Rais Samia kutunukiwa tena Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Cha Anga Korea (KAU)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara katika Jamhuri ya Korea Kusini kuanzia leo tarehe 30 Mei 2024 hadi 6 Juni 2024 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Korea Kusini Mhe. Yoon Suk Yeol.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam Jana tarehe 29 Mei 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amesema Mje. Rais Samia ataanza ziara rasmi ya uwii nchini humo itakayofanyika tarehe 1 na 2 Juni 2024.
Ziara hiyo itafuatiwa na ziara ya kikazi itakayomuwezesha kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Afrika na Korea utakaofanyika tarehe 3 na 4 Juni 2024.
Mhe. Makamba amesema ziara rasmi ya Mhe Rais Samia nchini humo inalenga pamoja na mambo mengine kukuza na kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili ambao umedumu kwa miaka 32 sasa tangu ulipoanzishwa mwaka 1992.
Mhe. Makamba ameongeza kuwa, akiwa nchini humo Rais Samia atakutana kwa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Yoon Suk Yeol yatakayofanyika tarehe 2 Juni 2024.
Amesema mazungumzo hayo yatajikita kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, elimu na miundombinu.
Mhe. Makamba amesema wakati wa ziara hiyo, mikataba saba (7) ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizi mbili itasainiwa. Ametaja mkataba mmojawapo unahusu msaada wa fedha kati ya Benki ya Exim ya Korea na Tanzania ambao utaiwezesha Tanzania kupata msaada na mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Bilioni 2.5 (sawa na Trilioni 6.5) ambao ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo yaani mwaka 2024/2028.
Pia amesema Hati ya Makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi ya Miamba na Madini ya Korea ambayo itahusu ushirikiano katika masuala ya utafiti, uchoraji ramani na shughuli za maabara itasainiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba, amesema Dkt Samia akiwa nchini humo, pia atatunukiwa Udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Anga Korea (KAU) kwa lengo la kutambua mchango wake wa kuleta mabadiliko, sera na uongozi wa kimantiki.