Mbobo
JF-Expert Member
- Jan 13, 2017
- 1,392
- 1,818
Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Marylin.SEHEMU YA KUMI NA NNE
Kwa nini watu wanapenda kumuamini Martin Lundi muongo?
“Hapana Tigga...hayo yote yamo katika fikira zako tu mwanangu...ni kutokana na...”
“Paranoid Schizophrenia?” Nilimkatisha mama yangu kwa uchungu, kabla hajamalizia ile kauli yake, na kuendelea; ”Hivyo ndivyo Dokta Lundi alivyokueleza mama? Kuwa hayo mambo ni fikira zilizojengeka bila msingi kichwani mwangu kutokana na huo ugonjwa unaosemekana kuwa ninao?”
“Tigga mwanangu, usiifanye hii hali iwe ngumu kuliko inavyohitajika...”
Nilitoa sauti ya kukata tamaa na kutikisa kichwa kwa masikitiko makubwa.
“Mama! Hivi kuna historia ya wazimu katika familia yetu? Kuna mtu yeyote...babu au bibi fulani huko nyuma, aidha upande wako au wa baba ambaye alipata kuugua wazimu?” Nilimuuliza kwa jazba. Mama alibaki akinitazama tu huku akivisogeza sogeza vile vyombo bila uelekeo maalum. Lile swali lilionekana kuwa lilimchanganya kidogo na niliona wazi kuwa wazo hilo halijawahi kumpitia kichwani mwake hata kidogo.
“Ennh, mama, hebu nieleze hilo...sijawahi kusikia hata siku moja...au mlituficha?” Nilizidi kumsukumia maswali.
“Hakuna Tigga, lakini...”
“Unaona? Mi’ najua magonjwa kama hayo yana namna ya kurithishwa katika familia, au nakosea?”
Mama hakunijibu. Niliona alikuwa amechanganyikiwa na nilimwonea huruma sana.
Nilihisi chuki ya hali ya juu kwa yule mjinga anayejiita Dokta Lundi kwa kutufikisha katika hatua hii mimi na mama yangu. Lakini kwa nini mama asiuone uongo huu? Mimi ni mwanae for God’s sake!
Nilimsogelea na kumuambia kwa kuomboleza: “Mama. Naomba uniamini mimi mwanao. Dokta Lundi ni muongo tena muongo mkubwa sana! Na wala sidhani kama ni dokta kweli yule. Anachofanya ni kupita akinipakazia uzushi wa ugonjwa huo wa uongo ili kuninyima nafasi ya kusikilizwa na kuaminika mahala popote nitakapokwenda. Na hiyo ni kutokana na mambo niliyoyaona kule msituni na ambayo nina ushahidi usiopingika...ushahidi ambao utamuathiri sana huyo Dokta Lundi na wenzake!”
Niliona kabisa kuwa hali ile ilikuwa ikimchanganya vibaya sana mama yangu, na nilizidi kumuonea huruma lakini ilibidi nimueleweshe.
“Mama, mi’ n’na ushahidi wa kuthibitisha kuwa Dokta Lundi si mtu mwema kama anavyotaka wewe umuone...”
“Amenionesha picha za kule msituni Tigga...watu wameuawa Tigga! Kama kuku...!Inatisha sana!” Alisema kwa sauti ya chini huku akilengwa na machozi.
“Na akakuambia kuwa ni mimi ndiye niliyewaua wale watu?” Nilimuuliza mama kwa uchungu. Hakunijibu, lakini katika macho yake niliona kuwa nilikuwa nimeuliza jibu. Iliniuma sana.
“Mama! How can you believe such rubbish?” Nilibwata huku nikitupa mikono yangu hewani,nikimuuliza ni vipi anaweza kuamini upuuzi kama ule, kisha nikaendelea kwa sauti ya chini huku nikisisitiza kauli yangu kwa mikono yangu.
“Mama...ni yeye pamoja na wenzake watatu ndio waliofanya yale mauaji kule msituni! Na hakuna mtu yeyote anayejua hilo isipokuwa mimi. Huoni kuwa anafanya kusudi kunipakazia ugonjwa huo ili taarifa nitakazotoa dhidi yake na wenzake zitiliwe mashaka na kila mtu? Si unaona jinsi wewe mwenyewe unavyoshindwa kuniamini? Hivi ndivyo anavyotaka, na ndivyo inavyokuwa kila mahali niendapo mama!How can you believe him mama?” Nilimueleza kwa hisia kali huku nikihoji uhalali wa mama yangu kuamini uongo wa Martin Lundi kirahisi namna ile.Na hata pale nilipokuwa nikiongea maneno yale, nilijihisi uchovu na usingizi mzito. Nilipiga mwayo mrefu na kujibwaga tena kwenye kiti. Mama alinisogelea na kunipapasa kichwani.
“Pole sana Tigga. Unaonekana una usingizi, kwa nini usijipumzishe kidogo halafu tutaongelea hili jambo baadaye?” Aliniambia kwa upole. Na hii ndio tabia ya mama yangu ambayo toka utotoni mwangu nilikuwa siipendi. Akiwa na jambo lake basi yuko radhi mliahirishe kwa muda kuliko kukubaliana na wazo jingine, akitumaini kuwa baada ya muda utakuwa umeelewa “ujinga” wako na kukubaliana na mawazo yake.
Sasa mimi sina muda wa kupoteza namna hiyo mama!
Nilimtazama mama yangu kwa kukata tamaa, na mwayo mwingine ukanitoka. Sikuwa nimepata usingizi wa kutosha usiku uliopita. Lakini huu sio wakati kulala!Dokta Lundi akitokea...
“Tafadhali usimruhusu Dokta Lundi anikamate mama...please!” Nilimwambia kwa sauti ya chini huku nikihisi macho yakiniwia mazito kuliko kawaida.
“Mi’ nakutakia yaliyo mema kwako mwanangu, na si vinginevyo.” Mama alijibu, lakini kauli ile haikunipa amani hata kidogo.Nilijilazimisha kuinuka na kwenda kujilaza kwenye kochi refu lililokuwa pale sebuleni huku nikiwa nimeukumbatia mkoba wangu. Mama alinishauri nikalale chumbani, lakini sikukubali, nilimwambia kuwa nataka kujipumzisha kwa dakika chache tu.
Nadhani nilisinzia kwa dakika chache sana, kisha nikahisi nikipambana na usingizi ule mzito, nikijitahidi usinielemee.
Lazima niamke! Lazima niamke!
Wazo hilo lilikuwa likinijia tena na tena ilhali usingizi ukizidi kunielemea.Kwa mbali nilisikia sauti ya mama yangu ikinisemesha. Niliinuka ghafla na kutazama kila upande, lakini nilikuwa peke yangu pale sebuleni. Ilikuwa ndoto? Hapana, nilisikia sauti ya mama ikitokea sehemu ndani ya nyumba ile. Alikuwa akiongea na nani? Aliniambia kuwa Koku alikuwa ameshaenda kazini, sasa huyo anayeongea naye ni nani? Niliinuka taratibu na kuelekea kule niliposikia sauti yake ikitokea.
Nilimkuta akiwa katika chumba cha kulia chakula. Alikuwa amekaa kwenye kiti akiwa amenigeuzia mgongo na alikuwa anaongea na simu, na alikuwa akimbembeleza kitu fulani huyo aliyekuwa akiongea naye. Nilisimama kando ya mlango wa kuingilia kule alipokuwepo na kujaribu kusikiliza maongezi yale huku moyo ukinienda mbio.
“...nataka nijue ni wapi hayo matibabu yatakapofanyika na mimi nataka niwepo...”
Usingizi ulinikauka mara moja, nikazidi kusikiliza.
“...yeye yupo hapa, lakini lazima na mimi niwepo...”
Moyo ulinilipuka na kuongeza mapigo.
Mama alikuwa anaongea na Dokta Martin Lundi!
Nilichanganyikiwa.
Haraka nilirudi kule sebuleni na kulinyakua lile begi langu dogo. Nilitembea haraka kuelekea mlango wa nyuma wa nyumba ile, na nilipopita tena kwenye ule mlango wa kuingia chumba cha kulia chakula, mama alikuwa ameshamaliza kuongea na simu.
“U...unaenda wapi Tigga...usingizi umeisha mara hii?” Aliniuliza huku akinisogelea. Moyo uliniuma kuliko kawaida. Sikuweza kumtazama.
“Na...naenda kulala chumbani...” Nilimjibu bila kumtazama na bila kupunguza mwendo wangu. Mwisho wa korido kabla ya kuufikia mlango wa nyuma wa nyumba ile kulikuwa kuna chumba cha wageni. Nilipokifikia nilisimama nje ya mlango wa chumba kile na kumgeukia mama yangu. Alikuwa amesimama akinitazama.
“Ennh...naomba uniamshe ifikapo saa saba...” Nilimwambia kwa sauti ya chini huku nikifungua mlango wa kile chumba.
“Sawa mama...” Alinijibu, kisha akanisogelea kwa hatua za haraka, nami nikamsubiri huku nikitazama sakafuni. Alinikumbatia kidogo na kunibusu kwenye paji la uso.
“Lala unono mwanangu...yote yatakwisha tu, muamini mama yako.”
Sikujua nimjibu nini, lakini machozi yalinitiririka nami nikageuza uso wangu ili asione jinsi nilivyoumia.Niliingia ndani ya kile chumba na kusimama nyuma ya mlango kwa ndani nikisikilizia mienendo ya kule nje huku moyo ukinipiga sana. Hakuna kilichotokea, kisha nikasikia maji yakimwagika jikoni na vyombo vikigongana. Nikahisi mama alikuwa akiosha vyombo jikoni.
No time to waste!
Nilitoka nje ya chumba kile taratibu na kufungua mlango wa kutokea nyuma ya nyumba ile taratibu mno. Nilitoka nyuma ya nyumba yetu na kuruka michongoma iliyofanya uzio wa kuizunguka nyumba ile na kutokea mtaa wa pili.
Huku nikitiririkwa na machozi, nilitembea kwa mwendo wa kasi kuelekea nisiKokujua.
Nilikimbilia kwa Kelvin, nikakutana na usaliti nisioutegemea na roho iliniuma sana. Lakini hili la kukuta usaliti kama ule kwa mama yangu liliniuma zaidi. Sasa nitakimbilia wapi? Kwa nini hawa akina Martin Lundi wanakuwa na uwezo wa kuwarubuni watu mpaka wanafikia hatua ya kunigeuka namna hii?
Au inawezekana ikawa ni kweli mimi nina huo ugonjwa ninaosemekana kuwa ninao na mambo yote ninayoamini kuwa nimeyaona ni fikara zangu tu zenye maradhi?
Lakini nilipopapasa begi langu na kuigusa ile kamera ya marehemu Gil, nilipata hakika kuwa niliyoyaona yalikuwa ni kweli tupu.
Sasa ni nini hii?
Hata mama yangu! Oh, My God!
Ama kwa hakika sasa nilikuwa peke yangu, nisiye na kimbilio.
Ili iweje sasa?
Nilijua kuwa mama alifanya vile akiwa na imani,kuwa ananisaidia, kwamba anafanya kwa faida yangu.
Lakini sivyo mama! Martin Lundi ni muongo na muuaji! Nitawezaje kusema hadi niaminike?
Nilikuwa nikiwaza mambo hayo na mengi mengine huku nikipotelea mitaa ya nyuma kutoka ule uliokuwamo nyumba yetu. Sikuwa na uelekeo maalum, na kwa wakati ule sikujali. Jambo pekee nililojali kwa wakati ule ni kujiweka mbali na mikono ya yule mtu mbaya anayejiita Martin Lundi, na kundi lake.
Bila ya kujua nilikuwa nimezunguka na kufuata mtaa uliotokea mwanzoni mwa ule mtaa ambao nyumba yetu ilikuwepo. Nikiwa nimesimama mwanzoni mwa mtaa ule, niligeuka kutazama upande ilipokuwepo nyumba yetu ambapo ni katikati ya ule mtaa. Nilishuhudia kwa kihoro magari matatu yakisimama kwa kasi na vishindo nje ya nyumba yetu na watu wakiremka na kukimbilia nyumbani kwetu, huku wengine wakiizingira nyumba ile kwa nje. Nilidhani nilimuona Dokta Lundi miongoni mwao. Lakini kwa umbali ule sikuweza kuwa na uhakika. Niliogeza hatua na kupotea eneo lile nikimwomba Mwenyezi Mungu amsaidie mama yangu.
iv.
S
iwezi kuelezea jinsi nilivyoumizwa na kitendo cha mama yangu kuamua kumuamini yule shetani anayejiita Martin Lundi na kupuuzia kabisa utetezi wangu. Kwa kweli hakuna maneno ambayo ninaweza kuyatumia hata yakatosha kuonesha ni kiasi gani jambo lile lilikuwa limeniumiza, kwani ilikuwa ni kupita kiasi. Ni kweli kuwa pale nilipogundua kuwa Kelvin aliamua kunisaliti kwa yule shetani Martin Lundi hata nilipompa maelezo yangu, niliumia hata nikahisi kama kuna ndoana iliyokuwa ikiuvuta moyo wangu kwa nguvu kubwa; lakini kuumia nilikoumia kutokana na hali iliyotokea pale kwa mama yangu, kulikuwa ni zaidi ya hivyo.
Lakini sikuwa na la kufanya, lililotokea lilikuwa limetokea, na aliyelifanya ni mama yangu.
Angalau kwa Kelvin niliweza kuamua kuvunja uchumba na kuachana naye, lakini huyu alikuwa mama yangu! Mama aliyenizaa kwa uchungu mwingi. Sasa vije mtu kama Dokta Lundi akaweza kumrubuni, kumlaghai na kumshawishi hata akaweza kumuamini yeye na akashindwa kuamini maelezo ya mwanae mwenyewe ambaye alipata uchungu usio mfano wakati akimzaa?
Nilishindwa kuelewa, na nilizidi kuchanganyikiwa iliponibainikia kuwa hata ningefanya nini, nisingeweza kumfuta asiwe mama yangu kama jinsi nilivyoweza kumfuta Kelvin kutoka katika maisha yangu (sijui naye yu hali gani huko aliko). Hivyo nilimwomba Mwenyezi Mungu amnusuru mama yangu na ghadhabu za Dokta Lundi baada ya kufika pale nyumbani na kukuta kuwa nimewatoroka kwa mara nyingine tena, wakati yeye aliwapigia simu na kuwahakikishia kuwa nilikuwepo pale nyumbani.
Baada ya kuwashuhudia kwa mbali akina Martin Lundi wakiizingira nyumba yetu, nilielekea moja kwa moja kituo cha basi na kupanda basi nililolikuta likipakia abiria pale kituoni bila ya kujali lilikuwa likielekea wapi, lengo likiwa ni kupotea kabisa eneo lile. Na njia nzima wakati basi lile likifanya safari yake ambayo nilikuja kuelewa baadaye kuwa lilikuwa likielekea posta, nilikuwa ni mtu niliyepigwa bumbuwazi. Woga ulinitawala kupita kiasi kwani sasa ilikuwa imenifunukia wazi wazi kichwani mwangu kuwa katika janga hili nilikuwa peke yangu.
Nilikwangua akili yangu nikijaribu kutafuta ni hatua ipi ifuate lakini niliambulia ukungu tu. Nilifikiria kumfuata dada yangu Koku kazini kwake, lakini nililifuta wazo hilo haraka, kwani nilijua kuwa asingeweza kunisaidia lolote katika mazingira yale. Nilijua iwapo mama ameamua kuchukua msimamo aliouchukua katika swala langu, hakuna shaka kabisa kuwa na yeye atakuwa na mtazamo ule ule.
Nilidhani kuwa Koku angeweza kusaidia kwa kumbana Dokta Lundi kwa maswali ya kitaalamu juu ya ule ugonjwa anaonipakazia na hatimye kubainisha uongo wake, lakini kama angefanya hivyo, basi hata mama angekuwa na mtazamo tofauti. Lakini pia nilikumbuka kuwa, dada yangu alikuwa ni nesi wa kawaida tu.Yumkini akawa hana uwezo na utaalamu wa kuuelewa ugonjwa ule kama jinsi alivyouelewa Dokta Martin Lundi muongo.
Sasa nifanye nini...?
Niliamua kwenda ofisini kwangu, katika jumba la Makumbusho ya Taifa. Huenda huko nikapata baadhi ya majibu ya maswali yangu. Kwani si huko ndipo iliposemekana kuwa ile barua ya uongo iliyopelekwa kwa mkuu wa wilaya ilikuwa imetokea? Sasa niliona kuwa iwapo nilikuwa nashutumiwa kwa mambo yasiyo na msingi, basi ni wajibu juu yangu kutafuta kiini cha shutuma hizo. Shutuma za kuwa nilikuwa mgonjwa wa akili zilikuwa ni nzito na mbaya sana. Nilijua kuwa ile barua ilikuwa imeghushiwa, na hata kule ofisini haijulikani kuwa kulikuwa kuna barua kama ile. Lakini sikuwa na namna ya kujithibishia hilo isipokuwa kwenda ofisini. Aidha nilijua kuwa kwa vyovyote iliniwajibikia kuripoti pale ofisini baada ya kutoka kwenye ile safari iliyozaa balaa niliyotumwa na ofisi. Sikujua ningekutana na nini huko nilipoazimia kwenda, lakini sikuona njia nyingine ya kuanza kutafuta ukweli wa mambo yale ya uongo niliyopakaziwa zaidi ya ile.
Niliingia ndani ya jengo la ofisi yetu na kuelekea moja kwa moja ofisini kwa afisa utumishi, ambaye ndiye muangalizi wa maswala yote ya wafanyakazi na ajira zao, lakini kabla sijaifikia ofisi yake niliwahiwa kwenye korido na baadhi ya wafanyakazi wenzangu ambao walinizingira kwa maswali kemkem kuhusu matukio ya huko msituni. Wapo walionipa pole, wapo walioulizia ilikuwaje hadi wenzangu wakaangamia kule porini, wengine walikuwa wakiniambia kuwa kwa kujipeleka pale ofisini nilikuwa nimejitia kwenye mtego na kunishauri niondoke haraka, huku wengine wakionesha wazi kuwa walikuwa wakiniogopa. Sikuweza kujibu swali hata moja, kwani yalikuwa yakija bila mpangilio maaluim, nami nilianza kuingiwa na woga na kujuta kwa nini niliamua kwenda pale ofisini. Niligundua kuwa habari zangu zilikuwa zimefika pale ofisini, na kwamba kwa ujumla ilieleweka kuwa Tigga si mtu salama tena kuwa karibu naye. Hili nililibaini kutokana na hali iliyojitokeza pindi nilipoingia pale ofisini, kwani wenzangu walikuwa wakiniuliza maswali yale na kunipa pole huku wakinitazama kwa wasiwasi, na muda wote walikuwa kikundi, hakuna hata mtu mmoja aliyekuwa tayari kukaa na mimi peke yake. Nikiwa nimezingirwa na wale wafayakazi wenzangu pale kwenye korido, nilimuona Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho akitoka ofisini kwake, iliyokuwa kwenye ghorofa ya kwanza, na kuchungulia pale chini nilipokuwa nimezongwa na wafanyakazi wenzangu. Tulitazamana kwa muda, kisha alirudi ofisini kwake na kufunga mlango.
Hatimaye nilifanikiwa kujichomoa kutoka kwenye lile kundi la wafanyakazi wenzangu na kuingia ofisini kwa afisa utumishi.
ITAENDELEA