Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amemjibu Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, akisisitiza kuwa uongozi wa nchi unahitaji mipango na kura za wananchi badala ya maombi ya ‘kupewa’ nchi ili kuijaribu.
Akizungumza leo katika mkutano wa hadhara wa kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimboni Ubungo mkoani Dar es Salaam kwa kipindi cha Novemba 2025 hadi Julai 2026, Prof. Kitila amerejea kauli ya Heche aliyoitoa hivi karibuni akidai kuwa upinzani ukipewa nchi kwa miaka miwili tu mabadiliko yataonekana.
“Sasa kuna kiongozi mmoja wa upinzani nimemsikiliza juzi akiongea na vijana wa chama chao... anasema hivi sisi watupe nchi miaka miwili tu waone... Sasa unafikiri nchi unapewa? Huwa inapewa hivyo? Hii nchi uongozi unapatikana kwa kura sio kwa kupewa,” amesema Prof. Kitila kwa msisitizo
Prof. Kitila amebainisha kuwa uongozi ni dhamana nzito inayohitaji mikakati na siyo majaribio. Amesema kuwa CCM kimejikita katika mipango ya maendeleo wakati wapinzani wamebobea katika "kuzodoa".
Soma Pia: Prof. Kitila: CCM haiwezi kufundishwa demokrasia na yeyote nchini
“Uongozi wa nchi sio uji kwamba kila mtu anataka apewa kuonja... uongozi wa nchi ni mipango, uongozi wa nchi ni mikakati. Uongozi wa nchi ni utawala bora... uongozi kuongoza sio kubobea kwenye kuzodoa. Wewe ukibobea kuzodoa, my friend, kuzodoa kupiga kelele nyingi hiyo inafurahisha,” ameeleza Prof. Kitila