TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Dar es Salaam, Desemba 24, 2022
KUZUILIWA KUINGIA NCHINI KWA VIFARANGA 62,730 VYA KAMPUNI YA PHOENIX FARMS LIMITED VILIVYOFIKISHWA AIRPORT KUTOKA NCHI YA UBELIGIJI
Ndugu wanahabari,
Tarehe
22/12/2022 saa nne usiku Wakaguzi wa Mifugo na Mazao yake walio katika kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walikamata vifaranga wa kuku wa mayai
62,730 mali ya Kampuni ya Phoenix Farms Limited ya Mkuranga, Pwani vilivyofikishwa uwanjani hapo vikitokea nchini Ubeligiji bila ya kuwa na vibali vya kuingiza nchini vifaranga (Import permit) pamoja na cheti cha afya (animal health certificate). Vifaranga hivyo viko kwenye makasha (crates)
697 na stakabadhi ya mauziano (Invoice) ya mzigo inaonesha vina gharama ya shilingi
200,262,706 ambayo ni sawa na
Euro 80,828.80 (Cost Insurance and Freight – CIF). Mkurugenzi wa Kampuni pamoja na Wakala wa Mmiliki wa vifaranga (clearing agent) hivyo walikiri kutokuwa na kibali hivyo kuwa amevunja Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Sura ya 156 na Kanuni za Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao yake ya GN. Na. 28/2007.
Ndugu wanahabari,
Kulingana na kifungu cha 54(2) cha Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Sura ya 156 kinakataza kuingiza nchini mifugo na mazao yake bila kuwa na kibali nanukuu; “
No person shall bring or cause or permit allow to be brought into the country any animal product, contrary to any order or regulation prescribing the introduction of animal products into the country or without animal products inspected and certified in the prescribed manner.” Hivyo kwa kitendo cha Kampuni ya Phoenix Farms kutaka kuingiza nchini vifaranga wa kuku wa mayai
62,730 ni kukiuka Sheria hii.
Ndugu wanahabari,
Aidha, Kanuni ya 26 ya Kanuni za Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao yake ya GN. Na. 28/2007 inabainisha kuwa, “Ikiwa wanyama au mazao ya wanyama yatafika nchini bila kibali na cheti cha afya ya wanyama au mazao ya wanyama, Mkaguzi aliyeko kwenye kituo cha ukaguzi azuie uingizaji wa wanyama au mazao ya wanyama husika nchini.
In the event, of any animal or animal products intended for importation arriving without the certificate required as aforesaid, an Inspector shall refuse to allow such animal or animal products to enter Tanzania ….”.
Ndugu wanahabari,
Hivyo, kutokana na tafsiri ya vifungu hivyo viwili hapo juu, vifaranga wa kuku wa mayai
62,730 walioletwa na Kampuni ya Phoenix Farms Limited waliopo katika Uwanja wa Julius Nyerere International Airport (JNIA) upande wa mizigo (cargo) wamezuiliwa kuingizwa nchini kwa kuwa ni mzigo hatarishi.
Aidha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Tawi la Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kuielekeza Kampuni ya Phoenix Farms Limited kuvirudisha vifaranga hivyo nchini Ubeligiji kwa sababu wanaweza kuhatarisha usalama wa kuku nchini. Vilevile, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kampuni ya Phoenix Farms Limited ameelekezwa kuviondosha vifaranga hivyo katika maeneo ya uwanja wa ndege na kuvirudisha alikovitoa.
Ndugu wanahabari,
- Kama mtakumbuka, Mwaka 2006 Tanzania iliweka zuio (karantini) la uingizaji wa kuku na mazao yake kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege duniani (HPAI). Kutokana na zuio hilo (karantini), nchi yetu imeendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa huo ambao umeathiri nchi nyingi duniani. Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege huambukiza wanyama na binadamu na hutokea kwa njia ya mlipuko na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo vingi vya kuku na ndege wa porini. Njia za kudhibiti ugonjwa huu ni pamoja na kuzingatia usafi kwenye mabanda ya kuku (biosecurity measures) na karantini ya kuzuia kuingiza kuku, ndege wengine na mazao yao. Nitoe wito kwa watanzania wote hususan wadau wa kuku kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ya kudhibiti kuingia na kuenea kwa magonjwa ya kuku nchini hususan Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege ili kulinda usalama wa kuku, na ndege wengine pamoja na afya ya jamii ya watanzania kwa ujumla.
Asanteni kwa kunisikiliza
Imetolewa na
Profesa Hezron E. Nonga
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI
24 DESEMBA 2022