Leo kwa mara ya kwanza Rais Samia amekuja hadharani na kukiri wazi kuwa anaongoza serikali iliyogawanyika vibaya, amezungukwa na wasaidizi wanao mhujumu wazi wazi na yuko kwenye vita kali ya kuupambania urais wake kwa hali na mali. Hali ni tete mnoo kwake, na hatakubali!
Bila kumumunya maneno, wacha tuuseme ukweli ili kumsaidia Rais Samia popote alipo na ikibidi utafute njia ya kutokea.
Kwanza niweke wazi jambo moja kubwa na muhimu, kwa sasa Rais Samia amepoteza uungwaji mkono kutoka makundi yote muhimu ya kijamii na kisiasa, yaani umechokwa. Hili halina ubishi na halihitaji takafari yote yote kubwa.
Kitendo cha mama Samia kuja hadharani na kukiri kuwa 'wenzake wanamzunguka' hivyo hatakubali! Hapo tunaona picha kubwa moja tu, maji yamezidi unga na mama Samia anahitaji msaada ili avuke.
Sasa kuna jambo moja kubwa pekee linaloweza kumuokoa mama Samia mahali alipo, hana ujanja inabidi alikimbilie. Kwa ufupi, jambo hilo ni;
Kutafuta muafaka wa kitaifa ili kuweza kuiunganisha nchi iliyoparaganyika vibaya kisiasa. Kama Samia hataweza kukaa na kumaliza tofauti zake na kundi kubwa la wafuasi wa Magufuli (sukuma gang) au wapinzani (hususani Chadema) basi ajue hawezi kutoboa. Hayo ndio makundi yenye nguvu kwenye siasa za Tanzania kwa sasa, na kwa sasa yote mawili kwa pamoja (pasipo kuongozwa na mtu yoyote) yanasema wazi wazi kuwa mama Samia hafai, hatoshei kwenye kiti cha urais na hayamtaki tena. Huo ni uasi wa kisiasa.
Wakati ukuta, na majuto ni mjukuu, wenye hekima wameshaelewa!
Sehemu kubwa ya matatizo amejisababishia yeye mwenyewe kwa kutokuwa na msimamo unaojulikana, na badala yake akawa anayumbayumba tu kama bendera na upepo.
Alipoanza, akawa anajitambulisha yeye na mtangulizi wake ni kitu kimoja kwa maneno, huko vitendo vikionyesha tofauti. Hii ilionyesha alitamani kurekebisha yale aliyoona hayafai katika yale yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi wake. Hili lilipelekea baadhi ya watu waanze kumtazama kwa karibu zaidi na kuwa na matumaini juu yake.
Wakati hajatulia vizuri ili atekeleze hayo aliyotaka kurekebisha, kama kufuta mashtaka kwa watu ambayo kesi zake hazikueleweka; mara ghafla kisharukia kwenye yale yale ambayo watu walidhani yanamchukiza. Mbowe kawekwa gerezanikihuni kihuni, pengine kuliko hata ilivyokuwa ikifanyika wakati wa dikteta Magufuli.
Watu wakawa wamechanganyikiwa na hawajui Samia anasimamia wapi.
Kuna mambo mengine yaliyoambatana na safari yake ya Kenya yaliyofanya watu wengine kumtazama kwa jicho la wasiwasi kutokana na aliyokuwa akitamka wakati wa ziara hiyo. Kiongozi mgeni, na hasa anayepokea uongozi ambao hakujinadi yeye mwenyewe kwa wananchi hupashwa kuwa na subira nayo. Huwezi kuingia mara moja na kutaka ubadili kila kitu kufuatana na matakwa yako.
Samia kajitambulisha yeye ni rais anayejali maslahi ya walanguzi/madalali na wapigaji kuliko maslahi ya wananchi wa kawaida. Hili nalo limestua watu na kuanza kuwa na wasiwasi juu yake.
Rais Samia Suluhu Hassan, kaingia akiwa na haraka ya kufanya yake ambayo ni tofauti na yale ya mtangulizi wake. Sijui haraka hii ni ya nini, na haieleweki itamfikisha wapi.
Sasa itabidi achague, ili kurudisha matumaini ya watu kwake. Akichagua kupambana kwa dhati na hawa wanaotafuta kila njia ya kuzoa mali za waTanzania, na akaonekana kweli kasimama kidete bila kujali muhusika, watu watarudi kwake. Na kama atataka kuwa Rais wa hilo kundi linalotumia kila mwanya wa kuwadumaza wananchi katika vipato vyao, sina shaka yoyote hapo atakutana na mapambano mazito zaidi katika miaka hii michache kabla ya 2025.
Mimi namuomba asimame na wananchi, asimamie kwa dhati kabisa juhudi za wananchi kuleta maendeleo ya nchi hii. Wawekezaji wenye hadhi zaidi ya wote ni wananchi wenyewe, hao wanaompapatisha ni kuunga tu juhudi za wananchi wetu.
Yeye anasema: "Tanzania inahitaji zaidi Wawekezaji wa nje, kuliko Wawekezaji wanavyoihitaji Tanzania"? Nadhani haelewi umuhimu wa Tanzania ulivyo kwa wawekezaji hao. Ndiyo, ni sawa kuweka mazingira mazuri ya kuwavutia waje, lakini hii haina maana ya kwamba thamani ya Tanzania kwa wawekezaji hao ni ndogo kuliko uwekezaji wanaouleta wao.