Shughuli mbalimbali za mwaka wa mawasiliano kati ya watu kati ya China na Afrika zinaendelea kufanyika katika sehemu mbalimbali za China na Afrika, na moja ya shughuli zilizofanyika hivi karibuni, ni uzinduzi wa sehemu ya sita Maonyesho la Filamu Bora za Kichina na Vipindi vya Televisheni, uliofanyika Julai 28 mjini Nairobi.
Kwenye mkutano wa Beijing wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka 2024, Rais Xi Jinping wa China alitangaza kuwa pande mbili zimeamua kuwa mwaka 2026 kuwa mwaka wa mawasiliano kati ya watu wa pande mbili. Matukio mbalimbali yanaendelea kufanyika kuhimiza mawasiliano ya watu wa pande mbili, na shughuli hiyo ya uzinduzi ya Nairobi, iliyoandaliwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China (China Media Group - CMG), ni sehemu ya shughuli hizo ambayo pia ni maadhimisho ya miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika.
Shughuli hiyo inaleta zaidi ya maonyesho 20 ya Kichina, yakijumuisha tamthiliya za televisheni, documentary, mfululizo wa michoro, na vipindi mbalimbali, kwa ajili ya wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wa Afrika kupitia vyombo 15 vikuu vya habari katika nchi 12 za Afrika. Maonyesho hayo yanalenga kuimarisha mabadilishano ya kitamaduni, kukuza uelewa wa pamoja, na kuimarisha urafiki kati ya China na nchi za Afrika.
Ushirikiano kwenye sekta ya habari kati ya China na nchi za Afrika umekuwa ukiimarika hatua kwa hatua, hasa ikizingatiwa kuwa China na Afrika zimekuwa wahanga wa upotoshaji na propaganda za vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Matangazo ya China kwenye nchi za Afrika yalianza kusikika kwenye miaka ya 60, na polepole yakaendelea kuboreshwa na kuwa kwenye mfumo wa vyombo vipya vya habari (New Media).
Kwenye kipindi cha katikati ya miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, kilichofahamika zaidi kuhusu China kilikuwa ni filamu za kungfu za Jackie Cheng na Bruce Lee, lakini baada ya sekta ya tamthiliya kupiga hatua, na hasa baada ya tamthiliya hizo kupatikana kwa lugha za kiingereza, kifaransa, kihausa na Kiswahili, ufuatiliaji mkubwa wa tamthiliya za China ulianza kuonekana. Hii ni kutokana na kuwa watu wengi waliona wanaweza kuwafahamu zaidi wachina kupitia tamthiliya zilizotengenezwa na wachina wenyewe.
Akitoa hotuba kwenye ufunguzi shughuli hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Idara ya Filamu na Televisheni ya CMG, Bibi Wang Lu, alisema kushirikiana na vyombo vya habari vya Afrika kuandaa maonyesho haya ni hatua madhubuti ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa China na Afrika na kuimarisha ushirikiano wa kitamaduni, na hata kuimarishwa mawasiliano ya watu. Bibi Wang anaona kuwa hadhira ya Afrika itapata picha halisi na ya wazi ya China ya sasa, tofauti na ile inayopotoshwa na nchi za magharibi.
Balozi wa China nchini Kenya Guo Haiyan, amekumbusha kuwa tamthiliya na filamu hizo, vinawapa watazamaji picha halisi ya mambo yanayoendelea nchini China kupitia mada kama vile ufufuaji wa vijijini, ulinzi wa ikolojia, na utamaduni wa jadi, mambo ambayo ni sehemu ya China ya sasa.
Pamoja na ukweli kwamba China na Afrika zinashirikiana kwenye sekta ya habari, bado kuna changamoto nyingi za kufahamisha mambo ya kila upande kwa upande mwingine, na hii ni fursa ya ushirikiano zaidi kati ya pande hizo mbili.