Rais wangu Kikwete, Richmond ni laana
Pascally B. Mayega
RAIS wangu Kikwete, nilipoandika makala yangu ya kwanza kabisa nilianza hivi: Laiti kama ningelikuwa mtabiri, ningetabiri hatima ya Rais wangu. Ningetabiri mustakabali wa nchi yangu. Ningemtabiria Rais wangu kama mtabiri wa Julius Kaizari alivyomtabiria Rais wake. Alimwambia: Kaizari jihadhari na tarehe za katikati ya mwezi Machi. Leo mimi ningetabiri: Rais wangu jihadhari na kurasa zinazokuja za ufunuo wa Richmond na EPA.
Rais wangu, katika makala iliyofuatia nilianza hivi: Mimi siyo mwandishi wa makala. Mimi ni mwandishi wa vitabu. Ukiona naandika makala sasa ujue utabiri wa wahenga unatimia. Walisema: Iko siku mawe haya yatakuja kuzungumza.
Rais wangu, kwa kuwa mimi si mtabiri na kwa kuwa mimi si mwandishi mzuri wa makala, na haya mawe sasa yamekwishakuzungumza, basi naona heri niandike hii makala iwe ndiyo makala yangu ya mwisho. Ada ya mja hunena muungwana ni kitendo.
Wengine husema ahadi ni deni. Naona sasa yanipasa niwarejee wasomaji wangu wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Niliwaahidi kuwa katika toleo lijalo majibu kuhusu kuweza au kutoweza kwa Rais ajaye yatapatikana. Mwisho kuna swali:
Je Rais aliyechaguliwa alikidhi matarajio ya waliomchagua? Na majibu ya maswali mengine.
Rais wangu, mchambuzi nguli, ndugu wa maswali magumu, Ansbert Ngurumo, katika uchambuzi wake wa Februari 24, 2008 aliandika hivi:
Maana tukizingatia Tanzania ya mzee Mwinyi ilipoishia, na mzee Mkapa alipoitoa na kuifikisha kwa miaka 10; tukipalinganisha, na ujanjaujanja na usanii unaofanyika sasa katika miaka miwili tu ya utawala wa Kikwete, baadhi yetu tunachelea kusema kwamba Watanzania walifanya makosa kukifungua kile ambacho kilifungwa na Mwalimu Nyerere... Na hapo ndipo ulipo ushindi wa Lowassa dhidi ya Nyerere. Mtandao wa Lowassa haukufa ukageuka na kuwa mtandao wa Kikwete.
Rais wangu, baada ya kusoma maneno haya nikayakumbuka maneno ya Mwalimu aliposema: Mkiwachagua vijana hawa watawapeni shida. Nimejikuta sina la kufanya isipokuwa kwa faida ya wasomaji wangu nalazimika kufafanua yale niliyoyandika katika Butiama kuna Kaburi.
Nilisema nilibahatika kualikwa nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Msasani, jijini Dar es Salaam. Alikuwa anazindua kitabu chake, Majukumu ya Nchi za Kusini. Katika maisha yangu ya kumfahamu Mwalimu nilikuwa sijapata kumsikia akiongea kwa hisia kali kama siku ile. Nathubutu kusema Mwalimu aliapiza.
Aliusia. Alitoa tamko ambalo kulivunja ni kujitafutia laana. Baadhi ya maneno yake yalikuwa hivi: ...Watu wazima wameenda Zanzibar, wakaamua waliyoyaamua. Wamerudi hawatuambii wameamua nini...
Najua mmekwishaiacha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na mtu kutaka kuisemea sasa itakulazimu uwe na moyo mkubwa kama wa mwendawazimu... Lakini Paolo... Paolo... na wengine, nawaambieni... (kimya kidogo, kisha kwa sauti ya juu). Mkilifuta kabisa Azimio la Arusha... (kimya kidogo kisha kwa msisitizo) Mtakuja kupata shida sana baadaye.
Paolo aliyekuwa anaitwa na Mwalimu hapo alikuwa mtu mkubwa sana serikalini. Sijui siku hizi yuko wapi. Lakini mara ya mwisho nilimsikia wakati wa pilipilika zake na Chavda wakimkwepa Mrema. Sisi tulikuwa tunamwita Paul.
Rais wangu, kilichonishtua mimi ni pale Mwalimu alipokuwa akisema na wengine. Kila aliposema na wengine, Mwalimu alimkazia macho waziri ambaye tulikuwa tumekaa kwa kukaribiana sana. Alimwita na wengine.
Hakumtaja jina hata mara moja. Baadaye tulipoingia katika chumba maalumu cha Mwalimu kwa maongezi ya faragha, alimshambulia waziri yule kwa maneno ya moja kwa moja kuhusu wizara yake. Naye alijibu: Tumekusikia Mwalimu, tumekusikia Mwalimu. Safari hii nilikaa mbali kidogo na waziri kuogopa macho makali ya Mwalimu.
Sononeko la Mwalimu lilikuwa dhahiri. Alionekana kama mtu anayeongea na mijitu isiyosikia. Mwalimu akiwa hai, waziri yule hakuwemo katika Baraza la Mawaziri lililofutwa.
Rais wangu, Baba wa Taifa alielewa fika kuwa wenye uwezo wa kulifuta Azimio la Arusha ni viongozi. Si wananchi. Hivyo aliposema: Mtakuja kupata taabu sana baadaye, alikuwa anawaapiza viongozi, si wananchi. Na hili ndilo linalotokea sasa. Wengine wanajiuzulu.
Wengine wanaondolewa. Ndesamburo akisema kama China hawa wangenyongwa, wanapapatika. Wananchi wanaposema wafilisiwe wanatetemeka na kutoka jasho katika makasri yao yenye mfano wa friji. Viongozi wanatikisika. Mwisho wao sasa ni mashaka matupu.
Rais wangu, kipindi chote hiki wananchi walikuwa safi. Hakuna aliyetikisika. Waliendelea vema na taabu zao za kila siku. Nchi si viongozi peke yao. Kusema nchi imetikisika ni kupotosha ukweli. Mtikisiko wa viongozi mafisadi hauwezi kuwa mtikisiko wa nchi. Nchi haikutikisika. Mafisadi bado wanatikisika. Wataendelea na laana ya Baba wa Taifa mpaka mwisho wa ufisadi wao.
Sasa wanaanza kujieleza wenyewe wakidhani wanajitetea. Wengine wanalipa wananchi ili wakusanyike. Wengine kwenye vyombo vya habari. Eti ajenda 21. Wanajisasua nguo mwilini mpaka watabaki watupu. Ingekuwa ni bora kwao wangebaki kimya, wananchi wakawadhania kuwa ni wezi, mafisadi, kuliko wanaposema sasa na kuthibitisha hivyo.
Kuna wale ambao upeo wao wakufikiri ni mdogo, wanatafuta sababu kama udini, ukabila, ukanda na sababu nyingine za kijinga kama hizi. Eti ripoti ya Richmond inanuka hujuma dhidi ya watu wa Monduli. Mawazo ya mtu aliyefilisika kabisa. Mawazo ya mtu anayekiri uovu alioufanya. Mtu yeyote anayetaka kutuingizia ukabila au udini katika ufisadi huu alaaniwe na sisi wote. Ashindwe na alegee. Mfa maji huyu. Anyoshe shingo yake, apokee stahili yake kwa amani.
Rais wangu, kwa nini nayajutia maneno ya Mwalimu sasa? Hivi kweli viongozi wetu, msingelifuta Azimio la Arusha wananchi wangekutana wapi na Richimond? Richmond ambayo bila huruma iliyatumia maumivu ya wananchi yaliyotokana na ukame kuwafanyia ufisadi wa kiwango cha juu kabisa.
Richmond ambayo serikali imekiri kuwa ni kampuni hewa, lakini bado inaendelea kuilipa hiyo hewa shilingi milioni 152 kila siku bila kuuziwa chochote. Richmond ambayo serikali inakiri mbele ya wananchi wake kuwa haijui inamlipa nani. Lakini inalipa kila siku bila kukosa. Richmond ambayo imekutanishwa na wananchi kwa nguvu ya ofisi ya Waziri Mkuu.
Sasa gazeti limeandika J.K. amlilia Lowassa. Eti umesema kwa utendaji kama huu, amelitumikia taifa kwa ujasiri na uzalendo mkubwa na kwamba alikuwa rafiki kikazi na kimaisha. Na sasa amepata ajali ya kisiasa. Si siri wananchi wameipokea ajali hii kwa shangwe. Wameanza tena kuwa na matumaini yaliyokuwa yamepotea.
Wakati wewe unamlilia, mimi namhurumia mtu huyu! Yuko mtaani peke yake. Kama kweli alikuwa rafiki, muwaishe kwenye vyombo vya sheria ili vikamsafishe. Vingenevyo chukua jukumu uwaeleze wananchi pesa zao milioni 152 zinazoendelea kulipwa kila siku bila kukosa analipwa nani? Hili ni muhimu sana liwekwe wazi mapema maana wananchi wengine wanaweza kudhani analipwa yeye au marafiki zake.
Hivi tunavyosema milioni 152 zinaendelea kulipwa kila siku, bila kununua chochote kwa kampuni hewa, waponda kokoto wanapiga hesabu zao. Wamachinga na wapiga debe nao wanapiga hesabu. Wanafunzi wa elimu ya juu wanapiga hesabu, wangesoma wangapi bure.
Wale wanaofiwa na ndugu zao kila siku kwa kukosa fedha ya matibabu wanawakumbuka marehemu wao. Wao wenyewe hawana uhakika wa maisha yao.
Wastaafu wazee wetu waliolitumikia taifa hili kwa uadilifu mkubwa ambao sasa wanalipwa pensheni ya sh 20,000 kwa mwezi au sh 670 kwa siku wanapiga hesabu.
Walimu wanaodai na wafanyakazi wa kima cha chini wanapiga hesabu, ambazo kila jawabu linavimbisha mioyo yao zaidi kwa hasira. Hawa hawatakoma kumlilia Baba wa Taifa. Na kwa kufanya hivyo, laana kwa viongozi mafisadi nayo haitakoma.
Rais wangu, ni nani aliwatuma wananchi kwenda kugawana mashamba na mali za Gavana Ballali? Nani aliwachochea wananchi kuwachoma moto vibaka? Machungu yote haya wananchi wataendelea kuwaona mafisadi wao kwa macho tu?
Lazima uwalinde watuhumiwa hawa kwa kuwapeleka mahakamani haraka. Watakapoangukia katika mikono ya wananchi wenye hasira kali atalaumiwa nani? Wananchi wanataka fedha yao irudiswe. Tuwarudishie mali yao kabla hawajaanza kugawana za kwetu.
Walionyanganywa mifugo pekee iliyokuwa imebaki au vyombo kama baiskeli, walioezuliwa mabati kwenye nyumba zao au kulazimika kujifungulia katika ofisi za watendaji na wale waliofungwa kwa kosa la kukosa fedha za kulipia ujenzi wa madarasa, leo wanapoambiwa kuna milioni 152 zao zinalipwa kwa kampuni hewa, nani anaweza kujua ukubwa wa fundo lililowakaba moyoni?
Maisha ya kifahari wanayoishi watuhumiwa ndiyo yaliyodunisha maisha ya wananchi hawa. Wamedhulumiwa. Wameibiwa. Hasira ya wananchi hawa dhidi yao ni kali, ngumu, tena inatisha. Ee Mungu wanusuru watu hawa!
Rais wangu, ulipovunja Baraza la Mawaziri nilikuuliza, Mawaziri wapya utawapata wapi? Ona sasa, umetuletea mawaziri wa zamani ambao wananchi wamekwisha kuwazomea.
Utawanunulia nguo gani za kutokea upya mbele za watu? Sasa tuna waziri ambaye hata kujibu swali dogo tu la nyongeza bungeni ambalo halikuandikiwa majibu, kwake haiwezekani.
Mtuhumiwa wa wizi mkubwa katika Benki Kuu eti naye ni waziri mpya. Msimamizi wa mikataba sumu karibu yote inayozidi kulinyongonyeza taifa, eti naye ni waziri mpya. Huyu mwenye migodi ambaye alipokuwa waziri wa zamani alifanya ndege za jeshi kama teksi ya kuendea kwao kusalimia, mikataba ya migodi yake imechunguzwa? Eti sasa naye ni waziri mpya.
Rais wangu, kama lengo la kuunda baraza jipya ilikuwa ni kuunda chombo safi, basi hawa wamelichafua. Sote twafahamu kuwa nzi akidondekea katika glasi ya maziwa, maziwa yote huwa hayafai tena.
Katika mapambano ya ufisadi, kwa hili tumepiga hatua moja kubwa kurudi nyuma. Kama yaliyotokea bungeni si unafiki. Hata kama ni uoga wa uchaguzi Mkuu ujao. Na kama ni kweli sera ya chama mbele wananchi wakafie mbele itakuwa imelegezwa na maslahi ya wananchi yatawekwa mbele, wabunge safi wa CCM watapimwa kwa hili. Watawazomea mawaziri hawa ndani ya Bunge lenyewe.
Sasa tuna waziri mpya ambaye yeye mwenywe ni wa zamani. Unaweza ukadhani kuwa ndiyo hirizi ya baraza. Kila baraza yumo, anachokifanya hakuna, miaka yote. Ingekuwa ni nguo imechuja kiasi kwamba hakuna anayeweza kusema kwa hakika rangi yake ya dukani ilikuwa rangi gani.
Mwandishi nguli Padri Privatus Karugendo ameandika hivi: Adam Malima alipoundiwa tume na Bunge alionyesha jeuri ambayo inaweza kuzua maswali juu ya utendaji wake. Kama Watanzania wana kumbukumbu, kuna wakati Malima na Zitto Kabwe walihojiwa kwenye kipindi cha TvT juu ya sakata la Buzwagi.
Majibu yake na utayari wake wa kutaka kuwakaribisha wawekezaji wa kila aina jimboni kwake, pia ni jambo la kutilia shaka uwezo wa utendaji kazi wake.
Nilikiangalia kipindi hicho. Mchango wake bungeni kuhusu Buzwagi pia niliusikia. Awamu ya nne, imefuta kabisa heshima yote aliyokuwa anapewa mtu anapoteuliwa kuwa waziri.
Wapo katibu kata hata baadhi ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa wenye sifa na uwezo wa kuwa mawaziri na wakaheshimika. Tunapoletewa mawaziri ambao kwa maoni ya wengi hata sifa za ukatibu kata hawana, tuna haki ya kuuliza uongozi wa nchi yetu, unatupeleka wapi?
Bado kidonda hakijapona. Wananchi bado wana uchungu wa fedha zao zaidi ya milioni mia moja zilizotumika kuthibitisha uzushi wa kipuuzi aliouanzisha bungeni. Kwa kuwa ilithibitika kuwa alisema uongo, wananchi wataendelea kudai adhabu dhidi yake mpaka itakapotolewa.
Kinyume cha hapo shilingi milioni mia moja za maskini walipakodi wa nchi hii zitabaki juu ya kichwa chake kokote atakakokwenda. Hili Mwenyezi Mungu atalisimamia maana hatakubali wananchi wageuzwe mpira wa malapulapu. Jina la Waziri Mkuu aliyejiuzulu lilitajwa kumbeba na vyombo vya habari. Sasa haya ni mazalia? Kwa nini hamtaki harufu mbaya ya Richmond iondoke kabisa? Hasara wee!
Rais wangu, mafisadi wapo, lakini wanawema pia wapo katika nchi hii hii. Reginald Mengi, mtu wa Mungu, wakati matajiri wenzake wanahangaika huku na huko kujibu au kukanusha tuhuma mbalimbali za kifisadi dhidi yao, yeye kutwa anahangaika na walemavu wake, wagonjwa wa moyo, waathirika na maskini ambao hawakujaliwa.
Kwa misaada yake mbalimbali kwa madrasa na jamii zingine bila kujali itikadi ya kisiasa, kabila au dini, Mungu atamlipa.
Najua alivyoumia kuona maskini wale wale anaowasaidia kwa kile kidogo alichonacho, wanakamuliwa zaidi ya sh milioni 100 kugharamia upuuzi. Asikate tamaa.
Mema yote anayoifanyia jamii yatageuka moto mkali wa adhabu dhidi ya wafitini wake. Aendelee kuwasaidia wenzetu wenye kuhitaji ambao wako vile walivyo kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Aelewe kuwa siku zote wanaotetea haki za wengi hukumbwa na misukosuko mingi. Hawa wataishi hata baada ya kifo. Watakumbukwa na vizazi vingi vijavyo, naam, pamoja na wote walioumizwa au kulazimishwa kuuondoka ulimwengu huu kwa sababu waliwaudhi wakubwa na hivyo wakawatanguliza mbele ya haki.
Rais wangu, kama tunayafanya haya bila kuelewa, basi Mungu atusamehe. Lakini kama tumeyafanya kwa lengo la kulinda ufisadi na mafisadi, basi laana ya Baba wa Taifa iko pale pale.
Mbunge amesema wakipita mtaani watoto wanaulizana: Wanafiki waseme ndiyo. Wanajibizana: Ndiyoooooo! Hapa ndipo kasi ya viwango feki ilipolifikisha Bunge letu. Kudharauliwa hata na watoto wa mitaani.
Kujiuzulu mpaka aundiwe tume. Saa imeenea ambako wabunge waadilifu hawatakubali kubeba mafisadi wachache ndani ya chama chao. Sasa imeenea ambapo wabunge waadilifu watataka kurejea maagano ya Azimio la Arusha. Na tuipishe basi laana ya Baba wa Taifa kwa viongozi wetu ili tuwarudishie wananchi matumaini yao.
Rais wangu, katika hili waonyeshe watu wako mfupa wako katika nyama ya mwili wako. Kata katikati ili ubaki na kipande kimoja. Usitake kuwa huko na huku. Chagua bega.
Wale waliokwishaanza kutafunwa na laana ya Baba wa Taifa waache waendelee kutafunwa. Wengi watafuata, Mwakyembe kafungua mzinga wa nyuki, watu wanatoka nduki. Kuwahurumia ni kujitafutia janga wewe mwenyewe. Richmond itafungua mengi na itaifungua Tanzania. Ajidhanie amesimama aangalie asianguke. Maisha bora kwa kila Mtanzania bila Azimio la Arusha HAIWEZEKANI.
Mungu akubariki msomaji wangu.
Simu: 0713 334239
Email:
ngowe2006@yahoo.com