Mgombea wa Urais wa Kenya kupitia NASA,Raila Odinga amejitokeza na kupinga matokeo ya awali ya Urais ya Kenya yanayotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya yakimweka mbele Rais Uhuru Kenyatta.
Hoja ya Odinga ni kukosekana kwa Fomu 34A na 34B zinazopaswa kujazwa na kusainiwa,ikiwa ni pamoja na mawakala, kisheria kabla ya kutangazwa matokeo. Fomu 34A hujazwa na kusainiwa katika Kituo cha Kupigia kura. Kimsingi,Fomu 34A hubeba taarifa za kura za kituo kimoja.
Fomu 34A huwasilishwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo. Taarifa zote za vituo vya Jimbo husika hujazwa kwenye Fomu 34B. Hatimaye,Fomu 34B huwasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kutangazwa matokeo rasmi.
Kujazwa kwa Fomu nilizozitaja,ni sharti la kisheria. Lazima kuzijaza na kuziwasilisha. Inataarifiwa kuwa Tume ya Uchaguzi ilitangaza matokeo bila Fomu 34A na 34B. Kwasasa,Tume inakusanya Fomu wakati matokeo yameshatangazwa na kubishiwa.
Hivyo,Odinga ana hoja ya kisheria kuyabishia matokeo hayo. Je,atayapinga matokeo ya Urais kisheria au kisiasa? Matokeo yaliyotangazwa bila fomu husika yanabakije kama halali? Raila Odinga ataamua muda ukifika.Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya,Tume ya Uchaguzi ina siku 7 kumtangaza mshindi wa Urais.