Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Habari za Kitaifa Habari nyingine zaidi!
Richmond yazidi kung'ang'aniwa
Oscar Mbuza
HabariLeo; Tuesday,January 02, 2007 @00:06
CHAMA cha NCCR –Mageuzi, kimesema kitaishinikiza Serikali kueleza ukweli wa mazingira yaliyoifanya kuingia mkataba wa uzalishaji umeme na Kampuni ya Richmond Development (RDC) ambayo ilishindwa kuzalisha umeme kama ilivyotarajiwa na kuuzwa kwa kampuni nyingine.
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, James Mbatia, aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, wakati akitoa tamko la chama hicho kuhusiana na matukio muhimu yaliyotokea nchini mwaka 2006.
Mbatia alisema kampuni ya Richmond imewaongezea mzigo wa madeni Watanzania kwa vile mkataba uliofikiwa baina yake na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) una gharama kubwa kuliko ule wa kampuni ya kuzalisha umeme ya IPTL.
Alisema wakati mkataba baina ya Tanesco na IPTL una gharama ya dola za Marekani milioni 150, mkataba wa Richmond una gharama ya dola za Marekani milioni 175. Mwenyekiti huyo alisema kutokana na Tanzania kujiingiza katika mikataba mibovu kama mkataba wa Richmond, unafanya deni lake nje ya nchi kuongezeka kutoka sh bilioni 7.8 mwaka juzi, hadi sh bilioni 9.9, mwaka jana.
"Ongezeko la deni hili linamfanya kila Mtanzania sasa kubebeshwa mzigo wa deni la sh. 350,000, badala ya sh. 200,000, walilokuwa wamebebeshwa mwaka juzi." Alisema uongozi wa chama hicho bado unatafakari hatua za kuchukua kuhusiana na mkataba huo baina ya TANESCO na kampuni ya Richmond. Alisema chama hicho pia kimesikitishwa na hatua ya Rais Jakaya Kikwete, kushindwa kulizungumzia suala la Richmond katika hotuba yake ya kuaga mwaka aliyoitoa juzi.
Alisema baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kutolizungumzia suala hilo, wakati akieleza utekelezaji wa ahadi za Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, mjini Dodoma Desemba 21, mwaka jana, chama hicho kilitegemea kwamba Rais Kikwete angelizungumzia suala hilo juzi. Alimwomba Rais Kikwete, kuwawajibisha mara moja, viongozi aliodai walimpa maelezo ya uongo.