Saint Ivuga
JF-Expert Member
- Aug 21, 2008
- 54,762
- 59,204
- Thread starter
- #361
Dar Young Africans
Kocha wa zamani Yanga atishia kushtaki Fifa
UONGOZI wa Yanga unadaiwa kumpiga chenga na kutomlipa aliyekuwa kocha msaidizi wa klabu hiyo, Spaso Sokolovski mishahara yake ya miezi saba, jambo ambalo limemlazimisha atishie kuishtaki klabu hiyo kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa.
Raia huyo wa Serbia ameiambia Mwananchi kuwa anadai mshahara wake unaofikia dola 6,000.
Alisema fedha hizo ni mshahara wake wa miezi saba tangu kusitishwa kwa mkataba wake pamoja na aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Dusan Kondic mwishoni mwa mwaka jana.
Sokolovski amekuwa akisota kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akitaka shirikisho hilo limsaidie kupata haki yake kutoka kwa uongozi wa Yanga.
Alisema, "Nimechoka kuvumilia, kila siku wamekuwa wananipa ahadi za uongo, ona kama leo, tuliahidiana na Mwalusako Lawrence, ambaye ni katibu mkuu waYanga, tukutane hapa (TFF) wathibitishe kwa maandishi ni lini watanilipa, lakini matokeo yake siwapati kwenye simu,"alilalama Mzungu huyo juzi.
"Nawapa siku mbili kama wataendelea kunizungusha, nitachukua hatua za kuwasiliana na wakili wangu, kisha nitashtaki Fifa, nashukuru TFF ipo upande wangu, nikiwashtaki Fifa klabu itafutwa kama ilivyofanyika kwa klabu moja ya Brazil.
Wao walimfanyia kocha kitendo kama wanachonifanyia Yanga hivi sasa, Fifa iliifuta ile klabu, ikabidi ishuke daraja na ibadili jina, nawaambia Yanga wasipoangalia,sitashindwa kuwashtaki Fifa,"alisisitiza.
Alisema tangu Yanga ivunje mkataba wake amekuwa akiishi maisha ya shida akisaidiwa na rafiki zake pamoja na TFF, kitendo ambacho kinampa simanzi kubwa ukizingatia ana familia inayomtegemea.
Hata hivyo, kocha huyo amedai kuwa tayari ameingia mkataba na timu ya Shanghai China ili ainoe timu hiyo.
Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela akizungumzia suala hilo alisema, "Tupo kwenye mazungumzo na Yanga, na tunataka wathibitishe kwa maandishi watamlipa lini kocha wa watu hizo haki yake ili aondoke kwa amani na usalama, wasiharibu sifa ya nchi,"alisema Mwakalebela. Katibu Mkuu wa Yanga, Mwalusako akizungumzia suala hilo alisema, "Tumeshaongea na TFF na tumewaambia baada ya mechi yetu na Lupopo tutafanya taratibu za kumlipa na tumeshamuarifu fedha zake atazichukulia TFF."