Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Kumekuwa na utata wa wasifu wa mwandishi wa habari mkongwe, Jenerali Ulimwengu, hasa baada ya kutakiw akuomba upya uraia, enzi za Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Jenerali Ulimwengu anasimulia safari yake tangu alipozaliwa wilayani Ngara mkoani Kagera hadi alipofika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye kuajiriwa kama mwandishi wa habari.
Swali: Naomba kujua historia yako tangu umezaliwa na shule ulizosoma.
Jibu: Mimi nilizaliwa wilayani Ngara (Kagera), tulizaliwa wawili, mimi na dada yangu. Ni kweli wazazi wetu wana asili ya Rwanda.
Swali: Baada ya hapo ulisoma wapi?
Jibu: Nilipofikisha miaka sita baba alihamia Bukoba na hapo nilisoma Shule ya Msingi Katoke baadaye nikaenda shule ya Sekondari Nyakato hapo hapo Bukoba. Elimu ya juu ya sekondari nilikwenda Tabora Boys iliyoko Tabora baada ya hapo nikajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Swali: Kuhusu jina lako “Jenerali Ulimwengu, ni jina halisi au ulijipa kwa makusudi fulani?
Jibu: Ni jina langu halisi nililopewa na baba yangu.
Alikuwa msanii msanii, nilimsikia akieleza watu kwamba kulikuwa na Jenerali wa vita ya pili vya dunia, akiitwa Rommel (General Erwin Rommel), Mjerumani ambaye aliwachachafya sana Waingereza ndani ya Jangwa la Sahara, kwa hiyo baba akaamua mtoto wake wa kiume atampa jina la General.
Niliwahi pia kusikia mahali pengine akimwambia mtu, tena Dar es Salaam miaka ya 1980, kwamba alikuwa dereva na alikuwa gari akiendesha kati ya Tanganyika Magharibi, Burundi, Rwanda na Uganda, akibeba manamba wanaokwenda kwenye reli na mashamba.
Sasa anasema alikuwa na rafiki yake Kaskazini Mashariki ya Congo (DR) wakawa wanashindana juu ya magari wanayoendesha.
Yule bwana alikuwa na gari aina ya Ford akazaa mtoto akamwita Ford, yeye anaendesha gari inayotoka General Motors, kwa hiyo akaniita General.
Kuna siku nikamuuliza, nikusikia unamwambia mtu kuhusu general wa vita vya pili vya dunia na pengine nimesikia unasema General inatokana na gari, ipi ni sahihi? Akaniambia, “Unapenda ipi? Alikuwa msanii wa aina fulani.
Baada ya kuwa nimetoka chuoni, nafanya kazi Daily News, na Ochieng anataka kuniachia niandike kolamu yake, akasema lakini hili jina la General Ulimwengu haitaonekana vizuri kwenye kolamu.
Nikasema sasa itakuwaje? Akasema kwani mama yako anakuitaje? Nikasema kama Jenerali hivyo, akasema basi jina lako ni Jenerali.
Kwa hiyo aliyelifanya liwe Jenerali ni Philip Ochieng. Sasa cha ajabu ni kwamba wakati naandika kwenye gazeti Jenerali Ulimwengu, passport niliyonayo nilivyokweda kupewa nyingine, wala hakutaka karatasi wala nini, waliandika tu Jenerali na ikabaki hivyo hivyo.
Swali: Ulimwengu nalo ni jina la baba?
Jibu: Ni jina la babu, baba yake baba.
Swali: Ulipofika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ulichukua kozi ya sharia, kwa nini uliipenda kozi hii wakati ulikuwa unapenda uandishi wa habari?
Jibu: Nilikwenda kusoma sheria kwa sababu nilielekezwa, nilishauriwa na kaka zangu. Kwamba chochote ninachotaka kufanya maishani mwangu, alimradi niko katika mlango wa humanities, kinafaa.
Sija... sijasoma fizikia, kemia hisabati, ambayo hiyo ingenipeleka labda kuwa mhandisi au kitu kama hicho au daktari. Kama ni humanities (masomo ya Sanaa ya binadamu), kitu cha msingi ni kusoma sheria halafu nikishahitimu nitakuwa na wigo mpana sana wa kuchagua nini nataka kufanya.
Mimi nikasoma sheria lakini wakati wote nikiwa chuoni sikufikiria hata mara moja, labda mara mbalimbali ilikuwa inakuja akilini lakini sikuwa si jambo nililofikiria sana kwenda kufanya kazi ya uanasheria. Hususan kazi ambayo sikuipata kabisa na niliwaambia ndugu zangu na kaka zangu na dada zangu, ni kazi ya uhakimu.
Kwa sababu sikuona kama nina uwezo wa kufanya kazi ya kuhukumu binadamu, njia moja au nyingine kwa sababu niliona kama ni kazi nzito sana.
Kwa hiyo nikawa nasoma sheria lakini hata watu walionifahamu chuoni, muda wangu mkubwa sana sikutumia katika kusoma sheria. Nilikuwa kwenye mihadhara mingi tu ya chuo pale, nilishiriki katika masuala ya kisiasa ya chuo. Tulipopata mgogoro mwaka 1971 nilikuwa mmoja wa viongozi wa wanafunzi katika huo mgogoro.
Nilipotoka chuoni kwa kweli hata mimi nilikuwa najitathmini kwamba uanasheria wangu una shaka kidogo kwa sababu sikusoma sana sheria. Nikienda maktaba nilikuwa natafuta vitabu vya Niccolò Machiavelli na Rousseau na nini kuliko kusoma mabuku mazito ya sheria ya jurisprudence na vitu kama hivyo, ingawa nilisoma na nilipita vizuri tu.
Lakini nilikuwa ni mtu zaidi ninaegemea kufanya kazi ya kiuandishi wa habari. Na nilikuwa nimeonyesha uelekeo huo nikiwa chini kule katika middle school, secondary na high school ambako nilikuwa nikishughulika na gazeti la shule na wakati ule katika sekondari ya chini tulikuwa na gazeti la kutundika ukutani.
Swali: Wakati ukiwa UDSM, unamkumbuka mwalimu nani? Maana pale kulikuwa na walimu ambao ukiacha tu kufundisha sheria walikuwa ni kama wana mapinduzi.
Jibu: Ah nawakumbuka, Profesa Issa Shivji, alikuwepo wakati mimi nadhani namaliza... naingia chuo yeye alikuwa anagraduate kitu kama hicho. Na katika mwaka mmoja akawa ni mhadhiri msaidizi (tutorial assistant), wakati huo akisoa shahda ya uzamili na alinifundisha nakumbuka nadhani insurance law (sharia ya bima) na jurisprudence nadhani. Kitu kama hicho.
Wahadhiri wengine alikuwepo nawakumbuka (Profesa) Josephat Kanywanyi, alikuwepo mwalimu (Profesa) Mgongo Fimbo, alikuwepo mwalimu mmoja ambaye hakuishi sana baada ya hapo aliugua akafariki mapema sana, El-Kato. Alikuwepo Mmarekani akiitwa Robert Seidman, alikuwepo Andrew Lyall na wengine, Paliwala nadhani alikuwepo pale vilevile.
Lakini kwenye ndaki nyingine walikuwepo walimu ambao walikuwa na mvuto mkubwa sana kama Walter Rodney ambaye alikuwa idara ya historia nadhani. Na wengine wengi wengi wengi tu.
Kuingia Daily News
Swali: Baada ya kutoka chuoni, uliomba kazi wapi?
Jibu: Nilipotoka chuoni, wakati ule tulikuwa mnaitwa baada ya kuwa mmefanya mtihani, hamjapata majibu lakini mnapewa barua za ajira. Mnaitwa pale Nkrumah Hall, kila mtu mnaitwa nyote, mnaitwa mmoja baada ya mwingine mnakabidhiwa barua zenu.
Mimi nadhani kulikuwa na mwenzangu mmoja anaitwa Najum Kakasike, mwingine alikuwa anaitwa nani? Saleh Msuya nadhani. Tukaitwa na tukapewa barua zetu za kwenda Tanganyika Standard (TSN), mmiliki wa gazeti la Daily News.
Swali: Kwa hiyo walijua kama mapenzi yako yako ni uandishi mpaka kukupeleka huko?
Jibu: Tulikuwa tunaomba. Wakati ule kabla hamjamaliza chuo, mnajaza fomu.
Kwa msingi huo, na kwa kweli isipokuwa tu kwa watu wachache, kulikuwa na kategore ya watu ambao hawakupata walichoomba kwa sababu ilikuwepo sera wakati huo ya serikali ya kupeleka idadi kubwa ya wahitimu kwenye ualimu.
Kwa hiyo mimi nikaenda nikapelekwa Daily News na nikawa nafanya mafunzo kazini.
Sikuenda chuo cha uandishi maanake hatukuwa na chuo cha ngazi ya chuo kikuu, nadhani kwa cheti wakati huo kozi ilikuwa ikitolewa Nyegezi Mwanza. Lakini wakuu wangu pale Daily News wakaniambia hiyo unayofundishwa Nyegezi tutakufundisha hapa hapa.
Nikafanya hiyo kazi na nikaipenda. Nilikuwa nafurahi... naifurahia sana.
Swali: Ulifanya kazi Daily News kwa muda gani?
Jibu: Sikukaa sana. Niliingia mwaka 1973 nikaondolewa mwaka 1974.
Mimi na watu wengine wawili watatu hivi tuliondolewa kwa sababu tulionekana tunashindwa kufuata maelekezo na matakwa ya TANU."
Swali: Kivipi tena hapo? Yaani mlikuwa hamtaki maelekezo au?
Jibu: Yaani kwamba fikra zetu, mawazo tunayoandika, maanake mimi sikuwa ripota tu."
Nilipokuwa Daily News, baada ya mwaka mmoja na nusu hivi, kulikuwa na mtu alikuwa maarufu sana Dar es Salaam kwa kuandika weekly column, alikuwa ni mtu anaitwa Philip Ochieng' kutoka Kenya.
Alikuwa ni mtu mwenye fikra za kisiasa za mrengo wa kushoto sana. Akiwa anafafanua ujamaa wa kisayansi, Marxism na akipenda sana kusoma na ku nukuu vitu alivyoandika waandishi wa mrengo wa kushoto wa duniani kote na alikuwa amesoma Ufaransa masuala ya falsafa.
Amesoma akina Voltaire, akina Jean-Jacques Rousseau na wanafalsafa wa karne ya 18 wa... ya 19, wa Ufaransa na Ujerumani na kadhalika. Kwa hiyo tulikuwa tuna klabu ndogo hivi hapo Daily News ambacho kilikuwa ni kama habu ya watu ambao ni left-leaning wa Dar es Salaam nzima.
Ilikuwa tukikutana sana, yaani hata vikao vyetu vya bia vilikuwa ni vikao vya majadiliano, tukiazimana vitabu tukimbiana ni wapi kwenye maduka ya vitabu ya Dar es Salaam kuna kitabu kipya kimeingia.
Kwa hiyo tukaweza kusoma vitu vingi sana. Carlos Marighella wakati ule Mbrazili alikuwa ni leftist anajulikana duniani, tukisoma makala za Angela Davis wakati ule na mtifuano uliokuwepo Marekani kuhusu haki za kiraia na vitu kama hivyo.
Waandishi wengine waliokuwa Daily News, wazungu waliotoka nje ya Tanzania walikuwa ni sehemu ya grupu hilo.
Tukilinganisha na chuo kikuu na wakati mwingine hata shule za juu za sekodari, vijana waliokuwa kidato cha tano na sita kwa Dar es Salaam wakija pale Daily News kwa ajili ya majadiliano na kutokana na wigo mpana sana wa watu ambao wanabadilishana mawazo ambayo siyo lazima yapendwe sana na viongozi wa chama tawala.
Swali: Hiyo klabu ndio ilileta mzozo?
Jibu: Kulikuwa na misuguano kidogo na mara mbili tatu, walishawahi kutulalamikia kwamba nyinyi mnaandika mambo ambayo si sera ya TANU na kadhalika.
Sasa tukawaambia sisi siyo kazi yetu kuandika sera ya TANU, sisi tunaandika mawazo yetu. Kama tunapotosha habari tunazoandika hilo ni jambo lingine, tutawaambia kwamba tumepotosha tumeweka fakts ambazo siyo sawasawa, lakini hatuweki mawazo yetu ya kisiasa ndani ya stori.
Kwa hiyo, Philip Ochieng' ikabidi aondoke sasa, maanake alisakamwa sana na wakuu wa TANU na serikali, ikawa mimi ndio naandika badala yake.
Swali: Kwa hiyo uliendeleza ule ule msimamo wake?
Jibu: "Ah siyo mawazo yake lakini staili ya kuwa huru. Kwamba haya naandika hayahusiani, yanahusiana labda na vitu vinavyoendelea nchini lakini siandiki mawazo yangu kutokana na mawazo ya TANU."
Kwa mfano ukienda Daily News hata leo utakuta kuna makala niliandika nadhani mwaka '73 namkritiki Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema kwamba hawa Mang'ati sijui akasema Mang'ati au Masai sijui kama wasipobadilisha mienendo yao ambayo hakuipenda yeye atawakamata atawapeleka vijiji vya ujamaa.
Mimi nikaandika This is not ujamaa, ujamaa si mahala pa kupeleka watu unaoona kama ni wahalifu. Ni watu wanatakiwa waende kwa hiyari yao, sasa wewe inakuwaje unataka kuwafanya wahalifu, vijiji vya ujamaa kwa kupeleka nani... kwa hiyo nilikuwa na siyo kwamba napinga sera ya TANU, lakini napinga matendo na matamko ya wakuu wa serikali ambayo nayaona mimi yanapingana na sera yao wenyewe.
Kwa hiyo, ikafika wakati nikalazimika nikaondolewa, hiyo ilikuwa mwaka 1974. Na nikapelekwa Mwanza, wilaya ya Mwanza kuwa ofisa wilaya.
Swali: Ofisa wilaya?
Jibu: Ofisa wilaya ni cheo kidogo sana nafasi ndogo sana ambayo ni kama karani mmoja umewekwa tu alimradi sikufukuzwa kazi.
Ni kwamba kulikuwa hakuna kufukuzwa kazi. Ni kwamba unapelekwa mahala ambapo hukutaka kwenda, unapata mshahara wako, nyumba utapata lakini unajihisi kabisa kwamba uko umetupwa nje ya kile ulichotarajia kufanya. Na nikakaa hapo tangu Aprili 1974.
Safari ya Algeria
Swali: Ulikaa muda gani Mwanza?
Jibu: Katikati mnamo Mei nadhani, mimi hapo sina habari, umoja wa vijana wa Afrika umekutana mjini Benghazi nchini Libya na unafanya mapitio ya muundo wake na wanachagua uongozi mpya wa umoja wa vijana na Tanzania ikachaguliwa katika sekreterieti ya umoja wa vijana ambayo iko Algeria.
Hawa vijana wa Tanzania, TANU na Afro-Shirazi kwa sababu walikuwa wana uhusiano wamejenga kamati ya pamoja kuhusu masuala ya nje, ndio wakaniteua kwenda kuwa mwakilishi Algeria.
Kwa hiyo mimi nimetimuliwa Daily News mwezi wa nne, Julai miezi mitatu baadaye nilikuwa niko Algeria ni mwakilishi wa vijana wa TANU na Afro-Shirazi.
Swali: Kwa nini walikuteua wakati ni kama vile msimamo wako haikuunga sana mkono TANU, waliona nini tena?
Jibu: Hii ni swali zuri. Ni hivi, ni kwamba umoja wa vijana mara nyingi ulikuwa unakinzana na TANU.
Kwamba wazee wa TANU wanazo sera katika vitabu vyao, katika katiba, katika miongozo na kadhalika, lakini mara nyingi kulikuwa na msuguano kati ya wazee w na vijana.
Kwamba vijana walikuwa wanaona kama vile wazee hawafuati mambo yale yale ambayo wamekubaliana kwamba watayafuata. Na kulikuwa na ubishi mkubwa sana.
Hiyo nayo ilikuja kutokea baadaye mimi nilienda... wakati nateuliwa hivyo kwenda Algeria, nikaambiwa nifanye haraka niondoke nchini kwa sababu wakuu wa TANU ambao walikuwa ni pale pale hapa Morogoro Road na ukivuka tu barabara ni makao makuu ya TANU, mimi niko hapa Morogoro Road lakini viongozi wa umoja wa vijana wananiambia nifanye haraka haraka niondoke kabla watu wa Lumumba hawajapata habari za mimi kwenda Algeria wasije wakazuia. Huwezi kuamini uhusiano uliokuwepo.
Swali: Algeria uliishi miaka mingapi?
Jibu: Nilikaa Algeria zaidi ya miaka 10. Ni muda mrefu sana, mpaka nikalalamika kwa Umoja wa Vijana kusema kwamba nimechoka, nilitakiwa nikae muhula mmoja kwa hiyo ilikuwa ni miaka mitano na nirudi, ilikuwa nirudi mwaka 1979 lakini nimerudi mwaka 1985.
Swali: Ulipokuwa kule uendelea kuwa mwandishi?
Jibu: Sikufanya kazi ya uandishi isipokuwa labda mara moja moja nilichangia kama ni katika Daily News, katika Uhuru au nilipokuwa nakuja nyumbani likizo maanake nilikuwa nikija sana nyumbani Tanzania.
Nilichukua fursa zote za mikutano mikuu ya TANU, shughuli zote za umoja wa vijana nilikuwa nakuja, sherehe za mwenge nilikuwa nikiija.
Kwa hiyo sikuwahi kukaa incommunicado na hali ya Tanzania. Na kwa sababu nilikuwa katika umoja wa vijana kuna safari nyingi sana za kutembelea nchi za Afrika kila nilipopata nafasi.
Kwa mfano kutoka Algeria ninatembea Magharibi ya Afrika ambayo ninateremka mpaka nafika tuseme Kinshasa (DR Congo) au Lusaka (Zambia). Lazima nitachukua fursa hiyo, lazima nipite Tanzania, nipite Dar es Salaam nipate kujua hali ikoje na mambo yanaendeleaje na nini kabla ya kurudi nyumbani Algeria wakati ule.
Nilikuwa napata nafasi ya kukaa muda mrefu kwa sababu ilitakiwa wawe wananilipa kila mwezi mshahara, lakini sijawahi kupata mshahara wangu kwa mwezi. Kwa hiyo nilikuwa nimekaa nje mwaka mmoja... sijakaa mwaka mmoja kwa kweli, labda miezi sita nitakuwa nadai mshahara wa miezi sita.
Swali: Sasa ulikuwa unaishije kama hupati mshahara?
Jibu: Kule unapewa fedha za kujikimu za makao makuu. Tulikuwa tunaishi vizuri kwa kweli. Nyumba ipo imetolewa na serikali ya Algeria, ofisi ilikuwa imetolewa na serikali ya Algeria, gari nilipewa pesa ya kununua kwa hiyo nilikuwa na gari yangu.
Kwa hiyo kwa kuishi pale tu niliweza kuishi hata miezi sita bila mshahara wa kutoka Tanzania.
Nikirudi Tanzania nakuta hela yangu imehifadhiwa, nachofanya sasa ni kufanya mahesabu halafu kwenda benki na kubadilisha kuwa Dola.
Sasa hiyo shughuli ya kuitafuta hiyo hela mpaka ubadilishe pesa na nini, hiyo mimi nafurahia kwa sababu nakaa Zaidi Tanzania.
Swali: Baada ya kulalamika, ulirudije?
Jibu: Hatimaye nilipiga kelele na mtu aliyenisaidia kurudi baada ya miaka kumi hiyo ni aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.
Wakati huo alikuwa bado hajaondolewa mimi nimeongea naye mwaka 1983 nadhani, akiwa Algeria, amekuja kwa mapumziko lakini anaonana na wakuu wa serikali na nini, lakini kidogo kidogo kwa sababu alikuwa amefanyiwa oparesheni sijui ya kitu gani anataka kupumzika.
Kwa hiyo nikaenda kumuona kila jioni nakaa nazungumza naye mpaka anapokwenda kulala na mimi naenda zangu kwangu.
Ndio nikamwambia ninapata taabu kuwashawishi i hawa watu wa umoja wa vijana kwamba nimechoka mimi kukaa huku. Nisaidie uwaambie kwamba nimechoka, nimepitiliza.
Mzee Jumbe akasema, 'yaani wewe wenzako kule nyumbani wanataka kutoka nje wewe unataka kurudi?'
Nikamwambia, 'ndio hawa wanataka kutoka hawajatoka, wanaona ni kutamu huko na hata kwangu ilikuwa ni kutamu miaka mitatu minne ya kwanza lakini sasa hivi naanza kurudia mambo yale yale niliyoyafanya miaka mitano iliyopita, kutembelea nchi zile zile na safari hazishi kila wikendi iko safari. Unachoka kupanda ndege'.
Basi aliporudi Tanzania, ndio akaja akaita Umoja wa Vijana akawaambia, 'huyu mwakilishi wenu wa Algeria anasema hivi na hivi na hivi, na anasema ameshawaandikieni barua kadhaa lakini hamchukui hatua.
Basi baada ya hapo ndio wakanifanyia utaratibu wa kurudi nyumbani. Kwa hiyo mwaka 1986 tuseme ndio nimerudi nyumbani.
Swali: Uliporudi Tanzania ukafaya kazi gani tena?
Jibu: Nikawa ni mwajiriwa wa Umoja wa Vijana mwaka 1987 nikaombwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Utamaduni, Vijana na Michezo, akiitwa Zahara Nuru.
Kwa hiyo nikahamishwa kutoka Umoja wa Vijana nikaenda kwenye wizara hiyo kwa cheo cha Mkurugenzi wa Vijana na michezo.
Nikakaa miaka mitatu hapo ndio nikawa Rais Mwinyi kwa ushauri wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Jaji Joseph Warioba, akaniteua kuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Ni kazi ambayo sikuipenda.
Swali: Kwa nini hukuipenda?
Jibu: Kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya niliteuliwa na Rais Mwinyi lakini kwa rikomendeshini ya watu wawili: Waziri Mkuu Joseph Warioba na Waziri wa Nchi chini ya Waziri Mkuu Charles Kileo, marehemu sasa.
Walikuwa wanataka wateuliwe vijana kushika nafasi za makatibu tawala wanaoeleweka kwa misimamo yao ili waweze kuweka utawala wa mikoa na wilaya chini ya watu ambao sifa yao si kwamba zamani walikuwa ni madereva wa TANU.
Hayo yalikuwa maneno ya huyo waziri Charles Kileo.
Wakataka kunipendekeza niwe niwe Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Nikakataa, kwa sababu na nilimwambia Kileo kwamba ikiwa mnataka niwe mkuu wa wilaya ninakubali lakini kwa masharti mawili.
Moja kwanza lazima mniruhusu kutoka maana yake nimetoka nje ya utumishi wa umma kwenda kuwa mkurugenzi, kwa hiyo sina hiyo sifa ya utumishi wa umma wa kudumu na mwenye pensheni mpaka nitimize miaka miwili.
Kwa hiyo nikawaomba wasubiri miaka miwili ndio waniondoe kwenye utumishi wa umma.
Pili, niliwaambia sitaki kufanya kazi ya mkuu wa wilaya ndani ya jiji la Dar es Salaam au jiji lolote jingine kubwa kwa sababu katika majiji hakuna mkuu wa wilaya.
Mtu anayefanya kazi ya mkuu wa wilaya ni mtoto wa kutumwa soda na chai. Kama mnataka kunifanya mkuu wa wilaya nipe wilaya ya kijijini ambako nitafanya kazi ionekane.
Kwa hiyo wakakubali. Moja nadhani waziri mkuu akiharakisha uteuzi wangu kuwa nafaa kuwa mtu wa utumishi wa umma katika mwaka mmoja badala ya miaka miwili. Kwa hiyo nikapelekwa Wiilaya ya Hai.
Sasa angalia kitu kilichotokea. Nimekaa mwaka mmoja ni mwaka wa 1990. Huo mwaka kulikuwa na uchaguzi. Ulivyoisha uchaguzi Ali Hassan Mwinyi akabadilisha serikali yake, waziri mkuu akawa si Warioba tena akawa ni John Malecela. Na kitu cha kwanza kilichonipata mimi ni kwamba nikahamishwa kutoka Hai nikaletwa Ilala Dar es Salaam.
Fikiria nilikataa kwenda Kinondoni nikaletwa Ilala. Nikaamua naondoka serikalini tangu wakati huo. Ikawa ni majadiliano na familia na marafiki zangu na hao hao tu akina Kileo, unaondokaje serikalini? Uende wapi sasa ufanye nini? Nikawaambia hapana, mimi naona hii serikali sasa haina nia njema na mimi.
Kwanza hawajui historia yangu, hawajali hata kuniuliza, hawaoni labda tuna manyaraka tuliyoandikiana mimi na Charles Kileo, naona sasa hii siyo.
Swali: Kwa hiyo walikubaliana na ombi lako?
Jibu: Ikaenda hiyo, nikaona yaani karibu nataka kuondoka serikalini, ndiyo kuhamishiwa Singida nikaona afadhali kidogo.
Lakini nilivyokwenda Singida nikawa na matatizo ya kufit-in maanake nishaona hawa serikali tena inataka kunizingua wanavyotaka wao mimi nifuate.
Kwa hiyo nikaandika mwishoni wa mwaka huo huo 1992 nikaandika barua kwa Rais Mwinyi kumuomba aniruhusu niache kazi.
Maana yake nilishaambiwa kwamba vilevile ukipewa kazi kama hii huwezi kujiuzulu tu hivi hivi, unamwandikia barua aliyekuteua ili aone umuhimu wa kukuachia uondoke utumishini.
Nikamwandikia nadhani nilimwambia kwamba nina matatizo ya kifamilia na nini, hakunijibu mpaka mwezi wa tatu mwaka 1993. Ndio nilipata barua ya kukubaliwa. Ndio nikaacha kazi.
Swali: Hapo lengo lako lilikuwa ukiacha uende wapi sasa?
Jibu: Sikujua. Mimi nilijua tu kwamba hii kazi sitaki tena. Katika maelezo yangu ya maisha nitaelezea kwa undani zaidi lakini sikuitaka tena ile kazi. Nilikuwa nakwenda tu alimradi niende lakini sikuwa na imani nayo kabisa.
Swali: Ni kipi kilikukwaza Singida?
Jibu: Pamoja na kuichukia ile kazi nilipokwenda Singida nikasema Mungu wangu ningejua kwamba hii ingetokea labda nisingemwandikia Rais.
Kwa sababu Singida ni vijijini nilipapenda, na kulikuwa na matatizo ya kweli.
Kwa mfano nimekaa Singida si zaidi ya miezi sita, lakini kuna kitu nimefanya mwaka wa 1992 mpaka leo nikipita Singida najivunia.
Kuna shule ya Maryknoll Sisters Singida ambayo imejengwa kwa juhudi zangu. Sio mimi nimeijenga lakini niliwashawishi wananchi wakubali eneo lao walitoe kwa ajili ya kujenga shule ya watoto wa kike ambao wameshindwa kwenda sekondari.
Ile nilisimamia mimi. Na hiyo najivunia kweli."
Inaenda kukupa mfano kwamba pamoja na kwamba wakuu wa wilaya ni kazi ya kijinga sana haina hata mashiko mara nyingi kwa sababu wanajifanya ni viongozi wa wilaya lakini hawatokani na watu.
Ni watu wamewekwa kutoka nje. Inaweza ikapelekwa mahala ambapo hapapendi, hapapendezi hapafurahishi na anafanya kazi alimradi na akishaondolewa katika wilaya hiyo hana hata hamu ya kwenda kuangalia tena alichokifanya kule nini kinaendelea kule.
Lakini mimi nilipenda Singida na pale nilipenda hiyo kazi ya... miezi sita ndani ya miezi sita Mkuu wa Mkoa alikuwa ni Galus Abeid nadhani yuko tume ya mwalimu Nyerere.
Alikuwa alijua liko tatizo hilo akaniita tukalizungumza nikamwambia niachie mimi nitalishughulikia hili maanake hiyo ni tatizo halizi.
Swali: Nakumbuka wakati huo ulikuwa pia Mbunge, uliingiaje tena huko?
Jibu: Nilikuwa mbunge mwaka 1990 mpaka 1995. Nilikuwa bado mkuu wa wilaya.
Swali: Ulikuwa mbunge ukiwakilisha kundi gani?
Jibu: Nilikuwa mbunge wa Vijana. Hiyo ilitokana na Katiba ya zamani ambapo katika bunge kulikuwa na viti 15 vya jumuiya za chama, ambazo ni Jumuiya ya Vijana, Jumuiya ya Wanawake, Jumuiya ya afanyakazi, Jumuiya ya Uashirika na Jumuiya ya Wazazi.
Sasa hawa walikuwa wakitakiwa kwa utaratibu wa zamani kila jumuiya moja inaleta watu watano wanakuwa 30 kwa maana hiyo. Halafu hawa walioteuliwa na jumuiya hizo wanakwenda bungeni kwenda kuonana na wabunge waliotoka mikoani wanaomba kura za hao wabunge.
Sasa wabunge wanapiga kura kutokana jinsi walivyo shawishika na mgombea 15 wa mwanzo ndio wanaingia bungeni.
Sasa mimi nilipitishwa na umoja wa vijana na umoja wa vijana waliopitishwa wote waliingia bungeni which means kuna jumuiya nyingine hazikupata watu wote watano, nadhani washirika hawakupata watu watano, nadhani wafanyakazi hawakupata watu watano, lakini sisi tulipata wote waliosimamishwa walipita kwa nguvu ya kampeni ya umoja wa vijana na jinsi tulivyojieleza tu mbele ya wabunge.
Hiyo kazi ngumu kwa sababu hawa watu wametoka mikoani huko wameuza nyumba, wameuza magari, wametoa hela yao ya mwisho ili kupata ubunge.
Lakini ndivyo tulivyoomba kura na ndivyo tulivyopita tukawa wabunge.
Swali: Kwa hiyo mpaka unastaafu ukuu wa wilaya ulikuwa unaendelea pia kuwa mbunge?
Jibu: Wakati naacha ukuu wa wilaya nilikuwa bado mbunge kwa sababu ubunge wangu uliisha 1995.