Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ziara zake za kikazi nje ya nchi zimekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 4, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa kipande cha nne cha Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) Isaka-Tabora chenye thamani zaidi ya Sh2 trilioni.
Katika hotuba yake, Mkuu huyo wanchi ametumia nafasi hiyo kujibu hoja za baadhi ya watu wanaobeza ziara zake za kikazi nje ya nchi.
“Kwa leo tumesaini mradi wa gharama Sh2.94 trilioni na Dar es Salaam-Mwanza ni Sh16.92 trilioni, siku ninasema tutajenga vipande vyote hivi sikujua pesa nitaitoa wapi lakini kwa sababu ya kufunguka, kufuata watu, kuita watu tuzungumze hii pesa imepatikana,”amesema.
“Tunakwenda kuanza awamu ya pili, tukaungane na wenzetu wa Kigoma. Kwa hiyo awamu ya pili pia tuko kwenye mazungumzo namna ya kuzipata hizo pesa, kwa hiyo mambo yote ni mazungumzo, tunapowaita watu, tunapowafuata kuzungumza matokeo yake ndio haya,
“Wenye akili za kawaida ni rahisi kulaumu ‘Rais anasafiri tu, Rais hakai, badala ya kutembelea mikoa anatembelea tu nje, lakini matokeo yake ndio haya.” amesisitiza