Hosea alitisha Bunge
Na Muhibu Said
3rd November 2009
Awaambia wabunge hawako juu ya sheria, watahojiwa
Awataka wampigie kura ya kutokuwa na imani naye
Asisitiza hana mpango wowote wa kujiuzulu Takukuru
Spika Sita asema Hosea anatapatapa na kupotosha umma
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk. Edward Hoseah.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, amelivimbishia msuli Bunge.
Katika kauli ambazo ni nadra kutolewa hadharani na kiongozi huyo wa taasisi nyeti dhidi ya muhimili mmojawapo wa dola, pia alisema tuhuma za kuisafisha kampuni ya kitapeli ya kufua umeme ya Richmond, anazohusishwa nazo na Bunge, kamwe hazimnyimi usingizi na kwamba, kama wabunge wanamuona hafai, basi watumie utaratibu wao wa kupiga kura bungeni ya kutokuwa na imani naye ili angolewe kwani Takukuru siyo mwisho wa maisha yake.
Dk. Hoseah alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa na Takukuru za kuwahoji baadhi ya wabunge kwa kupokea posho mara mbili kwa kazi moja kutoka taasisi tofauti za umma.
Ufafanuzi huo aliutoa katika mkutano wake na waandishi wa habari, aliouitisha makao makuu ya Takukuru, jijini Dar es Salaam.
Alisema mchakato wa Takukuru wa kuwahoji wabunge kuhusu tuhuma hizo, unaendelea kwa vile unalindwa na sheria na kwamba, kama wamemuona hafai, basi watumie utaratibu wao wa kupiga kura bungeni ya kutokuwa na imani naye, badala ya kuendelea kulalamika kuwa wamedhalilishwa.
Dk. Hoseah, ambaye jana alizungumza kwa kujiamini, alitoa kauli hiyo alipoulizwa na mmoja wa wanahabari kwamba, wabunge wameonyesha hawana tatizo na Takukuru, bali wana tatizo na Dk. Hoseah kuhusiana na kashfa ya Richmond, kwanini basi asijiuzulu kama kweli yeye ni muadilifu?
Zoezi linaendelea, kwa sababu sheria inatulinda, hatuhitaji kuomba kibali cha mtu yeyote. Kazi yetu ni kutafuta ukweli, hakuna kudhalilishana hapa. Kama wameona hawana imani na mimi, wapige tu kura,
mimi nachapa kazi yangu, sikosi usingizi, niko hapa kuwatumikia Watanzania.
Labda sura yangu mbaya, hiyo ni bahati mbaya. Lakini kuna maisha baada ya Takukuru, alisema Dk. Hoseah bila kufafanua na kuongeza:
(Wabunge) waache danganya toto hapa, kwani huo ni uchunguzi tu wa kawaida, mbona wananchi wengine tunawahoji, mbona hawalalamiki kwamba, wamedhalilishwa?
Alisema kamwe hawezi kujiuzulu kuongoza taasisi hiyo na hana mpango huo na kudai kwamba, hata taarifa ya Kamati Teule ya Bunge, kifungu cha 20, haijapendekeza afanye hivyo.
Tusome taarifa ya Kamati ya Bunge Ibara ya 20. Mpango huo (wa kujiuzulu) sina, nihukumu kwa makosa niliyotenda, si hisia. Siwezi kujitia kamba nionekane mzalendo, alisema Dk. Hoseah.
Alitoa kauli hiyo alipotakiwa na mwanahabari mwingine katika mkutano huo wa jana, aonyeshe uzalendo kwa kujiuzulu kama walivyofanya baadhi ya viongozi baada ya kutuhumiwa kuhusika katika kashfa ya Richmond.
Awali, alisema amelazimika kutoa ufafanuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa na Takukuru za kuwahoji baadhi ya wabunge kwa tuhuma hizo, baada ya kuwapo na kauli na mitazamo mbalimbali miongoni mwa jamii kuhusu jambo hilo, na pia, madai kuwa taasisi hiyo imekosea kuwahoji wabunge na kwamba, imeingilia haki na kinga ya wabunge.
Alisema miezi kadhaa huko nyuma, Takukuru imekuwa ikipokea taarifa zinazohusu baadhi ya wabunge kupokea posho mara mbili wanapokwenda kufanya kazi zao za Kamati za Bunge; kwa kulipwa na Ofisi ya Bunge kama ilivyo wajibu na wanapofika kwenye wizara au shirika la umma au idara inayojitegemea ya serikali, wamekuwa wakilipwa posho na yule wanayemkagua.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Takukuru alisema kitendo cha kulipwa posho mara mbili kwa kazi hiyo hiyo na taasisi mbili tofauti za umma, ni kinyume cha sheria za matumizi ya fedha za serikali.
Dk. Hoseah alisema kufuatia hali hiyo, Februari 26, mwaka huu, Takukuru iliandikiwa rasmi na Ofisi ya Bunge kuitaka ichunguze tuhuma hizo na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Alisema Takukuru ilipata taarifa hizo na ilifanya uchunguzi wa msingi kwa kutumia taratibu zake na matokeo ya uchunguzi umeonyesha kuwa tuhuma hizo zinaelekea kuwa ni za kweli.
Dk. Hoseah alisema baada ya Takukuru kuridhika kuwa kuna hoja ya msingi ya kuyafanyia kazi malalamiko hayo, waliona kuwa kuna haja ya kuwahoji wahusika ili kuwapa nafasi ya kujua tatizo na wao watoe maelezo yao kwa mujibu wa haki za asili ili waweze kukamilisha uchunguzi wao.
Hata hivyo, Dk. Hoseah alikataa kuwaonyesha wanahabari barua inayodaiwa kuandikwa na Ofisi ya Bunge kuiomba Takukuru iwahoji wabunge alipotakiwa na baadhi ya wanahabari kuionyesha na kusisitiza kuwa hata viongozi wa taasisi na mashirika ya umma waliowapa wabunge posho hizo, baadhi yao wameshahojiwa na Takukuru.
Nia yetu ni kutaka kujiridhisha iwapo tuhuma zilizotolewa kwetu ni za kweli na matokeo ya uchunguzi wetu yaweze kuthibitisha kama kuna ukweli kiasi gani kuhusu tuhuma hizo, alisema Dk. Hoseah na kuongeza kuwa uchunguzi wao hauwalengi wabunge waliomo kwenye Kamati ya Nishati na Madini na Kamati Teule ya Bunge na kusema kwamba, hata Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) pia, alihojiwa licha ya kwamba, si mjumbe wa kamati hizo.
Alisema wameshutumiwa kwamba, mahali na mazingira ya kuwahoji wabunge havilingani na hadhi ya wabunge na kusema kwamba, jambo hilo linaweza kuwa na ukweli kwa namna fulani kwa mtazamo wa mtu na
kulitaka Bunge liwapatie bajeti ya kutosha ili waboreshe mazingira yao ya kazi.
Dk. Hoseah alisema pia, wametuhumiwa kwamba wabunge wamekuwa wanahojiwa na maafisa wadogo sana na kusema kwamba, anayesimamia jambo hilo ni Ofisa Mchunguzi Mkuu, ambaye amekuwa katika fani hiyo tangu mwaka 1973 na kwamba, kwa umri alionao hadi sasa, anatarajia kustaafu mwakani.
Siamini mtu anayekaribia umri wa kustaafu mwakani ni kijana mdogo. Na kama hivyo ndivyo, ndiye mwenye umri mkubwa tuliyenaye ndani ya Taasisi kwa wakati huu, alisema.
Alisema Takukuru pia imetuhumiwa kwamba kwa kuwahoji wabunge imekiuka sheria inayohusu Kinga, Madaraka na Haki za Wabunge na kusema kwamba, wanachoamini kwamba taasisi haikukiuka sheria hiyo akisema kwamba, kinga ya wabunge haihusu vitendo kama hivyo wanavyovichunguza.
Dk. Hoseah alisema kinga ya wabunge inahusu kauli aliyoitoa bungeni au kwenye kamati yoyote ya Bunge, maandishi ya mbunge kwenye taarifa ya Bunge au Kamati ya Bunge na kwa chochote kitakachotolewa na mbunge bungeni kwa njia ya muswada uwe wa binafsi au vinginevyo.
Mtanzania yeyote awe wa cheo chochote hana kinga dhidi yake kwa tuhuma zinazoangukia katika makosa ya rushwa yanayotawaliwa na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 ambayo waheshimiwa wabunge wenyewe waliitetea na kuitunga kuwa sheria, alisema Dk. Hoseah.
Kwa heshima na unyeyekevu mkubwa kwa waheshimiwa wabunge nawaomba waiache Takukuru ifanye kazi zake kwa mujibu wa sheria. Waheshimiwa wabunge, nawaomba muongoze kwa mfano.
Bunge letu lina sifa kubwa ya kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi ambao ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka, tungependa suala hili lisiwe chanzo cha kulipunguzia heshima yake kubwa ndani na nje ya nchi ambayo Bunge letu tukufu limejijengea. Tupeni ushirikiano wenu ili tuwatumikie wananchi wa Tanzania vizuri, alisema Dk. Hoseah.
Hata hivyo, alipoulizwa na Nipashe jana kuhusu barua inayodaiwa na Dk. Hoseah kwamba, iliandikwa na Ofisi ya Bunge kuiomba Takukuru iwahoji wabunge kuhusu posho mbili, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alisema hakuna barua ya namna hiyo iliyoandikiwa na Ofisi ya Bunge.
Aionyeshe hiyo barua na imesainiwa na nani. Sababu ninachojua tuhuma ambazo ziliandikiwa barua tena na makatibu wa kamati mbili za Bunge, zilihusu tuhuma dhidi ya baadhi ya wabunge kudai rushwa ya fedha taslimu.
Tuhuma hizo zilitoka Ikulu ndio makatibu wa kamati hizo wakaiandikia Takukuru kuiomba ichunguze na hayakuwa maombi ya jumla ya kuvamia Ofisi za Bunge na kuanza kuwahoji waheshimiwa wabunge bila utaratibu, alisema Spika Sitta.
Kuhusu kauli ya Dk. Hoseah ya kuwataka wabunge wapige kura ya kutokuwa na imani naye kama wanamuona hafai, Spika Sitta alisema:
Anatapatapa, na ni upotoshaji kwa umma kwani kwa mujibu wa Katiba ya nchi, anayepigiwa kura na wabunge ya kutokuwa na imani naye ni Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Rais na wala si waziri wala mkuu wa taasisi.
Dk. Hoseah anaibuka na kauli hizi huku Bunge likitarajiwa wakati wowote kuanzia sasa kupokea taarifa ya Serikali ya utekelezaji wa maazimio ya Richmond, kati yake ikiwa ni kuchukuliwa hatua kwa kiongozi huyo kwa kutokuwa makini katika uchunguzi wa mkataba huo.
Takukuru kabla ya kamati teule ya Bunge kuchunguza mchakato wa Richmond na ripoti yake ikamfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri wawili, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha kujiuzulu kwa sakata hilo, Takukuru walikuwa wamechunguza mkataba huo na kuona ni safi.
CHANZO: NIPASHE