Kila ifikapo Julai 7 ya kila mwaka, dunia inaadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, ikiienzi mojawapo ya lugha zenye ushawishi mkubwa na zinazozungumzwa zaidi barani Afrika. Siku hii mbali na kusherehekea utamaduni wa Kiswahili, pia inaangalia umuhimu unaoongezeka wa Kiswahili katika mawasiliano ya kimataifa, elimu, diplomasia, biashara, na maendeleo endelevu.
Wakati huohuo kadri utandawazi unavyoendelea kubadilisha masoko ya kimataifa, taasisi na mashirika mbalimbali nayo yamekuwa na upeo wa mbali wa kuangalia lugha za kitamaduni, ili kushirikisha hadhira mbalimbali. Kiswahili kimeibuka kuwa lugha muhimu kwa makampuni yanayopanuka ndani ya Afrika Mashariki, mashirika ya maendeleo ya kimataifa yanayofanya kazi kote barani Afrika, na taasisi zinazotafuta ushirikiano wenye maana na mamilioni ya wazungumzaji wa Kiswahili.
Ikitambuliwa na UNESCO kama lugha ya kwanza ya Afrika kupangiwa Siku ya Lugha ya Kimataifa, Kiswahili kinawakilisha zaidi ya njia ya mawasiliano. Kinatumika kama daraja linalounganisha tamaduni, kurahisisha biashara, kusaidia mafungamano ya kikanda, na kuhifadhi urithi uliosheheni wa lugha inayoivutia mataifa mengi.
Miongoni mwa mataifa yanayovutiwa na lugha hii ya Kiswahili ni China. Kwani idadi ya raia wa China wanaojifunza Kiswahili inaongezeka kwa kasi siku hadi siku. Kiswahili kwa Wachina kinawakilisha hamu inayokua ya kuujua utamaduni wake, kuheshimiana, na mawasiliano ya kielimu kati ya China na nchi zinazozungumza Kiswahili za Afrika Mashariki.
Mwaka huu ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra zilizoanza mapema za kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani, chuo cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU) kupitia kitivo cha Lugha za Afrika kiliandaa mashindano ya wanafunzi Wachina wanaojifunza Kiswahili katika vyuo vya China, yaliyopewa jina la "Shindano la Kutia Sauti Lugha Mbalimbali: Kwa Wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Sauti ya Afrika 2026," wakitia sauti kwa Kiswahili filamu mbalimbali za Kichina, Kiingereza hata za Kiswahili pia.
Mashindano haya sio tu yalionesha weledi wa wanafunzi Wachina wa kuzungumza Kiswahili bali pia yalionesha namna Wachina wanavyofuatilia kwa undani jinsi ya kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha, matamshi ya lugha, lafudhi, usahihi, semi na uelewa wa utamaduni. Mashindano haya yalishuhudiwa yakiibua vipaji mbalimbali vya wanafunzi Wachina, na kuhitimishwa kwa kutolewa tuzo mbalimbali kuanzia ya mshindi wa jumla, wa kwanza hadi wa tatu.
Lakini mbali na vyuo mbalimbali vya China kufunza Kiswahili, walimu Wachina wanaofundisha Kichina katika Taasisi ya Confucius iliyopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nao wengi wao wanaonesha shauku ya kutaka kuijua lugha hii ambayo sasa ina wazungumzaji zaidi ya milioni 200 duniani.
Yang Xin, mwalimu wa lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius, anasema kujifunza Kiswahili kuna changamoto zake na umuhimu wake. Akiwa kama mgeni yeyote yule wa lugha, anasema mwanzoni hakuweza kuelewa chochote kile. Baada ya kujifunza kwenye Taasisi ya Confucius, sasa amezoea maisha ya Tanzania na kuweza kuwasiliana na wenyeji vizuri.
Mwalimu mwingine wa Kichina Zou Zhenzhen, anatilia mkazo maneno hayo, akisema hata kutumia maneno machache tu ya Kiswahili darasani kunaleta tofauti kubwa. Inaonesha wanafunzi kwamba tunaheshimu utamaduni wao, na inawafanya wafurahi zaidi kujifunza Kichina.
Kwa mujibu wa mwalimu wa lugha ya Kichina wa Tanzania anayefunza katika Taasisi ya Confucius, Emmanuel Legonga, ambaye pia huwa anafundisha Kiswahili kwa Wachina nchini Tanzania, kuzungumza lugha ya wenyeji yaani Kiswahili, kunaleta matokeo mazuri katika sekta zote. Akitolea mfano wa miradi ya miundombinu kama vile reli na bandari, anasema mameneja au wahandisi wa China wanapotumia Kiswahili, hujenga uaminifu na wafanyakazi wenyeji na pia kuondoa umbali baina ya wenyeji na wageni na hatimaye wafanyakazi wanahisi kwamba wanaonekana na kuheshimiwa.
Wakati jumuiya ya kimataifa inapoadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani Julai 7, moyo wa siku hii ulionekana waziwazi katika Chuo Kikuu kikubwa zaidi chenye Taasisi ya Confucius nchini Tanzania, ambapo raia wa China walikuwa wakikumbatia Kiswahili si kama lugha tu bali kama mlango wa kuelewa maisha ya wenyeji.
Kiswahili, ni mojawapo ya lugha zinazozungumzwa zaidi barani Afrika, kikitumika kama lugha ya biashara na mawasiliano kwenye eneo ambalo lina lugha nyingi mbalimbali, ambayo inazungumzwa kote Afrika Mashariki na Kati. Tunaposherehekea Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, pia tunasherehekea nguvu ya lugha kujenga mahusiano, kupanua fursa, na kuwaleta watu karibu zaidi hadi nje mipaka.