RAIS KIKWETE AMESAINI SHERIA YA MITANDAO, SOMA HAPA
TAARIFA YA SERIKALI
TAARIFA YA MHE. PROF. MAKAME MBARAWA (MB), WAZIRI WA
MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KUHUSU SHERIA YA MAKOSA YA
MTANDAO YA MWAKA 2015 KWA WAANDISHI WA HABARI
TAREHE 8 MEI, 2015
Ndugu Wananchi,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kukua kwa kasi kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) kumeleta mafanikio mengi katika nyanja mbalimbali za maisha ya
kila siku. Mafanikio haya yanathibitika kwa kuongezeka kwa huduma za
mawasiliano, huduma za kifedha na matumizi ya mitandao ya kijamii. Aidha,
mafanikio hayo yameleta changamoto nyingi katika jamii. Changamoto hizo ni
pamoja na kuibuka kwa makosa mapya ya jinai na pia mbinu mpya za kutenda
makosa ya zamani.
Ndugu Wananchi,
Makosa hayo hujumuisha uhalifu wa Mitandao ambao simu za mkononi,
kompyuta au mifumo ya kompyuta hutumika kama nyenzo za kutenda uhalifu
huo.
Mifano ya makosa hayo ni kama ifuatavyo:
1. Kumekuwepo na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao,
2. Kumekuwepo na ugaidi kupitia kwenye mitandao,
4. Kuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili,
3. Kumekuwepo na uharibifu wa miundombinu muhimu ya Taifa kwa
makusudi, Kwa mfano kukatwa kwa makusudi Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano. [Hii imepelekea kuisababishia Serikali na Sekta binafsi hasara na
kusababisha kukosekana kwa huduma mbalimbali za kiuchumi na za kijamii].
Ndugu Wananchi,
Kama mnavyofahamu kwenye kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania lililopita, Serikali ilipeleka Mswada wa kutunga sheria ya uhalifu wa
mtandao (Cyber Crimes) na Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge. Madhumuni ya
kutunga sheria hii kama sheria nyingine zilizotungwa na Bunge hapa nchini ni
kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii hasa kwenye matumizi ya
TEHAMA.
Ndugu Wananchi,
Ndugu Wandishi wa Habari,
Tanzania siyo nchi ya kwanza kutunga sheria kama hii. Kuna nchi mbalimbali
duniani zimetunga sheria kama hii, kwa mfano nchi ya Uingereza (UK
Computer Misuse Act, 1990), India (IT Act, 2000), Malaysia (Computer Crime
Act 2. ) Uganda (Computer Misuse Act, 2010), Korea ya Kusini (Information and
Communications Network Act na Information and Communication
Infrastructure Protection Act), Singapore (The Computer Misuse and
Cybersecurity Act), Maturities (Computer Misuse and Cybercrime Act, 2003),
Afrika ya Kusini, Marekani (Computer Fraud and Abuse Act, 1984) na nyingi
nyinginezo.
Ndugu Wananchi sasa mmepata pahala pa kukimbilia, kwani mukitendewa
uhalifu kupitia mitando sheria hii itawasaidia kupata haki zenu. Ninawashangaa
sana wale wanaopinga kutungwa kwa sheria hii hapa Tanzania. Haikubaliki
hata kidogo kuona Wantanzania wengine wanakumbana na uhalifu kupitia
Kwenye mtandao na wachache kwa faida zao binafsi wanataka Serikali ikae
kimya. Sheria hii haina tofauti na sheria za nchi nyingine nilizozitaja hapo awali.
Sheria hii imetungwa kwa mazingira ya nchi yetu ya Tanzania.
Ndugu Wananchi,
Sheria hii sasa imeshasainiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kupitia hatua zote za
kuiboresha. Hatua ya MWISHO ilikuwa ni ile ya marekebisho yaliyofanywa na
Bunge ambapo baadhi ya vifungu vilivyolalamikiwa viliboreshwa. Kwa hivyo
wananchi sasa tuipokee sheria hii na kuitumia. Sheria hii ni nzuri na itasaidia
sana kuwalinda wananchi, mitandao na miundombinu yetu muhimu ya kitaifa.
Katika kuitumia sheria hii na kama ilivyo kwa sheria nyingine yoyote,
patakapoonekana kuna mapungufu, marekebisho yatafanyika. Kwa hivyo kama
kuna mtu yeyote mwenye maoni ya kuiboresha sheria hii anaweza kuleta
maoni Serikalini hapa Wizarani. Ninarejea tena: Waheshimiwa Wabunge,
Waheshimiwa Mabalozi, wadau mbalimbali wa Sekta ya Mawasiliano,
waandishi wa habari, wana-bloggers, na wananchi kwa ujumla kama kuna
yeyote mwenye maoni ya kuboresha kifungu chochote cha sheria hii alate
maoni hayo hapa Wizarani.
Serikali kupitia Wizara yangu itapokea maoni au ushauri huo, tutayatafakari na
kuyafanyia kazi kwa kina. Haitosaidia sana kusema huko pembeni, jukwaa zuri
la kuleta maoni ni kupitia Wizara yangu.
Ndugu Wananchi, na
Ndugu Waandishi wa Habari,
Hii haitokuwa sheria ya kwanza kufanyiwa marekebisho kama itaonekana kuna
umuhimu wa kufanya hivyo.
Ahsanteni na Ninawashukuru sana kwa kunisikiliza.