Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu amesema wakati anachukua kijiti cha Urais kuna baadhi ya Watu (Wahafidhina wa Mfumo Dume) hawakuamini kwamba Mwanamke anaweza kuwa Rais na akaongoza vizuri na kwamba wapo walioenda mbali na kusema hatuna Rais tuna House Girl na maamuzi yake ni ya kitchen party lakini kwa sasa kwa kazi nzuri aliyofanya, Watu hao wote wamebadili mitazamo yao na wamekubali kuwa inawezekana Mwanamke akaongoza kiti cha Urais vizuri.
Rais Samia amesema hayo leo February 21,2025 wakati akiongea kwenye Maadhimisho ya Miaka 10 ya Programu ya Mwanamke Kiongozi yaliyofanyika Jijini Dar es salaam.
Rais Samia amesema
“
Bakari amesema kuna wakati kunja speech yako tuambie ya moyoni, hapa nataka kusema ya moyoni, kwenye Wahafidhina wa Mfumo Dume, wakati ule hakukuwa na imani kabisa, hakukuwa na imani au kuamini kwamba yule Mwanamke anaweza kufika hapa, kuna waliothubutu kusema tuna Rais wa kuambiwa fanya tu na atafanya, kuna waliothubutu kusema hatuna Rais tuna House Girl, kuna waliothubutu kusema maamuzi ya kitchen party yake ambayo nilikuwa nafanya, kwahiyo unaweza kuona imani ya wenzetu anaposimama Mwanamke”
“Lakini leo nadhani wote wamebadilika, kwahiyo unapotaka kuondoa na kujenga imani kwa wenye mtazamo mwingine fanya yale yanayotarajiwa ili yaleta imani na kuaminiwa, tumefanya yaliyotarajiwa na sasa yule House Girl hayupo tena, maamuzi ya kitchen party hayapo tena yanakuwa ya maana sasa”
“Kwahiyo Wanawake wasomi na Viongozi wenzangu tambueni kuwa jitihada za kuendelea kuielimisha Jamii yetu kufahamu kwamba usawa wa kijinsia sio mapambano ya Wanawake kutaka kuwa juu ya Wanaume hapana, bali ni hitajio la Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungani wa Tanzania isemayo Binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, kinachotutofutisha mbele ni malezi na makuzi”