RIWAYA; URITHI WA GAIDI
NA; BAHATI MWAMBA
SIMU; 0758573660
SEHEMU YA KUMI
ma.
Remi aliguna tu.
“Sawa!! Naomba tuonane Panda hotel chumba namba 10,ila itabidi wote tusaidiane” alisema Kagoshima.
“Nikusaidie nini upande wangu” Alihoji Remi huku fikira fulani zikipita kichwani mwake.
“Ni mapema sana kusema ila lazima ujue ili nikusaidie lazima ujitoe” alisisitiza Kagoshima.
Toba!!
Remi alishika midomo yake huku akisikia utulivu wa hali ya juu kutoka upande wa pili.
“Sawa!!” alijibu Remi na kukata simu.
Naibu Kamishina P Kagoshima alitabasamu tabasamu fulani la ushindi.
“Namkula na kumfunga!! Mtoto safi huyu” Alisema Kagoshima akiwa peke yake ofisini kwake.
**
Mida ya saa mbili na nusu usiku ilimkuta Remi akiwa Pamba hotel na tayari alikuwa amekwishaingia ndani ya chumba namba kumi na alikuwa anatazamana na sura yenye ujivuni mwingi.
“Unakunywa wine?” alihoji Kagoshima.
“Hapana!” alijibu kwa mkato Remi.
Kagoshima alivuta funda moja la wine kisha akafinya midomo yake huku macho yake yakimtizama Remi.
“Ni kwamba hujawahi kunywa kabisa au ni leo tu” Alihoji tena Kagoshima.
“Sijawahi kunywa” Remi alijibu.
“Ooh sawa!! Na inakuwaje mrembo kama wewe unakosa kunywa lau hata tone la kileo?” Alihoji Kagoshima huku akigida tena funda la wine nzuri alioipenda.
Remi hakusema kitu.
“Mumeo Haji Makame hakika alifaidi sana kuwa na mwanamke mzuri kama wewe” Alisema tena Kagoshima.
“Afande nadhani tungelizungumza zaidi kilichotuleta hapa moja kwa moja” Alisema Remi huku akijitahidi kuzuia jaziba zilizoanza kumzonga kwa aina ya maongezi yale.
Kagoshima alitabasamu kifedhuli.
“Hata maongezi ya aina hii pia ndio yamenifanya nikubali kuonana na wewe japo wewe ni mtuhumiwa wangu” Alisema Kagoshima huku akitikisatikisa miguu yake aliokuwa ameibebanisha.
“Nadhani ulipaswa unisikilize shida yangu kisha utumie cheo chako kusimama katika haki na si uelekeo unaotaka tuelekee afande” Alisema tena Remi.
Kagoshima alicheka kwa sauti kisha akasema…
“Kwanza nikiwa mitaa hii huwa siruhusu kuitwa afande, na pia mwanadamu ni mwanadamu tu haijalishi ni yapi anakutana nayo ila hisia zinabaki kuwa pale pale” Alisema Kagoshima huku akiwa sasa ameifumbata mikono yake pamoja na kuikunja usawa wa kinywa chake.
“Kabla sijakwambia shida yangu naomba unambie unalenga nini” Alihoji Remi.
“Hakuna nacholenga zaidi ya mahusiano na wewe kisha nitajua namna ya kukusaidia” Alijibu Naibu Kamishina Kagoshima.
Remi alihisi mwili ukipitiwa na upepo baridi mithili ya pumzi za panya kwenye kidole cha mguu.
“Ila si wajua mi ni mke wa mtu?” Alihoji Remi.
“He is no more,hayupo tena na ni kama amekutelekeza tu huku akiwa amehamia na kuwa gaidi” Alisema kwa kebehi Kagoshima.
Remi alikunja ndita na kushusha pumzi ili kujaribu kuzuia gadhabu zilizoanza kumpanda.
“Lakini utawezaje kuwa na mahusiano na mkimbizi ambae habari zake zimetapakaa kote nchini ama ni vipi utakuwa na mtuhumiwa wa utekaji na mauaji?” Lilikuwa ni swali muhimu sana ambalo Remi aliuliza.
Kagoshima akacheka kisha akasema
“Lakini usasahu mi ni nani katika nchi hii”
“Sawa! Lakini usisahau ya kuwa cheo ni dhamana na nyakati hazidumu pia ila hatia ama tuhuma zinaishi milele na zaweza ibuliwa wakati wowote” Alisema Remi.
Kagoshima aliingiwa vyema na maneno yale nae akaamua kuhamisha mada.
“Anyway naomba unambie kilichofanya ukahitaji tukutane hapa”
“Nimegairi, kwa sababu ili unisaidie utanidai ngono” Remi alitamka wazi wazi mbele ya Kagoshima.
“Hapana,yote ni mapenzi yangu tu nilionayo kwako tangu siku ya kwanza niliokuona hivyo kuhusu tuhuma ni nje ya haya” Alijitetea Kagoshima.
Remi akasimama kwa lengo la kutoka ndani ya chumba kile, lakini kwa wepesi wa hali ya juu alijikuta akidakw mkono na mikono imara ya Kagoshima.
Vipi mrembo mbona unaenda tukiwa hatujamalizana” Alihoji Kagoshima.
“Kwani wataka tumalizaneje?” Alihoji huku akitetemeka.
“Aah kwani mi nimekwambiaje?”
“Lakini wajua utahukumiwa kwa kutaka kulala na mtuhumiwa?” Alihoji Remi.
Kagoshima akatoa macho kwa gadhabu na kumnasa kibao kikali Remi.
“Mimi sijawahi kataliwa wewe..iweje wewe unipe kebehi?” Alihoji kwa gadhabu Kagoshima.
Remi alijishika shavu lake lililokuwa linachonyota kwa ukali wa banzi alilopigwa.
“sasa naita maafande wakukamate”
Remi alinyoosha mikono na kumwambia..
“funga pingu, na unipeleke kituoni, matatizo yangu sio fursa kwa mafisi”
Kagoshima akaishia kumtazama Remi na asimmalize kwa ujasiri aliomuonesha.
Remi hakuwa mwanamke wa kutishika kwa vitisho vidogo; Remi tangu anakuwa hadi anafika hapo alipo ameshuhudia mengi kuliko hilo alilotaka kufanyiwa na Kagoshima.
Remi hakuteteleka kamwe. Remi alijali utu wake na kumvulia nguo Kagoshima ilikuwa ni kama kuutupa utu wake na kumdhalili mumewe.
Hata!! Hilo asingeweza kulifanya kamwe, huku akiwa hajui kama kukubali kudhalilishwa inaweza kuwa bado ni hasara, akachezewa na bado akaingizwa kwenye hatia!!.
Remi akaona bado afande amepigwa na butwaa,akavua mkoba wake na kuutupia kwenye sofa kisha akaanza kuvua T-shirt aliokuwa amevaa akaitupa pembeni na kubaki na braa kisha akaanza kufungua zipu ya suruali yake.
Dah!!
Kagoshima akabaki akiwa amebutwaika bila kujua lengo la Remi.
Kagoshima akamdaka mikono Remi wakati akianza kuishusha suruali yake.
“Sasa nini mana yake?” Alihoji Kagoshima.
“Nimekwambia wapigie wanikamate umeshindwa, sasa nataka nikuvulie nguo unifanye unavyotaka ili roho yako iridhike,shida yako si mwili wangu?” Alizungumza kwa jaziba Remi huku akifanya jitihada za kujinasua mikononi mwa Kagoshima.
“Ni kweli nakuhitaji ila unanishangaza kidogo kwa…”
“sio nakushangaza ila wewe ndie wanishangaza, hakuna haki inayopatikana kwa kuhongana mwili ndani ya Pamba hotel” alifoka Remi.
Kagoshima aligwaya na aliona amekosea mbinu, ikabidi awe mpole.
“Tafadhali naomba uvae nguo zako na uende” Alisema Kagoshima huku akirudi kukaa kwenye sofa lililokuwa mle ndani na kubaki akimtizama Remi akishugulika kuvaa nguo zake.
Remi alipokwisha kuvaa akadaka mkoba wake na kutoka nje.
Alipofika tu nje ya chumba akapumua kwa ahueni huku akitikisa kichwa kwa kushindwa kuamini kama kweli amejinasua mikononi mwa baradhuli yule anaetaka kutumia matatizo yake kujistarehesha.
“Kagoshima mtu mwenye tamaa nyingi sana” Alijisemea Remi huku akitokomea mbali na hotel ile.
Kagoshima nae alibaki akiwa amenuna na asiamini kilichomkuta kutoka kwa mwananke yule.
Akatoa tusi zito na kujitupa kitandani huku akimalizia kutuma ujumbe kwa kimada wake aende kumsindikizia usiku wake ulioharibiwa na Remi.
Usiku ukapita na ikaja ahsubuhi yenye mauzauza yake.
***
Ahsubuhi ilimkuta Sajenti Kobelo akiwa na gazeti mkononi mwake huku akiwa kwenye foleni akielekea mwananyamala.
Kurasa ya mbele ya gazeti lile ilikuwa imepambwa na picha kubwa ya Remi akiwa ameinama kutazama maiti iliokuwa chini huku kichwa cha habari kikisomeka “Balaa la mkimbizi laondoa uhai wa polisi” huku maneno ya pembeni yaliosindika picha zile yakisema “ni yule aliekwepa kulipa kodi na kuishi nchini kinyemela, aua askari aliefuatilia kesi yake…”
Sajenti akalikunjua kwa ndani na kuanza kusoma yaliondikwa kuhusu sakata lile.
Alipomaliza akarudi kutazama tena picha ile.
“Mbona hajaonekana kuwa na bastola au silaha yoyote? Lakini kama sie ni nani muuaji na aliepiga picha ni nani na alijuaje kuna mauaji tena ndani ya jumba lenye uzio?”
Akiwa anajiuliza hayo akapigiwa honi na gari lililokuwa nyuma yake kuashiria atembeze gari foleni inasogea!!
Kichwani mwake maswali yalikuwa ni mengi kuliko majibu.
Ahsubuhi ile radio mbali mbali zilikuwa zinatangaza vichwa vya habari vya magazeti mbali mbali huku ikionekana habari kubwa ni ya mauaji ya ofisa wa jeshi la polisi.
Remi pia ambae hakuwa na usiku mzuri pia alikuwa ameamka na habari zake zilizoonekana kutikisa ahsubuhi ile.
Remi aliishiwa nguvu na kubaki akiwa anachuruzikwa na machozi sambamba na kamasi.
Remi alijuta kuijua Tanzania; na bado hakujua kiini cha yale yote na nini hatima ya mchezo ule na kwanini alilengwa yeye.
Hakika alitatizika!.