Tokea mwaka 1992, nchi yetu iliamua kuirejesha nchi hii kwenye mfumo wa vyama vingi na mfumo huo ukaingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 3(1) ambayo inatamka wazi kuwa "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ni nchi ya vyama vingi" mwisho wa kunukuu
Ingekuwa Rais Magufuli anaurejesha mfumo wa chama kimoja, kutokana na ridhaa ya wananchi wake, kutokana na wananchi hao kupiga kura katika uchaguzi ulio huru na wa haki, mimi nisingekuwa na hoja ya kupinga
Lakini kwa njia hii tunayoiona tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo Rais huyu "analazimisha" ionekane wananchi ndiyo wameupokea mfumo huo wa chama kimoja, ndipo ninapokataa na kuiona njia hiyo ni uhuni wa hali ya juu na uvunjifu wa waziwazi wa Katiba yetu ya nchi!
Dunia nzima imeshuhudia namna ambavyo utawala huu wa awamu ya tano ulivyovunja Katiba ya nchi, kupitia kwa wasimamizi wa uchaguzi, ambao ni makada wa kindakindaki wa CCM, wakionekana kupewa "maagizo" maalum, kutoka juu, kuanzia zoezi la uandikishaji wapiga kura, uchukuaji fomu na urudishaji wa fomu hizo na namna walivyowa-disqualify, wagombea wa vyama vya upinzani, ambapo zaidi ya asilimia 95, wakakatwa majina yao, kwa kile wasimamizi hao wamekiita ni ujazaji mbaya wa fomu hizo za kuomba uongozi wa serikali hizo za mitaa
Wakati hayo yakifanyika kwa upande wa vyama vya upinzani nchini, hali imekuwa tofauti kabisa kwa upande wa Chama tawala cha CCM, ambapo wagombea wake wote wameonekana kama "malaika" kwa asilimia 100 ya wagombea wake kuzijaza kwa usahihi mkubwa na hivyo kuwa- qualify kuwa wagombea waliopita bila kupingwa!
Kutokana na hali hiyo, vyama vinane, vikiongozwa na chama kikuu cha upinzani nchini cha Chadema, kutangaza kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho katika huo "uchafuzi" unaotarajiwa kufanyika hapa nchini, tarehe 24 ya mwezi huu
Kumetolewa miito kadhaa na vyama hivyo vya upinzani, pamoja na viongozi wa dini mbalimbali, kuomba uchaguzi huo ufutwe na upangwe katika tarehe nyingine, chini ya Tume mpya ya uchaguzi iliyo huru, lakini miito yote hiyo, imekuta masikio ya watawala wetu yakiwa yamewekwa "pamba" masikioni na kuamua kuendelea na uchaguzi huo.
Ndipo hapo ninapoona kuwa Rais Magufuli ameamua kuivunja Katiba ya nchi hii waziwazi kabisa kwa kutaka kuurejesja mfumo wa chama kimoja kwa nguvu, bila ridhaa ya wananchi hao.
Je Rais Magufuli aendelee kuchekewa na aendelee kuimbiwa mapambio na wananchi wote wa nchi hii kwa kuungana na kujiunga na "praise and worship team for Magufuli" kwa huu uvunjifu wa Katiba ya nchi wa waziwazi kabisa?
Tunajua kuwa watawala wetu wanakuwa na kiburi na kulewa madaraka kwa kiasi cha kutisha, kwa kuamini kuwa wao ndiyo "wanaolimiliki" Jeshi la Polisi nchini na ndiyo sababu kuu, inayowafanya watishie wananchi wote kuwa atakayeupinga huo UCHAFUZI wao atashughulikiwa ipasavyo!
Nakaribisha maoni katika kuirekebisha hali hiyo ambayo inanyemelea Taifa letu ambapo zoezi muhimu sana la kidomokrasia la kutoa Uhuru kwa wananchi wa nchi hii, kuchagua viongozi wanaowataka wenyewe katika uchaguzi ulio huru na haki, ukiwa umenyongwa.
Nitoe wito kwa watawala wetu walioamua kuweka pamba masikioni, kuwa zoezi la wananchi kuchagua viongozi wao katika uchaguzi ulio huru na haki, kupitia sanduku la kura, ndiyo njia pekee, inayoweza dumisha AMANI na UTULIVU hapa nchini.
Watawala wetu watakuwa wanajidanganya kupita kiasi kwa kuamini kuwa risasi, magari ya washawasha na mabomu ya machozi ya Jeshi letu la Polisi, ndiyo yatakayowadumisha wao CCM madarakani.
========
Mawazo ya wachangiaji