MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Kanisa Kuu, Jimbo Katoliki la Geita kutokana na uvamizi na uharibifu wa mali usiku wa Februari 25 mwaka huu.
Shigella jana alitembelea kanisa hilo na kuahidi kwamba serikali itashiriki ukarabati wa vitu vilivyoharibiwa.
Alisema serikali itatoa ushirikiano kwa uongozi wa Kanisa Katoliki kipindi chote cha uchunguzi na ipo tayari kuchangia gharama za ukarabati unaohitajika ili waumini waendelee na ibada.
"Ninalaani kitendo hicho, na Rais ameelekeza kwamba anatoa pole nyingi kwa kanisa na kwa waumini wote, lakini kama serikali, tupo wote, tutashirikiana," alisema Shigella na kuongeza:
"Kwa hiyo tutaendelea kufanya uchunguzi na ukifika muda wa kumpeleka mhusika kwenye vyombo vya sheria, tutafanya hivyo na tutahakikisha hatua zinachukuliwa.
Aidha, alielekeza Jeshi la Polisi lipanue wigo wa uchunguzi ili kubaini wengine walioshiriki katika tukio hilo ama kujiridhisha kama mhusika ni mmoja aliyefanya uhalifu huo.