Bunge la walafi na waroho na wabinafsi wakubwa Afrika
PENGINE tufanyeni utafiti kuhusu ni wabunge wa nchi ipi Afrika ambao ndio wanaoongoza kwa uroho, ulafi na ubinafsi.
Na wakati huohuo tuangalie Spika Kigeugeu na mbelenyuma mkubwa kuliko wote Afrika huku tukizingatia kuwa haijawahi kutokea fisi kuwa wakili katika kesi ya simba, mbweha, chui, paka na nyauduma kuiba nyama ya jamii husika.
Mimi ninaamini kabisa kwamba kuna nchi hapa Afrika ambao wanakula posho kumi kwa hivyo mbili za wetu sio kitu cha kutisha.
Ninaamini pia kwamba wabunge wetu kwa viwango vya Afrika wanalipwa mshahara kidunchu kuliko wote na wao ni safi mno kiasi ambacho yule ambaye ni tajiri ana pikipiki tu kama sio baiskeli.
Na ndio maana mnashangaa kuona kwamba nyie mkizungumzia wao kuacha mashangingi na kukubali magari madogo kama wenzao wa Kenya wao wanakaa kimya kwa sababu HAWANA, HAWANA KABISA!
Na wabunge hawa na mawaziri hawataki kuishi Dodoma kwa sababu hakuna bahari na ndito za IFM, CBE na UDSM ambazo kwao ni hasusa.
Wabunge wetu wanaoongoza kwa kutetea maslahi ya wale waliowatuma kuwawakilisha gizani kama sio bungeni na nitaorodhesha mafanikio yao kadhaa.
1. Kila Mtanzania katika kila jimbo hivi sasa angalau ana kiwanja kilichopimwa na kanyumba angalau ka vyumba kimoja na nusu.
2. Kila mji na kijiji Tanzania sasa kina barabara ya lami.
3. Kila jimbo Tanzania lina shule 100 za msingi, 200 za sekondari na Vyuo Vikuu vya Kikakoliki 3 vya Kiislamu Kimoja, vya Kiaghakan viwili na vya makafiri 4.
4. Kila mji na kijiji Tanzania hivi sasa vina umeme wa uhakika.
5. KIla jimbo Tanzania lina mfuko wake wa maendeleo ambao wa chini kabisa una shilingi bilioni 1,000.
6. Shule zote hapo juu zina walimu wenye nyumba nzuri na samani za Modern Furniture na hakuna anayepata mshahara chini ya shilingi milioni 2.
7. ATCL, yaani, lile shirika la ndege mnalodhani limekufa ndio shirika bora kuliko yote Afrika.
8. TRL na TAZARA ni baadhi ya mashirika bora ya reli duniani.
9. Barricks inalipia umeme wa vijiji vyote mkoani Mara kwa miaka 50 ijayo.
10. Wanafunzi wa vyuo vikuu toka kila jimbo sasa sio chini ya laki moja.
11. Wagonjwa katika kila jimbo hivi sasa wanatibiwa bure asante kwa hisani ya wachimba dhahabu nchini.
12. Kila mwananchi ana simu za mkononi. Moja ambayo ataitumia kupigia kura mwaka 2010. Nyingine kupokelea fedha kiasi cha shilingi milioni moja atakazotumiwa na mifuko ya rais wastaafu kila mwezi.
13. Ndege 1,000 zimenunuliwa ili kupiga mabomu mawingu ili yanye mvua kila jimbo.
14. Hivi leo kila Ubalozi wetu nchi za nje una hosteli yake ambayo kila Mtanzania anaweza kukaa kwa gharama ndogo na kupata huduma zote ili kurahisisha shughuli yake iwe ni kusoma, kuwekeza, biashara au diplomasia.
15. Mtanzania yoyote sasa anaweza kusoma hadi levo ya digrii kwa kutumia lugha mama yake ya Kiswahili.
16. Kila jimbo Tanzania litakuwa na intaneti ya bure kwa wasio na hela na pia redio na televisheni stesheni na gazeti lao la kutoka mara mbili kwa wiki maana mawasiliano ndio ufunguo wa maendeleo.
17. Maji kutoka Ziwa Mama Nyerere (VIctoria), Lake Nyasa, Lake Rukwa na Tanganyika yatatumika sio tu kunyweeshea mashamba makubwa ya ujima bali pia kuzalisha umeme kwa matumzi ya nyumbani na kuuza nchi za nje.
18. TBC sasa ni kama BBC na inasikika kote Afrika, Uarabuni na Ulaya kitlevisheni na kiredio.
Nchi kadhaa Afrika sasa zimekubali Kiswahili kuwa lugha ya taifa au angalau lugha ya pili au ya tatu nchini mwao.
19. Ubia katika ya wahandisi binafsi na wale wa vyombo vya dola sasa unasaidia kuzalisha magari ya aina mbalimbali, matrekta, friji, televisheni, mitambo ya kurusha matangazo, vifaa vya hospitali, satelaiti, kompyuta na kadhalika.
20. KUbwa zaidi ni kwamba uko bado TANZANIA na yote hayo bado ni ndoto maana wabunge badala ya kuyazungumzia wao wanazungumzia POSHO ZAO MBILI, TATU, NNE na Mungu awalaani kwazo milele na milele na hasa mwaka 2010! Upinzani acheni use..... unganeni msidanganywe kwa serikali kuahidi kuwapa wagombea urais wenu takrima au mtakwenda na maji kama kawaida yenu....