Binafsi nimefurahishwa sana na matokeo ya safari za Mh. Kikwete nje ya nchi, zimekua na manufaa makubwa kisiasa , kiuchumi na kujenga mahusiano mema na chanya kwa nchi yetu na nchi nyingi Kimataifa.
Ingawa wapinzani na wananchi wengine wanaweza tazama safari za Rais wetu, kama kupoteza rasilimali nyingi, lakini badala yake zimekua chachu, na nchanzo cha kujenga nchi yetu katika siasa za kimataifa.
Kwa ufupi na wote tumeona na kushuhudia, ujio wa viongozi wakubwa duniani, akiwemo Rais wa Marekani Barak Obama, Rais wa Jamhuri ya watu wa China, mawaziri wakuu wa nchi mbali mbali, na marais wengine ambao wote wameleta neema kubwa ya kiuchumi.
Ujio wa marais hao na viongozi mbali mbali wa dunia, umeifungua Tanzania kiuchumi, na kua kiongozi katika nchi za Afrika mashariki kwa uchumi bora, tukiwa na faida ya amani inayotufanya tuwe sehemu bora ya kuwekeza Afrika mashariki.
Bila shaka na haipingiki, kwa sasa Tanzania inakua sana kiuchumi, kuliko nchi nyingine afrika mashariki jambo lililozifanya mataifa makubwa duniani kuichukulia kama mshirika mkubwa wa kiuchumi.
Kwa kuzingatia hilo, Rais wa marekani kwa kuona umuhimu wa Tanzania, kwa siasa za sasa na baadae, kutokana na nguvu ya uchumi ambayo inayo na itakayokuja kuwepo, akambadili balozi wa Marekani Tanzania, na kumleta mshauri wake wa karibu katika ikulu yake kuwa balozi wa Tanzania, hili ni jambo la kujipongeza kwa kukubalika.
Safari za Rais wetu zimetujenga katika siasa za kimataifa na si jambo la kupingika kua kwa sasa Tanzania ni moja wapo ya nchi zinazokubalika kimataifa na kutazamwa kama super power siku zijazo.
Safari za rais wetu, zikienda sambaba na ukuaji wa uchumi na kufunguliwa milango kwa miradi mbali mbali mikubwa, zimeibua mengi yaliyojificha nyuma ya pazia katika mahusiano yetu na majirani wetu.
Bila shaka kila mmoja anafahamu ni kwa jinsi gani nchi nyingine za maziwa makuu zinavyoendelea na kampeni za kuitenga tanzania katika shirikisho la kisiasa, hii ni baada ya kuona kua ukuaji wake ni mkubwa na hatarishi kwa mataifa mengine ya maeneo haya.
Kwa mtazamo wangu kutengwa huku, ni matokeo ya wivu na woga wa ukuaji wa kiuchumi wa Tanzania, pamoja na mbinu mbadala ya kuilazimisha Tanzania kuingia katika shirikisho hilo la kisiasa ili hatimae nchi hizo zifaidike moja kwa moja na neema iliyopo ndani ya Tanzania.
Watanzania , tunapaswa kushukuru kutokana na matokeo haya ya ziara hizi, kwani zisingekuwepo, ingetuchukua muda kutambua agenda ya siri ya marafiki zetu juu ya neema za taifa hili.
Binafsi naziunga mkono safari za Rais wetu na nina mtakia kila la heri katika kuikuza nchi yetu kiuchumi, kisiasa, kulinda amani ya nchi, rasilimali zake, mipaka na Raia kwa ujumla.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mdau,
Stroke.