RIWAYA; MTOTO WA RAIS
HALFANI SUDY
0652 212391
Sehemu ya Ishirini na Tatu
Wakati Martin, Daniel, Amini, Amani na Karimu walitoka nje. Safari ya kuelekea Masaki nyumbani kwa Joash Mtoto ilianza. Walitoka na gari mbili, ya mbele ilikuwa imepandwa na Daniel Mwaseba, Martin na Karim. Wakati nyuma walifuatiwa na wakina Amini.
Kutokana na foleni waliyokutana nayo barabarani iliwachukua wakina Daniel saa zima kufika Masaki, nyumbani kwa Joash Mtoto. Wakiwa njiani mara kwa mara waliwasiliana na Hannan, na mara zote Hannan aliwaambia kuwa simu ya Aneth bado ilikuwa ndani ya nyumba namba hamsini na tisa, Masaki.
Walifika Masaki, walipaki gari mita chache nje ya nyumba ya Joash Mtoto. Na kama kawaida wakina Amini wao walipaki kwa mbali kidogo wakifatilia kila kitu.
"Timu ya wadunguaji wametuambia kila kitu kipo sawa. Sasa tunaenda kuingia katika hii nyumba, ambayo tunaamini Aneth yupo ndani yake. Umakini unahitajika kama ilivyo ada ya Mpelelezi yeyote yule duniani" Daniel aliwapa tahadhari.
"Tunaingiaje? Kwa kuvamia au kistaarabu?" Karim aliuliza.
"Tutaingia kistaarabu kwa kwenda kugonga geti. Mbinu itabadilika kutokana na tutakavyopokelewa huko ndani. Lengo la kwanza la misheni hii ni kumpata Aneth akiwa hai. Lengo la pili la misheni hii ni kumpata Aneth akiwa hai. Na lengo la tatu la misheni hii?" Daniel aliuliza.
"Ni kumpata Aneth akiwa hai" Martin na Karim walijibu kwa pamoja.
Walishikana mikono huku Daniel akigawa majukumu. Na misheni ilianza. Karim alibana upande wa kushoto wa geti. Daniel alibaki upande wa kulia, wakati Martin alienda kugonga geti. Kila mmoja alikuwa karibu sana na bastola yake. Hawakujua nini kitatokea katika sekunde inayofuata.
"Ngo ngo ngo" Martin aligonga geti kwa mkono wake wa kushoto.
"Ngo ngo ngo ngo" Aligonga tena kwa mara ya pili baada ya ile ya kwanza kupokelewa na ukimya. Lakini bado iliendelea kupokelewa na ukimya.
"Jaribu kusukuma geti" Daniel alisema kwa sauti ndogo iliyofikiwa na masikio ya Martin Hisia.
Martin akasukuma geti dogo. Geti likafunguka. Martin aliutumia upenyo huo kuchungulia ndani. Hakuona kitu chochote zaidi ya maua yaliyopangiliwa kwa mpangilio mzuri.
"Ingia ndani, kuwa makini sana Martin" Daniel alisema kwa kunong'oneza.
Martin alinyata taratibu, bastola ikiwa mbele. Aliingia mle ndani na kwa kasi alielekea katika kibanda cha mlinzi. Ilianza kufika bastola yake kibandani kabla ya yeye. Akiwa kibandani aliangalia mazingira yote ya mle ndani. Kulikuwa kimya kabisa, kimya, kimya, kimya.
"Mnaweza kuja kuko salama" Martin aliongea kwa kutumia vifaa walivyovaa masikioni. Wakina Daniel nao wakaingia ndani na bastola zao mikononi. Wote wakichukua tahadhari kubwa sana. Walielekea pale katika kibanda cha Mlinzi.
"Haujakuta mtu hapa?" Daniel aliuliza naye alipofika.
"Hapana, hakuna mtu" Martin alijibu.
"Yatupasa kwenda ndani. Bila shaka Aneth yupo ndani ya nyumba hii. Hannan kanitumia meseji kusisitiza bado simu yake ipo humuhumu ndani" Daniel alisema kwa uhakika.
"Sawa, tunaenda ndani kwa kulindana. Tuhakikishe hakuna anayefanya kosa lolote lile, kosa moja tu litaamua hatma ya mwengine" Martin alisema akitoa tahadhari.
Alianza Daniel Mwaseba, alijibiringisha kwa namna ya ajabu hadi mlangoni. Ilikuwa ni mithili ya tairi la gari likisukumwa na mtoto mdogo. Martin naye akafata kwa mtindo uleule, mwisho Karim alienda, lakini hakuweza kuwaiga wale wanaume wawili. Wakipekee. Yeye alitambaa kama nyoka wa kijani.
"Tunaingia ndani, umakini zaidi unahitajika. Nitapiga hodi, isipojibiwa tutaingia kwa namna yetu" Daniel alisema.
Alijaribu kupiga hodi. Lakini kulikuwa kimya. Akabisha tena hodi, bado kulikuwa kimya. Akajaribu kuufungua ule mlango. Ulikuwa umefungwa. Akatoa rundo la funguo mfukoni. Akajaribu funguo ya kwanza, ikakataa. Akajaribu ya pili, ikakataa, akajaribu funguo ya tatu, mlango uliitika. Mlango uliwachekea.
Daniel alitangulia kuingia ndani akifatiwa na Karim, kisha Martin. Wote bastola zilikuwa zimetangulia mbele ya vifua vyao. Walikuwa makini sana.
Pale sebuleni napo, hawakukuta mtu. Ila zaidi ilionesha sebule ilikuwa imetawanya vibaya sana. Wakajua kuwa kuna mtu asiyehusika alikuwepo pale kusaka kitu kisicho chake, ni nani huyo? Na alikuwa akisaka kitu gani?.
Wanaume walijigawa. Wakasonga mbele kila mmoja akipita upande wake. Walipekua kila chumba ndani ya nyumba ile, cha kushangaza mle ndani hakukuwa na mtu katika vyumba vyote vitano. Baada ya dakika nane wote walirejea tena sebuleni. Zaidi ya bastola zao mikononi, hawakuwa na Aneth wala Joash Mtoto...
"Lakini bado inaonesha simu ya Aneth ipo humu ndani" Daniel alisema akisisitiza.
"Tuitafuteni, pengine ipo sehemu fulani" Karim alishauri. Wakaingia kazini tena, wote wakaanza kuisaka simu ya Aneth katika kila chumba. Kila mmoja akitanguliza tahadhari na umakini kabla ya bastola yake.
Ni Karim ndiye aliyeikuta simu ya Aneth uvunguni mwa kitanda katika chumba cha tatu, upande wa kushoto. Ilikuwa rahisi kwake maana alipoingia tu chumbani, simu iliita. Na jina la mpigaji lilisomeka juu ya kioo cha simu.
'Kaka'
Kama walikuwa sahihi, basi Aneth alikuwa anapigiwa na kaka yake. Rais Mark alijaaliwa kupata watoto wawili katika uzao wake, wa kwanza alikuwa ni Moses na wa uzao wa pili ni Aneth. Kwa maana hiyo kaka wa Aneth ni Moses, je ndiye aliyekuwa anapiga simu?
Karim aliichukua ile simu hadi kwa wenzake.
"Simu ni hii hapa, lakini inaita" Karim alisema.
"Nani anapiga?" Daniel aliuliza.
"Jina limeandikwa Kaka" Karim alisema. Na simu iliacha kuita. Hapo ndipo Karim alipoangalia kwenye kioo. Kulikuwa na simu zilizopigwa bila kupokelewa thelathini na saba, na zote zilitoka kwa mtu mmoja tu 'Kaka'.
"Kuna kitu hakipo sawa" Daniel alisema.
"Unahisi Aneth ametekwa?" Martin aliuliza.
"Hilo ni jibu Martin. Sasa ni wakati wa kutafuta ni kina nani waliomteka? Na kwanini wamteke? Pia lazima tujiulize kwanini simu yake ije kutelekezwa nyumbani kwa Joash Mtoto?"
Wakiwa pale sebuleni, simu ya Daniel iliita.
Alikuwa ni Hannan.
"Daniel vipi mmempata Aneth?" Hannan aliuliza kwa pupa.
"Bado, vipi kuna taarifa zozote umezipata?" Daniel naye alitupa swali, huku hofu ikianza kumwandama moyoni mwake.
"Nimeona habari sasahivi mtandaoni. Kuna taarifa kuwa mwili wa Aneth umeokotwa katika ufukwe wa bahari ya Coco, inaonesha ameuwawa na kutupwa huko!"
"Aneth ameuwawa?" Daniel alistaajabu.
"Ndio, Daniel tokeni humo ndani kwa Joash Mtoto haraka sana, inawezekana ikawa ni mtego" Hannan alisema kwa sauti ya uwoga.
"Sawa Hannan, tunatoka na tunakuja nyumbani sasahivi kuongea vizuri" Daniel alisema.
Harakaharaka walitoka nje. Wakaingia kwenye gari. Wakawasiliana na kina Amini, kila kitu kilikuwa sawa. Mkuumkuu walirejea Tabata, kwenye makazi mapya ya Daniel Mwaseba.
***
Ilichukua dakika zipatazo sita tangu wakina Daniel waondoke nyumbani kwa Joash Mtoto. Gari tatu za Polisi na askari zaidi ya thelathini na tatu walifika pale nyumbani kwa Joash Mtoto. Mbele ya askari hao alikuwepo Moses, mtoto wa kiume wa Rais Mark. Moses akiambatana na askari walianza kuipekua ile nyumba ya Joash Mtoto.
Dakika kumi na mbili ziliwarejesha Polisi katika sebule ya Joash Mtoto. Hawakukiona walichokuwa wanakitafuta. Moses alitoa simu yake mfukoni na kupiga.
"Denis" Alianza kuongea mara tu simu ilipopokelewa. "Angalia tena mahali ilipo simu ya Aneth, tumefika katika nyumba namba hamsini na tisa lakini simu haipo"
Kilifata kimya. Moses akimsikiliza Denis,
"Unasema?" Moses alipayuka baada ya kusikiliza kwa muda.
Akasiliza tena.
Baada ya dakika mbili alijikuta akikaa chini bila kupenda. Kisha akasema kwa sauti ndogo.
"Simu imezimwa"
Itaendelea...