Wanabodi,
Hii ni makala yangu kwenye gazeti la Mwananchi la leo. Hakuna ubishi kuwa kilichotokea October 29, kimesababishwa na chuki iliyopitiliza!. Japo Ripoti ya Jaji Chande, imepunguza kidogo kiu ya taarifa kwa kuitaja idadi ya vifo, lakini bado haijapunguza machungu ya October 29 na kupooza chuki dhidi ya kilichotokea!. Chuki hii inaendelea kututafuna taifa, kimya kimya, chini chini, mdogo mdogo na kidogo kidogo kidogo kwa mtindo wa panafuka moshi. Chuki hii ni ugonjwa, ambao unakuwa na kuambukiza kwa kasi, usipotibiwa kikamilifu, hautakuwa na mwisho mwema!. Andamana nami jinsi ya kuutibu.
View attachment 3587941
Je ni wangapi miongoni mwetu, wajua kuwa chuki ikizidi ni ugonjwa?.
Chuki ni ugonjwa hatari na unaua!, tena unaoambukiza haraka kwa kasi ya kidigitali, hata kwa simu, sms, whatsapp, TV, Redio, magazeti au mitandao ya kijamii!. Natoa wito kwa Watanzania tuacheni chuki iliyopitiliza!.
Tiba ya ugonjwa huu wa chuki,ni kuwa na upendo,kwanza kwa kujipenda wewe mwenyewe,kisha kumpenda na jirani yako kama unavyo jipenda mwenyewe na hata ikitokea kuna mtu ni adui yako amekutenda visivyo,usimjibu kwa kumlipizia au kumtenda,bali mjibu kwa upendo, Adui Mpende!.
Kwa wale za zamani, tulioshuhudia ile Genocide ya Rwanda ya 1994, ilisababishwa na chuki tuu ya kikabila!, tena ni kabila moja hilo hilo , Watutsi na Wahutu, wote ni Wanyarwanda!. Waliuana kwa kuchinjana mpaka!. Kiwango hicho cha chuki kwa hapa nchini kwetu, kilifikia kikomo, October 29.
Naomba kueleza kisa kidogo cha kweli, wakati nikiwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDSM, nikiishi Block F, Mabibo, kunatokea visa vya wizi wa vitu vidogo vidogo, simu, vitabu, nguo, etc, kama kawaida, kwenye wengi kuna mengi,watu wakaanza kujenga chuki na wizi.
Kuna siku kuna mwanafunzi wa kike, alimpigia mtu yowe la mwizi, huyo kijana alivamiwa na wanafunzi wenye hasira za chuki ya kuibiwa, kijana yule alipigwa na alikufa papo hapo, na watu waliendelea kuupiga mwili wa marehemu, kumaliza hasira na chuki zao licha ya kujua ameishakufa!.
Polisi chuo walipokuja kuubeba, mwili, na kuuliza, aliyeibiwa ni nani, hakuna jibu, marehemu ameiba nini, hakuna jibu kumbe yule kijana ni mwanafunzi wa chuo, alikuwa amekwenda kwa rafiki yake wa kike, binti akapiga yowe la mwizi, kikatokea kilichotokea!. Mtu ukiwa na chuki iliyopitiliza, unarukwa na akili, unaweza kufanya jambo lolote hata kuua!.
Kufuatia kilichotokea ile October 29, ugonjwa huu wa chuki umeongezeka kwa Watanzanzia kwa kasi ya ajabu, huko mitandaoni ni hakufai, imefikia kiwango, mtu anakufa, badala ya watu kuhuzunika,ndio kwanza wanashangilia!.
Kufuatia kueneo kwa kasi kwa gonjwa hili la chuki miongoni mwa Watanzania, taasisi ya
Family Vibes Foundation (Family Vibes) ambayo ni shirika lisilo la kiserikali la Tanzania linalojihusisha na kuhamasisha na kuimarisha afya ya akili katika jamii nchini Tanzania, waliandaa semina maalum ya waandishi wa habari kuhusu Tiba ya Chuki iliandaliwa kama jukwaa la kitaifa la kuanzisha mjadala wa kijamii na kisera kuhusu namna bora ya kushughulikia changamoto za chuki, migogoro na upungufu wa mshikamano na upendo katika jamii.
Semina hiyo, ilihutubiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Family Vibes, Dkt. Mayrose Majinge ambaye alijenga msingi wa kitaaluma wa dhana ya Tiba ya Chuki kwa kuunganisha afya ya mwili, akili na jamii Semina hii ilihudhuriwa na waandishi wa habari zaidi ya 150 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, ikiwemo vikiwemo TV, Redio, Magazeti na mitandao ya kijamii.
Ushiriki huu mpana unaonesha nafasi ya kimkakati ya sekta ya habari kama “behavior change communication platform” katika kueneza elimu ya tiba ya gonjwa hili kwa jamii yetu, kwasababu vyombo vya habari vimebeba jukumu la kuwa daraja kati ya wataalamu, serikali na wananchi katika kueneza elimu ya afya ya akili na ustawi wa kijamii.
Dr. Majinge, alieleza katika mazingira ya sasa ya maisha yenye mabadiliko ya haraka, kutokuwa na uhakika na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi, kumekuwa na ongezeko la matatizo ya afya ya akili. Matatizo hayo yanajitokeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo migogoro ya mahusiano (mtu na nafsi yake, marafiki na wenza), majeraha ya utotoni, msongo wa mawazo wa muda mrefu, kuvunjika kwa familia pamoja na changamoto zinazohusiana na masuala ya kijinsia na mahusiano.
Shirika linafanya kazi kwa kutumia mbinu bunifu zinazolenga kushughulikia changamoto za kijamii, kiuchumi na kitamaduni zinazoathiri afya ya akili. Katika utekelezaji wake, linatumia dhana ya
Akili ya Kihisia (Emotional Intelligence – EI) pamoja na mbinu nyingine zinazokubalika na zinazoweza kutekelezwa kwa urahisi katika jamii.
Huduma hizi hutolewa kupitia programu yake ya
Mahusiano & Family Clinic ambayo ni mfumo wa huduma unaolenga kusaidia na kuimarisha ustawi wa familia, taasisi, jamii na taifa kwa ujumla kupitia huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia na kijamii (
Mental Health and Psychosocial Support – MHPSS).
Tafiti za kijamii na uchambuzi wa mwenendo wa kijamii zinaonesha kuwa, mivutano ya kihisia na kisaikolojia imeanza kujitokeza kwa uwazi zaidi katika jamii, hali inayohitaji mbinu mpya za elimu, uelimishaji wa umma na uimarishaji wa afya ya akili, changamoto hizi kwa Tanzania zilifikia kiwango cha juu tarehe 29 October, kwa vijana wenye chuki, kufanya uharibifu wa mali, na miundombinu ya umma, bila wao kujijua kuwa ni wagonjwa na vyombo vya dola navyo bila kujua vina deal na wagonjwa wa afya ya akiki,vikajibu mapigo kwa risasi za moto,na matokeo yake watu 518 wakipoteza maisha!
Vijana walioshikwa, walifikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa uhaini, hata hivyo, Rais wa JMT, Dr. Samia Suluhu Hassan, aliwasamehe kwasababu wengi wao walifuata mkumbo kwa kuambukizwa na ugonjwa huo wa chuki, bila wao kujua watendalo.
Baada ya Tume ya Uchunguzi wa Vurugu za Tarehe 29 October, 2025 kuwasilisha ripoti yake kwa rais Samia, kilichofuatia kwenye mitandao ya kijamii, ni watu wenye ugonjwa huu wa chuki, walifungulia matusi kwa kutukana, na Tume ilipokea simu zaidi ya 300 zikiwatukana matusi!. Kitendo tuu cha mtu kupiga simu na kutukana matusi,ni uthibitisho wa changamoto ya afya ya akili ya ugonjwa wa chuki.
Najua saa hizi Jeshi la polisi linaendelea na kamata kamata ya watukanaji hawa, bila kujua hawa ni wagonjwa wa afya ya akili, nashauri, kama wale waandamanaji wa October 29 walivyosamehewa kwa maana hawakujua watendalo, nashauri jeshi la Polisi, baada ya kuwashitaki ili kutoa funzo kwa wengine, Family Vibes waitwe, wakawatibu watu hao, na baada ya kupata tiba ya chuki, wasamehewe na kwenda kuieneza hiyo tiba kwa wengine, taifa liponywe na hili gonjwa la chuki iliyopitiliza.
Waandishi wamependekeza kuanzishwa kwa vipindi maalum vya kitaifa vya afya ya akili na mahusiano ya kijamii katika vyombo vya habari, na Makala elimishi kama hii kwenye magazeti na mitandao ya jamii ili kuliponya taifa letu na gonjwa hili la chuki.
Paskali