Riwaya ya Kijasusi Mabaduni wa serikali

Riwaya ya Kijasusi Mabaduni wa serikali

Karibuni tuendelee,
Watag na wenzetu .


Mabaduni wa serikali



Sehemu ya 2



M
jini Homa Bay, barabara ya tano iliyomimina watu lango la jiji, ikiwa imetenganisha mitaa kadhaa kushoto na kulia.

Kushoto pakiwa makazi ya watu wa hali ya kawaida na kulia wakiwa watu wa kipato cha kati na juu kiasi.

Napa street. Ni mtaa uliopatikana huko changanyikeni upande wa kushoto barabara ya tano.



Katika nyumba moja yenye vyumba takribani nane vilivyojengwa kwa kutazamana ,

ndipo aliishi mtu mmoja maarufu katika mitaa hiyo, kwa jina Seif.

Seif huvaa kanzu muda mwingi na kibandiko kwa juu, ni mkimya na anaishi peke yake, hana mchumba wala mpenzi.

Ukimsalimu hujibu vyema,

Hana majivuno, ni mstaarabu ila kimya chake na maisha ya peke yake ndio huwapa watu mashaka.

Kama ujuavyo watu hupenda wakusome kama gazeti.



Seif anaishi na wapangaji wenzake ambao watano ni wanawake, mchanganyiko wa rika lakini hakuna aliye ndoani.

Ila wote wana wapenzi wao.

Wawili ni vijana wa kiume, hivyo kufanya Idadi ya kiumeni kuwa watatu.



Hawa vijana wawili, wao wako katika mapenzi muwawana.



Seif hutoka alfajiri na kurejea giza, ni kawaida kuwakuta majirani zake koridoni wakipiga mdomo.

Huwasalimu na kuingia zake ndani, kisha hubeba taulo na ndoo ya maji kwenda bafuni.

Humo ndani pia yumo Mwana,

Mwana ni Mwana kweli, kaumbika pia kavunjika kike haswa.

Ana nyonga zilizotanuka,

Nyuma kabeba pia kwa niaba ya wenzake, maana kafungasha mzigo wa tani kadhaa mlaini na mteke mteke.

Ambao huacha gumzo na matamanio kwa wanaume kila apitapo.

Ana rangi maji ya kunde, macho yake malegevu ya kurembuka muda wote humtia mtu ashki bila ridhaa yake.

Ana sura ya kitoto na mikono iliyobeba vinyweleo vifupi vya udhahabu maarufu kama malaika.



** **

Siku hii Seif alirudi mapema kutoka atokako, maana ilikuwa yapata saa kumi na moja jioni.

Aliwakuta majirani zake koridoni, kama ilivyo ada aliwasabahi kisha akaziendea hatuaze.

Akatoka na taulo kiunoni na ndoo ya maji mkononi kwenda bafuni.

Akaiacha korido sasa yupo nje ya mlango, kutoka alipo mpaka bafuni ni mita kadhaa.

Mara Mwana nae huyo! Ndio anatoka bafuni na kanga yake mwilini iliyolowa kwa maji. Daah!!

Mwanamke anajitupa kimikogo na kukuonesha namna gani ana uwezo wa kumfanya mwanaume yeyote rijali akang’ata kidole kwa uchu.

Mwana alipomfikia Seif alimsalimu kwa tabasamu lililobeba huba ndani yake, na kuufanya moyo wa Seif kwenda mbio isivyo kawaida.

Hata Seif mwenyewe alijishangaa, maana ni kama kuna mwizi kapenya ghafla na kuingia kwenye uvungu wa moyo wake.

<<< Mpenzi msomaji usiombe ukampata mtu wa kuupendeza moyo wako!! Maana hata ukimwona kwa mbali anakuja, moyo wako unajawa na furaha ya ajabu. Ujue hapo umependa, na yeye akiwa amekupenda, ndio kabisa utahisi umeipakata dunia mapajani mwako.

Ila Daaahh!! pesa mwanaizaya huyu katuharibia dunia yetu ya mapenzi, >>> turudi mchezoni.

Seif alizipiga hatua taratibu akionekana kuuza umakini wake kwa muda, almanusura ajikwae kwenye ngazi za kuingia bafuni.

Muda wote alikuwa akiwaza, ni hali gani inataka kumtokea kwa mwana.

Alihisi hisia za ajabu na za kweli zikimsukuma kwenye ulimwengu wa huba kwa binti Mwana

Moyo wake ulikuwa tayari kujisalimisha kwa huyu mlimbwende wa aina yake.

Lakini Seif hakuwa tayari kuukubali huu ukweli.

Alijikuta akitamka kwa nguvu bila kutarajia “haiwezekani,” huku akijimwagia kopo la kwanza la maji mwilini mwake.

Haikueleweka ni kwanini, lakini hali ilidhihirisha kuwa Seif hakuwa tayari kuingia katika mbilinge za mapenzi.



Seif alimaliza kuoga akatoka na kuingia chumbani kwake, akiwaacha majirani zake pale pale koridoni.

Lakini awamu hii walionekana ni kama walikuwa wakimjadili yeye kwa kauli aliyoisikia kutoka kwa mmoja wao “Asije akawa Hanithi huyu.

Haikumshughulisha sana kauli hii, maana kama ni kunenewa mabaya, ni mengi yashapita masikioni mwake.

Tena mazito sana, lakini hakuwa tayari kuvunja msimamo wake ajili tu waridhike walimwengu.

Kwani yawatosha’ni kushiba?

Baada ya kujiandaa vyema ndani ya kanzu, aliwahi Masjid kwa swala ya magharibi.

Msikiti wa Diyarbakir ni msikiti uliopo mtaa wa Gonza, upande wa kulia wa barabara ya tano

Watu mashuhuri na matajiri hufanyia ibada zao hapo.

Hapa ndipo unaweza kukutana na wakwasi wengi wa Songomo, akiwemo Fanton Mahal.

Mara kadhaa baada ya swala utawaona Seif na Fanton Mahal, wakiwa pamoja nje ya msikiti kama sekunde thelasini.

Kisha baada ya hapo kila mtu huchukua njia yake, na kutoweka hapo msikitini.



Leo kidogo ilikuwa tofauti, maana baada ya swala wawili hawa walionekana pamoja kwa muda mwingi,

Mpaka pale Imam alipotoka nje ya msikiti na kumwendea Fanton mahali, akaanza kuzungumza nae ndipo Seif aliaga na kuondoka.

Seif baada ya kutoka kwenye Ibada, alielekea sehemu moja ambapo kulikuwa kumezoeleka watu kukusanyika jioni baada ya kazi za kutwa nzima .

Hapo watu wangeongelea mambo ya siasa, mpira na baadhi ya habari ambazo ziligusa hisia za watu kutoka medani mbali mbali ndani nan je ya nchi.

Leo hii Seif alikuta watu wakijadili hali ya kisiasa nchini kwao, baadhi wakidai Raisi Mwibale Moha hawezi kupita katika kura za seneti.

Ndipo mmoja akasema “Jamaniee! mimi mbona nasikia tu za kunyapia nyapia kuwa mwamba kaisha, nyie kwani hamjaziskia za chini ya kapeti ?”

Mabishano yalikuwa makali kiasi cha kuibua zogo, ili mradi tu kila mmoja anazungumza lile analoona ndio sahihi.

Akiwa anaendelea kusikiliza porojo za hapa na pale, huku akikiadhibu kikombe kifupi cha Gahawa, mara simu yake ikaanza kuita.

Akasogea pembeni ili aweze kuipokea.

Akatazama kwenye kioo cha simu lakini, namba ilikuwa ni private mhusika hakutaka kutambulika.

Basi aliipokea na kuiweka sikioni.

Kesho Saa tatu asubuhi fika Shai Resort ukiwa na karatasi yenye Tarakimu na namba hizi BUN/k8.” Kisha simu ikakatwa.

Alitumia takribani dakika mbili kutafakari juu ya ile simu. Kisha akakata shauri la kuondoka eneo hilo, na kwenda moja kwa moja anapoishi.

Njiani alipitia chakula katika mgahawa mmoja uliokuwa ukitoa huduma ya chakula kizuri sana, alichukua vifurushi viwili na kwenda navyo mpaka nyumbani.

Alipofika aligonga mlango wa chumba anachoishi Mwana, haukupita muda Mwana alifungua mlango.

Akamkabidhi furushi lake na juice ya embe, aliyoinunua pale mgahawani.

Mwana alipokea kwa furaha, lakini iliyochanganyikana na mshangao wa kutoamini anayoyaona. Maana imekuwa ghafla na hakuwa ametarajia hilo kutokea tena likifanywa na Seif.

Lakini hakutaka kuuliza sana, maana yeye mwenyewe nafsi yake ilimwangukia Seif mzima mzima tangu zamani.

Maana yapata miaka mitatu sasa toka ahamie kwenye nyumba hii aliyomkuta Seif na wanawake wengine wawili wa vyumba jirani wakiwa wanaishi hapo.

Alitamani hata amwambie jinsi anavyomuhusudu nafsini, lakini hakuona ni namna gani hilo litatokea.

Maana hata alipojaribu kutumia mbinu zake za kike, Seif alimkwepa na kumuoneshea kutojali wala kuelewa shabaha ya Mwana.

Seif baada ya kumkabidhi mwana furushi lake, alimtakia usiku mwema na kugeuka akipiga hatua kukiendea chumba chake. Ambapo cha mwana kipo mwanzoni upande wa kushoto wa korido, na cha Seif kipo mwishoni upande wa kulia.

Hivyo milango yao ya vyumba imeachana kiasi chake.

Alipiga hatua tatu mara akaitwa “Seif”, sauti ya mwana.

Akageuka na kumtazama, Mwana akababaika kama mtu aliyesahau ghafla alilolikusudia kulisema.

Akawa anafikicha vidole, kigumba kikitalii kuanzia kwenye kidole cha shada mpaka kidole kidogo.

Alitatanika kidogo kisha bila kuyapangilia maneno, akamwambia kwa lugha tetemeshi isiyo ya kujiamini. “A-hs-a-nte kwa zawadi Allah akufanyie wepesi na akuongezee ulipotoa Usiku mwema na kwako pia” Kisha kwa taswira ya uso uliokumbwa na aibu, akageuka na kurudi ndan mwake alikuwa amejitanda mtandio mwepesi ulioruhusu sehemu za nyuma kubingirika bila kizuizi na kutengeneza picha murua kwa aliemtazama pigo lingine kwa Seif

Seif aligeuka na kukiendea chumba chake, tabasmu usoni furaha tele moyoni.

Asielewe hata chanzo cha furaha ni nini haswa muda huo, labda amekuwa mjinga wa mapenzi.



Asubuhi ilikaribishwa kwa mwanga uliokuwa ukipiga chumbani mwa Seif kupitia dirishani, kupitia upenyo ulioachwa wazi na pazia ambalo halikutanda vyema kuvisitiri vya ndani.

Aliamka maana saa yake kwenye simu ilionesha ni saa moja na nusu tayari, alichukua mswaki na ndoo ya maji akajiongoza bafuni ambapo baada ya dakika kumi alitoka na kujiandaa.

Alivuta begi moja toka uvunguni, akafungua na kutoa Bastola yenye midomo miwili akaipachika kiunoni.

Alitoa na pochi ambapo baada ya kuinyoosha, ndipo ilibainika kuwa ni bastola nyingine ya dharula.

Ambayo unaweza kuikunja na kuishikilia tu mkononi kama kikasha, na adui asijue kama ni silaha.

Baada ya kujiandaa vyema alitoka na koridoni alimkuta Mwana ambae alikuwa anaandaa kifungua kinywa, wengine bado walikuwa vyumbani mwao wakiwa bado wamelala.

Alimsalimia mwana, salamu ambayo haikuyazingatia sana ya jana yake. Kisha alitoka mazingira hayo na kusogea karibu na barabara ili akodi usafiri, kweli baada ya kufika kwenye kituo cha taxi alikodi usafiri mpaka Songomo Resort.

Alipofika pale hotelini alichukua chumba ambapo alipewa chumba namba 33.

Aliingia humo na begi lake dogo mkononi, akaingia maliwatoni, akasimama mbele ya kioo akashika chini ya shingo kidogo na kuivua sura ya Seif.



Na sasa mbele ya kioo alisimama mtu wa tofauti kabisa.

Sio tena yule Seif aliezoeleka bali ni Jiga Kinamba.

Jasusi bora wa wakati wote, wazungu huita “The greatest of all time.”

Mtu mwenye heshima iliyotukuka katika ulimwengu wa ujasusi.

Wengi wamezisikia sifa zake lakini hawajawahi kumuona ana kwa ana, japo baadhi hutamani hata kufikia walau nusu ya uwezo wake.

Ni jasusi aliefahamika kama mkamilifu katika majukumu yake, hajawahi kufanya makossa kwenye kazi na mara zote alizotumwa hakuacha alama.

Ni mtu mwenye akili kubwa sana na mbunifu, hasa linapokuja suala la mauaji ya mtu ambae kifo chake kitaibua uchunguzi mkali.

Baada ya kuvua sura ya seif alivaa sura ya mtu mwingine ambae haikujlikana jina lake.

lakini huenda ndio sura aliyotakiwa kuwa nayo wakati huu, kisha alitoka chumbani humo bila kuacha chochote kile.

Mfuko wa koti la suti aliweka vichupa vya sumu, ambapo mojawapo ilikuwa ni cyanide.

Alienda mpaka kaunta ya chini akaagiza juice akaimimina kwenye glasi, lakini hakuwa akiinywa muda mwingi alikuwa akimsubiri mtu hapo.

Punde alifika mtu mmoja kwa jina la Malone, huyu alikuwa ni mratibu mkuu wa shughuli zote za intelijensia ndani ya Shirika la kijasusi la Junior Intelligency & Security Agency.

Alipofika alitoa kikaratasi na kumuonesha Seif kikiwa kimeandikwa BUN/K8, kisha Bw. Seif wakati huu akiwa katika sura tofaut nae alitoa kikaratasi cha aina hiyo hiyo.

Baada ya kila mmoja kuridhika na utambulisho wa mwenzake, ndipo Malone aliketi, wakawa wanatazamana kisha,

Malone alitoa karatasi yenye maelezo mafupi na kumpatia Seif, ambae alikuwa anaisoma kwa kuifungua kidogo kama anaekunjua jamvi, lakini pia na ile sehemu anayokuwa ameshaisoma nayo anaikunja vile vile mpaka akaimaliza yote. Kisha,

Akamuitikia Malone kwa kufumba macho mara mbili kwa haraka ishara ya kuwa amemwelewa.

Malone nae alimkabidhi bahasha iliokuwa na kiasi kikubwa cha Dolari, kama sehemu ya malipo ya hiyo kazi.



Baada ya hapo Malone aliondoka kuelekea gari aliokuja nayo, alipofika alifungua mlango wa gari lakini muda huo huo iliingia gari nyingine kama ile aliokuja nayo Malone. na kupaki usawa kabisa na upande aliokuwa Malone nayo ikafunguliwa mlango. Hivyo, Malone hakuingia kwenye ile ya mwanzo, bali hii ya pili kisha ikaondoka eneo hilo kwa kasi ya kawaida tu. Na ule mlango wa gari ya mwanzo ulikwisha kufungwa, hivyo ungehisi kuwa Malone aliingia kwenye ile gari aliyokuja nayo.

Kama sekunde tano baada ya ile nyingine kuondoka, hii gari aliyokuja nayo Malone ililipuliwa kwa bomu na kusambarika vibaya.

Lilikuwa ni bomu lenye nguvu sana, maana mshindo wake ulipelekea mtikisiko na kupelekea baadhi ya watu pale hotelini kuanza kukimbia hovyo kusalimisha nafsi zao.



Seif alilifuatilia tukio hilo, mwisho alitoa tabasamu hafifu tu na kujisemea kwa sauti “Wanahisi wanaweza kukabiliana na Malone,? Malone you are too good for them.

Ni suala la muda tu mpaka pale watakapogundua kuwa wanapambana na kikosi cha zamani cha MABADUNI WA SERIKALI, ila kwa sasa tupo dhidi ya Serikali.”




Hapa ndipo tunagundua kuwa, kumbe hii miamba ni kile kikosi cha zamani cha Kazi chafu, zilizotekelezwa na kundi lililoogopewa ndani na nje ya Songomo.

Kosi la watu Saba, lakini likitumwa kazi ni kama jeshi la maangamizi la malaika wa shetani.



Likiongozwa na shetani mwenyewe Bwana Fantoni Mahal.

Huyu Fanton Mahal sio tu kwamba ni tajiri, pia ni jasusi wa kwenda, na ndiye mtu pekee anaewatambua MABADUNI WA SERIKALI wote.

Hivyo kumgusa huyu mtu ilihitaji kujitia uchizi, na ni kama ulisaini hati ya kifo mwenyewe.

Raisi Mwibale Moha alikuwa ameibua vita na Shetani huyu.



Baada ya lile tukio Seif alitoweka pale na kuingia chumbani, maana alihisi hata yeye alikuwa hatarini kuendelea kubaki hapo.

Maana ni lazima kivyovyote nae alikuwa kwenye darubini za wauaji.

Wauaji ambao alijua fika, ni watu kutoka Serikalini waliotumwa kwa agizo la Raisi ili kuhakikisha ushindi unaenda kwa Raisi Mwibale Moha.

Baada ya kuingia chumbani aliingia maliwatoni akiirudishia sura ya Seif. Lakini alihisi kama kuna mtu anacheza na security system ya mlango wa chumba chake.

Maana mlango una lock za PIN.

Akavuta kisu kidogo sana chembamba chenye sumu kisha, akashika begi lake mkono mwingine. Muda huo akiwa na sura Seif.

Sasa ile mlango unafunguka alishuhudia mtu akiingia na bastola mkononi, bastola ambayo aliitambua kuwa hutumiwa na wanajeshi wenye cheo cha Colonel.

Hivyo alitambua uwezo wa wanajeshi wa kiwango hiki haukuwa wa kubeza, hasa linapokuja suala la Shabaha.

Akiwa bado nyuma ya mlango wa maliwatoni, aliweza kumuona mtu huyu vizuri akiwa anapiga hatua zote zilizobeba umakini ndani yake.

Akakagua hiki chumba kisha akahamishia hisia zake kuja uelekeo wa alipo Seif.

Kwakuwa mlango ulikuwa wazi kidogo, hivyo Muuaji aliushika kwa tahadhari na kuingia nao huku bastola ikiwa mkononi.

Lakini ni kitendo cha nukta kadhaa tu, ambapo Seif alipishana na Huyu muuaji mlangoni hapo kwa kasi kama ya kimbunga. Huku akimwacha huyu Colonel na jeraha la kisu kifuani usawa wa moyo.

Ni tukio lililosindikizwa na mlio wa risasi mbili, zilizotoka kwa mkupuo mmoja bila kumpata Seif, nakwenda kutua kwenye maru maru zilizobandikwa ukutani.



Seif huyo koridoni, huku chumbani akiacha maiti inayotiririsha damu.

Alitumia njia za kujipenyeza mpaka alipofika barabarani, akapiga taxi mkono ikasimama akaingia na kuondoka eneo hilo.

Njiani alikuwa akiifikiria kazi aliyopewa, na alikuwa akiwaza namna ya kuikamilisha kwa muda.

Maana karatasi ilieleza kuwa ilitakiwa ikamilike ndani ya masaa 48. Hivyo hakuwa na muda wa kupoteza, ilikuwa ni kujiandaa kimwili na kiakili. Ili kuweza kukabiliana na majukumu mazito yanayokuja mbele yake, maana kazi ndio sasa imeanza.



** **




Seif alifika nyumbani mida ya saa nane mchana, jua likiwa kali sana. Aliingia ndani na kujipumzisha, ili kuipa akili yake tulizo kujiandaa na kazi ilyopo mbele yake.

Alilala mpaka saa kumi ambapo aliamka na kuvaa nguo simple tu maarufu kama casual, akatoka nje na kufunga mlango .

Alitafuta sehemu ambayo angekaa apate walau kinywaji huku akisikiliza mziki taratibu kama sehemu ya starehe tu.

Basi alichukua piki piki iliyompeleka hadi club moja ambayo haikuwa maarufu sana, iliyofahamika kwa jina la Club Ravena. Hii sehemu ilikuwa ni kama chimbo na watu walikuwa wengi huku pilika zikiwa nyingi tu.

Mashanta walikuwa wengi, hivyo biashara haramu zilishamiri sana humu ndani.

Japo hazikuwa kwa ukubwa na uwazi kiasi cha kila mtu kuweza kung’amua.

Alipoingia alitafuta sehemu iliyojitenga kiasi akakaa, mara alifika muhudumu kumsikiliza.

Seif aliagiza wine, ikaja akawa anavimba nayo mdogo mdogo huku akiwatizama watu taratibu.

Mara akafika dada mmoja pale kwenye meza na kuomba ajumuike nae, lakini Seif alimpa ishara tu ya mkono kuwa hahitaji kampani yake, yule dada aliondoka huku akisonya na kubetua midomo.

Lakini pia akihisi aibu kwa kuona ni kama amedhalilika.

Wakati akiwa pale, mara ilitokea vurumai.

Kuna vijana walikuwa wanamshika makalio dada mmoja hivi kwa lazima, wakati akiwa anacheza na mpenzi wake.

Kitendo kile kilimuudhi sana yule jamaa, akajaribu kumtetea mpenzi wake kwa kujaribu kuwazuia na kuwasukuma wale vijana ambao walionekana ni genge la wahuni.

Akiwa katika zile purukushani, mara kijana mmoja alimvuta kwa kumkwida shati shingoni kisha jamaa alipigwa kisu mara tatu. Pale pale akaanguka chini, huku damu nyingi zikichuruzika pale chini na kutengeneza dimbwi.

Watu baada ya kuona hivyo, hakuna aliyekuwa tayar kukamatwa na kwenda kuisaidia serikali.

Walianza kutoka mbio mle ndani, yule dada kutokana na kujawa hofu alijaribu kukimbia huku akijaribu kumfanya kila aliemkaribia kuwa kinga na msaada kwake. Lakini wote walikuwa wakimkimbia, wale vijana walizidi kumfuata na ilionekana nia yao ilikuwa kumfuta pia, maana ndie mtu alieshuhudia hivyo kumuacha haikutakiwa.

Katika kurudi nyuma ndipo akampamia Seif ambae muda wote alikuwa ametulia tuli, kana kwamba hakuna kinachoendelea hapo ndani.

Lakini tukio zima alikuwa amelishuhudia, huyu dada ndie alisababisha wale vijana wamuone Seif.

Wakamsogelea wakiwa na visu mikononi mwao, na mmoja wao akatoa tusi chafu. Tena akimhusisha mamaake Seif, ile anataka kuendelea na sentensi inayofuata, alivunjwa koromeo pale pale na Seif kwa vidole viwili, tena kwa kasi ya ajabu.

Kitendo hiki kilileta hofu kuu kwa wenzake wote, wakabaki wanashangaa maiti ya mwenzao ilivyolala pale sakafuni. Kwa uwezo waliouona,waliogopa sana wakabaki wamevishikilia visu vyao wanatetemeka.

Maana walihisi hata wangemkata asingekatika, lakini punde wakajitokeza watu wengine watatu. Hawa wakionekana watu wazima, na ni kama sehemu ya uongozi wa hili genge.

Wakatoa bunduki viunoni mwao, lakini Seif alitoa tu beji ya dhahabu tupu na kuwaoneshea.

Aisee!! Hii beji ndio iliwafanya wale watu watatu wapige magoti na kusujudu kwa kugusisha vichwa vyao kwenye miguu ya Seif.

Waliielewa ile beji maana yake , Beji iliyomaanisha kifo mbele yao.

Beji iliyohusishwa na MABADUNI WA SERIKALI, malaika wa mauti toka enzi na enzi.

Kikosi chenye historia nzito na ya kutisha nyuma yake, wakifahamika kama THE SEVEN ANGELS OF LUCIFER.

Wamemwaga damu za watu wengi sana huko nyuma.





Seif hakuwa na muda wa kupoteza, aliwapita tu na kumwacha yule dada akiwa anashangaa asielewe kinachoendelea.

Lile genge halikuamini kama wameachwa hai, waliinuka haraka na kwenda kumsujudia yule dada kama ishara ya kumuomba msamaha wa dhati.

Seif hakuwa na muda nao alizidi kupiga hatua Zaidi huku akitoa kauli aliyokuwa akiitumia zamani alipokuwa akikamilisha kazi “Everybody Gangster, until the Devil shows up.”

Haukupita muda magari ya polisi yaliwasili, na kupanya mahali hapo kuwa pa kwao kwa muda, na sio sehemu ya starehe tena.

Vijana wale na viongozi wao walikamatwa kwa mahojiano Zaidi, lakini kwakuwa Seif ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kufika eneo hilo hakuna ambae alikuwa na taarifa za kutosha juu yake.

Taarifa zilizotolewa na wale waliokamatwa ni kwamba kuna uwepo wa MABADUNI WA SERIKALI mjini.

Kikosi ambacho kilikuwa kimebaki kama hadithi tu za uongo kwa watu, lakini sasa taarifa zilianza kuibuka kuwa huenda ni kweli washawahi kuwepo watu wa aina hiyo tena kwa siri sana kupitia mwamvuli wa serikali.

Japo mara kadhaa serikali imekanusha vikali juu ya kuwahi kuwepo kwa kosi hilo la the SEVEN ANGELS OF LUCIFER, lakini taarifa zimekuwa zikichomoka kutoka pande mbali mbali za nchi juu ya uwepo wao na ni kama walikuwa wakirudi upya.

Yaani ni kama vile walikufa, na sasa wanafufuka. Mmh ogopa sana!!!!



Seif alifika chumbani kwake tayari kujiandaa kwa ajili ya majukumu mapya yaliyo mbele yake. Alivuta begi lake jeusi la kijasusi lenye mifuko mingi ya siri, akakagua zana zake zote kuanzia viroboto wa upelelezi mpaka mabomba ya sindano na chupa zote za sumu.

Bastola zenye mdomo mpana, silaha nyingi za kijasusi alizimiliki mtu huyu mpaka zile sindano ndogo za sumu kama sindano rungu saa yenye screen pana ya kuongozea viroboto wa surveillance aliivaa mkononi.

Mwanaume alipigilia suti nyeusi na kofia ya duara maarufu kama pama, kiatu cha ngozi wanchoma kumoyo.

Alitoka na kuufunga mlango wake, akawakuta majirani zake wawili koridoni, akawaaga na kuondoka.

Alifika barabarani akakodi taxi iliyompeleka mpaka kwenye basement za hoteli moja ambapo aliingia pale na kukutana na msaidizi wa Malone ambae ni Sarah.

Sarah akampatia funguo za gari ambalo angelitumia kwenye kazi yake hii.

Mwanaume alifungua mlango na kulikagua gari, akaona linafaa kwa kazi yake akaingia ndani akafunga mlango na kulitekenya akiliondoa eneo hilo kwa kasi, akakamata bara bara ya kumi iliyokuwa inaelekea sehemu maalumu wanakoishi Viongozi wazito wa serikali ya SONGOMO.

Akiwa njiani alikuwa anajaribu kutupa macho yake upande wa kulia na wa kushoto kwa zamu, mpaka pale alipofika usawa wa Hoteli ya MORE LIFE akapunguza mwendo na kusimamisha gari pembezoni kabisa akiwa haamini amini anachokiona.

Na hii ni baada ya kumuona Mwana akiwa na Fanton Mahal kwenye mgahawa mkubwa uliopo hapo hotelini, wakiwa wamekaa meza moja tena ya peke yao wakizungumza.

Alitulia sana eneo hilo barabarani akijaribu kutafakari ni kitu gani kinaendelea baina ya wawili hawa.

Ina maana wanafahamiana au ni wapenzi ?

Maswali mengi yalipita kichwani mwake bila majibu,

Wivu na hasira vilimuadhibu vyema na kupelekea kukosa utulivu wa nafsi, hata asielewe kwanini apatwe na wivu mkali kiasi hicho, kana kwamba yule mwanamke alikuwa ni mke wake halali?.

Baada kuwaza sana bila kupata ufumbuzi aliamua kuendelea na safari yake huku akijisemea “Isije kuwa Fanton anajaribu kumuingiza mwana kwenye hizi kazi, kamwe sitoruhusu hilo kutokea.

Unahisi Seif anaenda wapi na ni kazi gani aliyopewa kuitekeleza?

Vipi kuhusu Mwana na Fanton Mahal je kuna uwezekano wa kuwepo mahusiano baina yao na je Seif atalipokeaje hilo? Usikose sehemu ya tatu. Wako katika utunzi, Sonko Bibo.
 
So mabaduni ni kama old guard.?
Weka episode hata 5 tujue uelekeo.
 
Episode 3
Songomo witnesses a massacre it has never!! and possibly it'll never.
Stay focused.
 
Tatizo bado sijaielewa ww mwandishi uchwara labda ukituma 5 ntaelewa
Tuliza akili mkuu utaielewa tu, ukitaka kuielewa angalia Heading na utangulizi kiini kiko humo.
So unapoflow nayo ukumbuke Heading na ile intro, na hii ni kwa wote wanaosema hawaielewi, Hii ni riwaya ya kimkakati sio Love story. So usitarajie mwandishi aende direct maana kila msomaji anajenga picha yake kichwani na picha zetu haziwezi kufanana kamwe ndivyo fasihi ilivyo.
 
Back
Top Bottom