Date::4/13/2010 Tumejiandaa kutibua sherehe Simba- Yanga
Jessca Nangawe
SIKU tatu kabla ya pambano baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga wachezaji wa Yanga wameibuka na kuanza kutamba kuwa watapunguza furaha ya ubingwa ya wapinzani wao.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti,wachezaji hao walisema ili kupunguza furaha ya wanasimba na Msimbazi kwa jumla, wao wana jukumu la kuwafunga katika mchezo huo wa Jumapili usiku.
"Ni lazima tuhakikishe tunashinda mchezo huo unaosubiriwa na mashabiki wengi kwani tutakuwa tumejiwekea heshima licha ya kuwa mwaka huu tumeny'ang'anywa ubingwa," alisema mchezaji mwandalizi wa klabu hiyo.
Huku akiungwa mkono na wenzake kadhaa, alisema wanajipanga vizuri ili kuhakikisha mchezo huo wa Jumapili wanashinda kwa namna yoyote ile na mbali ya wapinzani wao kuwa tayari wamejitangazia ubingwa wamedai wanaamini kushinda kwao kutapunguza furaha kwa Simba kwani ni mchezo wa kuweka heshima.
"Tunajipanga kuhakikisha tunashinda katika mchezo wetu na Simba Jumapili na ili kulinda heshima ni kutimiza lengo letu la kuwafunga Simba licha ya wao tayari wamejitangazia ubingwa mapema, tutahakikisha tunawapunguzia furaha yao,"alisema Boniface Ambani.
Naye beki Nurdin Bakari alisema ili kulinda heshima ya Yanga katika mchezo unaohusisha timu hizo mbili kongwe, watahakikisha wanashindana kwa wao wote na kuahidi kutoa ushirikiano baina yao na kocha wao (Kostadin Papic) ikiwa ni pamoja na kuongeza juhudi baina yao ili waweze kutimiza azma yao ya kushinda katika mchezo huo.
Naye mshambuliaji Mrisho Ngasa ambaye anawania nafasi ya ufungaji bora akiwa na mabao 14 sawa na Mussa Hassan Mgosi wa Simba na John Boko wa Azam alisema ushindi dhidi ya Simba ndio utakuwa nafasi yake ya kuchukua kiatu cha dhahabu kwa kuwapita wapinzani wake hoa wawili.
Alisema atajitahidi na kuhakikisha siku hiyo anafunga goli ili kuzidi kuwakimbia wapinzani wake na kujitengenezea
mazingira mazuri ya kuvaa kiatu hicho msimu huu.
Mchezo huo uliokuwa uchezwe Jumapili iliyopita uliahirishwa kwa sababu ambazo zimekuwa zikidaiwa kuwa za kiusalama zaidi kutokana na klabu hizo kutaka kutumia Uwanja wa Uhuru huku serikali ikitaka ule wa Taifa.
Tayari Simba wametangaza ubingwa baada ya kufikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikishwa na timu yoyote ikiwamo Yanga yenye pointi 48.
Simba, kwa upande wao wamekuwa kambini visiwani kwa maandalizi ya mchezo huo ingawa habari zilizopatikana juzi zilieleza kuwa kocha wao, Patick Phiri amesafiri kwenda kwao, Zambia kwa sababu binafsi akiacha jukumu hilo kwa msaidizi wake,Amri Said.
Simba ambayo haijapoteza mchezo msimu huu imedhamiria kuendeleza rekodi yake.
Kiingilio cha juu cha mchezo huo kitakuwaSh 40,000 na kile cha chini kikiwa Sh5,000.