Mzee wa Busara
Naondoka kutoka kwa Rafiki yangu naona ngoja nizunguke zunguke kupoteza mawazo, ingawa najua ni hatari na aibu takutana na wanaonidai... ila tafanya nini bora nianze kuzalisha na kuwalipa kidogo kidogo kuliko kuendelea kuhahirisha tatizo.
Sijui cha kufanya, takimbilia wapi, tafanya nini Maisha yangu yote nilikuwa najichanga ili mwisho wa siku nikimbilie kijijini na familia yangu, hilo sasa ni historia, sina pa kwenda wala kukimbilia.
Inabidi sisi machinga tuwe wamoja, inabidi tupate misaada, inabidi tuwezeshwe, tupate mikopo isiyoumiza inabidi na sisi tuwe kama wananchi huru katika nchi yetu…,
Samahani Mzee….!!! Katika lindi la mawazo yangu nilijikuta natembea bila kuangalia mbele na kujikuta nimemkanyaga mzee mmoja wa makamo…, hii sio sura ngeni kwangu huwa namuona ona anatembea tembea hapa na pale hakuna ajuaye alitokea wapi wala anafanya nini alikuwa mzee wa umri kama miaka 70, mvi zimejaa mpaka kwenye nyusi, sura ya makunyanzi na muda wote alikuwa akionekana kama mtu mwenye fikra sana…
Usihofu kijana wangu…, pamoja na kwamba huyu bwana nilikuwa namuona kila siku kwa muda kama wa miaka miwili hii ndio ilikuwa mara ya kwanza kusikia sauti yake na kusemeshwa nae, wengine walikuwa wanamuogopa labda ni mchawi au usalama wa taifa, au alitelekezwa na ndugu zake, au alikuwa mwizi, sababu ingawa hakuna aliyejua anafanya nini ila alionekana ameshiba, na nguo zake ingawa hazikuwa za gharama (kanzu, kibaraghashee na kandambili) lakini vilikuwa nadhifu na visafi.
Mbona unaonekana unatazama bila kuona, vipi unawaza nini?
Mzee sifurahishwi na hali iliyopo, nimechoka kuishi Maisha ya kubangaiza, hapa sina mtaji… mke watoto wananitegemea, nikienda benki siwezi pata mkopo, taishi vipi mimi, nikisema nifanye uharifu tafia gerezani.
Unasema mkopo?
Ndio Mzee…..
Ili uchukue nini au ufanye nini ?
Bidhaa mbona nyingi mzee?
Naam najua bidhaa ni nyingi si unaona umati huu wote wana bidhaa?
Unamaanisha?
Unaona yule kijana pale mchonga vinyago…, kweli ana kipaji na anafanya anachokipenda…, anatumia muda mwingi kutengeneza kinyago chake ila bei anayouza haikidhi mahitaji yake, Nina uhakika ingawa wewe ni mpenda vinyango, ila unaishia kuangalia tu kwa macho sababu hauna uwezo wa kununua…, sasa huyu akipewa pesa itasaidia…
Ndio Mzee itasaidia kununulia vifaa na…
Kasema hana vifaa ? huoni kwamba msaada zaidi kwake ni kama angekuwa amezungukwa na watu wenye kipato na uwezo wa kununua…
Unamaanisha masoko ?
Ndio masoko, ila masoko hayo yatatoka wapi iwapo watu hata mkate wa kila siku unawashinda kupata, kweli watanunua vinyango?, alisema mzee wa Busara kwa masikitiko…, au mpaka tungojee watalii wakija ndio huyu bwana apate faida ya jasho lake, yaani uhai wetu unategemea hisani ya mtu wa magharibi ya mbali…
Niliwaza kwamba ni kweli hata Ashura tukisema apewe mtaji labda akafungua mgahawa je wateja wake watabadilika au tutakuwa kina sisi…, na hata Ashura akitoka kwenye huu ubangaizaji itakuwa bora kwake ila tutawasaidia kina Ashura wangapi iwapo hata Mangi ni mwaka juzi tu kafunga mgahawa wake kwa kukosa wateja. Hivi anachohitaji Ashura ni kuboresha huduma au kupata wateja? sababu hapo mwanzo alikuwa mpaka anaishiwa chai na vitafunio kwa huduma hii hii wala hajaibadilisha!!!
Aliendelea Mzee Busara…., sifurahishwi na ninachokiona ingawa bidhaa zipo hakuna wanunuzi, nguvu kazi inapotea bure, kuna wasamaria wema huwa wanajitahidi kutoa kamsaada hapa na pale ila misaada hiyo haitatui tatizo, ni kama inawasaidia hawa masikini kuendelea kuwa masikini…
Kwahio mzee wangu hukubaliani na kazi nzuri wanazofanya hawa wahisani kusaidia watu?!! Niliuliza kwa hasira.
Unadhani hata kama ingewezekana, ingawa haiwezekani kuwapa watu wote hawa pesa ingesaidia? aliuliza Mzee Busara.
Naam, shida ya hawa wengi ni mitaji na… na….
Hata kama kungekuwa na uwezo wa kuwapa masikini wote pesa isingesaidia… kwa Maisha haya wanayoishi wengi wangecheza kamari ili kufikia ndoto zao ambazo hazifikiki au wengine wangetumia vilevi ili kujisahaulisha matatizo yao…, alisema Mzee Busara
Sikuelewi Mzee!!! nilimjibu kwa hasira.
Mtu pekee wa kumsaidia masikini ni masikini mwenyewe, na kwa masikini kumtegemea mwenye nacho ili amuondoe katika lindi la umasikini ni kama muwindwa kutegemea hisani ya muwindaji ili amsaidie kwenye maisha yake. Kwenye dunia ya leo ya ushindani ni vigumu kwa aliyenacho kumsaidia asiyenacho ili na yeye awe kama yeye…
Unamaanisha nini Mzee mbona kama unazungukazunguka?
Ni vigumu mwenye nyumba kumsaidia mpangaji ajenge nyumba yake, hata wachache wakifanya hivyo, ni kwa sababu wanajua wapangaji ni wengi, akitoka huyu kesho atakuja yule…, ila kwa mawazo hayo ni vigumu kutegemea mtu mwenye fikra hizo kusaidia kutokomeza umasikini sababu anaona ni jambo la kawaida na ni lazima kuishi nalo, yaani wasionacho lazima wawepo na wataendelea kuwepo.
Lakini mzee ni kweli, wote hatuwezi kuwa sawa, watu tunatofautiana… Wachache wakianzisha viwanda hata sisi huku chini tutafaidika na ajira, bidhaa na... na…
Kijana ulimwengu wa sasa wa mashine yaani sayansi na teknolojia hauhitaji nguvu kazi kama zamani, ili kiwanda kiweze kutoa bidhaa zenye ushindani katika soko lazima zipunguze gharama za uzalishaji na moja ya hizo gharama ni kutumia mashine na teknolojia na sio kuajiri watu wengi…
Kwahio ni kwamba hakuna cha kufanya, yaani tukate tamaa na kungojea kifo…, au kila mtu ajitahidi kutoka kivyake kwa kuwakanyaga na kuwakandamiza wengine? Nilijibu kwa dhihaka.
Hapana Kijana, Umasikini wowote kwa yoyote ni hatari kwa wote popote…, yaani wewe uliyenacho ukizungukwa na wasionacho muda wowote watakuja kuchukua kilicho chako.
Aliendelea mzee kuzungumza taratibu na kwa masikitiko…, ila nakubaliana na wewe, wote hatuwezi kuwa sawa, ingawa sidhani tunapoongelea usawa, tunaongelea kitu kimoja.
Mzee sikuelewi!!
Wakati wewe unaongelea utofauti wa matabaka (walionacho na wasionacho), utofauti niuonao mimi ni kwenye ujuzi na uwezo…. Hivyo basi kwangu mimi utofauti huo ndio unaofanya kikundi au jamii ya watu kuwa yenye nguvu na sio sababu ya kutengeneza matabaka.
Mzee Sikuelewi!!
Umesema wote hatuwezi kuwa sawa…, nadhani umesema hivi kwa sababu watu tuna uwezo tofauti, lakini mimi naona utofauti huo wa uwezo ni faida na sio mapungufu.
Mzee unazidi kunichanganya!!!
Kama mwili ulivyo na viungo mbalimbali ili uweze kufanya kazi au mkono ulivyo na vidole vyenye urefu na umbo tofauti ili tuweze kushika vitu vizuri…
Mzee kuna cha maana chochote unachotaka kumaanisha zaidi ya kunichanganya
Maana yangu ni kwamba tukiunda timu ya mpira yenye kina Pele 11, au Ronaldo au Maradona au Messi haiwezi kuwa timu bora, timu bora inahitaji golikipa, walinzi na watu wanaojituma sio wenye vipaji pekee…., hivyo basi hata kwenye jamii tuna watu tofauti wenye nguvu tofauti, wengine ni wabunifu, wengine wana maono na wengine wanaweza wakabadilisha nadharia kuwa uhalisia…, mmoja mmoja hatuwezi kufika popote ila kwa umoja wetu hakuna cha kutuzuia.
Na kama nilivyosema awali, kwavile hakuna wa kutusaidia au kukusaidia ni aidha tunaishi kwa umoja au tunakufa mmoja mmoja… hakuna mbadala…., alimalizia mzee huku machozi yakimlengalenga.
Mzee tunahitaji msaada ili kuondokana na hii hali nilisema kwa msisitizo huu sio muda wa kukata tamaa
Msaada kutoka kwa nani?
Serikali!!!
Ili ikufanyie nini? Aliuliza mzee kwa hasira…, tofauti kati ya walionacho na hawa ombaomba ni fursa ya kujipatia kipato cha uhakika…, watu wakiwa na kipato cha uhakika watamudu mahitaji yao yote bila kutegemea au kusubiri hisani ya Fulani wala serikali.
Sasa mzee naona tunazunguka… nilimjibu kwa hasira…, sasa si tukiwezeshwa tutafanya biashara na kupata hicho kipato…
Cha uhakika ? Aliuliza Mzee
Unasema?
Kwanza unawezeshwa vipi, na nani anawezeshwa na nani?, na kama ni mkopo una uhakika wa unachokifanya kwamba utalipa huo mkopo au ni kudumbukizana kwenye lindi la matatizo juu ya matatizo. Alisema mzee kwa hasira.
Wewe mpaka leo umeshakopa mikopo mingapi kutoka Saccos, Vicoba n.k. Aliendelea Busara…., unaweza ukasema labda ilikuwa ni mikopo ya kuumiza, ila hata ungepewa pesa bure kwa shughuli hizi za kubahatisha una uhakika huo mtaji hautakatika ? Hata kama wawili katika kumi wakifanikiwa…, kweli kwa marejesho hayo tunaweza kusema kama jamii tunafanikiwa. Hivi wewe na marafiki zako wote, hata wale wachache wenye bahati za ajira za uhakika baada ya kulipia kodi, elimu kwa watoto wao na chakula ni wangapi wanabaki na akiba au wengi wao ni kukopa mwezi kesho kulipia madeni ya mwezi huu… aliendelea kusema mzee kwa hasira.
Kwahio mzee ni nani wa kutukomboa naona kama vile unazidi kunikatisha tamaa…
Hakuna wa kuwakumboa sio wewe, serikali au mtu binafsi yoyote.
Unasema ?!!
Hakuna mtu mmoja mwenye uwezo wa kuwakomboa bali nyie masikini wenyewe ndio wa kujikomboa kwa kutumia nguvu ya wingi wenu…
Mzee sikuelewi nilisema kwa hasira!!!
Hivi wazalishaji ni kina nani? aliuliza Mzee
Viwanda, Matajiri, Wamiliki na Mataifa ya mbali nilijibu…
Ambao ni WATU alisema Mzee Busara kwa kusisitiza wazalishaji wote, wakulima wafanyakazi, wabunifu waliotengeneza hizo mashine… wote ni WATU…. Na watumiaji? aliendelea kuuliza
Ni Watu… nikajibu kwa kusita.
Naam wazalishaji ni Watu na Watumiaji ni watu, tena unaweza ukasema uzalishaji unaweza kufanyika kwa kutumia mashine, lakini mwisho wa siku ni watu ndio watumiaji, na ni watumiaji hao ambao wanafanya wazalishaji waendelee kuzalisha.
Mzee aliendelea…, Kwahio kijana utaona kwamba watu ndio mtaji mkubwa kuliko chochote kile katika jamii, na kwa watu kutokupata fursa ili kuchangia na kufikia tamati ya uwezo wao ni upotevu mkubwa wa rasilimali katika jamii husika.
Sasa mzee mbona sikuelewi unasema hakuna wa kutusaidia alafu unaongelea kwa watu kama sisi kukosa fursa ni hasara kubwa kwa jamii… sasa hizo fursa zinatoka wapi.
Mzee aliendelea kama vile hajanisikia…, kwahio kwa kuwawezesha watu yaani (wale wasio na makazi, wasio na ajira, watoto wa mtaani na masikini wa kutupwa) ili waingie katika kundi la wazalishaji na kupata kipato ili waweze kumudu mahitaji yao (yaani wanunuzi) itakuwa ni njia bora ya kubadilisha hiki ambacho tunakiona kama mzigo wa taifa na kuwa faida yenye mchango mkubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mzee aliendelea…, kama wanajamii watakuwa na ujuzi wa kufanya kazi zilizopo kwenye jamii zao na wakawa wazalishaji kipato wanachopata kitawasaidia kuishi na kujikimu katika jamii husika.
Lakini mzee si ndio maana kuna mashule, veta n.k. na serikali na watu binafsi wanahangaika kila siku kutengeneza ajira kwa kukaribisha wawekezaji.
Mzee aliniangalia kama vile nimechanganyikiwa…, unamaanisha shule ambazo zinahitaji kuwa na utajiri au kipato ili upate elimu bora au ajira ambazo unahitaji darubini kuziona? Mzee aliendelea…, wote tutakubaliana kwamba kinachofanyika sasa hakikidhi mahitaji.
Nini kifanyike mzee wangu…, nilimuuliza kwa dhihaka, sababu naona sasa unakuwa kama mwasiasa kuorodhesha matatizo ambayo wote tunayajua bila kuleta suluhisho lolote.
Kijana takupa hizi kurasa zangu…, akanionyesha kakitabu kachafu ambako amekuwa akiandika andika kwa muda mrefu, na kufuta futa…, inaonekana kama ilikuwa ni kazi yake ya muda mrefu na amekuwa akifikiria hili tatizo kwa muda sasa…, nikaanza kutabasamu kwamba huenda mzee anajua njia ya mkato ya haya matatizo yangu…. Mzee akakirudisha mfukoni kitabu chake na kuendelea… humu ndani nitakuelezea HATUA KUMI za kuchukua ambazo zitahakikisha huu umasikini unatoweka bila kumwacha mtu yoyote nyuma.
Aah!!! Tabasamu langu likayeyeka…, mzee naona sasa unaleta nadharia wakati tunachohitaji ni uhalisia…
Sikiliza kijana, na hizi hatua sio tu zitaufanya umasikini kuwa historia, bali hakutahitajika ruzuku au kodi kutoka kwa baadhi ya watu ili kufanikishwa. Ila kabla sijakupa kitabu changu kwanza naomba nikuonyeshe jinsi tunavyoishi Maisha yasiyo na Ufanisi.