[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: contentheading, width: 100%"]Usajili:Simba wamchomoa Walulya, wamrudisha Okwi [/TD]
[TD="class: buttonheading, width: 100%, align: right"]
Send to a friend [/TD]
[/TR]
[/TABLE]
[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: createdate"] Wednesday, 20 July 2011 20:54 [/TD]
[/TR]
[TR]
[TD] 0digg
Mwandishi Wetu
SIMBA imeliondoa jina la beki wake wa Uganda, Derick Walulya katika usajili iliowasilisha kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na badala yake imemrudisha kundini, Emmanuel Okwi.
Makamu Mwenyekiti Geofrey Nyange 'Kaburu' aliliambia Mwananchi jana kuwa, sababu kubwa iliyowafanya kumtoa Walulya ni majeruhi ambayo yatamuweka nje kwa miezi miwili.
"Okwi alikwenda kwenye majaribio sehemu mbalimbali, lakini ni kama ameshindwa, hivyo kwa sababu Walulya atakuwa nje kwa miezi miwili, tumeona ni bora nafasi hiyo achukue Okwi. Hata hivyo Walulya ataendelea kupata huduma zote za Simba kwani bado ni mchezaji wetu," alisema Kaburu.
Ukiondoa Okwi, wachezaji wengine wa kigeni wa Simba ni Jerry Santo (Kenya), Patrick Mafisango (Rwanda), Gervais Kago (Jamhuri ya Afrika ya Kati) na Felix Mumba Sunzu (Zambia).
Awali, Kocha Mkuu wa Simba, Moses Basena alisema hafahamu kinachomsumbua Okwi kwa sababu alijaribu kumtafuta mjini Kampala, lakini hakumpata.
Basena alikuwa mjini Kampala kwa mapumziko mafupi ya wiki moja baada ya kumalizika mashindano ya Kagame na hivi sasa yupo na kikosi cha Simba jijini Da es Salaam akikinoa kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu 2011/2012.
"Nilijaribu mara nyingi nilipokuwa Kampala kumpigia simu Okwi, lakini alikuwa hapokei simu zangu,"alisema kocha wa Simba.
Alisema,"Sijui ni nini kimemsibu kijana Okwi na sifahamu kwa nini alikimbia katika klabu ya Kaizer Chiefs alipokuwa amekwenda kufanya majaribio nchini Afrika Kusini, lakini Okwi kwa sasa ni mtu mzima na anajua afanyalo."
Hata hivyo; kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, kocha Basena alikiri kwamba Okwi yupo mjini Kampala.
Pia, kwa mujibu wa gazeti hilo, kocha wa Kaizer Chiefs, Vladimir Vermezovic alishangazwa na Okwi ambaye alivutiwa naye baada ya kufanya majaribio kwa wiki moja mwisho wa msimu uliopita, lakini Okwi hakuenda kwa mara ya pili kama alivyotakiwa kufanya na klabu ya Kaizer Chiefs mwezi uliopita.
Vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimekuwa vikilizungumzia tukio hilo huku vingine vikisema Okwi yupo nchini Uturuki akifanya majaribio, lakini gazeti la Daily Monitor la Uganda lenyewe limesema Okwi alikwenda Afrika Kusini na kukaa siku moja Afrika Kusini kabla ya kumuambia wakala wake Ivica Stankovic kwamba anarudi nchini Uganda kwa mazishi ya ndugu yake.
Gazeti hilo la Uganda pia limemnukuu makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange Kaburu akisema,"Tupo katika mchakato wa kumuuza Emmanuel Okwi katika klabu nyingine."
Pia, gazeti hilo limesema Okwi ambaye ana mkataba na Simba mpaka 2014 ameachwa kwenye usajili wa Simba msimu wa 2011/12.
Okwi alitakiwa afanye majaribio kwa mara ya pili na klabu ya Kaizer Chiefs ambayo ilionyesha nia ya dhati ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo hatari akiwa karibu na lango.
Wakati huo huo; Calvin Kiwia anaripoti kuwa beki chipukizi wa Simba, Shomari Kapombe ameitaka timu yake ya zamani Polisi Morogoro kuacha kumwekea vikwazo kwenye usajili wake kwani alishamalizana nao toka kumalizika kwa fainali za Ligi Daraja la Kwanza.
Hayo yamekuja baada ya klabu hiyo kuwasilisha barua katika shirikisho la soka chini, TFF kuweka pingamizi usajili wa kinda huyo.
Kapombe aliliambia Mwananchi jana jijini Dar es Salaam kuwa alishamalizana na timu hiyo toka pale Ligi Daraja la Kwanza hatua ya fainali ilipomalizika, lakini anashangaa uongozi wa timu hiyo umemwekea pingamizi kwenye usajili wake.
"Nilisaini fomu za kuichezea Polisi Morogoro mpaka Ligi Daraja la Kwanza hatua ya fainali itakapomalizika, lakini nashangaa wanataka nini tena kwangu wakati makubaliano yetu yameshamalizika,"alisema Kapombe.
Alisema anautaka uongozi huo uachane naye kwani tayari makubaliano yao yalishamalizika tangu kumalizika kwa Fainali za Ligi Daraja la Kwanza zilizofanyika jijini Tanga kuanzia Januari 30 hadi Februari 22 mwaka huu.
"Sina mkataba na Polisi Morogoro nawaomba waniache niweze kucheza mpira kama kazi yangu ambayo naamini ipo siku moja itaninufaisha na kuwa na maisha bora kama walivyo wengine," alisisitiza Kapombe. [/TD]
[/TR]
[/TABLE]