Ndugu zangu watanzania wazalendo wa kweli wa nchi hii. Kwa takribani miaka minane sasa tumeshuhudia hali ya nchi ikizidi kudhoofu kiuchumi, maisha yamezidi kuwa magumu, hali ya elimu imekuwa ikishuka kiviwango, hali ya usalama wa raia imekuwa mbaya kiasi cha kufikia watu kuuawa na polisi hadharani. Kimsingi ni kwamba uongozi wa kisera umefikia tamati ya uwezo wake kifikra na uwajibikaji. Tuna wajibu mimi na wewe wa kurekebisha hali hii, na kuna namna nyingi za kukomesha mfumo kandamizi. Tulio wengi tungechagua mtindo wa mapinduzi ya umma. Njia hii ni nzuri na ina majibu ya haraka, lakini ina maumivu ya muda mrefu pia.
Nadhani tujadili njia ya kuidhoofisha serikali iliyoko madarakari, ambayo inapata nguvu kubwa kutoka kwetu wenyewe. Magari ya maji ya kuwasha, risasi, mabomu, fimbo, na zana zote za uhalifu wa utu wa mwanadamu zinatokana na kodi zetu. Matumizi ya anasa ya serikali yanatokana na kodi zetu.
Sasa ndugu watanzania, tunaweza kuiadhibu serikali yetu na ikatusikiliza iwapo tu tutainyima mapato. Na hili linawezekana pasipo kuvunja sheria yoyote ya nchi hii, tena ni njia yenye ufanisi wa hali ya juu na isiyo na madhara yoyote ya kiafya kwa tutakaoitumia.
Tuhamasishane kususia unywaji wa pombe na vinywaji jamii ya soda, tuhamasishane kususia uvutaji wa sigara. Hii ina madhara makubwa kwa mapato ya serikali, lakini si kwa uchumi wetu kama taifa, kwani kutatokea substitution effect, isiyo na madhara kwa uchumi lakini yenye madhara kwa serikali kikodi. Badala ya serikali kununua silaha za kupambana na wananchi wake, hicho kidogo itakachokipata italazimika kulipa mishahara ya watumishi wake.
Chaguo sahihi ni kunywa maji, na kula pipi kali (kwa wavuta sigara). Hii itadhoofisha serikali, hivyo itasikiliza kilio cha watu wake.
Napenda kusikia mawazo toka kwenu.