Sehemu ya 3
Raisi Mwibale Moha alishtuka sana,baada ya kumuona mtu ambae hakutarajia kumuona kwa wakati huo. Mtu huyu ni mwenye ushawishi mkubwa sana ndani ya taifa la Songomo.
Maana amewahi kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi hapo mwanzo, japo kwa wakati huu hakuwa kwenye mamlaka, lakini umuhimu na uzito wake haukuwa wa kubezwa.
Ni mtu ambaye kauli yake ilisikilizwa sana.Bw. Joel Nogeri.
Raisi alimtazama Bw. Joel huku akiwa na shauku ya kujua ana taarifa zipi kwake je ni za kumfaa au ni za kumuangamiza. Maana mpaka hapa Raisi aliona dalili zote za giza katika pambano lake hili,hakuwa akimuamini mtu yeyote yule.
Bwana Joel alikuwa mtulivu sana ni mtu ambae alikuwa na mahesabu makali sana hasa katika nyakati zenye utata kama hizi.
Ushauri wake mara nyingi ulibeba viini vya suluhisho juu ya matatizo yaliyowakabili viongozi na hata Taifa kwa nyakati baadhi.
Kwa ishara ya mkono alimuashiria Raisi kuwa wasogee kwenye skrini moja kubwa sana iliyokuwa inapokea picha kutoka kwenye satellite.
Joel aligusa picha mojawapo kwenye skrini hii na kuikuza kwa ukubwa na ukaribu zaidi, ilikuwa ni picha inayoonesha mazingira ya Sehemu hii walipo.
Kisha akamwambia Raisi, “ Kama kweli unataka kushinda basi hakikisha Fanton anakuwa kaburini, tofauti na hapo futa mawazo ya ushindi.
Lakini pia fikiri kwa usahihi unawezaje kupambana na mtu ambae ni taasisi tayari? Mtu ambae anamiliki mpaka hapa tuliposimama, tazama haya mazingira na uone ni nguvu kiasi gani imetumika,pia usisahau kuwa anamiliki taasisi ya ujasusi.
Ana majasusi wengi kila kona ya nchi na baadhi wameajiriwa kwenye mfumo wa Serikali bila wewe kuwajua kama ni watu wake.”
Joel ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifahamu mambo mengi tu katika Taifa hili kulingana na nyadhifa alizowahi kuhudumu.
Maana alinzia Jeshini huko, ambako alihudumu mpaka kufikia cheo cha Ubrigedia Jenerali, baadae akahudumu katika wizara ya ulinzi.
Kisha akaja kuwa Kaimu mkurugenzi wa shirika la kijasusi la SIA (Songomo Intelligence Agency) ana historia kubwa sana nyuma yake ya kijasusi iliyotukuka. Maana alihudhuria vikao vingi katika mataifa mbali mbali, vilivyowakutanisha wakuu wa mashirika yote ya kijasusi Ulimwenguni na akajifunza mengi ikiwa ni pamoja na mbinu na mikakati mbalimbali.
Raisi alimtazama Joel kama mtu ambae alikuwa akihitaji msaada kutoka kwake, na hilo Joel alilitarajia tangu hapo mwanzo.
Kama aliyejikumbuka kuwa yeye ni Raisi wa Nchi, Mwibale Mwoha aliuvaa ujasiri na kumwambia Joel, “Ikiwa utanihakikishia ushindi katika mbinu zako, basi awamu ya pili hii nitakuteua kuwa Waziri mkuu. Na juu ya yote nitakuwekea kinga ya kiuchumi.”
Kama ujuavyo mpenzi msomaji, tamaa haijawahi kumuacha mtu salama, ndio maana unaweza kuwa na elimu kubwa mfano Degree nne, ninyi mnaita (PHD). Bado ukapewa majukumu ya kukuvua utu na mtu ambae kielimu yuko chini sana pengine theruthi kwako.
Ila, ajili ya pesa na madaraka, ukajikuta unasahau wewe ni nani na kujikuta unageuka kuwa kibaraka wake au Chawa kwa lugha ya leo.
Na mnayashuhudia sana haya huko nchini kwenu, tamaa imetamalaki kuliko utashi. Siwashawishi mchukue hatua, maana kwenye nchi zenu… It’s too dangerous for you to be right when your government is wrong . Turudi mchezoni.
Joel baada ya kusikia ahadi hii alihisi msisimko wa ajabu ghafla ukimvaa, akamwambia Raisi kuwa wako pamoja.
Akaanza kumpa mikakati kabambe, ambayo aliamini kwa uzoefu wake ushindi ulikuwa upo mlangoni.
Kisha alichukua simu na kuwapigia watu baadhi ambao aliamini wangefaa kutumiwa katika mikakati yake.
Ni mikakati ambayo ililenga kutekelezwa ndani ya siku tano tu ushindi uwe umepatikana,
Kabla ya kikao cha mwisho cha seneti.
Moja ya mbinu ilikuwa ni kuwamaliza baadhi ya wajumbe wa seneti, ambao walikuwa na ushawishi kwa wengine hivyo hao walikuwa ni mwiba.
Mbinu nyingine ilikuwa ni kufanya mashambulizi katika Masoko makubwa na Makanisa na misikiti iliyokusanya watu wengi.
Na vikundi hivi vilitakiwa kutumia jina la Junior Intelligence & Security Agency. Huku Raisi kupitia vyombo vya habari akilaani vikali matukio hayo ambayo wangeyapa jina la ugaidi.
Magaidi hao wangezua taharuki na kupelekea watu kuogopa kukusanyika hivyo ingepelekea hasara katika biashara mbali mbali za watu.
Na kitendo hiki kingeamsha hasira kwa wananchi juu ya Bwana Fanton Mahal ambapo baadhi ya wakurugenzi katika kampuni ya Gimonchy Group of Companies wangetaka aachie ngazi katika kampuni hiyo ambayo ndio mhimili mkuu wa uchumi wa Bwana Fanton mahal.
Baada ya kupanga mikakati yao waliondoka eneo hilo kwa gari la bwana Joel. Maana Raisi hakuwa na walinzi waliobaki baada ya baadhi kuuawa na waliobaki kukimbia ili kuzinusuru roho zao pengine kujipanga Zaidi maana kikosi cha Black Assassins hakikuwa cha kawaida na walikodiwa mashuhuri kwa ajili ya siku hii ni kama Bwana Fanton Mahal alijua kitakachoendelea kikaoni. kwa maana nyingine jamaa alikuwa hatua kumi zaidi mbele kuliko Raisi.
Raisi Mwibale Moha alipofika Ikulu alimpigia simu mkuu wa majeshi Gen.Floyd Balehl na kumwambia aandae vijana kutoka jeshini kwa ajili ya majukumu ambayo angemweleza pindi wakikutana na sehemu ya kukutanikia alipanga iwe nje ya jiji la Homa bay.
Walipanga wakutane jijini Cadmon, maana alihisi ingekuwa salama kulingana na kwamba mji huu kwanza una watu wachache. Pili umejengeka kiustadi sana kiasi cha kuwa na majumba makubwa mengi yaliyojengwa katika viwanja vikubwa.
Kiufupi huu mji haukuwa wa kibiashara, bali ni wa kiuwekezaji. Maana kila aina ya watu wa mataifa mbali mbali walipenda kufika katika huu mji mtulivu, maana haukuwa na heka heka nyingi kama Homa bay.
Baada ya mapumziko ya siku mbili, Raisi alichukua ndege binafsi iliyompeleka hadi mjini cadmon na kutua uwanja wa Jens Airport.
Aliteremka kwenye ndege akiwa amevaa casual, tisheti na Kaptula ya jeans na kofia ya bosholi kwa juu maarufu kama mzula, ungemwona usingehisi ni raisi wa nchi maana alionekana kama chekibobu Fulani lakini mwenye maisha yake.
Akiwa ndio amepiga hatua saba toka kwenye ngazi za ndege mara hatua kama sabini mbele aliweza kumuona Fanton Mahal akiwa anatembea kuondoka hapo uwanjani.
Jambo hili kidogo lilimvuruga akili yake, maana kuna maswali kadhaa yalipita kichwani mwake wakati huo akijiuliza hasa “Ni nini ujio wa huyu mtu ndani ya mji huu wa Cadmon?”
Akawaza aghairi huu mpango wake na amwambie General wakutane mji mwingine baada ya kuhisi uzabizabina kuwepo hapo mjini.
Lakini alihisi ni unyonge kwa namna moja ama nyingine maana ilitakiwa ajue pia Fanton ana mikakati gani katika mji huu wa Cadmon.
Hivyo aliagiza watu wake kumuwekea jicho kwa ukaribu mtu huyu.
Aliondoka hapo uwanjani na kuelekea ikulu ndogo iliyopo cadmon, rohoni kuna hisia zilikuwa zikimshawishi kuwa ndani ya PSU (Presidential Security Unity) kuna wasaliti wanaovujisha taarifa kwa kila analolipanga. Si ajabu akawa anafuatiliwa kwa ukaribu zaidi tofauti na anavyofikiri.
Alipokuwa amekaa peke yake ndani, alichukua simu na kumpigia Team Leader wa hiki kitengo na kumwambia anahitaji mabadiliko ya haraka sana kwa walinzi wote. Kuanzia Ikulu na wale anaotembea nao mara nyingi maana pia replacement ilitakiwa ifanyike kwa umakini baada ya baadhi kuuawa na wengine kufutwa kazi kutokana na lile tukio lililotokea pale Shatoto complex.
Hivyo baadhi pia walikuwa wakishikiliwa chini ya ulinzi mkali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Vijana waliokuwa wamekuja na raisi jijini Cadmon wakiwa kwenye majukumu yao ya ulinzi, wakiwa wamekaba section kikamilifu, walishangaa inaingia gari ikiwa na Team Leader.
Muda huo huo wakawekwa chini ya ulinzi na kunyang’anywa vifaa vyao vya kazi mpaka vitambulisho na kupakiwa kwenye gari tatu zilzofika hapo ikulu ndogo, na gari hizo zikashika kasi kuelekea kusikojulikana.
Section walikaba maafisa wengine wapya kabisa wakiwa wameweka sura za kazi au wa’meee!! Kama wasemavyo vijana wa leo.
Saa tatu usiku Raisi alimpigia General ili kumpa maagizo ni sehemu gani wakutane kwa mazungumzo, walikubaliana eneo liwe ni The Blue Grand Lodge.
Baada ya dakika arobaini na tano, Raisi alitoka Ikulu ndogo Cadmon na kuelekea kwenye hotel hiyo akiwa na ulinzi wake mdogo tu.
Ambapo baada ya kufika tu, alielekea eneo la upper-class. Ni mahususi kwa ajili ya watu wazito tu au vibopa.
Na hotel hii ni ya aina yake kwa namna ilivyojengwa maana kwa sasa ilikuwa na miaka takribani 120, tangu kujengwa kwake lakini ilikuwa imezipita hotel nyingi za kisasa kwa ubora na muundo wa kiusanifu. Hapa ndipo pia waliapishwa wanachama wote wa kile chama cha siri cha waashi huru.
Nembo ya jicho ilikuwa iking’ara vyema juu kabisa ya mnara wa hii hoteli, kitu ambacho pia kilikuwa kikiongeza mvuto kwa namna ilivyosanifiwa. Na ilijengwa na waashi huru wenyewe wala si kificho, nafikiri mnazifahamu kazi za hawa watu vizuri, hawabahatishi katika jambo lolote.
Baada ya kuingia eneo la upper-class alimkuta General alikwishakuwasili muda tu, akiwa ameketi huku kwa mbali walinzi wake wakionekana kuimarisha ulinzi.
Hivyo baada ya Raisi kuwasili ulinzi uliongezeka maradufu mpaka vichochoroni watu walikuwa wamekaba section, huku wakiwa na nguo za kiraia hakukuwa na sare ya jeshi hata moja, na hii ni ili kutovuta attention za watu.
General alisimama ambapo walisalimiana kwa General kusimama kikakamavu mbele ya Raisi kama ishara ya heshima kubwa kwa Bosi wake na kisha kumpatia mkono wa kulia na wote wakaketi ili kuanza mazungumzo yao.
Raisi: Habari ya majukumu ndugu rafiki yangu ?
General: Salama tu bosi wangu, sijajua upande wako .
Raisi: Ni salama kiasi chake,kwanza awali ya yote nikuulize, vipi zile nyaraka za mikataba ya LOBENG zipo sehemu salama? Na uliihifadhi wapi?
General: Ipo salama ondoa wasi wasi maana……)
Hakumalizia sentensi yake mara simu yake ikaanza kuita, akaomba udhuru kwa Bosi wake na kuipokea haraka kijeshi, akaiweka sikioni.
Kadri muda ulivyokuwa ukisonga, ndivyo sura yake ilizidi kudhihirisha kuwa taarifa aliyokuwa anapatiwa haikuwa njema kabisa kwake.
Taratibu alianza kunyong’onyea huku sura yake ikzidisha mashaka na unyonge, hatimaye akaitua simu mezani huku hamu ya kuendelea kutoa maelezo juu ya swali la Raisi ikipotea kinywani mwake maana alihisi kuchanganyikiwa.
Taarifa aliyopokea ilimvuruga sio kidogo na hii ni baada ya kupewa taarifa kuwa nyumbani kwake kumevamiwa na walinzi wake wote wameuawa kinyama sana, Na familia yake imetekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana.
Alipagawa sana akawa kama bubu kwa muda, huku wakati huu Raisi alitaka kujua ni nini kinachoendelea juu ya ile simu na vipi kuhusu zile nyaraka za LOBENG.
Lakini jibu alilolipata baada ya maelezo ya General alibaki ameduwaa, akijiuliza vipi kama zile nyaraka zikifika mikononi mwa maadui zake?, jibu ni kwamba watakuwa wanakaribia kwenye zone ya ushindi, maana mikataba iliyokuwa mle ilikuwa ni ya aibu mno na haikutakiwa kuwafikia wana Songomo kwa gharama yoyote ile.
Raisi Mwibale moha akiwa anaendelea kutafakari nae simu yake iliita, akaitazama kwa haraka iliyosindikizwa na presha ndani yake.
Kutazama anaempigia akaona ni Team Leader wa PSU, akaipokea na kupewa taarifa ambayo sasa ndio ilimuondolea matumaini aliyokuwa amebakia nayo.
Sasa ilikuwa ni zamu yake kutaabika huku simu ikiwa sikioni.
Hakuamini alichokuwa anaambiwa, hadi akajisahau na kuropoka kwa nguvu “Hivi unayoniambia ni kweli kuwa Joel Nogeri ameuawa? Kauawa na nani na katika mazingira yapi?”
Taarifa kutoka kwa Team Leader ilieleza kuwa, “Joel aliuawa kwa kupigwa sindano ya sumu, lakini hii ni baada ya kushambuliwa kwa silaha za mikono kutokana na alama zilizoweza kubainika mwilini mwake.
Inaonekana muuaji alitumia mapigo mazito sana, sehemu za shingo kwenye koromeo, kwenye uti wa mgongo na ubavu wa chini kabisa wa kulia.
Ambapo bila shaka kwa muuaji wa kiwango cha juu alidhamiria kuudhuru mfumo wa neva, mfumo wa upumuaji na ini, ili mwili uwe dhaifu na ushindwe kukabiliana na sumu ambayo ililengwa kuzamishwa mwilini baada ya hapo. Na hivyo kulifanya zoezi hilo kuwa la ufanisi mkubwa.
Ni muuaji anaejua ni nini anafanya, na pia vijana tuliowaagiza kumfuatilia Fanton Mahal wote wameuawa na miili yao imeachwa ikiwa na majeraha ya ndani kama yaliyokutwa katika mwili wa Joel Nogeri .” hayo yalikuwa maelezo ya Team Leader.
Raisi Mwibale Moha alichanganyikiwa na akamuamuru General aandae mashambulizi kupitia ndege za kivita zenye sura ya Fanton Mahal wazi wazi.
Maana vita tayari imeanza na vijana kutoka vikosi vya vilipuzi na mabomu walitakiwa kuanza kushambulia maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi. Na wanajeshi wanatakiwa kusambazwa kila sehemu ili kuhakikisha Fanton Mahal na washirika wake wanakamatwa na kuuawa
Agizo hili lilitekelezwa mara moja kwa njia ya simu tu, wakiwa hapo mara kilipita kipepeo kikubwa cha kutengenezwa, kwa ajili ya kupeleka taarifa. Maarufu kama drone. Kutokana na hofu ya kushambuliwa, walikipiga risasi kile kipepeo na ndani yake kulidondoka flash ndogo.
Ambapo baada ya kuichomeka kwenye tarakishi waliweza tu kusikia sauti ya Fanton Mahal ikimuonya Raisi kuwa “Stop everything and give-up. One step ahead then LOBENG is to be published. Your words our actions”
Ikimaanisha kuwa Raisi anatakiwa aache yote anayoyafikiria, na hatua yoyote ile itasababisha nyaraka za LOBENG kuwekwa hadharani mbele ya Uma. Na matendo yao yatafuatana na maagizo kutoka kwa Raisi.
Raisi aliona aondoke sahemu hii maana alihisi usalama wake ni mdogo sana,lakini hakuwa na nia ya kusitisha mashambulizi juu ya watu wa Songomo.
Maana aliamini kupitia mashambulizi hayo angefanikiwa kwa kiasi Fulani kuichafua taswira ya Fanton Mahali.
Hivyo kumpunguza nguvu kiuchumi na kuivuruga mikakati yake, kitu ambacho Raisi hakujua,
Ni kwamba Fanton Mahal na wenzake wamejikita na kuweka nguvu nyingi kwenye silaha na mbinu za maangamizi, kuanzia teknolojia, ikimaanisha vifaa vya kijasusi na silaha za kibaiolojia.
Na mbaya zaidi ni kwamba Arsenal yao ilikuwa ndani ya Manuari moja kubwa sana ya kivita.
Ambayo ilikuwa imekita kitako chini kwenye kina kirefu sana cha bahari kwenye maji huru (International water). Huku juu duniani kulikuwa na doria za vikosi vya askari wenye silaha nzito za kivita.Wakiwa na sare nyeusi zenye jina la JISA (Junior Intelligence & Security Agencies),huku wakitumia boti zenye Nembo ya Fuvu linalovuja damu sehemu za macho.
Unaambiwa hiyo ndiyo manuari kubwa na ya kisasa kuwahi kuwapo katika hiyo bahari ya Blue Ocean.
Raisi Mwibale Moha kwake roho za halaiki kuteketea haikuwa ajabu, maadam jambo lake litimie tu apate ushindi wa kiti chake.
Kwa ajili ya ufalme alikuwa tayari kumwaga damu za mamilioni ya watu bila huruma yoyote. Hii ilkuwa ni nguvu ya tamaa juu ya madaraka, lakini nyuma ya pazia inaonekana kuna kitu kilikuwa kikimsukuma kuhakikisha anashinda duru hii ya uchaguzi. Na haya yote yalikuwemo kwenye zile nyaraka za LOBENG.
Baada ya kufika Ikulu aliwasiliana na waziri mwenye mamlaka na Tasnia ya habari, na kumpa maelekezo juu ya nini kinatakiwa kufanyika kupitia vyombo vya habari. Ambapo ilitakiwa habari nyingi zifanyiwe Deceiving-manipulation ili kuwalaghai wananchi.
Huu mpango ulikusudia kupeleka picha kwa wananchi ikionesha kuwa Raisi amekuwa akihujumiwa sana utawala wake na watu wasiolitakia mema Taifa la Songomo, ambao wanawatumia baadhi ya vibaraka waliopo nchini kwa manufaa yao na kiongozi wa vibaraka hao kuonekana kuwa ni Fanton Mahal.
Songomo ilikuwa imefanikiwa kupata Raisi ambae alikuwa ni mchafu wa fikra na mwovu sana nafsini, huku akiwa anaitumia vyema Victim-card kuvuna huruma kwa wananchi wakati huo yeye akionekana mwema. lakini ni watu wachache sana na wa juu ndio waliijua michezo yake michafu na sasa wakiwa wanahitaji kumuondoa madarakani lakini yeye akiwa anang’ang’ania madaraka.
Baada ya hapo aliwasha tarakishi yake mpakato ili kupitia ripoti kutoka kwa wakurugenzi wake.
Kulingana na hali ilvyokuwa, aliona aanze na ripoti kutoka kwa jasusi mkuu wa SIA, Bwana Martin Kasoka.
Ripoti ya Martin haikuwa na mengi mapya zaidi ya aliyokwisha kuyasikia, ila kilichomshangaza kidogo ni taarifa zilizomuhusisha Fanton Mahal na kundi la Mabaduni wa serikali.
Japo hakuwa na uhakika nazo sana maana ni watu wachache sana waliokuwa wakijua kuhusu kosi hili la damu na hakujua hasa majukumu yao na malengo yao ni yapi ila alimsisitiza sana Bwn. Martin Kasoka ahakikishe analeta mezani taarifa zote zinazohusiana na Mabaduni wa Serikali.
Alitaka ajue historia ya kundi hilo kuanzia kuanzishwa kwake, mahusiano yake na mashirika mengine ya kijasusi Duniani, muunganiko wake na serikali tangu hapo awali mpaka kufikia kuwekewa neno milikishi “ Wa” serikali.
Kuna muda alihisi kwamba pengine kuwa Raisi wa nchi pekee hakutoshi kukupa mamlaka yote juu ya nchi tofauti na alivyodhani kabla hajawa Raisi.
Maana mwanzo alidhani kuwa Raisi ni kuwa mtu mwenye kauli ya mwisho juu ya jambo lolote lile.
Bwana Martin Kasoka aliahidi kuwasilisha ripoti iliyokamilika kuhusiana na Mabaduni wa Serikali kwa Raisi ndani ya siku mbili.
* ** *****
General baada ya kupata taarifa ya kuvamiwa kwa makazi yake na familia yake kutekwa nyara hakuwa na utulivu kabisa, kwanza aliona ni dharau kubwa na tusi baya kwake akiwa kama kiongozi wa juu kabisa wa Taasisi hii ya ulinzi na usalama.
Alipata hasira sana na aliamua kurudi jijini Homa bay muda huo huo ili kuongoza operesheni aliyoitaka iwe ya kibabe sana kuwahi kutokea Nchini Songomo.
Aliwasiliana na wakuu wote wa idara za jeshi ili kuwapa taarifa maafisa wote wa kijeshi kwa nafasi zao ili zoezi lianze mapema sana kabla hakujapambazuka ikiwa ni State of Emergency.
Kisha yeye angebaki kuongoza mapambano akiwa na maafisa wachache wa juu kabisa na vikosi vya makomando walioiva haswa kimkakati na kimapambano.
Mkuu wa kitengo cha ujasusi jeshin (Military Intelligence Unity) Bwana Kau Kamale ni miongoni mwa Mabaduni wa Serikali.
Huyu ni kiumbe mwingine ambae nae ni homa ya Dunia, kwanza ni mbobevu wa masuala ya Teknolojia ya Habari na mawasilano TEHAMA.
Ana shahada ya uzamili ya masuala ya ujasusi, ni mtu mtulivu na mwenye tahadhari kubwa linapokuja suala la kutekeleza kutuma taarifa fiche.
Akiwa amepandikiza watu karibia idara zote za jeshi ili kufanya kazi yake kuwa rahisi huyu ndiye aliyehusika na ukusanyaji wa taarifa mkakati kutoka Jeshini na taasisi nyingine za kijasusi na zisizo za kijasusi na kuwapatia Mabaduni wenzake.
Akiwa amejenga ukaribu na ujamaa na wakuu wa Idara zote nchini Songomo, hivyo hii kufanya kazi ya kupandikiza watu wake kuwa rahisi sana.
Taarifa ziliweza kumfikia kuwa General na Raisi wanapanga kusambaratisha kikosi chote cha Mabaduni wa serikali na wana nia ya kuumiza watu wengi kwa wakati mmoja.
Movement Order iliweza kunaswa na kutumwa kwa Mabaduni wa serikali kupitia kwa vijana wa Kau Kamale.
Na hapo ndipo Fanton Mahal aliweza kuwaita Mabaduni wote kwa pamoja ili kugawana majukumu kikamilifu.
Walikutana miamba yote Saba. Kwenye “Arsenal” yao ndani ya meli la kivita(manuwari ) la ajabu ubavuni kulia likiwa na maandishi yaliyosomeka The Seven Old Guards. Wakiwa wanatumia nembo kubwa ya Fuvu linalovuja damu kwenye vishimo vya macho.
Baada ya kupeana mikakati yote, wote walifanya ibada kwa mujibu wa taratibu za imani yao tangu hapo kale. Ikiwa ni lazima kula kiapo cha kukamilisha kazi hata kama ingegharimu mpaka tone la mwisho la damu la Baduni wa mwisho.
Waliamini wao ndio watetezi na sauti ya watu wanyonge wengi ambao hawawezi kutoa kauli kutokatana na vitisho kutoka kwa watawala waliolewa madaraka na kujisahau.
Kwa ufupi hawa ndio walikuwa walinzi wa katiba na Taifa kwa ujumla japo kwa siri sana. Hahahaaa!! Ogopa sana.
Wakati Raisi na General wake wakiwa wanasubiri kuanza mashambulizi pale itakapofika saa tisa za usiku, Mabaduni wao walikuwa wamepanga kabla haijafika saa saba Raisi na General wanatakiwa wawe wameshatekwa ama kuuawa.
Watu waliotumwa kushambulia maeneo mbali mbali ya raia wasio na hatia, wao wanatakiwa waione sura halisi ya mauti.
Baada ya hapo Mabaduni wote walisambaa kila mtu na uelekeo wake.
** *** *****
Saa 00:00 usiku ilimkuta General akiwa ofisini kwake Makao makuu ya jeshi alikuwa mara akae kwenye kiti na kupekua baadhi ya makabrasha mara anyanyue simu ya ofisi apige na kutoa maelekezo mara apokee simu yake binafsi kifupi alikuwa katingwa sana na kazi.
Na tarakishi mpakato na makabrasha mengi yaliyokuwa yamezagaa mezani bila mpangilio ndivyo vilithibitisha hilo.
Alikuwa amevaa sare ya kazi suti ya kijani, hakika alikuwa amependezea vazi hili lililochafuka nyota za kutosha na bendera za nchi mbalimbali alizowahi kuzuru kioperesheni na mafunzo.
Wakati akiwa hapa ofisini, mara aliingia mtu ndani ya hii ofisi akiwa hana haraka, naye akiwa amevaa sare za Jeshi kama General.
Alipomkaribia kama mita tano alisimama kikamavu na kutoa salute ambapo General nae aliitikia papo hapo kwa salute huku akijaribu kumuangalia kwa umakini mtu huyu maana sura yake haikuonekana vyema kutokana na kofia ya kijeshi aliyovaa.
Huyu si mwingine bali ni Jiga Kinamba, muda huu hakuwa na ile sura ya Seif tena.
Wakati General akiwa bado kamkazia macho kwa umakini ili aweze kumtambua mtu huyu vyema, hapo ndipo mtu huyu alitoa kofia kichwan na kumfanya General aweze kumuona vizuri
Jiga Kinamba!!! General alihamaki, hakutarajia kumuona mtu huyu mahali hapa tena akiwa amevaa sare yenye Insignia ya Lieutenant General.
General aliupeleka mkono wake kiunoni kuchomoa bastola yake mara baada ya kutambua kuwa mbele yake yupo malaika wa mauti, alikuwa amechelewa kwani kasi yake haingetosha kumuokoa kutoka kwa huyu mtu, maana pale pale alikwisha kufikiwa na kushikwa mkono ule kwa nguvu kisha alipigwa shingoni upande wa kulia kwa konzi kama ya wakoma ambapo vidole hukunjwa nusu, semi-claw .
Pigo hili lilimlegeza sana, konzi nyingine ilipigwa kwenye uti wa mgongo usawa wa mabega, kisha ngumi nzito ilitua kifuani upande wa kushoto na kusababisha madhara makubwa kwenye moyo kisha alipigwa konzi nyingine ya tatu, hii ilikuwa mbaya zaidi maana ilipigwa kwenye koromeo sehemu maarufu kwa jina la Cervical Spine
Kwa mapigo haya manne General alikuwa ameanza kuona giza mbele yake na kutema damu ingawa bado hakuwa ameanguka kutokana na kushikiliwa vyema lakini hakuwa na uwezo hata wa kukimbia achilia mbali kujitetea.
Akiwa hoi bin taabani, mara alishikwa kwa nyuma kati kati ya shingo na mabega kushoto na kulia na kwa kasi ya ajabu Jiga kinamba alijiinua kwa kumfanya General kama ngazi alivyomshikilia, kisha miguu ilienda hewani na kwa nguvu aliweza kuvunja vioo vya dirisha kwa miguu yote wakati huo huo akichomoka na General mikononi mwake kuelekea nje ya ofisi hii ambayo ilikuwa floor ya tano kutoka chini.
General akiwa haamini kitendo kile mara alihisi kuachiwa akiwa angani ni kama alikuwa anatelekezwa akajibamize chini afe. lakini ile anakaribia kutua chini alitua kwenye bega la mtu ambae alipita nae kama kipanga tena kwa kumdaka kwa kutumia bega moja na kwenda kumtua chini taratibu mita ishirini mbele.
Na hapo sasa ndipo General aliishuhudia sura ya mtu aliemdaka ambae ni Malone na wakati huu Jiga Kinamba hakuwa mbali alikwisha kutua muda mrefu na sasa alikuwa akijongea taratibu kuwafuata pale walipo General na Malone.
Alipofika alisimama kwenye mstari sambamba na Malone.
General hajawahi kuona uwezo wa aina hii yeye mwenyewe aliwakubali na alikiri kuwa uwezo wa hawa viumbe ulikuwa wa tofauti sana hajawahi kuona sehemu yoyote ile maana hata baada ya kutazama huku na huko alichokishuhudia ni miili mingi tu ya wanajeshi waliopoteza roho baada ya ujio wa hawa watu.
Hakuwa na uwezo wa kusimama lakini alilazimika kupiga magoti huku akiwa kajikunja kisha alinyanyua mkono wa kulia na kutoa saluti japo ya kichovu lakini ilionekana ishara ya wazi ni kutoa heshima kuu kwa hawa miamba kifupi aliwakubali sana.
Kisha alijilaza chini mavubini akiwa hoi sana.
Mabaduni hawakuwa na muda wa kupoteza Malone alimuweka General begani na wakaondoka nae kwenda kwenye gari ambalo ndani yake kwenye usukani alikuwa kaketi Macka Shinea mtu mmoja mbaya sana linapokuja suala la mbio za magari Huyu nae ni Baduni wa Serikali pia hivyo tunafikisha idadi ya Mabaduni watano ambao tushawatambua mpaka sasa wakiwa wamesalia wawili tu ambao tutawaona huko mbeleni.
Baada ya Malone na Jiga Kinamba kuingia kwenye gari, gari ilitekenywa ikatii amri ikatolewa kwa kasi eneo hilo la kambi na kuwafanya baadhi ya maaskari waliokuwa wakipiga doria katika kambi hii kujiuliza kulikoni? hawakujua kuwa Mkubwa wao alikuwa anaondolewa kambini humo bila wao kujua.
Wakati huu Fanton Mahal na mabaduni wenzake watatu walikuwa wakifanya mauaji yaliyojaa ushetani kwa vikosi vya wanajeshi waliotumwa kulipua na kufanya mauaji kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Wanajeshi wale watiifu kwa Raisi waliangamizwa wote hakuna hata mmoja ambae alipata nafasi ya kutoroka. Maana wengi walitangwa njiani na kuuawa kwa hewa ya sumu.
Waliokuwa wameshafanikiwa kupenya nakujichanganya na raia walikutana na mashambulio ya silaha za kale kama kisu cha uvuvio wa kishetani wa kale. Ni kisu kilichokata mpaka mifupa, kikiwa kimetengenezwa kwa madini adimu kutoka sayari ya mbali.
Uwezo wa visu hivi ulikuwa wa maajabu sana, maana vilitoa mwanga wa kuvutia sana. Wenye rangi nne ndani yake yaan bluu, njano, kijani na nyekundu. Na vilikata huku vikiacha jeraha la kuungua kama unaunguzwa kwa moto wa gesi.
Platoon nyingi ziliangamizwa kinyama maana makamanda wenye vyeo vya lieutenant colonel na Colonel hawakufua dafu kwa kwa hii miamba japo ilikuwa minne tu, lakini ilisababisha anguko lenye kishindo kikuu. Na ilikuwa ikishambulia kwa kuhama na chopa za kivita kutoka mji mmoja hadi mwingine kulingana na movement-Order ilivyokuwa inaonesha.
Na wao walijua sehemu zilizokusudiwa hivyo waliweza kudhibiti vikosi hivi kwa weredi mkubwa bila kusababisha madhara kwa raia wa kawaida ambao wengi walijifungia ndani mwao mara baada ya taarifa kuenea kuhusu kuwepo kwa vita ya ndani.
Vikosi vya maaskari jeshi vilizidi kumiminika kuelekea mjini Cadmon baada ya kupata taarifa kuwa general ametekwa na yuko njiani kupelekwa Mji wa Lobeng ambao njia yake inapitia mjini Cadmon hivyo walihisi anaefuatwa ni Raisi ambae alikuwa Cadmon.
Hivyo chopa za kivita zenye bendera ya nchi zilitanda angani ili kuweza kutoa msaada wa uokozi maana wasingeweza kushambulia ile gari iliyokuwa ikitoka kasi sana, maana ndani alikuwemo general hivyo walikuwa wakitafuta namna ya kuifanyia mbinu ya kijeshi ya Engulfing.
Chopa zikiwa takribani ishirini angani zilitengeneza picha ambayo kama isingekuwa hatari kwa maisha ya watu, basi ingependeza kuitazama. Maana ilileta msisimko fulan wa kibabe sana kwa wale wapenda vitu vya kibabe.
Chopa hizi zikiwa zinaendelea kufanya surveillance angani, mara kwa mbele lilitokea chopa moja kubwa jeusi likiwa umbali wa kama mita miatano. likaanza kuachia mionzi mikali kuzielekea hizi chopa na hapo ndipo kamanda alitoa amri ya ku-back off baada ya kugundua mashambulizi ya Lasser System lakini mpaka wanaondoka Combat zone tayari chopa kumi na mbili zilikwishakuteketezwa na kusalia nane ambazo ziliondoka eneo la mapigano.
Lieutenant General Salem Badro baada ya kukaimu majukumu ya Mkubwa wake akiwa kama Chief Commander aliamua ku-back off mapigano kwa Battalions zote kwanza ili atafute mbinu sahihi ya kupambana na hawa Mabaduni wa Serikali.
Maana kuna baadhi ya silaha hakutegemea kuziona zikitumiwa na hawa miamba, lakini aliziona na kujiuliza wamezitoa wapi na ni vipi ziliingizwa bila kikosi cha kupambana na kuzuia silaha za maangamizi kuwa na taarifa.
Alihisi kuna uwalakini katika Kitengo cha Ujasusi jeshini hasa katika kutekeleza majukumu yao kwa namna moja ama nyingine alihisi kuna mtu mzito ndani ya kitengo ambae anazuia watu kutoa taarifa nyeti kama hizi.
Ni kweli hisia zake hazikuwa mbali na ukweli maana hii pia ilikuwa ni kazi ya Kau Kamale Chief of Military Intelligence.The C.M.I himself.
** **** *****
Jiga kinamba akiwa na Malone na Macka Shinea walifika Ikulu ndogo Cadmon, getini hawakupata kipingamizi chochote tofauti na walivyotarajia.
Hii iliwapa mashaka, lakini walikausha. Baada ya geti kufunguliwa wakazama na kuifuata barabara, wakizidi kuchanja safari kulifuata kasri la ikulu.
Mashaka yakiwa rohoni, pia wakiwa tayari kwa lolote maana uwezo wa Baduni mmoja ni sawa na makomando wa jeshi walioiva haswa zaidi ya mia tatu.
Miamba ina uwezo mkubwa sio uongo, na ukisikia uwezo, sio huo uliotoka nao mafunzoni unakuja kutishia raia wa kawaida mtaani.
Huu ni uwezo wa ajabu wa kivita, uliochanganyikana na nguvu za kishetani ndani yake maarufu kama Cultivation skills.
Miamba ilifika mpaka geti la mwisho, nalo likafunguliwa bila hiyana, wakazama ndani. Wakati huu General akiwa amewekwa kati kati akiwa hajitambui kutokana na sindano ya usingizi aliyochomwa ili asilete usumbufu safarini.
Baada ya kupaki walishuka, Jiga Kinamba na Malone.
Wakimuacha Macka Shinea na General kwenye gari wote wakiwa wamepiga sare za jeshi. Walizunguka kasri hili la Ikulu kwa tahadhari juu ya hatari iliyojificha. Na walikuwa wakipishana na wanajeshi waliokuwa wakilinda eneo hili na walichoishia kukiona ni saluti tu walizokuwa wakipewa kila walipokatiza.
Hatimaye walifika kwenye bustani moja nzuri sana iliyopo hapo, ambapo kwa walichokiona ndicho kiliwaacha hoi na kugundua ni kwanini njia nzima hawakuwa wakikaguliwa, huku wakiwa wanaachwa waende tu mithili ya mbwa anaejipeleka mwenyewe katika mdomo wa chatu.
Walichokiona kilimfanya mpaka Malone amtazame Jiga Kinamba usoni, lakini haikuwazuia kusonga mbele kuelekea pale bustanini.
Je nini kitaendelea? Na ni nini Jiga Kinamba na Malone walichokiona? Na pia eneo hili lile lina usalama kwao kwa kiasi gani? Na ni nini hatma ya General na Raisi? Kuyajua yote haya tukutane sehemu ya nne inayofuata. Wenu katika utunzi Sonko Bibo.