SAFARI YA KWANZA YA RAIS SAMIA NJE YA BARA LA AFRIKA: NINI MANUFAA YAKE KWA NCHI?
Imeandikwa na Seleman Kitenge na Mhandisi Fatma Rembo
Umuhimu wa Diplomasia kwa Mustakabali wa Taifa
Ulimwenguni kote hakuna nchi ama taifa lolote iwe lililoendelea au linaloendelea ambalo limejitosheleza kwa mahitaji yake yote ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata ya ulinzi na usalama wa raia na mipaka yake bila kutegemea mataifa mengine. Ushirikiano baina ya nchi hutoa fursa kwa nchi husika kushirikiana katika kushughulikia changamoto au hatari mbalimbali zinazoweza kuhatarisha uhai wa mataifa hayo.
Mahusiano ya kidiplomasia ni nyenzo muhimu katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoyakumba mataifa mbalimbali duniani. Changamoto hizo ni kama vile magonjwa ya milipuko, mabadiliko ya tabia nchi, uhaba wa nishati, uhaba wa chakula na maji, ugaidi, uhamiaji haramu, utoroshwaji wa fedha haramu nje ya nchi, uhalifu wa kuvuka mipaka na migogoro mbalimbali inayohatarisha amani na usalama wa dunia.
Lakini pia, diplomasia haishii tu kwenye ushirikiano wa kutatua changamoto ambazo zinahatarisha maslahi ya pamoja baina ya nchi bali inakwenda mbali zaidi katika kuhakikisha nchi zinapata mahitaji yake muhimu. Mahitaji hayo yanaweza kupatikana kupitia biashara za kimataifa, kubadilishana taarifa na maarifa, misaada ya kisayansi na teknolojia, pamoja na misaada ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwa mantiki hiyo, pasipo kuwepo na urafiki na ushirikiano wa uhakika baina ya mataifa si tu itakuwa ngumu kwa nchi kukidhi mahitaji yake bali pia itajihatarishia usalama na nafasi yake kwenye majukwaa ya kimataifa ya utoaji maamuzi juu ya ajenda mbalimbali za maendeleo ya dunia.
Kama ilivyo kwenye familia udugu huimarishwa kwa kutembeleana na kujuliana hali, hivyo hivyo kwenye nyanja ya diplomasia kutembeleana huongeza uhai wa ushirikiano na urafiki baina ya mataifa.
Umuhimu wa Ziara ya Rais Samia Marekani
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mabadiliko katika sera yake ya awali ya mambo ya nje ambayo ilijikita zaidi kwenye ukombozi wa uhuru wa kisiasa wa bara la Afrika ili kujikita kwenye ukombozi wa kiuchumi. Ni wazi kwamba nguvu ya kiuchumi sio tu inatuhakikishia usalama wa kisiasa, kijeshi na kijamii ila inatupa fursa pia ya kuweza kulinda tunu na maslahi ya taifa letu kwenye dunia yenye ushindani mkubwa.
Hivyo basi, Rais Samia Suluhu Hassan ametambua fika ili tuweze kufikia dhana ya nchi yetu ya kutekeleza diplomasia ya kiuchumi ni wajibu wetu kama taifa kushirikiana na kutojitenga na mataifa mengine ikiwemo Marekani. Ni wazi kuwa nchi yetu ni miongoni mwa nchi ambazo hazijasalimika na janga la UVIKO-19 ambalo limeathiri uchumi wa dunia. Hivyo iko haja ya kujumuika pamoja na mataifa mengine katika kutafuta suluhu ya kujikwamua kwenye madhara ya janga hili lakini pia kujipanga kwa pamoja ili magonjwa mengine ya milipuko ya aina hii yasiweze kuleta athari zaidi katika uchumi na jamii zetu hapo siku za usoni.
Kwa sababu hiyo, ziara ya Rais Samia nchini Marekani sio tu imempatia fursa ya kushiriki Mkutano Mkuu wa 76 wa Baraza la Umoja wa Mataifa kama Mwanadiplomasia wa kwanza na Mkuu wa Nchi bali pia itasaidia kuimarisha ushirikiano baina yetu na taifa rafiki la Marekani.
Kuongozana kwake na wafanyabiashara kutoka Tanzania na kushiriki kwenye mkutano wa pamoja baina yao na wenzao wa Marekani kumetoa mwanya kwa Rais Samia kuvutia uwekezaji na utalii nchini ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Dunia (WB), ukuaji wa Pato Ghafi la Ndani (GDP) wa Tanzania ulishuka kufikia wastani wa asilimia mbili (2%) kwa mwaka 2020. Ambapo kushuka huku kwa ukuaji wa Pato Ghafi la Ndani (GDP) na kuathirika kwa mauzo ya biashara, utalii na usalama wa kifedha ulipelekea kuongezeka kwa idadi ya masikini takribani 600,000 mwaka 2020. Ukuaji wa uchumi umeshuka kutoka wastani wa asilimia saba (7%) kwa mwaka 2019 na 2018, na wastani wa asilimia 6.8 kipindi cha miaka mitano iliyopita hadi kufikia wastani wa asilimia tano (5%) kutokana na athari za UVIKO-19.
Kuongezeka kwa uwekezaji na utalii ambako kutachangiwa na ziara hii kutasaidia kuirejesha nchi kwenye mstari wa ukuaji wake wa kiuchumi na pato la taifa kwa ujumla. Hii itasaidia kuinua maendeleo ya wananchi na kukabiliana na janga la ajira ambalo limeongezeka kwa kasi tangu kuanza kwa ugonjwa wa UVIKO-19 duniani. Kwa mujibu wa Shirika la ILO, soko la ajira liliathirika kwa kiasi kikubwa. Kwa mwaka 2020 takribani ajira milioni 114 zilipotea duniani na Tanzania kwa kuwa ni sehemu ya dunia haikunusurika na athari hiyo.
Vikao vya pembezoni vya ana kwa ana alivyofanya Rais Samia na wakuu wa taasisi muhimu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres na Bw. David Malpass wa Benki Kuu ya Dunia (WB) pamoja na kile alichofanya na Mh.Charles Michael, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU), vilizaa matunda ambapo wamemuhakikishia kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kupambana na athari za UVIKO-19. Upande mwingine, Rais alikutana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Filippo Grand ukizingatia Tanzania imekuwa mwenyeji kwa wakimbizi kutoka nchi jirani kwa muda mrefu. Pia, kikao chake na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Dkt. Ngozi Okonjo-Iweala nacho kilizaa matunda ambapo naye alimuhakikishia Rais Samia kuwa wataisaidia Tanzania kuweza kufikia malengo yake kibiashara.
Hivi karibuni Tanzania iliridhia mkataba wa soko huru barani Afrika (AfCFTA) ambao utatoa fursa ya nchi yetu kuuza bidhaa zake kwenye soko la ndani la Afrika linalokadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani trilioni 3.4. Kuongezeka kwa uwekezaji kutoka Marekani kwenye sekta muhimu ya viwanda na kilimo ambako kutatokana na ziara hii kutaisaidia nchi yetu kuwa na uwezo mkubwa wa ushindani wa kibiashara. Lakini pia, kutokana na Marekani kuwa na uwezo mkubwa wa kiteknolojia kutasaidia kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitamudu ushindani katika soko huria na kupunguza kama si kulimaliza kabisa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi nchini.
Umuhimu wa Ushiriki wa Rais Samia Kwenye Mkutano Mkuu wa 76 wa Umoja wa Mataifa
Kitendo cha Rais Samia kuhutubia Mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa kunamfanya kuweka historia ya kuwa mwanamke wa tano kutoka barani Afrika kufanya hivyo kama Mkuu wa Nchi. Ajenda za mabadiliko ya tabia nchi, UVIKO-19, usalama wa nishati, chakula, usawa wa kijinsia, amani na usalama wa dunia ambazo kwa kiasi kikubwa zimebeba taswira ya mkutano huu ni muhimu sana sio tu Tanzania bali kwa bara la Afrika na dunia kwa ujumla. Hivyo basi, Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa 76 wa Baraza la Umoja wa Mataifa inatoa muelekeo kwa viongozi wa mataifa mbalimbali duniani juu ya matamanio na matarajio ya watanzania.
Matarajio hayo ni pamoja na kufikia Malengo Endelevu ya Dunia na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ambazo utekelezaji wake umeathirika kwa kiasi kikubwa na janga la UVIKO-19. Hata hivyo, katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza kwamba hatuwezi kutumia UVIKO-19 kama kisingizio cha kutofanya jitihada za kutosha kufikia Malengo Endelevu. Kauli hii sio tu imedhihirisha utayari wetu kama taifa kwenye kufikia ajenda za maendeleo lakini pia inatoa hamasa kwa wadau na washirika wetu wa kimaendeleo ulimwenguni kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kuyafikia Maendeleo Endelevu licha ya changamoto na madhara yaliyotokana na UVIKO-19.
Msisitizo wa Rais Samia wa kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa kimataifa katika hotuba yake umetoa picha kwa mataifa rafiki kuwa tuko tayari kama taifa kuendelea kushirikiana nao kwenye ajenda zote muhimu zenye maslahi ya pamoja. Na kama alivyonukuu methali ya kiafrika katika hotuba yake inayosema, “ukitaka kwenda haraka nenda peke yako, ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako.” Kauli hii imedhihirisha wazi kuwa Tanzania haitajitenga na jumuiya za kimataifa katika jitihada za pamoja za kupata maendeleo bali itashirikiana nao kama wadau muhimu ili kuweza kuipaisha nchi katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa ujumla.
Mwisho, kugusia kwake masuala ya usawa wa kijinsia ambao yeye mwenyewe ameonesha kwa vitendo kwa kuteua wanawake wengi kwenye nafasi mbalimbali zikiwemo wizara nyeti za Ulinzi na Mambo ya Nje kumeitangazia dunia utayari wa Tanzania kulifikia lengo la tano la Maendeleo Endelevu linalojikita kwenye usawa kijinsia. Masuala mengine kama athari za mabadiliko ya tabia nchi, maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya vijana ambayo yalibeba ujumbe wa hotuba yake yametoa mwanga wa vipaumbele vya serikali yake katika kuboresha maisha ya watanzania. Pia yametoa fursa kwa nchi wahisani kupata picha halisi ya maeneo gani washikirikiane nasi ili tuweze kupiga hatua za kimaendeleo.
View attachment 1953517