RIWAYA: MWANAMKE KAMA MAMA YANGU
MTUNZI: KELVIN KAGAMBO
SEHEMU YA KUMI NA MOJA (11)
#Tembelea
http://riwayatakatifu.weebly.com kwa Riwaya zaidi.
ILIPOISHIA…
Zilikuwa ni meseji fulani ambazo zilinifungua mara nilipozisoma.
Moja ilisomeka. "Ashura wenzio hali yangu mbaya laazizi hebu naomba urudishe moyo wako nyuma ili nikomboke katika dhahama na mateso haya nipatayo"
Nyingine ilsomeka “naomba pokea simu yangu mahabuba" na ya tatu ilisomeka"Nidharau lakini kuna siku utahitaji huduma yangu"
ENDELEAAAA….
Ni nani huyo? Ndiyo lilikuwa swali langu la msingi mara baada ya kumaliza kusoma jumbe zote hizo lakini hapo tayari nilishapata picha ya kila kitu kilichojificha.
Kupitia meseji hizo niligundua kwamba kumbe wakati mke wangu ananifanyia vituko vile alikuwa na kijaamaa kilichokuwa kikimzuzua lakini sasa ameachana nacho na kurudi katika mstari nyoofu wa ndoa.
Lakini swali la msingi lililosalia ni kufahamu nani huyo jamaa mwenye kujigamba kwamba kuna siku Mke wangu atahitaji huduma yake.
Nikachukua simu ya Mke wangu na kumpigia, simu yake ikaita kidogo tu na kupokelewa.
"Haloo" nikazungumza na pengine hilo lilikuwa ni kosa kwani jamaa huyo alikata simu punde tu aliposikia sauti yangu. Bila shaka alichukua uamuzi huo baada ya kung'amua kwamba mwenye mali nimegundua hila zake.
Nilimpigia tena na tena lakini hakupokea na sasa nikaamua kubadili uamuzi na kumpigia kwa kutumia simu yangu.
Nikainakiri namba ile kutoka kwenye simu ya Mke wangu na kumpigia lakini sikuamini kile ninachokiona mara baada ya kupiga namba ile.
Unajua simu yangu ina tabia fulani, kama unaandika namba kama hivyo nilivyofanya na kuipiga hujiandika jina kama tayari namba hiyo iko kwenye "phonebook".
Namba hiyo pia ilikuwa kwenye phonebook ya simu yangu na nilipoipiga tu ilijiandika jina la Maige; hiyo ikiwa na maana ya kwamba namba ile ilikuwa ya Maige.
Unajua sikutaka kuamini kirahisi kama hivyo unavyoamini wewe, nilichukua simu ya Mke wangu na kutazama kama namba niliyoiandika ilikuwa ndiyo ile iliyotuma meseji.
Nilikuwa sawia, wala sikukosea kuinakiri namba ile.
Sasa nikaamua kupiga moja kwa moja ili nimueleze kuwa nimekwishafahamu kila kitu.
"The number you are calling is not reachable, please try againi later" (Namba ya simu unayoipigia haipatikani kwasasa, tafadhali jaribu tena baadae) nilijibiwa hivyo na sauti ya mtandao iliyorekodiwa maalum kwa kutoa taarifa pindi simu ya unayempigia inapokuwa haipo hewani.
Jibu la haraka lililokuja kichwani mwangu ilikuwa ni Maige kanizimia simu baada ya kugundua kuwa ni mimi ndiye niliyempigia. Bila shaka hata hofu ilimtawala huko alipokuwa.
Nikatuliza jazba na hasira zangu ili nisitende bila hekima, halafu nikamtoa Mke wangu katika sekeseke hilo nikiamini si yeye mwenye makosa kwani yawezekana alikwishaachana na Maige muda mrefu ndiyo maana Maige akatuma meseji za aina hiyo, zenye kumbembeleza waelendeze wizi wao.
Lakini kweli Maige anastahiki kunifanyia hivi? Mtu ambaye nilimuamini na kumchukulia kama ndugu yangu, rafiki yangu wa kufa na kuzikama lakini ni kinyume.
Kumbe ni ADUI NYUMA YANGU, anayejikinga jua kwa kivuli changu. Hakika Wahenga ni watu wenye hekima na hunena kwa busara sana, nimesadiki hilo waliposema 'Kikulacho kinguoni mwako' na ndiyo hiki ninakiishi mimi.
"Hata kama hapokei simu yangu, kesho nitakutana nae kazini na huko ndipo mambo yatanoga zaidi kwani nitazungumza nae ana kwa ana na hakika sitaacha jambo hili liende hivi hivi" niliahidi.
Ili kuweka uthibitisho niliamua kubadilisha kadi ya simu (Line/Sim Card) ya Mke wangu na kuiweka kwenye simu yangu halafu 'Line' yangu nikaiweka kwenye simu yake.
Nilifanya hivyo ili zile meseji siendelee kubaki kwenye simu kwani endapo Ashura angeziona angezifutilia mbali.
Alirejea baadae nyumbani na wala hakuwa na hofu wa haraka ya kutaka kujua chochote kuhusu simu yake na hiyo ilitosha kuwa dalili ya kwamba hivi sasa ni mwanamke msafi.
"Khadija amekusumbua?" hilo ndilo lilikuwa swali lake la kwanza kuniuliza. Alishughulika na mtoto kwanza kabla na nusu saa baadae ndiyo akaulizia kuhusu simu yake.
"Baba Khadija, mbona hii simu haina majina yangu" aliniuliza hapo akimaanisha 'contacts' alizozikuta kwenye simu hiyo hazikuwa zile alizozihifadhi yeye.
"Nimebadilisha line, yako ipo kwenye simu yangu" nilimueleza na wala sikuona kama alichukia suala hilo.
Akachukua simu yangu na kumpigia Mama yake.
Hakujua kilichotokea kwani hakufanikiwa kuziona meseji zile za kishetani zilizotumwa na Maige.
********************
Usingizi haukuja usiku kana kwamba nimefunga ndoa na Kukesha. Hata jua nililihisi limechelewa kutoka, yaani kwa kifupi usiku wa siku hiyo ulikuwa ni mrefu kweli kweli.
Majogoo yaliwika na kumpa ruhusa ya Mke wangu kuniamsha. Niliamka na kuelekea bafuni ambapo tayari mke wangu alikwishniandalia maji na mswaki.
Nilijisafi huku mawazo na hasira juu ya IBILISI Maige zikinitawala. Nilipomaliza kuoga nilipatiwa chai na Mke wangu na baada ya kunywa nilianza safari ya kuelekea kazini.
Njia nzima mawazo yalikuwa ni Maige na huwezi amini hiyo ilinisababishia nione safari ndefu ingawa siku hiyo hakukuwa hata na foleni kama ilivyokawaida ya Dar es Salaam.
Nilifika kazini na nilipoingia ofisini tu jicho langu liliangaza pahala ambapo Maige huwa anakaa. Sikumuona.
"Maige amefika?" nilimuuliza mfanyakazi mwenzetu niliyemkuta.
"Ndiyo amefika muda mrefu tu" nikajibiwa.
"Yuko wapi?"
"Sifahamu ila yupo" akanambia.
Basi nikatulia kwenye sehemu ya kazi na kuanza kazi ndogondogo huku nikiwa sina 'mood' ya kufanya kazi hata kidogo.
Punde akaingia Maige na alipofungua mlango tu macho yangu yalivaana naye. Nilitamani niwe chui mkali wa mbugani Serengeti, nimrukie, nimjeruhi kwa kumkwaruza kwa makucha hadi kufa.
Lakini hiyo isingewezekana, mimi ni binadamu tu, tena niishie kwenye jamii yenye kufuata sheria ina maana kuua kungesababisha nipandishwe kizimbani na kugongwa nyundo kadhaa jela.
"Kaka, kaka, nina majanga kweli kweli" akasema akiwa mbali kabla hapa hajafika nilipokuwa mimi na hiyo ilinifanya niwe makini kusikiliza hayo majanga anayoyazungumzia.
"Niulize majanga gani basi" akanambia.
"Majanga gani?" nikamuuliza.
"Jana nimepigwa ngeta aisee, bonge la kabali mbao mitaa ya Mwananyamala hadi nikaona mtoa roho huyu hapa" akanambia.
"Duuuh!" nikashituka kinafki. "Ikawaje sasa?"
"Wamenikomba kila nilichokuwa nacho braza, pochi yangu ilikuwa na laki moja na elfu kumi na simu pia" akanambia na kunifanya nipagawe kwani mpango wangu wa kumueleza ukweli juu ya kile nilichokiona kwenye simu ya Mke wangu ungekosa nguvu.
"Hadi simu!?" nikamuuliza.
"Hadi simu, yaani wamenirudisha nyuma sana na ni heri wangechukua pesa wakanachia simu yangu" akanambia.
Nikaishiwa 'pozi', unadhani ningeanzia wapi kumshutumu. Bila shaka ingekuwa ni rahisi sana kwake kukwepa shutuma zangu.
Angenambia tu kwamba pengine meseji hizo zilitumwa na mtu aliyemuibia simu.
Na unajua ni ngumu sana kumshuku mtu wako wa karibu kwenye kesi kama hizo. Kama si kweli basi atahisi humuamini na hiyo inaweza ikahatarisha hata urafiki wenu.
Nikatulia na kujaribu kukumbuka Maige ni mtu wa aina gani katika maisha yangu.
Nikakumbuka jinsi alivyowahi kunieleza kwamba kuna siri kati ya Mke wangu na Mama yake, kipindi kile ambacho Mke wangu alijifungua.
Hilo jumlisha na mengine mengi yalimtafsiri Maige kama mtu wa muhimu sana kwenye maisha yangu, rafiki wa karibu mwenye msaada hasa nyakati za shida na matatizo.
Lakini bado nilikuwa na shaka naye, si unakumbuka kuna siku simu yake iliingia meseji kutoka kwa mtu ikimueleza kwamba anawashwa na anahitaji kukunwa, na ndiyo siku hiyo ambayo nilirejea nyumbani na kukuta Mke wangu amekwenda kusipojulikana tena kwa kumuacha mtoto.
Mawazo hayo yakasababisha ukinzani katika mtazamo wangu juu ya Maige. Nikashindwa nimuweke upande gani. Hasi ama chanya, moto ama baridi au hata wa kusuka ama kunyoa.
Nilichanganyikiwa.
Nikatuliza akili na kuona itakuwa hekima zaidi kama nitafanya uchunguzi wa kimya kimya kabla ya kumuibukia na tuhuma za uhakika zenye ushahidi wa kujitosheleza.
Sikumuonesha hata zile meseji, nilitaka mpaka nitakapohakikisha kwamba ni yeye aliyetuma ama ni huyo aliyemuibia kwa kumpiga kabali mbao.
"Pole sana" ndiyo lilikuwa neno langu la kwanza kumwambia.
"Nishapoa, vipi umekunywa chai" akaniuliza swali la kawaida kutoka kwake.
"Hapana" nikamjibu.
"Kuna chapati hapa, unaweza kuzitumia" akanambia na kazi ikaendelea.
Nilifanya kazi lakini si kwa ari kama ili kawaida yangu, na kuhusu zile chapati sikuzigusa, niliogopa nikiamini angeweza kuniwekea hata sumu.
Sikuwa na mazungumzo naye na hata yeye aligundua kuna tofauti, akaniuliza lakini sikumueleza ukweli.
Mda wa 'lunch' tuliongozana nikiwa katika hali ile ile ingawa yeye alijitahidi kunipigisha stori.
*****************
Nilirejea nyumbani nikiwa na mbinu mpya ambayo ningeitumia kung'amua ukweli. Mbinu hiyo nilipata njiani nilipokuwa nikifikiria jinsi gani nitafanya ili kupata ukweli.
Niliwaza kumuuliza Mke wangu moja kwa moja bila kuzunguka wala kujiumauma na muitikio wake ndio ungenijuza kwamba ni kweli alikuwa na mahusiano na Maige au laa.
Nilifika nyumbani na kumkuta mke wangu anaanda chakula cha jioni.
Nilioga kwanza na kisha nikajumuika mezani na tukapata msosi wa pamoja na mtoto wetu Khadija, tulipomaliza ikawa ni muda wa kulala na ni muda huo ndio niliopanga kuutumia kuzungumza na Mke wangu.
"Kwanini uliamua kutembea na Maige?" nilimuuliza hivyo mara tu tulipozima taa na kupanda kitandani.
Akashituka na nikawa nasubiri jibu lake ili nijue ni kweli alifanya hivyo ama si kweli.
"Lakini Jamal Mume wangu, hayo si yalishapita" akanijibu na hilo likawa jibu tosha la kuthibitisha kwamba Ashura alitembea na Maige.
"Yamepita, mbona bado anakutumia meseji?" nikamwambia.
"Meseji gani?"
"Hivi unadhani kwanini nimebadilisha line yako na kuiweka kwenye simu yangu?" nikampa taarifa kwa mtindo wa swali.
"Nisamehe Mume wangu, lakini mimi tayari nimekwishaachana naye ila ni yeye ambayo bado anaendeleza usumbufu"
"Nilikuwa siyafahamu yote hayo lakini sasa ndio nimepata kujua laana ulizo nazo mwanamke wewe, unawezaje kutembea na rafiki yangu na nawezaje kukusamehe" nikamwambia.
Kweli sikuwa nikifahamu lakini kwasababu nimefahamu sidhani kama naweza kumsamehe.
Je, ungelikuwa ni wewe ungelisamehe?
Eti Mke wako atembee na rafiki yako wa karibu kabisa halafu umsamehe, unaweza?.
Binafsi siwezi kumsamehe wala kusahau labda tu kuvumilia kuendelea kuishi naye kwasababu tayari tuna mtoto, tena mdogo ambaye hajatimiza hata mwaka.
Nililala nikiwa nimevimba kwa hasira na uchungu, sikutegemea kwamba Maige na Mke wangu wangekuwa wabaya kwangu namna ile.
Sasa nilipanga kesho kumuamkia Maige na kumchana 'live', tena si kumchana tu bali kulifikisha mbali suala hilo, hata kwa mabosi kama itawezekana.
Nilidamka asubuhi na mapema na kuondoka kuelekea kazini bila hata kumuaga Mke wangu na hiyo ilikuwa ni kwasababu ya hasira. Sikutaka hata kumuona na ingewezekana ningemcharaza talaka tatu na nikabaki mwenyewe ila kilichokuwa kikinizuia kufanya hivyo ni mtoto wangu alikuwa mdogo sana.
Nilifika ofisini lakini 'mbaya' wangu bado hakuwa amewasili, hata hamu ya kufanya kazi sikuwa nayo, nilikaa kishari na laiti kama ningelikuwa na bastola ningelimuua Maige ili nikanyee debe Segerea, Keko au hata Ukonga.
"Jamal, unaitwa na Bosi ofisini kwake" mara nikasikia nikiambiwa hivyo, halikuwa jambo la kawaida na hiyo ikasababisha niogope kidogo.
"Kuna nini tena?" nikamuuliza aliyenipa taarifa huku nikadhani labda niliboronga kazi ya jana kutokana na kuifanya nikiwa na hasira na kisirani.
"Acha maswali ya mtani jembe wewe, nenda kamuulize anayekuita" akanijibu jamaa huyo huku akiendeleza na kazi zake.
Nikanyanyuka toka kwenye kiti changu, nikazunguka meza yangu ambayo ilikuwa na kompyuta pamoja na makaratasi kadhaa. Nikatembea kuelekea ofisi kwa Bosi na nilipobisha hodi akaniruhusu nipite.
**************************
KWANINI BOSI ANANIITA? USIKOSE SEHEMU YA KUMI NA MBILI KUPATA JIBU LA SWALI HILO.
KUPATA RIWAYA HII NA NYINGINE NYINGI UNAWEZA WASILIANA NA NDUGU MWANDISHI KWA NAMBA TAJWA HAPO JUU.