliza viongozi wetu kutoa matamko yanayoambatana na ushahidi. Haiwezekani Waziri akasoma kwenye gazeti habari za kununua digrii nchini Marekani, alafu akahisi kwamba, watanzania wamekwisha zinunua. Sidhani kama hisia zinatengeneza mikakati na ajenda za kuiongoza Wizara. Itabidi tuwe tunawabana viongozi wetu palepale wanapotoa matamko. Profesa Msolla alikuwa na ushahidi gani kuwa watanzania wananunua digrii? Tena Marekani? Au ni ile ya waswahili wa pwani ujuana kwa vilemba? Mimi naamini alikuwa anajua kwa undani alichokuwa anasema. Imekuwa kitambo toka atoe tamko hilo, lakini sasa hivi tunaona wananchi ndio wanalivalia njuga hili suala.
Wakati wa kampeni za Uraisi huko majimboni, Kikwete alikuwa anawasihi na kuwahimiza wananchi kumsaidia kwa kuwachagua wasomi kwenye majimbo ambayo wagombea wa CCM walikuwa wanasema wanaelimu kadha wa kadha. Nawahitaji hawa wasomi, wachagueni jamani alinukuliwa na vyombo vya habari wakati akiwauza wabunge hao.
Hata alipochagua baraza lake la mawaziri, ingawa alikana kuwa hakuwachagua mawaziri kwa sababu ya usomi wao, lakini vyombo vyake vya propaganda kama IPP media, vimeandika kuwa wananchi wamelisifia baraza la Mawaziri la Kikwete kuwa lina jumla ya Madaktari na maprofesa kumi na kitu. Huu ni upotoshaji wa hali ya juu. Niliwahi kuandika mahala pia kuwa hakuna anayekwenda ndani na kuchunguza uhalali wa udaktari wa viongozi wetu. Tunachotajiwa ni idadi ya wasomi tu. Si ajabu kukuta udaktari wa kiongozi fulani ni wa vitunguri gourd uliopatikana kutokana na home schooling karibu na Mlima Kolelo au Kaole Bagamoyo, na wala sio wa mifupa kama tunavyodhani. Au Uprofesa wa kiongozi fulani ni wa kutajirisha watu kama ule wa Profesa Majimarefu na wala sio wa daraja la ufundishaji vyuoni kama tunavyoamini. Au ile inayoitwa diploma ya mazingira iliyopatikana Bulgaria, ni Certificate of attendance tena ya warsha ya mazingira ya siku moja.
Viongozi wote wanaonunua vyeti, wanaweza kuchaguliwa katika hali ya kawaida bila hata kuongopa juu ya viwango vyao vya elimu. Ikumbukwe kuwa wengine walishakuwa mawaziri kabla ya kuanza huu ulaghai. Wasiwasi wangu ni kuwa, kama wameweza kutuongopea katika suala la elimu, ni kitu gani kingine wametuongopea? Baadhi yao wametuweka kwenye mikataba ya ulaghai wakishirikiana na wasomi wa kweli. Rai yangu ni kuwa hawa wote hawapashwi kuwa viongozi wetu. Hili suala siyo la kuwaachia wenyewe wajiamulie hatima yao. Ni suala la sisi raia wote kuwapigia makelele mpaka wakaachia ngazi.
Nakumbuka Mzindakaya alikuwa mkuu wa mkoa wa Kigoma mwaka 1991/1992 na akapata ziara ya siku mbili nchini Ireland kwa mwaliko wa rafiki zake wa kizungu aliojuana nao huko Kigoma. Haikuwa safari ya kiserikali. Cha kushangaza, kwenye mtandao wa wabunge ameweka kuwa ana cheti kilichopatikana huko Ireland. Hivi wanao hakiki vyeti wapo? Labda akiwa ziarani alipata kozi ya siku mbili.
Jenerali Ulimwengu aliwahi kutoa makala katika gazeti la Rai, yenye kichwa cha habari Simwogopi Nsanzugwanko. Ulimwengu alibainisha wazi kwamba, Mheshimiwa Nsanzugwanko anajipachika digrii ambazo hana, yaani hakuzipata kwa njia halali ya kwenda shule. Haya maneno siyo ya Kyoma, Mzee Sam, au Mzee ES manake inaweza ikaonekana ni porojo. Ni maneno ya mtu aliyewahi kushika kushirikiana na hawa waheshimiwa katika ngazi za uongozi wa kitaifa. Ni mtu wa karibu nao na anawajua vizuri. Sijawahi kusikia kauli au maelezo ya Mheshimiwa Nsanzugwanko ya kukana maandishi ya Ulimwengu kwa watanzania, au kutetea digrii alizokuwa anaziongelea Ulimwengu. Wote tunajua nyazifa mbalimbali alizoshika huyu Mheshimiwa katika historia ya nchi yetu.
Jalada la Mbunge mmoja lafika ofisini kwa DPP, DCI asema tayari upelelezi umekamilika. Well, labda tuvute subira tukiwa na imani kuwa utawala wa Raisi Kikwete utajenga utamaduni mpya tofauti na ule tuliouzoea. Lakini lazima tukumbushane kuwa imekuwa ni kawaida kwa serikali kutoa kafara kwa mtu mmoja awe kiongozi au mtumishi wa kawaida ili kutuliza hasira za raia juu ya masuala ya msingi yanayohusu nchi yetu.
Pamoja na ufisadi wa kiwango cha juu uliokuwa unaendelea chini, na hata kazi yote aliyoifanya Warioba, ni kiongozi mmoja tu wa ngazi za juu aliyefikishwa mahakamani bila hata kutiwa hatiani. Tuliona tukio lililotokea uwanja wa ndege wa Dar wakati Waziri wa mambo ya ndani kwa wakati ule Ndugu Mrema alipowakamata waliokuwa wanatorosha madini nje ya nchi. Tulichoambulia ni msamiati wa neno vigogo.
Tumeshuhudia mikataba ya wendawazimu ya kuiuza nchi yetu ambayo inaonyesha bayana kuwa yalikuwepo mazingira ya rushwa. Raia wa kawaida wakihoji, viongozi wanasema walete ushahidi. Raia wa kawaida atapata wapi ushahidi wa mikataba inayofanyika sirini? Ili kuwapoza raia wa kawaida, wasiendelee kuhoji, tunapewa habari kuwa mtendaji wa kijiji afikishwa mahakamani kwa kutoa rushwa katika kesi ya wizi wa kuku.
Tumeendeleza pia utamaduni wa kihuni toka enzi za Kambarage. Mtu akifuja mali za shirika fulani, anahamishiwa shirika lingine. Hawa watu hawapashwi kuchaguliwa, kuhamishwa, au kuteuliwa kwa nafasi yoyote ya uongozi. Tukifanya hivyo, tunakuwa tunawachanganya. Ni sawa na mtoto mdogo anapofanya kosa unampa zawadi, na anapofanya kitu cha maana unampa adhabu. Ataendelea kufanya makosa akitegemea kuzawadiwa.
Ripoti ya gazeti la leo linalomilikiwa na Serikali Daily News ambayo imetolewa na Mkaguzi mkuu wa Serikali, inaonyesha kuwa shilingi bilioni 2.2 ni mojawapo ya fedha zilizopotea ndani ya wizara moja ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa kimataifa katika mwaka wa fedha wa 2004/2005. Fedha hizo hazijarudishwa hazina hivyo, hazijulikani zilipo. Pamoja na kuwa tulikuwa hatujuhi hizo habari, na wala hatuna utaratibu wa kujua habari kama hizo kabla ya kuwachagua viongozi wetu, kiongozi wa wizara hiyo kwa mwaka huo wa fedha tumemzawadia na kumpandisha cheo kuwa Raisi wa nchi yetu. Sidhani kama kuna mtu anaweza thubutu kumuuliza swali.
Mambo tunayoyafanya mara kwa mara, na kwa muda mrefu mpaka yakazoeleka na mwishowe yakakubalika katika jamii yetu yanaitwa utamaduni. Inakuwa ni sehemu muhimu ya maisha yetu na ndiyo hasa tunawaridhisha watoto, wajukuu, na vitukuu vyetu. Watanzania hatutambuliki nje na ndani ya nchi kwa sababu ya rangi yetu, bali kwa sababu ya historia, maisha, na utamaduni wetu. Hatuwezi kujikomboa na balaa la ujinga na umasikini, na tukajenga nchi inayotambulika duniani kwa utamaduni wa wanataaluma na wanasiasa wetu kuwa na vyeti vya kununua.