THOMAS Nkola, mkazi wa Mtaa wa Majengo wilayani Maswa mkoani Simiyu, ameamua kufungua kesi mahakamani kushinikiza kuwajibishwa kwa watendaji wa serikali waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi katika ripoti ya mwaka 2021/22 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika mazungumzo na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Nkola (57), alisema ameamua kufungua kesi hiyo kwa kuzingatia Ibara ya 27(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
Kifungu cha (1) cha ibara hiyo kinatamka: "Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine."
Pia inatamkwa katika kifungu cha (2) cha ibara hiyo kuwa: "Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao."
souce: Nipashe