KWENYE HIZI AJALI NIT WANAYO KAZI (ROLE) YA KUFANYA KUSAIDIA KUZIPUNGUZA KUPITIA MAFUNZO WANAYOTOA
Sote tunafahamu kuwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (National Institute of transport) yaani NIT, ndicho tunaweza kusema Chuo Kikuu pekee cha Madereva nchini Tanzania ambacho kinafundisha wataalamu katika Nyanja ya Usafiri na Mawasiliano katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Ni kwa kutambua umuhimu huu, Serikali ikakipa mamlaka Chuo hiki kufundisha madereva wanaotaka kuendesha mabasi ya abiria(PSV) na hata yale ya mizigo, hata hivyo kimekuwa maarufu sana kwa kufundisha madereva wetu.
Bila shaka kabisa ubora wa bidhaa inayotolewa na Chuo hiki lazima itafsirike sio tu kwenye matokeo ya mitihani bali pia matokeo ya kivitendo barabarani. Iwapo tafiti zetu kwa mfano zitasema, ajali nyingi zinatokea barabarani kutokana na makosa ya dereva ambapo inahusisha upungufu wa mafunzo au ujuzi duni basi, bila shaka NIT watahusika kabisaa pamoja na wale watahini wa Polisi (Driver examiners) ambao wao ndio wenye kazi ya kumuaminisha TRA kwamba huyu mwombaji wa Leseni Pingilinene Mfupi, ana sifa na ujuzi unaotakiwa kuendesha gari katika mazingira yote barabarani, hivyo apewe daraja C.
Chuo chetu cha NIT, kwa namna yoyote ile kinahusika katika kuhakikisha usalama barabarani unaimarika. Hakiwezi kujitoa kamwe kwa kusema tu, chenyewe kazi yake ni kufundisha tu, lazima kiende mbele kuhakikisha inatoa mchango katika kupunguza janga la ajali nchini. Kwa nini? Kwa sababu:
1. Chenyewe ndicho kinachofundisha madereva wanaoenda kuendesha magari ya abiria
2. Chenyewe ndicho kinawafundisha wakaguzi wa magari ambao baadae ndio wanakuwa watahini wa madereva (driver examiners) kule Polisi na pia wakaguzi wa magari (vehicle inspectors).
Ina maana Chuo hiki kikimtoa mkaguzi wa magari ambaye hajaiva vizuri, tafsiri yake ni kwamba huyo mkaguzi wa magari anaenda kuruhusu magari mabovu yaendeshwe barabarani, lakini sio hivyo tu, bali pia anaenda kuruhusu madereva wasio na sifa kuingia barabarani. Kwani, kwa mujibu wa sheria, TRA hawezi kumpa mtu leseni kama Mtahini wa madereva hajasema huyu mpe huyu usimpe. Ndio kusema kwamba Polisi wanapolalamika “madereva wa siku hizi wabovu kweli kweli, kimsingi wanakuwa wanajisema wenyewe kwamba sisi tunaowapitisha siku hizi na sisi ni wabovu kweli kweli.”
SASA kwa upande wa NIT, mchango wao kwenye kuzuia ajali au kupunguza vifo na majeruhi ukoje? Maswali yafuatayo, yanalenga kuibua mjadala au kufikirisha tu jinsi ambavyo NIT wanaweza kuwa na nafasi katika kuzuia ajali:
1. Je, kwenye hizi ajali zinazotokea wenzetu NIT wanajifunza nini? Je huwa wanaenda kufanya tafiti kuhusu hivi vyanzo na kuona ni namna gani matokeo ya tafiti hizo yatasaidia kuwanoa madereva? Je, wanatumia picha na video za ajali hizo kama mifano ya kufundishia?
2. Je, wenzetu NIT wana jitihada zozote za kuhakikisha wanapata taarifa na kusoma kwa kina aina zote za mabasi au malori yanayoletwa nchini na taratibu za uendeshaji wake, ili dereva anayepita pale kwa kozi ya PSV au HGV aweze sio tu kujua Scania 9XYZ bali ajue pia Zhongtong au Asia Star bus yenye engine ya PXW inaendeshwaje?
3. Je, NIT wamejaribu kutengeneza taratibu mbalimbali za msingi (standard operating procedures) za ukaguzi magari kabla hayajaondoka (pre-departure inspection procedures) ili kuwasaidia madereva au wamiliki kuzitumia, au taratibu mbalimbali za uendeshaji wa magari katika mazingira tofauti tofauti? Mfano, katika mazingira Fulani dereva aendeshaje? Ikipasuka tairi afanyeje nk? Maana vitu vingine tunaambizana mtaani tu.
4. Lakini je, NIT wanafanya tafiti kujua ubora wa madereva wao baada ya kuwa wamehitimu pale? Kwa kufuatilia takwimu za ajali kwa mfano na kufahamu, je madereva wangapi waliopita mikononi mwao walipata ajali na ni ajali za namna gani kwa mwaka au kipindi cha miaka mitatu. ili kusudi wajue wanaboresha nini katika mitaala yao? Na kama zipo je ni nani mlaji wa taarifa hizo? Zinachapishwa wapi? Kama ni kwenye machapisho ya kingereza je, zinatusaidia vipi sisi walaji ambao ni wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili? Maana nchini hapa wengi waliojaliwa hela hawakufanikiwa kwenda vidato sana. Na hata idadi kubwa ya madereva wetu ni shule ya msingi na sekondari zetu za kawaida tu.
5. Je, ni kwa kiasi gani NIT wanatumia uzoefu wa madereva wakongwe katika kufundisha madereva pale ili kupata uzoefu wa barabarani kila siku? Kwa maana ya kuoanisha nadharia na vitendo au uhalisia ulioko barabarani? Je, kwenye kozi za PSV kule NIT madereva wanafundishwa uendeshaji wa usiku? Au wale walimu wao wenyewe washaendesha magari usiku au katika hali tofauti tofauti za hewa na miundo ya barabara?
6. Lakini pia Serikali inakitumiaje Chuo hiki katika kuvikuza na kuvisimamia vyuo vingine vidogo vinavyofundisha udereva wa awali ili kuhakikisha ubora wa madereva hao, ili hata baada ya miaka 3 wakifika huko NIT isiwe kwamba ndio kama wanaanza kujifunza na moja? Labda kwenye hili pia kuna kazi ya kufanya.
7. Je, NIT wanafundisha somo la usalama barabarani au ni ule udereva tu wa kujua kulimudu gari na alama za barabarani? Kwa msingi huo, madereva wetu wanajua dhana nzima ya road safety?
Ndugu zangu, kwa leo tuishie hapa tu kwa haya maswali fikirishi yenye kulenga kuibua mjadala. Karibu wale mliopita katika chuo hicho lakini pia NIT wenyewe tulionao humu.
C&P
Usalama Barabarani ni Jukumu Letu Sote
17/08/2022