Wasalaam,
Nilipokuwa kidato cha tatu, mwanafunzi mwenzetu alijiua kwa kunywa vidonge 16 vya chloroquine.
Binti huyo aliyekuwa akiitwa Rebeka, alikuwa mzuri wa sura, umbo, na tabia na kwa kweli hakuna hata mtu mmoja aliyewaza kuwa mrembo huyo angeweza Kujitoa roho kikatili hivyo. Kifo chake kilizua mtafaruku mkubwa mno katika familia, lakini kubwa zaidi ni kuwa kanisa lake lilimsusa. Rebeka alikuwa Mkatoliki (RC) na kwa taratibu za kanisa hilo mtu akijiua anakuwa ameikana imani, hivyo hawezi kuzikwa Kikristo.
Ndugu zake walizunguka makanisa kadhaa kutafuta Padre wa kumzika, lakini wote walikataa. Padre mmoja mzee kwa jina la Werawera alipoambiwa tu habari za msiba huo mara moja akakubali kuongoza mazishi bila kipingamizi.
Ajabu baadhi ya waumini wakageuka kumlaumu Padre huyo kwa kukiuka taratibu za kanisa. Wakati wa ibada ya mazishi, ndipo padre huyo akatueleza sababu zilizomsukuma kuja kumzika binti huyo aliyejiua. Akasema “Mama mmoja alikuwa na mume mlevi sana. Kila siku mwanaume huyo alienda kilabuni kunywa pombe na kurudi nyumbani usiku. Kwa vile mama huyo alikuwa Mcha Mungu, hakuweza kumkimbia mumewe; bali kila siku alimuombea kwa Mungu ili abadilike na kuwa mcha Mungu kama yeye.
Lakini siku moja mumewe alipokuwa akivuka daraja kuelekea kilabuni aliteleza na kudumbukia mtoni, akafa maji. Kifo hicho kilimuumiza sana yule mama Kila siku alimlilia Mungu kwa kutosikia maombi yake, na kumuacha mumewe kufa akiwa mlevi, jambo linalothibitisha kuwa amekwenda jehanam.
Lakini siku moja wakati huyo mama amekaa peke yake akisononeka, mpita njia mmoja akamwambia, mama bado unasonononeka kwa ajili ya mumeo? Yule mama akasema ndiyo, na sisononeki kwa sababu amekufa, bali kwa sababu amekwenda jehanam, maana amekufa akiwa mlevi. Yule mtu akamwambia “Mama jiombee nafsi yako wewe, mumeo amemaliza safari yake na yuko peponi” Mama akasema HAIWEZEKANI alikuwa mlevi sana, na alikufa akienda Kutafuta pombe. Yule mtu akamwambia “ mama, alipokuwa akianguka mtoni, katikati ya daraja na maji ALITUBU dhambi zake” halafu yule mtu akatoweka. Kumbe alikuwa ni malaika mjumbe wa Mungu.
Padre akasema mara nyingine tunajipa nafasi ya Mungu na kupora haki ya kuhukumu ambayo ni Kazi ya Mungu tu. Si ajabu tunawazika kwa heshima wale walio machukizo kwa Mungu kwa sababu walifanikiwa kutuhadaa, na tunawadhihaki wale ambao mwenyezi Mungu amewapokea kwa sababu mioyo yao haikuwa na hila, au Walijaliwa KUTUBU kabla mauti haijawachukua. Ni Mungu tu ajuae KWA HIYO Kabla hujasema maneno mabaya kwa mtu aliyekufa, jiulize kama kweli una macho yanayoweza kuona SIRINI kama Mungu.
Inafaa sana KUMKEMEA VIKALI mtu yeyote anayetenda uovu wakati AKIWA HAI ili aziache njia zake mbaya. Lakini akishakufa hawezi kusikia wala kujirekebisha Hivyo hakuna haja ya kumtukana. Matusi kwa marehemu hayamuumizi yeye, bali wana familia yake ambao kimsingi hawana hatia yoyote. Mkaidi achapwe viboko akiwa hai, kwani maiti haijali hata ukali wa moto.
Kujiua sio suluhisho la kutatua matatizo yako.
UWE NA AMANI
1. Kinachozikwa ni mwili sio roho. Mwanadamu ni mavumbi tu na huko atarejea bila kujali ni mdhambi au mwenye haki. Rejea Biblia Takatifu:
Mhubiri 2
15 Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
16 Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu!
2. Utaratibu wa ibada ya Mazishi ni wa kidunia wala hauna uhusiano na mbingu. Tunausindikiza "mwili" kaburini lakini mwenye huo mwili huwa hayupo hapo. Kwa hiyo basi, hadhi ya huo mwili ni sawa tu, haijalishi kama amekufa kwa ukimwi, au ajali, au usingizini nk.
Sasa Mungu anashughulika na roho. Hata kama tungefanya ibada mara mia kuombea marehemu, Mungu anashughulika na roho. Hizi habari za KUNYIMWA HUDUMA YA MAZISHI kwa sababu eti hukuhudhuria ibada mara kwa mara, au umejinyonga, ni hofu za kidunia kabisa, wala hazina uhusiano na Mungu. Ni mbinu mojawapo ya kuwalazimisha watu wawe na mafungamano na dini.
3. Kuhusu kujinyonga, hili ni dhambi mbele za Mungu. Why? Kitendo cha kuwazia kuutoa uhai tayari ni dhambi ya kuua na shetani ameshakata roho. Hebu tuichambue dhambi hii:
>> ni dalili dhahiri za kutokuwa na imani kwa Mungu. Kwamba Mungu anasamehe, au ana uwezo wa kubadili majira mabaya kuwa mazuri.
Waebrania 11
6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
Habari za Danieli ana wengine wengi kwenye Biblia zimelenga kutupatia ujasiri katika Mungu kwamba tukiamini tu, atatujibu.
>> ni kuliharibu hekalu la Mungu.
1 Wakorintho 3
16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Hii miili yetu sio mali yetu bali ni yake Yeye aliyetuumba. Kujaribu kubadili matumizi yake kwa namna yoyote ile ni kuhujumu mpango wa aliyeiumba.
4. Kuhusu kutubu. Mungu ni mwingi wa rehema, mtu akitubu kww kumaanisha atamsamehe dhambi zake zote. Sasa mtu aliyokusudia kujinyonga tayari amekwisha tenda dhambi hiyo:
Mathayo 5
21 Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.
22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.
Kumbe kule kuwa tu na wazo la kujiua NI DHAMBI YA KUJIUA. Hizi ndizo amri za ufalme wa Mungu. Hazihukumu kitendo bali nia ya kutenda. Hazihukumu mwili bali mawazo yaliyo rohoni. Sasa kama mtu yuko hewani wakati ameamua kujirusha ghorofani, ndipo akabadili mawazo kabla ya kufika chini, hilo Mungu ndiye ajuaye. Kwamba mtu anapata wazo la kuzini, hashtuki kama ni dhambi, anatongoza mke wa jirani yake, haoni dhambi, wanapanga tarehe na saa ya kuzini, bado tu haoni, siku ikifika anazunguka mji mzima kutafuta gesti ya mafichoni, hajajua tu kama dhambi inamtafuna, anaingia na mke wa mtu kwa kujificha ili asionekane chumbani, bado tu!! Halafu wakati akiwa katikati ya tendo la ngono ndipo fahamu zinamrudia, ghafla anagundua kuwa anatenda dhambi, anafanya toba.
Sasa Yesu Kristo alileta sheria za ufalme, sheria ambazo zilikuja kuthibitisha kuwa torati asili yake ni rohoni. Mwana wa ufalme wa Mungu HAWEZI KUFIKIA KUTENDA HAYO. Dhambi itabinywa mapema tu, kabla ya kufika kwenye tendo na maungamo yatafanyika. Huo ndio ufalme aliohubiri Kristo.