Shughuli za usafirishaji jana zilisimama kwa zaidi ya saa mbili, baada ya msafara wa mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk. John Pombe Magufuli, kupita jijini hapa.
Licha ya kusimama kwa usafiri, msafara huo pia ulizuiwa kwa muda na wananchi katika eneo la Pasiansi, Kona ya Bwiru na Makongolo, wakishinikiza kusalimiana na mgombea huyo.
Magufuli ambaye aliongozana na viongozi mbalimbali wa CCM, serikali, madhehebu ya dini na wananchi wengine kutoka ndani na nje ya mkoa wa Mwanza alitua Uwanja wa Ndege saa 7:50 mchana.
Baadhi ya viongozi wa CCM taifa waliokuwa wameongozana na Dk. Magufuli ni pamoja na Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Rajabu Luhavi.
Kadhalika, Dk. Magufuli alikuwa amefuatana na mkewe, mama Janet Magufuli. Msafara wa Magufuli kuelekea ofisi za CCM mkoani hapa uliondoka uwanja wa ndege Mwanza majira ya saa 8:30.
Akijitambulisha mbele ya maelfu ya wakazi wa mkoa wa Mwanza waliofurika nje ya ofisi ya CCM mkoani hapa, Dk. Magufuli aliwapongeza wananchi kwa mapokezi yao makubwa, huku akiwataka Watanzania wote kuendelea kulinda umoja wao kwa nguvu zao zote.
Ninawashukuru sana kwa mapokezi yenu makubwa
lakini pia ninawaomba muulinde umoja wetu na tuendelee kushirikiana bila kujali itikadi za vyama wala rangi zetu,Dk. Magufuli.
Aliahidi kuisimamia kwa kikamilifu Ilani ya CCM. Alisema atahakikisha wafanyabiashara ndogo ndogo hawanyanyaswi.
Awali akimkaribisha, Dk. Magufuli, Nnauye alisema CCM hakitasita kuwashughulikia wanachama wake ambao hulalamika kwamba mchakato wa kuwapata mgombea urais kupitia chama hicho ulikiuka taratibu.
Ninapenda kuwaambia kuwa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama uliisha salama na tulimaliza salama ingawa kuna baadhi ya watu wanalalamika lalamika, alisema.
Alisema wanaCCM hao watashughulikiwa na chama iwapo wataendelea na malalamiko hayo ambayo alisema hayana ukweli wowote.
Wakiendelea tutawajibu, hasa wazee wetu. alisema huku akishangiliwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk. Magufuli kufika Mwanza tangu achaguliwe na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho kuwania nafasi ya urais kupitia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu
chanzo nipashe