BEFORE I DIE
SEHEMU YA 23
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Jennifer amekwenda kuwachukua” akajibu yule msichana
Hata sekunde ishirini hazikupita wakatokea Sabrina na Grace wakiwa ndani ya suti nzuri nyeusi na kofia .Wakakaribishwa mezani na wahudumu wale wenye adabu .Innocent bado aliendelea kushangazwa na mambo yaliyomo ndani ya jumba lile.Latoya alikuwa akiheshimiwa kama malkia.
“Sabrina nomba utuongozee maombi ya chakula tafadhali.” Latoya akasema na wote wakafumba macho Grace akatoa maombi mafupi kukiombea chakula kile halafu Latoya akawakaribisha .
“Huyu hawezi kuwa kiumbe wa kiroho kama ninavyodhani kwani viumbe wale hawapendi maombi” akawaza Innocent huku akiweka chakula katika sahani yake
“Innocent hiyo ni pili pili samahani .Nafahamu kwamba hutumii pilipili kabisa” Latoya akamweleza Innocent mara tu alipomuona amelishika bakuli lililokuwa na pilipili iliyokuwa imetengenezwa vizuri.Innocent akashangaa na kuuliza huku aitabasamu
“Umejuaje kama situmii pili pili ?
Latoya akatabasamu na kusema
“Nilipewa vidokezo na Sabrina kwamba hutumii kabisa pilipili”
Wote wakaangua kicheko
ENDELEA……………………………
“Jenniffer naomba mkaendelee na shughuli nyingine.Nina maongezi kidogo na ndugu zangu” Latoya akawaambia wale wahudumu waliokuwa wakiwahudumia .Wakaondoka na kwenda kuendelea na shughuli nyingine.
“Innocent,Sabrina na Grace,kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi hii kutoa pole nyingi kwa msiba uliotokea.Naomba mfahamu kwamba msiba huu ni wetu sote .Marina alikuwa ni rafiki wa Innocent ambaye ni kaka yetu na rafiki yetu.Kwa maana hiyo Marina pia alikuwa ni rafiki yetu sote.Naomba msiendelee kusema kwamba Marina hakuwa na ndugu hapa mjini.Ndugu zake wapo.Ndugu zake ni sisi .Kwa bahati mbaya sote tumemfahamu katika nyakati za mwisho za uhai wake.Laiti kama tungeweza kufahamiana naye kwa muda mrefu kabla tungeweza kufanya kitu kikubwa cha kuweza kumsaidia.Ni mapenzi ya mungu iwe hivi kwa sababu juhudi zilizofanywa na Innocent ni kubwa lakini Mungu alimpenda zaidi.Napenda niwahakikishie kwamba marina atasitiriwa kwa heshima kubwa tofauti na alivyokuwa akiishi.” Latoya akatulia kidogo na kuchukua glasi ya juice akanywa kisha akasema
“Jambo la pili ninapenda sana kuwakaribisha nyumbani kwangu.Hapa ni nyumbani kwangu .Ndipo ninapoishi.Nafahamu nyote bado mnaogopa nadhani ni kutokana na ukubwa wa jumba hili.Tafadhali naombeni msiogope.Jisikieni nyumbani.Masaa ishirini na manne ukihitaji kitu chochote kile kuna wahudumu wa kuwahudumia.Ninafurahi mno kuwa nanyi hapa saa hizi .Hakuna awezaye kuona furaha ya kuwa nanyi.Ninyi ni ndugu zangu .Kwa kuwa bado tuko katika kipindi cha majonzi sitaki kuongea mengi kwani bado tuna mambo mengi sana ya kuongea baada ya kumaliza msiba.Narudia tena kuwaomba kwamba jisikieni mko nyumbani.” Latoya akanyamaza tena akanywa juice yake na kuendelea
“jambo la tatu ni kwamba baada ya kumaliza kupata chakula tutakwenda kuonana na kuwasalimu waombolezaji ambao ni rafiki zangu na watu wangu wa karibu ambao kwa sasa naomba muwahesabu ni moja ya marafiki zenu pia .Wote hawa wamekuja kuungana nasi katika kuomboleza msiba huu tulioupata.Wengi wao watakesha pamoja nasi siku ya leo na watakuwa nasi mpaka hapo tutakapohitimisha msiba huu.Nategemea siku ya kesho idadi ya watu kuongezeka zaidi kwa sababu taarifa hizi za kuwapo kwa msiba hapa nyumbani kwangu zinasambaa kwa kasi sana.Baada ya kukaa na waombolezaji kwa muda mfupi,tutarejea ndani ili Innocent aweze kupata muda wa kupumzika,lakini kabla ya kupumzika tutakaa na viongozi wa kampuni niliyowakabidhi kazi ya kushughulikia msiba huu ambao wanahitaji maelekezo kadhaa toka kwetu.Kuna baadhi ya mambo kadhaa ambayo yalikuwa nje ya uwezo wangu kuyatolea maamuzi.masuala kama ya imani ya dini,sehemu ambayo ingependelewa kwenda kumsitiri marehemu na maelekezo mengineyo kama yatakuwepo.Kwa hiyo sisi kama ndugu wa marehemu, tutakaa na viongozi wa kampuni ile na kuwaelekeza mambo hayo ikiwamo siku gani tungependelea kumzika marehemu” latoya akatoa maelekezo .
Baada a kumaliza kupata chakula Latoya akawaongoza kuelekea bustanini ambako shughuli za msiba zilikuwa zikiendelea.Muziki wa maombolezo uliokuwa ukiwafariji waombolezaji ulikuwa ukipigwa na bendi maalum iliyoletwa kwa ajili ya shughuli hiyo.Kwa mbali mawimbi ya bahari yalikuwa yakisikika.Upepo mzuri wa bahari ulikuwa ukivuma na kuelekea mahala iliko bustani ile nzuri iliyokuwa imepambwa kwa maua na miti mizuri.Pamoja na familia yao kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha lakini Innocent hakuota hata siku moja kama kuna watu hapa nchini Tanzania wanaishi maisha kama aliyoyaona hapa kwa Latoya.Bado aliendelea kushangazwa na kila kitu alichokiona.
“Ndugu waombolezaji,mabibi na mabwana watu tuliokuwa tukiwasubiri tayari wamefika..” Ilikuwa ni sauti ya muongozaji wa shughuli ile mara tu alipopewa taarifa kwamba Latoya na akina Innocent walikuwa wakija pale bustanini.
Watu wote pale bustanini wakasimama.Latoya akawaongoza akina Innocent,Grace na Sabrina hadi mahala walikokuwa wameandaliwa.Wakaketi katika sofa nyeusi .Innocent akastaajabu idadi ile kubwa ya watu waliokuwa wamekuja katika msiba wa Marina ndani ya kipindi kifupi namna ile cha kupata tarifa za kufariki kwa Marina.Wote walionekana ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha.Walikuwepo pia watu wa mataifa tofauti kama wazungu ,na wahindi.
“ watu wote hawa wamefika hapa baada ya kupata taarifa kwamba Latoya amefiwa.Nikiwaangalia nawaona wote ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Nina kila sababu ya kumfahamu kiundani mtu huyu.Amenifanya nisahau kama nina msiba mkubwa na kubaki nikimuwaza yeye na maisha yake ya kushangaza.Sikutegemea kama msiba wa Marina binti masikini anayejiuza mtaani ungewakusanya watu wazito namna hii.Yote imewezekana kwa sababu ya Latoya.” Akawaza Innocent wakati Latoya akijadiliana jambo na muongozaji wa shughuli.
Baada ya majadiliano mafupi Latoya akasimama akaongozana na muongoza shughuli hadi katika jukwaa dogo
“ndugu waombolezaji,naomba tafadhali tumsikilize ndugu yetu,mpendwa wetu Latoya anataka kuongea nasi machache" akasema muongoza shughuli
“ Ndugu waombolezaji,sipati neno la shukrani kwenu nyote ambao mmefika kuungana nasi mara tu baada ya kupata taarifa za msiba huu.Mimi na ndugu zangu wote tunawashukuru sana kwa kuja kuungana nasi katika usiku huu mgumu kwetu na hadi pale tutakapohitimisha safari ya mwisho ya mpendwa wetu Marina.Napenda nichukue nafasi hii niliyopewa ya kusema maneno machache,kuwaelezea kwa ufupi kuhusiana na msiba huu.Leo mchana tumempoteza ndugu yetu,mdogo wetu aitwaye Marina.Ndugu yetu huyu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo na alifariki akiwa katika maadalizi ya kufanyiwa upasuaji ili abadilishiwe figo.Ndugu yangu Innocent ambaye ni yule pale mnayemuona alikuwa amejitolea figo yake ili awekewe ndugu yetu huyu lakini pamoja na jitihada zote hizo Marina alifariki dakika chache kabla ya upasuaji huo kufanyika.Ni msiba mkubwa sana umetupata mimi na ndugu zangu kwa sababu Marina amefariki akiwa bado mdogo .Amefariki akiwa ni binti wa miaka kumi na tisa.Hii yote ni kazi ya Mungu na siku zote kazi ya Mungu haina makosa.Bwana ametoa na na bwana ametwa.Jina lake lihimidiwe.Amen”
Watu wote wakaitika
“Amen”
Baada ya muitikio ule Latoya akaendelea
“Kwa niaba ya ndugu zangu,ninapenda kwa mara nyingine tena niwashukuru wote mliofika na kujumuika nasi katika msiba huu.Naomba moyo huo wa upendo mlio nao muendelee nao na Mungu awabariki .kwa kuwa ndugu yangu Innocent amechoka sana baada ya shughuli zote za hospitali ninaomba mumruhusu akapumzike na sisi wengine tuendelee na maombolezo .Kesho ratiba nzima itatolewa kuhusiana na msiba huu.Ahsanteni sana.”
Latoya akamaliza kuongea machache akarejea katika sehemu waliyokuwa wameandaliwa akamshika mkono Innocent wakaelekea ndani na kuacha maswali mengi miongoni mwa waombolezaji.Ilikuwa ni mara ya kwanza Latoya kuonekana akimshika mkono kijana wa kiume na kutembea pamoja.Kwa wengi waliomfahamu Latoya ilikuwa ni jambo la ajabu na la kushangaza sana .Kingine kilichowapa maswali mengi ni kutoonekana kwa wazazi wa Latoya msibani.Wengi walitegemea kwamba kwa kuwa msiba ule ni wa familia basi wazazi wa Latoya wangekuwepo msibani lakini wakashangazwa na kutomuona hata mzazi mmoja.Bado maswali kuhusiana na maisha ya Latoya yakazidi kuongezeka.
Latoya,Innocent ,Grace na Sabrina walitembea taratibu kuelekea ndani na kuwaacha watu wakiendelea na maombolezo.Kulikuwa na vinywaji vya kila aina,chakula cha kila namna kilikuwa kikipatikana.Matajiri walikuwa wakishindana katika kujitolea michango mbali mbali kwa ajili ya msiba ule.Gari zilizobeba vinywaji zilikuwa zikiingia na kuteremsha masanduku yaliyojaa vinywaji vya kila namna.Ilikuwa ni zaidi ya msiba.
“Innocent pamoja na kwamba umechoka na unahitaji kupumzika lakini kuna wawakilishi toka ile kampuni niliyoikabidhi kazi ya kushughulikia msiba huu wako tayari wakitusubiri.Naomba tuongee nao machache halafu uende kupumzika” Latoya akamweleza Innocent
“hakuna taabu Latoya.” Innocent akajibu kwa ufupi na moja kwa moja wakaelekea katika ukumbi ambao wawakilishi wa kampuni ile ya mazishi walikuwa wamekaa wakiwasubiri.
Mara tu walipoingia katika ule ukumbi mdogo ambao uliotumika kwa mikutano midogo,watu wote wapatao saba wakasimama ili kuonyesha heshima na Latoya akawafanyia ishara waketi.Akakohoa kidogo na kusema
“Ndugu zangu nawashukuru sana kwa kazi nzuri mliyoifanya toka nilipowapa taarifa ya msiba.Mmefanya kazi kubwa na kwa haraka licha ya idadi ya watu kuwa kubwa.Sikutegema kama kungekuwa na idadi hii kubwa ya watu namna hii .Sielewi hata taarifa hizi zinasambaa vipi kwa watu.” akasema Latoya
“Madam , hata sisi tunashangaa sana kwa jinsi taarifa zinavyosambaa kwa kasi.Tulitegemea kungekuwa na watu wachache lakini imekuwa tofauti kabisa.Tumeshangaa kuona idadi hii kubwa ya watu iliyofika kwa jioni hii.Kwa hali inavyoonekana ,siku ya kesho kutakuwa na idadi kubwa ya watu kwani kadiri muda unavyozidi kusonga taarifa zinazidi kusambaa.” Akasema mtu mmoja mnene ..
“Ok ! hakuna tatizo ila jitahidini kudhibiti idadi ya watu kwani eneo letu haliwezi kuhimili mkusanyiko mkubwa wa watu.Kwa ufupi tu ningependa kuchukua nafasi hii kumtambulisha kwenu ndugu yetu Innocent.Ndugu yetu huyu ndiye aliyekuwa na marehemu hadi dakika za mwisho za uhai wake na ndiye aliyekuwa amejitolea figo yake awekewe marehemu Marina.Innocent walioko mbele yako ni wawakilishi toka kampuni inayoratibu na kusimamia shughuli zote za msiba huu Kwa kuwa Innocent amechoka kutokana na pilika pilika nyingi za siku ya leo ,anahitaji kwenda kupumzika,kwa maana hiyo tunahitaji kuongea kwa kifupi sana kuhusu masuala ya muhimu ya msiba kwa usiku huu.Ningependa kwanza kupata taarifa wapi mlipofikia kuhusianana maandalizi ya mazishi na kama kuna tatizo lolote hadi hivi sasa.”
Sylivester kushishi ambaye ndiye alikuwa kiongozi akafungua faili lake na kusema
“Madam Latoya,mpaka sasa hivi tumekwisha kamilisha kila kitu kwa asilimia tisini.Watu wengi wamekuwa wakijtolea vitu mbalimbali kwa hiyo mpaka sasa hivi hakuna sehemu yenye upungufu wa kitu chochote kile.Chakula na vinywaji viko vya kutosha sana na bado vinazidi kuletwa.Kitu peke ambacho tungependa kupata maelekezo kutoka kwako ni lini mmepanga iwe ni siku ya mazishi na tumzike wapi.Hayo ndiyo mambo pekee ambayo yamebakia na tunasubiri maelekezo yako madam Latoya”
Latoya akamtazama Innocent na kumuuliza
“Innocent wewe ndiye mwenye kutoa uamuzi ni lini tumzike Marina na tumzike wapi”
Innocent akafikiri kidogo na kusema
“Latoya , hakuna haja ya kuweka siku nyingi za msiba kwani watu wanatakiwa waendelee na shughuli zao za maendeleo.Mimi nadhani hata kesho tunaweza tukafanya mazishi halafu kila mmoja akaendelee na shuguli zake.Suala la wapi atazikwa ni jambo la kuamua tu ,sehemu yoyote ile itakayoonekana inafaa mimi sina kipingamizi” Innocent akasema kwa sauti ndogo.
“nadhani mmemsikia Innocent alivyosema lakini na mimi ninapenda kuongezea machache katika hilo.Sioni tatizo lolote hata kama msiba huu utachukua mwezi mzima.Lakini kwa kuyaheshimu mawazo ya Innocent ningependekeza mazishi yafanyike kesho kutwa.Marina ni mtu muhimu kwetu na anastahili heshima kwa maana hiyo ninapendekeza azikwe katika makaburi ya Kivule wanakozikwa watu matajiri .Shughulikieni suala hilo na mpaka kesho jioni maandalizi ya kaburi yawe yamekamilika na kesho kutwa tufanye mazishi.Nataka mazishi haya yawe na hadhi na heshima ya kipekee sana.Tutaongea na kupanga zaidi siku ya kesho.Kama kuna jambo lolote ambalo litawasumbua msisite kunitaarifu mara moja..Naomba sasa nimruhusu Innocent akapumzike tutaonana tena kesho asubuhi” Latoya akasema na kisha akainuka na kumuongoza Innocent kuelekea chumbani kwake.
“Innocent naomba upumzike na tutaonana kesho.Iwapo utahitaji kitu chochote kile hata kwa usiku wa manane piga simu namba 200 wapo wahudumu ambao watakuhudumia mara moja .Kama una lolote la kuniambia unaweza ukanipigia simu muda wowote wa usiku lakini kuanzia saa tisa za usiku hadi saa kumi na moja za asubuhi huwa sipokei simu.Usiku mwema Innocent.”akasema Latoya na kuondoka.
“Sikutegemea kama msiba wa Marina ungekuwa namna hii.Mtu masikini asiye na ndugu yeyote,msichana ambaye anafanya biashara ya ukahaba lakini msiba wake umekuwa ni msiba wa kifahari na wa kitajiri.Kila mtu aliyefika hapa anajaribu kuonyesha uwezo wake wa kifedha kwa Latoya.Kwa mujibu wa Latoya shilingi millioni mia na hamsini tayari zimeshatolewa hadi hivi sasa kama mchango.Inanishangaza sana kwa watu kujitolea fedha hizo zote kwa ajili ya msiba badala ya kumsaidia mtu akiwa bado hai.Baada ya msiba huu nitaanzisha taasisi yangu ya kuwasaidia watu wenye matatizo kama ya Marina.Kuna watu wengi ambao nina imani wana matatizo makubwa na wanahitaji msaada mkubwa.Kuna kila sababu ya kuwaelimisha watu juu ya thamani ya mtu akiwa hai.Tusisubiri kumthamini mtu wakati amefariki.” Alikuwa akiwaza Innocent akiwa amekaa kitandani.Picha ya Latoya ikamjia kichwani
. ” Kuna kila sababu ya kumfahamu Latoya kwa undani.Ninataka nifahamu ni kwa nini binti mdogo namna ile ananyenyekewa na watu wakubwa na matajiri..Ni binti wa namna gani anayeweza kuwafanya watu wenye fedha na nyadhifa zao wajishushe kwake?.Nitajitahidi kumfahamu kiundani baada ya msiba huu kuisha.Kwa sasa nitakuwa nikiumiza kichwa changu bure.Ninachotakiwa ni kuelekeza mawazo yangu katika msiba huu mkubwa unaonikabili.Natakiwa kwanza kumzika Marina na kisha nijue nini kitakachofuata.Masikini Marina amekufa bado msichana mdogo .Hakufanikiwa kutimiza ndoto zake alizokuwa akifikiria kuzitimiza.Nasikitika sana kufahamiana naye katika siku za mwisho za maisha yake hapa duniani.Pamoja na kasoro zake ambazo zilichangiwa na maisha aliyoyaishi ,lakini nitakiri siku zote kwamba marina alikuwa na uzuri wa kipekee.Kinachoniuma zaidi ni kwamba tayari nilikwishavutiwa naye na alikuwa tayari kuyabadili maisha yake.Pamoja na jitihada zote nilizozifanya ili kuyaokoa maisha yake lakini Mungu amempenda zaidi.Nitazidi kumuombea siku zote ili apumzike kwa amani.”
Wakati Innocent akifumba macho yake na kulala,Latoya alikuwa amepiga magoti katika meza yake ambayo anayoitumia kila siku kwa ajili ya kufanyia maombi.Taa za chumbani kwake zilikuwa zimezimwa na mishumaa tisa ndiyo ilikuwa ikiwaka na kuleta mwanga mle chumbani.Uso wake ulikuwa umeloa machozi na alikuwa akilia kwa kwikwi.
“ni siku nyingi nimekuwa nikiota ili kabla sijafa niwe nimempata mtu ambaye nitampenda kwa moyo wangu wote.Ninahitaji kuwa na mtu nitakayempenda na ambaye atanipenda na kunithamini.Naamini nimekutana na Innocent kwa makusudi kabisa.Naamini Innocent ndiye yule mtu ambaye nimekuwa nikiomba kumpata mchana na usiku.Kadiri siku zinavyokwenda ninazidi kuwa dhaifu na nilikuwa ninaogopa ninaweza kufa kabla sijaitimiza ahadi hii niliyoiweka ya kumpata mtu nitakayemkabidhi moyo wangu.” Latoya alikuwa akiwaza huku uso wake umeloa machozi.Hali aliyokuwa nayo muda huu ilitia huruma sana.Taratibu akajiinua na kwenda kukaa katika kitanda chake kikubwa.Akakishika kichwa chake na kuzama katika mawazo mengi
TUKUTANE SEHEMU IJAYO…