Jambo la kwanza, nadhani mama ni lazima aambiwe kwamba Kenya sio majirani zetu pekee, kiasi cha kumchukulia muda wake mwingi kushughulika nao.
Tunao majirani zetu wengine ambao kwa kweli hatujafanya juhudi kubwa za kushirikiana nao. Hata Uganda mwenyewe, nchi ambayo tumeimwagia damu zetu, mpakani kuna njia moja tu hapo Mtukula inayotuunganisha, Kenya karibuni tunazo njia nne kuu za mwingiliano kati yetu; tena barabara zote zimechongwa vizuri.
Kwa nini sasa tuingie gharama nyingine tena kujenga barabara ya kuambaambaa pwani toka Malindi hadi Bagamoyo?
Kwa nini, angalao tusitumie pesa ya namna hiyo kuimarisha bandari ya kutuunganisha kwa uhakika zaidi na DRC ambao hatuna hata njia moja ya moja kwa moja kati ya nchi hizi?
Ninachoona kilichobaki kati yetu na Kenya, ni wao kutusambazia uchafu wao wa rushwa na ufisadi ili vishamiri zaidi hapa kama vilivyo huko kwao.
Hii ndiyo hatari kubwa tunayoweza kukumbana nayo kama tutalegeza misimamo aliyokuwa ameiweka marehemu Magufuli.