Habari wanajukwaa, kuna softcopy kadhaa nnazo za hadithi tofauti nkaona si vibaya ku-share ikizingatia watunzi wake wameziweka public hivyo kutohesabika kama wizi wa kazi za watu au kuharibu mapato.. Kila siku nitaweka sehemu moja, watakuwepo ambao wameshazisoma lakini pia kutakua na wengi ambao hawajahi kuzisoma,
MWANDISHI: BEKA MFAUME
SEHEMU YA KWANZA
JUDI alimalizia kujifunga mkufu shingoni baada ya kukamilisha kujikwatua kwa vipodozi tofauti vya gharama huku akiwa amevaa vazi lililompendeza mwilini. Alikuwa ameamkia nyumbani kwa Richard ambako alikuja usiku uliopita na kulala hadi asubuhi hiyo. Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kumaliza kuoga na alikuwa akimsubiri Richardamalize kuoga kisha watoke pamoja kwenye gari la Richard. Kituo chao cha kwanza kingekuwa kwenye mgahawa wa Monde uliopo katikati yajiji kwa ajili ya kifungua kinywa, kisha baada ya hapo, Richard angempeleka kazini kwake.
Akiwa amekaa kitandani baada ya kutoka kujiangalia kwenye kioo kilichopo kwenye kabati la kuvalia, Judi alianza kujiuliza kama ulikuwa ni wakati mwafaka wa kumuuliza Richard kuhusu matumaini yake ya kuolewa naye. Walikuwa ndani ya uhusiano wa mapenzi kwa muda mrefu na alikuwa akijisikia fahari mbele ya wanawake wenzake kuwa na uhusiano huo na Richard ambaye ni mtoto wa mfanyabiashara tajiri na maarufu jijini Dar es Salaam. Pamoja nakuwepo na uhusiano huo wa muda mrefu, lakini haikuwahi kutokea hatasiku moja kujikuta wakizungumzia suala la kuoana. Haikuwa ni marayake ya kwanza kulala nyumbani kwa Richard.
Alishakuwa mwenyeji wanyumba hiyo tokea uhusiano wao ulivyoanza na kumfikisha hadi sikuhiyo. Mara nyingi, husan siku za mwishoni mwa wiki kuanzia Ijumaahadi Jumatatu alikuwa na mazoea ya kuhamia nyumbani kwa Richard nakuumiliki umama wa mwenye nyumba kuanzia usafi hadi mapishi namengineyo, kiasi kwamba hata nguo zake zikawa zimegawanyika sehemumbili; baadhi zikiwa nyumbani kwao ambako aliishi na wazazi wake nanyingine zikiwa nyumbani kwa Richard.
Uhusiano wao ulifahamikahadi kwa wazazi wao na kila mmoja alikuwa amejenga uhusiano mzuri kwaupande wa wazazi wa mwenzake. Richard alikuwa na uwezo wa kwendanyumbani kwa akina Judi na kuomba kuondoka naye kwa muda wowote. Halikadhalika, Judi aliweza kwenda nyumbani kwa Richard kwa muda wowotealioamua. Ingawa wote walikuwa huru kuyafanya mambo hayo, lakiniwalikuwa wakitofautiana kimawazo. Kwa upande wa Judi, yeye alikuwahajiamini kama alikuwa peke yake kwenye penzi la Richard. Hakujua nikwa nini alikuwa akipatwa na hisia hizo mara kwa mara, kuna wakatialikiri huenda ni kwa vile Richard alikuwa ni mtoto aliyezungukwa nautajiri wa baba yake na mwonekano wake kumvutia msichana mwingineyeyote kutaka awe naye!
Wivu! Hilo ndilo lililokuwa likimsumbua nakumwingiza kwenye wasiwasi huo. Alikiri dhana hiyo ya wivu ndioiliyokuwa ikiisumbua
nafsi yake na kumjengea woga kuwa, Robertalikuwa na wanawake wa nje! Pamoja na kuwa na hisia za aina hizo,lakini hakuwahi kumfumania na mwanamke mwingine japo mara moja!
Kwaupande wa Richard, yeye mawazo yake yalikuwa yakikinzana kimkabalana mawazo ya Judi. Yeye alikuwa akiamini Judi alikuwa hanamwanamume mwingine zaidi yake kutokana na uaminifu aliokuwa nao Judi.Pamoja na kuwa na mitazamo tofauti kati yao, ajabu ni kwamba, hakunahata mmoja aliyediriki kuzizungumza hisia hizo kwamwenzake.
Mahusiano yao ya muda mrefu yaliwawezesha kuwajengeamazoea ya kuzoeana, wakawa na uhuru kwa kila mmoja kwenda kwamwenzake kwa muda wowote na wakati mwingine bila hata yakutaarifiana. Uhuru huo ulimfanya Judi na wazazi wa pande zote mbilikuamini kuwa, suala la ufungaji wa ndoa kati yao lilikuwa lipo njianina lingetangazwa wakati wowote. Lakini kama ilivyo ada kwa tamaduniza Kiafrika, mwanamume ndiye aliyepewa jukumu la kutamka dhamirahiyo, Judi akaamini, ipo siku Richard angekuja kulitamka jambo hilokwake. Richard hakufanya hivyo! Na Judi naye akashindwakuvumilia! Ndipo asubuhi hiyo, Judi alipoamua iwe siku ya kuuvunjaukimya huo!
* * * * *
Richard alitoka kuoga nakuingia chumbani. Kitendo cha kufunguliwa kwa mlango wa maliwatoniambayo ilikuwa imo humo humo chumbani, ile hali ya kutoka kuogaaliyokuwa nayo Richard na kufunguliwa kwa mlango huo kulisababishaharufu ya sabuni ya kuogea iingie chumbani humo, lakini ilichukuasekunde chache harufu hiyo kumezwa na manukato yenye harufu ya nuniyaliyokuwa yamepulizwa mwilini na kwenye nguo alizovaa Judi.
Judiakaanza kumpigia mahesabu Richard aliyekuwa ameanza kuvaa nguo yandani na kisha akamwona akivaa suruali aliyoitoa kwenye kining'inizocha kuwekea nguo kwa kutumbukiza mguu mmoja baada ya mwingine kwenyesuruali hiyo. Judi akashusha pumzi kwa nguvu bila ya kutarajia. Halihiyo ilimjia baada ya kugundua jambo alilokuwa anataka kulizungumzakwa Richard lilikuwa na uzito mkubwa kwenye mustakabali wa maishayake ya baadaye.
Hali ya utambuzi wa mustakabali huo ilimuwekakwenye unyonge, hata kule kujiamini kuwa yeye ndiye mwenye nafasi yakuolewa na Richard, ghafla kukaanza kumuweka kwenye njia panda. Hofuhiyo ikamuweka kwenye mizani kwa kuzivuta kumbukumbu za matukio kwakipindi chote alichokuwa na Richard, ikawa kama vile anajifanyiausaili utakaomwezesha kumpa moyo wa kuendelea na dhamira yakealiyoidhamiria; dhamira ya kulizungumza suala la ndoa kwaRichard!
Aliyakumbuka matukio mengi mazuri yaliyoonyesha upenzikati yao; kama vile kununuliwa vito na nguo za thamani kwenye madukayanaouza bidhaa hizo kwa bei ghali; kutoka pamoja kwa ajili ya kulachakula cha usiku kwenye hoteli za kifahari au migahawa ya Kimataifa;kuhudhuria kwa pamoja mialiko tofauti ya sherehe walizokuwawakialikwa au wakati mwingine kufurahisha nyoyo zao kwa kwenda kwenyemahoteli yaliyopo nje ya jiji la Dar es Salaam au kwenye majumbatofauti ya starehe.
Ujumla wa kuyakumbuka matukio hayo ulimfanyaajione ni nembo maalumu ya Richard na kuamini kuwa, ni yeye ndiyealiyechaguliwa! Lakini pia, pamoja na kuyakumbuka mazuri yoteyaliyofanyika kati yao, pia aliikumbuka mizozo waliyokuwa wakizozanakwa mambo madogo. Kama vile kukasirikiana kutokana na maudhiyaliyokuwa yakisababishwa na vijijambo vya kipuuzi, wakati mwinginekuwafikisha kununiana kwa saa kadhaa au zaidi ya hivyo.
Baadhi yamatukio waliyoudhiana waliweza kuombana misamaha, lakini pia kunabaadhi yaliyowafanya wasiombane misamaha kwa sababu kila mmojaalijiona ana haki ya kuvuta kamba upande wake. Mizozo ambayohakuwakuombana misamaha iliweza kumalizika kimya kimya na kuwa kamavile hakukuwepo na mtafaruku uliotokea kati yao. Alipoyawekakwenye mizani matukio hayo, mengi yakawa ni mazuri na zile kasorochache zilizokuwa zikijitokeza, akazichukulia ni sehemu ya kawaidakwa binadamu wanaoishi kwa karibu. Ukweli huo ukamuweka Judi kwenyeimani aliyoikubali kuwa, walikuwa wakipendana kwa dhati.
Akajionayupo kwenye nafasi kubwa ya kuolewa na Richard! Hali hiyoikamrejeshea nguvu ya kuitupa karata yake juu ya meza! "Richie,"Judi aliita. Alikuwa amezoea kumwita Richard kwa jina hilo. Richardaliyekuwa amesimama mkabala na kioo kilichopo kwenye kabati lakuvalia akiwa anazichana nywele zake, aligeuka na kuitikia hukuakimwangalia Judi aliyekuwa bado amekaa kitandani. "Kuna jambonataka nikuulize," Judi alisema huku akijaribu kuyatuliza machoyake kumwangalia Richard usoni na wakati mwinginekuyakwepesha. Richard alishitushwa na kauli hiyo baada ya kugunduaJudi alikuwa amekosa utulivu usoni mwake wakati akiitamka. Akahisikulikuwa na tatizo! "Jambo gani?" Richard aliuliza huku akiwaameganda na kitana chake mkononi.
"Una mpango wowote wakunioa?"
Richard alionekana kama aliyesukumiwa ngumi ya ghaflailiyotua usoni mwake! Akiwa ameishiwa nguvu ghafla baada yakupigwa swali hilo, alijikokota kwa kujisogeza taratibu hadi kwenyekabati la kuvalia, akaliegemea. Uso wake ulikuwa umepigwa na tahayari iliyomwonyesha kuwa, alikuwa akihaha kulitafuta jibu. Macho yakeyalishindwa kuyakabili macho ya Judi yaliyokuwa yakimwangalia.Akaiangalia sakafu iliyojengwa kwa marumaru kama vile eneo hilo ndilolingetoa majibu ya swali alilokuwa ameulizwa. Ukimya uliofanywa naRichard ukaanza kumchanganya Judi. Akili yake ilianza kukataakuamini kile anachokishuhudia kutoka kwa Richard.
Richard alikuwaakionekana kupata kigugumizi kulijibu swali ambalo lingehitimishandoto ya Judi; ndoto ya kuolewa! "Mbona hunijibu?" Judialiuliza huku sauti yake ikionyesha ukakamavu wa kutaka ajibiwe,lakini moyo wake ukisambaratika kwa maumivu yaliyoanza kumkatishatamaa. Woga na hofu ya kupewa jibu litakalomwumiza vikawa vinaitafunanafsi yake, hali hiyo ikauweka moyo wake kwenye mapigo ya kasiyaliyotishia uhai wake!
Richard alianza kwa kupiga kite nakushusha pumzi huku uso wake ukiwa bado unaangaliasakafuni."Hapana Judi!" Richard alijibu kama vile alikuwaakiongea na sakafu aliyokuwa akiitazama. Kisha akauinua uso wakekumwangalia Judi. "Sina mpango wowote wa kukuoa!"alimalizia. "Yesu wangu!" Judi alinong'ona peke yake nakuishiwa nguvu huku
akiwa amefumba macho. "Najua haitokuwarahisi…" Richard alianza kuutetea uamuzi wake.
Judi akawahikumnyooshea mkono Richard kumzuia asiendelee kuzungumza. Kimyakikapita kati yao. Judi akashusha pumzi kwa nguvu akiwa badoamefumba macho. "Uko serious na jibu lako?" aliuliza. Richardakaonekana kuwa kwenye wakati mgumu, lakini pamoja na kuwa kwenyehali hiyo, bado alikusudia kuwa kwenye msitari wa ukweli. "Ndiyo!Niko serious!" Richard alisema.
Judi akanywea, kila kiungo chakecha mwili kikaonekana kama kimekataa kufanya kazi! Akatulia palekitandani alipokuwa. Ghafla
akalikumbuka tukio la kufanya mapenzina Richard saa chache zilizopita baada ya kurudi kutoka disko kablahawajalala na kuamka asubuhi hiyo.
Halikuwa tukio geni kwao,lakini tukio hilo la saa chache zilizopita likawa kama tukio pekeekatika maisha yake na Richard lililompa picha halisi jinsi Richardalivyokuwa akimchezea katika maisha ya ngono walizokuwa wakizifanyahuku yeye akiamini kwa imani zote kuwa, ilikuwa ni njia ya kuelekeakwenye kufunga ndoa!
Lilikuwa pigo kwenye maisha yake! Aliusikiamoyo wake ukikatika pande mbili kwa maumivu makali aliyokuwahajawahi kukumbana
nayo. Alihisi kama anayeelekea kuzirai,akajaribu kupambana na hali hiyo isimtokee akiwa ndani ya nyumba hiyoambayo sasa ilishakuwa ni nyumba asiyotaka aendelee kuwemo tena.Akamudu kuizuia hali hiyo, lakini akashitukizwa na tukio jingineambalo laiti angepatwa na hisia za mapema kuwa lilikuwa njianikumtokea, kamwe asingeweza kuliruhusu limtokee mbele ya Richard;Richard alishakuwa Shetani mbele yake! Yalikuwa machozialiyoshindwa kuyazuia! Kitu kikaja kumbana kooni na kumwanzishiakilio chenye kwikwi iliyomuweka kwenye kilele cha majuto! Richardakamsogelea na kumshika maungoni ili ambembeleze, Judi akaupangua kwanguvu mkono wa Richard usimshike! "Tafadhali usinishike!" Judialisema kwa sauti yenye chuki iliyotawaliwa na hasira zilizokuwakatikati ya kilio. Kuanzia siku hiyo uhusiano wao ukawa umeingiadoa!
*****
JOHN Sailas akiwa varandani mwa nyumbaanayoishi yenye chumba kimoja cha kulalia, varanda moja, jiko na chooambayo alipanga, alitengeneza tabasamu dogo mdomoni mwake wakatiakiisoma barua iliyoletwa na mshenga wake iliyokuwa imejibu baruayake ya uchumba aliomchumbia rafiki yake wa kike anayeitwa Dina sikukadhaa zilizopita. Barua aliyokuwa akiisoma ilikuwa ikielezeajinsi alivyokubaliwa uchumba wake na tabasamu alilokuwa amelijengalilikuja baada ya kusoma masharti yaliyokuwa yanahitaji yatimizwesiku itakayopelekwa mahari. Baadhi ya masharti aliyaona kama aina yamzaha unaochekesha.
Kukubaliwa kwake kumuoa Dina alikutarajia kwasababu alikwisha kuizungumza nia yake hiyo kwa mwenyewe Dina,wakakubaliana na ndipo alipomtuma mshenga kuipeleka posa hiyo. Lakinipia, hata kabla ya kulizungumza hilo, uhusiano wao wa mapenziuliokwishadumu kwa zaidi ya mwaka mmoja, nao ulikuwa ukifahamika nawazazi wa Dina, hali kadhalika na wazazi wake mwenyewe. Pamoja yakuwa mila za Kiafrika huwa zinawaweka mbali mtu na mkwewe, lakiniuhusiano wake na Dina
uliweza kumuweka karibu na mama mkwe wakekiasi kwamba kukawa na urafiki fulani ulioongezea aina ya utani wahapa na pale.
Ukaribu huo na mama mkwe wake ndio uliompa Johnuelewa kuwa, posa yake hiyo isingekumbana na vikwazo vyovyote.Alikuwa akijua mama yake Dina ndiye aliyekuwa na sauti ndani yanyumba huku baba yake Dina ambaye ni mstaafu akiwa hana kauli yakumpinga mama huyo. Mama yake Dina ambaye bado ni mwajiriwa, ndiyealiyekuwa mwendeshaji wa nyumba kwa karibu kila kitu.
Johnaliikunja barua aliyokuwa akiisoma na kuirudisha kwenye bahasha,kisha akaiweka juu ya meza na yeye mwenyewe kujilaza kivivu kwenyesofa aliyoikalia. Uso wake aliuelekeza juu na kuliangalia pangaboilililokuwa likizunguka kwa kasi ndogo. Uzungukaji wa pangaboialiokuwa akiuangalia ilikuwa ni kama vile alikuwa akizirudisha nyumatafakuri zake kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita kwakuikumbuka siku ambayo yeye na Dina walionana kwa mara ya kwanza.Ilikuwa siku ya Jumamosi!
Aliikumbuka vizuri siku hiyo. Siku hiyoalikwenda eneo la Ndege Beach akiwa na pikipiki yake. Hakuwa mgeni naeneo hilo, alikuwa na mazoea ya kwenda mara kwa mara kwa ajili yakuogelea kutokana na fukwe ya eneo hilo kuwa ya kupendezaukilinganisha na fukwe nyingine zilizopo Dar es Salaam kamaukiziondoa zile za eneo la Kigamboni.
Akiwa na begi lakelililobeba nguo yake ya kuogelea baada ya kufika kwenye fukwe hiyo,alilitua begi juu ya mchanga mweupe hatua chache kutoka baharini.Aliwaangalia kwa sekunde chache watu waliokuwa wakiogelea kwenyebahari ambayo haikuwa na mawimbi makubwa kwa siku hiyo. Kishaaliinama tena, akalifungua begi lake na kutoa bukta aliyoiandaakuogelea nayo. Kabla ya kuivaa bukta hiyo, alijifunga taulo kubwailiyoziba maungo yake ya kati hadi miguuni, akaivua suruali yake yajeans kwa kuiunganishia na chupi aliyokuwa ameivaa na kuzikunjavizuri nguo hizo kisha akaivaa bukta ya kuogelea. Baada ya kuwakamilifu kwenye hali ya kwenda kuogelea, alizichukua nguo zakealizozivua na kuzitia kwenye begi pamoja na ile taulo. Badalaya kwenda kuogelea, John alikaa kwenye mchanga kando na lilipo begilake na kuanza kuwatizama waliokuwa wakiogelea baharini.
Akavutiwana kundi dogo la wasichana watatu, wawili wakionekana angalauwanaweza kujaribu kuogelea na yule watatu akiwa hajui kabisakuogelea. Msichana huyo wa tatu ndiye aliyemvutia; na si kwamba kwavile alikuwa hajui kuogela, lakini pia alikuwa na mvuto kulikowenzake aliokuwa nao. Msichana huyo mwenye umbo la kupendeza lenyeurefu wa wastani, alipendezwa na nguo za kuogelea aina ya bikiniambayo ilimfanya John apate ushawishi wa kumkaribia msichana huyo iliamwone vizuri!
Aliendelea kumwangalia msichana huyo alivyokuwaakijilaza kwenye maji kama anayetaka kuogelea, lakini kwa kukosaustadi wa kujua kuogelea, akawa anaishia kwenye mwelekeo wa kuzamakila alipokuwa akijaribu kuogelea. Wakati wote alipokuwa akijaribualijikuta akiishia kupiga magoti na sura yake kuangukia majini.Kitendo hicho kilimfanya ajiinue kwa haraka kila tukio hilolilivyofanyika na kuonyesha woga wa kuogopa kuzama huku akijifutamaji ya usoni na kuhema kwa kuacha mdomo wazi na kuzitafuta pumzikwa kuruka ruka kwenye maji huku akipenua macho yake. Hali hiyoilimfanya John atabasamu peke yake. John aliondoka alipokuwaamekaa na kuelekea kwenye maji, akaenda upande walipokuwepo wasichanahao na kumfuata yule aliyekuwa hajui kuogelea. "Samahani,"John alimwambia yule msichana. "Una nia ya kujua kuogelea?" Usowa msichana yule ukajengwa na aibu kwa kugundulika kuwa hajuikuogelea, hata hivyo aibu hiyo akaiziba kwa tabasamu lenye haya. "Kwajinsi unavyojaribu kuogelea, katu hutojua kuogelea,"John aliendelea bila ya kusubiri jibu la msichana huyo. "Kwanzani mwoga. Pili, maji hayawezi yakakuinua kwa sababu tu, unatakakuelea. Kuna mbinu za uogeleaji ambazo lazima ufundishwe ndipoutakapoweza kuogelea," John alisema. Akakumbuka kujitambulisha."Jina langu ni John, John Sailas. Unaitwa..?" Moja kwa mojamacho ya msichana yule yakawaangalia wenzake walioacha kuogelea,nao wakawa wanakuja pale aliposimama na John. "Vipi?" mmoja wawale wenzake wawili alimwuliza huku akijaribu kumwangalia John kwakutaka kujua kinachoendelea. "Nataka kumfundisha mwenzenu namnaya kuogelea," John alijibu ingawa swali lililoulizwa lilikuwahalikulenga kwake.
Nyuso za mshangao zikajengwa na wasichana haowawili na kuonyesha dhahiri hawakulitarajia jibu hilo. Wakajikutawakimwangalia mwenzao kama kutaka kujua ameliafiki vipi wazo hilo.Mwenzao hakujibu chochote, ukimya wake ukawajumuisha wote watatu kupigwa na ganzi ya kutojua wajibu nini kwa mtu huyo au wawili haowamshauri vipi mwenzao. "Nitarudi baadaye nijue mmeamuaje!"John alisema kisha alijilaza kwenye uso wa maji na kuanza kuogeleakwa ustadi wa kukusudia kuwaonyesha wasichana hao namna gani jinsianavyojua kuyakata maji. John aliogelea kwa umbali mrefu kama njiaya ushawishi kumfanya msichana huyo endapo atakubali kufundishwanaye basi ajione atakuwa salama mikononi mwake.
John aliporuditena kwa wale wasichana, wakakubali amfundishe mwenzao, lakini kwasharti kuwa hata nao walihitaji kufundishwa.
"Basi nitaanza nahuyu ambaye hajui kabisa," John alisema. Wazo la Johnlikakubaliwa.
Wakiwa wawili peke yao kabla ya kuanza kufundishanakuogelea, John akakumbuka kujitambulisha tena, "Jina langu ni John Sailas…" Macho ya John na yule msichana yakaangaliana. Johnakauhisi moyo wake ukipiga kwa kasi. Akakijua kilichopo moyoni mwakedhidi ya msichana huyo. "Naitwa Dina," msichana alisema hukuakionyesha tabasamu dogo lililojificha kwa dhamira. Ni sikuambayo John hakuisahau kamwe!
ITAENDELEA KESHO..