Rostam azua kizaazaa
Maelezo yake yaficha siri nzito
na Happiness Katabazi
Tanzania Daima~Sauti Ya Watu
MAELEZO binafsi ya maandishi ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz yanayolenga kutoa utetezi kuhusu kuhusishwa kwake katika sakata la mkataba wa kufua umeme wa dharura kati ya Kampuni ya Richmond na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), yanaonekana kuwashtua Spika wa Bunge, Samuel Sitta na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka Dodoma zinaeleza kuwa, Rostam aliwasilisha maelezo yake binafsi kwa Spika juzi jioni majira ya saa 12:30, saa chache baada ya kupewa maelekezo yaliyokuwa yakimtaka afanye hivyo, siku moja kabla hajapewa fursa ya kujibu Azimio la Bunge.
Hata hivyo pamoja na kukidhi maelekezo hayo ya kikanuni, Rostam alishindwa kutoa maelezo yake hayo binafsi bungeni jana kutokana na sababu ambazo hadi hivi sasa gazeti hili halijaweza kuzithibitisha.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya Bunge zinaeleza kuwa, maelezo hayo ya Rostam yanaonekana dhahiri kubeba ujumbe unaoweza kusababisha kutokea kwa mtikisiko mwingine ndani ya Bunge, baada ya ule wa Richmond ambao ulisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa mwanzoni mwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari hizo, uzito wa maelezo hayo ya Rostam ambayo kwa kiwango kikubwa yanaonekana kukilemea chama tawala, ulisababisha mapema jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alazimike kuitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi ya CCM muda mfupi baada ya Bunge kuahirishwa jana mchana.
Tanzania Daima ilipowasiliana na Rostam kuhusu maelezo yake binafsi jana, mbunge huyo hakuwa tayari kueleza lolote kwa undani zaidi ya kumtaka mwandishi kuwasiliana na ofisi za Bunge kwani yeye alikuwa ameshatekeleza maelekezo ya Spika.
"Nadhani mimi sina lolote la kusema la zaidi. Ninachoweza kukwambia ndugu yangu ni kwamba, niliwasilisha maelezo yangu ya maandishi kwa Spika jana jioni (Jumatano). Nasubiri kupangiwa muda wa kuyasema ndani ya Bunge kama nilivyoelekezwa katika mkutano uliopita wa Bunge. Watafuteni wahusika," alisema Rostam huku akikataa kutoa maelezo mengine yoyote ya ziada.
Tanzania Daima ilipowasiliana kwa simu na Spika Sitta jana mchana, alikiri kupokea maelezo ya mbunge huyo kwa maandishi juzi majira ya saa 12:00 jioni na akasema tayari alikuwa ameshaanza kuyafanyia kazi.
Alisema baada ya kukabidhiwa maelezo hayo, jana asubuhi aliyapeleka kwa washauri wake ambao ni maofisa wa Bunge ili waweze kuyachambua kitaalam na kisha kumpatia ushauri unaofaa, kabla ya kumruhusu Rostam kuwasilisha utetezi wake huo.
"Mimi ni Spika, nina washauri wangu, hivyo nimewakabidhi maelezo (ya Rostam) ili wayachambue kitaalam na wakimaliza watakuja kunishauri, na ushauri huo ndiyo utakaoniruhusu nimpangie tarehe ya kuwasilisha maelezo yake bungeni au la," alisema Spika Sitta.
Alipotakiwa kueleza iwapo kikao cha Kamati ya Uongozi cha CCM kilichoitishwa jana kinahusu maelezo hayo ya Rostam, Sitta alisema aliyekiitisha ni Waziri Mkuu na si yeye.
Pamoja na kukiri kuwa katika kikao hicho cha Kamati ya Uongozi ya CCM kilichoketi jana hiyo, suala hilo la Rostam lilikuwa moja ya mambo yaliyojadiliwa, Spika alisema kililenga kuzungumzia ajenda mbalimbali ambazo zimeibuka ndani ya Bunge hilo katika siku za karibuni.
Alipotakiwa kueleza nini kilikuwa kimejiri ndani ya kikao hicho kuhusu hatima ya maelezo binafsi ya Rostam, alisema yeye binafsi alishindwa kuhudhuria kwa kuwa, wakati kikifanyika alikuwa na ugeni wa Balozi wa Uingereza hapa nchini, aliyekwenda ofisini kwake kumuaga.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kwamba, hoja ya Rostam ilijadiliwa kwa zaidi ya saa moja, na kwamba baadhi ya wajumbe walifikia hatua ya kumtaka aiondoe, pendekezo ambalo hadi jana jioni mbunge huyo alikuwa amelikataa.
Mbunge mmoja wa CCM aliyezungumza na gazeti hili jana jioni ambaye alikiri kuyaona maelezo hayo binafsi ya Rostam, anasema kikubwa kinacholeta wasiwasi ni nini kinachoweza kutokea iwapo mbunge huyo wa Igunga ataruhusiwa kutoa utetezi wake bungeni.
"Mambo yamekuwa mazito, wakubwa wamejadili hoja hii kwa zaidi ya saa nzima. Tumeambiwa kuwa wamemtaka ayaondoe maelezo yake yanayoeleza mambo mengi mapya kuhusu Kamati Teule ya Richmond iliyoongozwa na Dk. (Harrison) Mwakyembe. Mimi nimeyasoma maelezo hayo ya Rostam, tunasubiri tuone nini kitatokea ingawa naamini ni mambo mazito," alisema mbunge huyo.
Alisema, katika maelezo yake hayo, Rostam anatarajia kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu namna Kamati ya Mwakyembe ilivyofanya kazi, kujiuzulu kwa Lowassa na mawaziri wengine wawili, na namna yeye mwenyewe alivyohusishwa katika sakata hilo.
Hali hii imefikia hapo baada ya juzi, Sitta kumzuia Rostam kuwasilisha maelezo yake binafsi bungeni akimtaka kwanza atimize masharti ya kanuni za Bunge yanayomtaka kuwasilisha kwake (Spika) hoja yake kabla hajaitoa bungeni.
"Nilimwambia haiwezekani akawasilishe maelezo yake kabla hajawasilisha kwa Spika kwa maandishi na nimemwelekeza arudi akayaandike maelezo yake, kisha ayawasilishe kwangu, angalau siku moja kabla, ndipo nitamruhusu asimame bungeni na kutoa maelezo yake.
"Baada ya kumwelekeza hivyo, Rostam alinielewa na akaniaidi kwamba atafanya kama nilivyomwelekeza, hivyo akileta kesho (jana Alhamisi) maelezo yake, basi kesho kutwa (leo) nitamruhusu ayatoe," alisema Sitta alipozungumza na gazeti hili juzi.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge Na.50 (1), mbunge yeyote anaweza kwa idhini ya Spika, kutoa maelezo binafsi bungeni yanayolenga kufafanua kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia jamii.
Hata hivyo kanuni hiyo ya 50 (2) inaonyesha dhahiri kutoa unafuu kwa mbunge mwenye maelezo binafsi, ambayo akishayatoa katika muda usiozidi dakika 15, basi hakutakuwa na mjadala kuhusu jambo hilo.
Uamuzi wa Rostam kutoa maelezo yake binafsi unatokana na Azimio la Bunge lililofikiwa baada ya ombi lililotolewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wenye utata wa Kampuni ya kufua umeme ya Richmond, iliyoingia na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), Dk. Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe alilazimika kutoa hoja ya kulitaka Bunge lidai maelezo binafsi kutoka kwa Rostam, baada ya mbunge huyo wa Igunga, ambaye jina lake lilitajwa katika ripoti ya kamati teule ya Bunge likimhusisha na mkataba huo wenye utata wa Richmond, kuipinga ripoti ya kamati teule.
Rostam katika mchango wake wa kujadili ripoti hiyo ya kamati teule, alikanusha kuhusika katika na kampuni hiyo, na akaeleza wasiwasi wake kwamba, kamati hiyo iliendelea kufanya kazi nje ya muda wake ambao ulimalizika Desemba 31, mwaka jana.
Maoni ya Wasomaji
hapo rostam apewe haki yake a kueleza anachotaka kusema,ili tumjue mchawi nani!!hapa kunasiki kubwa lazima,kuna mambo ya kuchafuana.rostam kama unajiamini ukinyimwa nafasi ya kujieleza ndani ya bunge waite waandishi wa habari ueleze kwa kina.watanzania wameamka watachambua na kujua ukweli uko wapi.
na john - 11.04.08 @ 12:51 | #6016
inashangaza kuona baada ya taarifa ya harrison kutoka ndo viongozi na wabunge waliohitajika kutoa maelezo yao kabla na wakakataa kutoa ushirikiano ndio walewale sasa hivi wanaanza domodomo! tumeshachoka na wasanii hawa, ukweli umewekwa wazi, taarifa ya harrisson itawekwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo kama mwanamapinduzi aliyekuwa tayari kufa kuipigania nchi yake kwa kueleza ukweli mbele ya matawala *******,thank
God!
na Elsaid barak, south afr., - 11.04.08 @ 13:08 | #6022
Hakuna lolote hawa watu wameamua kuifilisi nchi hii na hawana jipya. Watanzania tumeona pumba na mchele na tunamuomba mola wetu amlaze mahali pema peponi Mwalimu Nyerere. Alikuwa ni mtanzania wa kweli na kiongozi wa Watanzania. Hawa wengine ni akina kajamba nani. Hawana utu wala ubinadamu na watanzania wenzao. Watanzania tumechoka sana na hawa watu wanaoitwa viongozi kwani hawana cha uongozi wowote ni wahalifu wote kazi yao kupanga madili ya kuifilisi nchi na kuongeza umasikini Tanzania. Utasikia rais yuko China, mara London, Mara Japani n.k. Miaka yote wamekuwa wanasafiri nchi hizo hizo na hakuna jipya na wanatumia fedha nyingi za umma wacha hizo wanazojichotea kwa kupitia mikataba hewa, unafikiri kuna uongozi hapo. Yana mwisho.
na Aziz Said, Dar, - 11.04.08 @ 13:09 | #6024
Kaka Rostam kwa hili tunakuunga mkono. Tulijua wakati Lowassa anajiuzulu kulikuwa na ajenda zilizofichwa nyingi tu zikiwemo hata za makundi yaliyoshindwa urais kwenye kura za maoni za ccm 2005. Spika alikuwa mwepesi sana kuunda kamati teule na kushabikia ripoti yake.Iweje sasa Rostam azungushwe kupewa nafasi yake ya kidemokrasia tena akiwa tayari kufuata maelekezo ya azimio la kamati hiyo ya bunge? Kulikoni Spika uanze kumbana Rostam na kumchelewesha kama vile matokeo ya uchaguzi wa Urais wa Zimbabwe? We umekuwa Mugabe? Mnaogopa nini? Mkuki kwa nguruwe kwa binaadamu mchungu? Moto si mliuwasha nyie wenyewe? Mpeni nafasi Rostam wananchi tujue ukweli.