BEFORE I DIE
SEHEMU YA 17
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Hali yake imebadilika sana.Siwezi kusubiri hadi asubuhi.Ngoja nimuwahishe hospitali” Innocent akawaza huku akivaa viatu vyake halafu akambeba Marina na kumpakia katika gari lake na kwa kasi ya ajabu akaelekea hospitali.
“Kwa kuwa vipimo alivyofanyiwa jana vinaonyesha kwamba kinachomsumbua ni figo sina haja ya kumpeleka hospitali nyingine zaidi ya Agape kidney hospital.Nasikia pale kuna madaktari mabingwa wa masuala ya figo wanatokea Marekani.” Akawaza Inno .Usiku huu hakukuwa na magari mengi barabarani kitu kilichomfanya atumie dakika thelathini na tano kufika katika hospitali hii maalum kwa ajili ya magonjwa ya figo.Hospitali hii inayoongozwa na wamisionari ,ilifanya kazi kwa saa ishirini na nne.Mara tu Inno alipowasili ,marina akachukuliwa na kupelekwa katika chumba maalum kwa ajili ya huduma ya kwanza wakati wakisubiri maelekezo ya daktari.Innocent akaitwa ofisini kwa daktari na kutoa maelezo ya ugonjwa wa Marina ikiwa ni pamoja na majibu ya vipimo alivyofanyiwa siku iliyopita.Daktari akamuomba Inno akaendelee kusubiri katika sehemu ya kupumzikia wakati wakiendelea na zoezi la kuchukua vipimo zaidi ili walifahamu tatizo la Marina kiundani zaidi .
ENDELEA………………………………
Saa mbili na nusu za asubuhi daktari akamuita Innocent ofisini kwake.
“Innocent mgonjwa wako anaumwa sana.Tumemfanyia uchunguzi wa hali ya juu na tumegundua kwamba kwa sasa hali yake si nzuri kwa sababu figo zake zinashindwa kufanya kazi” Akasema daktari yule na kumtazama Innocent usoni.
“Daktari kuna namna yoyote mnayoweza kufanya ili figo zake ziweze kufanya kazi tena? Inno akauliza
“Hilo ndilo limenifanya nikuite hapa ofisini.” Akasema daktari na Innocent akamuangalia kwa wasi wasi.
“mgonjwa wako anatakiwa kubadilishiwa figo.Akipata walau figo moja inaweza kusaidia kuokoa maisha yake” Daktari akamwambia Innocent , akastuka na kusimama.
“Dokta ina maana figo nyingine ikikosekana Marina anaweza kufariki?
“Uwezekano wa kupona kama hatabadilishiwa figo ni mdogo sana” Daktari akasema na kuzidi kumchanganya Innocent ambaye alikuwa akimtazama daktari kwa wasi wasi mkubwa.
“Hizo figo zinapatikana wapi dokta.Niambie kiasi chochote cha pesa nitatoa ilimradi marina apone” Inno akasema
“Innocent nasikitika kwamba figo inatakiwa kutolewa kwa mtu.Unatakiwa kutafuta mtu ambaye atajitolea figo yake moja kwa ajili ya mgonjwa wako.Hakuna figo ya kununua” Dokta akazidi kumkatisha tamaa Innocent.
“My Gosh ! Marina is going to die.I cant let that happen” Akaongea mwenyewe na kumfanya daktari amuangalie kwa makini.
“Daktari iwapo akijitokeza mtu wa kutoa figo yake kwa ajili ya Marina itamlazimu kusafirishwa nje ya nchi kwa upasuaji? Innocent akauliza
“hapana Innocent,hii ni hospitali maalum kwa ajili ya magonjwa ya figo na kuna madkatari bingwa wa figo wako hapa kwa hiyo kila kitu kinafanyika hapa hapa.hakuna haja ya kumpeleka mgonjwa nje ya nchi.”
Maneno yale ya daktari yanampa moyo Innocent
“Daktari nashukuru naomba unipe muda nikatafute namna ya kuweza kupata mtu wa kujitolea figo.Nitapata figo daktari .marina hawezi kupoteza uhai kwa sababu ya Figo” Innocent akasema huku akiondoka mle ofisini akapanda gari lake na kuondoka .
“Lazima figo ipatikane.Siwezi kukubali kumpoteza Marina kwa sababu ya figo.Ngoja kwanza niende ofisini nikaangalie shughuli zinakwendaje halafu nianze jitihada za kutafuta mtu wa kujitolea figo” Akawaza Inno akiwa njiani kuelekea ofisini.
Alipofika ofisni akashuka garini na kutembea kwa haraka kuelekea ofisini kwake.Kila aliyemuona alikuwa akimshangaa kwa hali aliyokuwa nayo.Alikuwa amesawajika mno.Hawakuzoea kumuona katika hali ile.Kila mmoja alijua kuna jambo limemsibu.Mara tu alipoingia ofisini kwake akakutana na sura ya baba yake.Kwa muonekano wa baba yake ulivyokuwa alihisi kuna jambo si zuri.
“baba shikamoo” Inno akamsalimia baba yake.
“marahaba Inno.” Baba yake akaitika
Inno akaketi kitini na kumpigia simu katibu muhtasi wake.
“Devotha siko kikazi leo.Naomba futa ahadi zote za kukutana na watu niliokuwa nikutane nao leo”
baba yake akamuangalia kwa jicho kali.
“Innocent jana umelala wapi? Baba yake akauliza mara tu alipoweka chini mkono wa simu.
“Baba ni hadithi ndefu nadhani mama alikwisha kueleza.Niliamua kuondoka nyumbani”
“Uliondoka nyumbani kwa ruhusa ya nani? Akauliza mzee Benard na muda huo simu ya Innocent ikaita.Akatazama mpigaji alikuwa ni Sabrina.
“samahani baba naomba kupokea hii simu ni muhimu” Akasema Inno akiinuka na kusogea pembeni
“Hallo Sabrina”
“Kaka Innocent habari za toka jana? Sabrina akauliza
“habari si nzuri sana Sabrina”
“marina anaendeleaje?
“Marina ana hali mbaya sana.Amezidiwa usiku nikampeleka hospitali na amelazwa .Kwa mujibu wa madaktari ni kwamba figo zake zinashindwa kufanya kazi kwa maana hiyo ili kuokoa maisha yake anahitaji kubadilishiwa figo.”
“Ouh Mungu wangu !” Sabrina akastuka.
“sasa umefikia wapi katika kupata figo? Sabrina akauliza
“Bado natafuta mtu wa kuweza kujitolea figo moja.” Innocent akajibu.
“Kaka Innocent jana nilikwambia kuhusiana na dada Latoya ambaye ndiye mwenye hii taasisi ninayofanya kazi.Anasaidia sana wanawake wenye matatizo kama ya kansa za matiti ,vizazi n.k.Unaonaje kama nitakuunganisha naye uone kama anaweza kuwa na namna yoyote ya kukusaidia? Ni mtu mwenye roho ya huruma sana.”
Sabrina akamwambia Innocent ambaye baada ya kufikiri kwa sekunde chache akasema
“Ok Sabrina nitafurahi kuonana naye”
‘Usijali kaka Innocent.Ninakwenda kuongea naye sasa hivi na kumweleza kuhusu umuhimu wa jambo hili.Nitakupigia simu baada ya muda mfupi”
Walipomaliza maongezi Innocent akarudi mezani na kuketi kitini.
“Innocent yule Marina ni nani wako? Baba yake akauliza
“Ni rafiki yangu”
“Innocent katika watoto niliokuwa nawategemea ni wewe.Sikutegemea hata siku moja kwamba ungeweza kufanya jambo kama ulilolifanya jana.Kwa ajili ya mwanamke kahaba unadiriki kuhama nyumbani kwenu? Umeidhalilisha sana familia yetu.Wewe ni kijana msomi ,ambaye unatakiwa utafute binti mzuri,msomi mwenzako ambaye atakupenda na mtaishi wote na kutengeneza familia na si hawa makahaba mnaowaokota mitaani ambao hawana lolote zaidi ya kutumia fedha zako na kukuachia maradhi.Nimekuja hapa kwa lengo moja tu ,kutaka kuisikia kauli yako kwamba unachagua kitu gani kati ya familia yako au huyo kahaba wako.Innocent tunakupenda na hatutaki upotezwe na hawa wasichana wasiokuwa na mwelekeo.Naomba urudi nyumbani na kama utasisitiza kuendelea na huyo kahaba wako basi utakuwa umejiondoa katika familia wewe mwenyewe.Sisi hatutakutambua tena.Sitaki hayo yatokee Innocent ,nakuomba uniahidi kwamba utaachana na huyo msichana wa mitaani” Mzee Benard akasema kwa sauti isiyo na masihara.Innocent anamfahamu vizuri baba yake,akiwa katika hali kama hii huwa hana masihara.Ni wazi alimaanisha kile alichokisema.Maneno yale ya baba yake yakamchoma moyo Inno.Aliumizwa sana na maneno yale.Sura ya Marina akiwa katika maumivu makali hospitali ikamjia tena kichwani akawaza.
“hapana siwezi kumuacha Marina apoteze maisha .Pesa mali na kila kitu vinapita lakini uhai wa Marina ni muhimu mno kwangu.Akipotea leo hakuna pesa itakayoweza kumrudisha.I cant let that happen”
Kwa sura iliyojaa simanzi,Innocent akaenda juu ya kabati akachukua funguo nyingi na kuziweka mezani.Baba yake akazidi kumshangaa.
“Baba funguo hizo hapo”
“Za nini” baba yake akauliza
“I quit.I’m out of here”
Mzee Benard akastuka sana kwa kauli ile ya Innocent
“Ina maana kahaba ni bora zaidi kuliko familia yako?
“baba vyovyote itakavyokuwa ninyi mtabaki kuwa familia yangu mpaka kufa.lakini kwa sasa uhai wa Marina ni kitu muhimu sana kwangu.I cant let her die.Nimekurudishia ofisi baba.” Innocent akasema na kutoka mle ofisini.
“Innocent !!..Innocent !……” mzee Benard akaita kwa sauti ya juu iliyowastua wafanyakazi wengine lakini Innocent hakugeuka ,akaingia garini na kuondoka.
“Sikutegemea kama baba angeweza kunitamkia maneno kama yale.Nashindwa kuelewa ni kwa nini familia yangu wamekuwa hawapendezwi kila ninapojitahidi kuwasaidia watu wenye matatizo.Mungu ameibariki familia yetu na kuipatia mali na fedha,lakini isiwe ni sababu ya kutowapenda na kuwabagua wale ambao hawakujaliwa kuwa navyo.Huu ni msimamo wangu na sintakubali mtu yeyote aniyumbishe katika msimamo wangu huu.Nitamsaidia yeyote mwenye shida kama nitakuwa nacho.Familia yangu ni muhimu sana lakini kuokoa uhai wa Marina ni muhimu zaidi kwangu sasa.Natakiwa nipambane kadiri nitakavyoweza ili niweze kuokoa maisha ya binti yule masikini.” Mawazo ya Innocent yakakatishwa na simu yake iliyokuwa ikiita.Akapungua mwendo wa gari na kutazama mpigaji.Alikuwa ni Sabrina.
“Helo Sabrina” Innocent akasema baada ya kubonyeza kitufe cha kupokelea simu
“Kaka innocent uko wapi sasa hivi? Sabrina akauliza
“Niko barabarani naenda kuonana na rafiki yangu mmoja ni daktari nione kama atanisaidia”
“Kaka Innocent ,nimeshaongea na dada Latoya na ameonyesha kuguswa na jambo hilo na yuko tayari kukusaidia.Kwa kuwa anatakiwa kuhudhuria kikao muhimu mchana huu amesema kwamba kama una nafasi fika sasa hivi hapa ofisini kwake ili muweze kuongea na kuangalia ni namna gani mnaweza mkayaokoa maisha ya Marina”
“Ok Sabrina nielekeze zilipo ofisi zenu nifike hapo mara moja”
Sabrina akamuelekeza Innocent zilipo ofisi zao ,akageuza gari na kuelekea huko.
“Nadhani kuna haja ya kuanzisha mfuko maalum wa kuwasaidia watu wenye matatizo kama anavyofanya huyo Latoya.Nimegundua kwamba ukiwa na maisha ya juu kamwe huwezi kuzitambua shida walizonazo watu wenye maisha ya chini.Watu wenye uwezo mkubwa kifedha hawafahamu nini maana ya kulala njaa,nini maana ya kukosa ada ya kumsomesha mtoto,kiujumla hawafahamu nini maana ya shida.Hii ni sababu hata wazazi na ndugu zangu hawaniungi mkono katika jitihada zangu za kuwasaidia watu wenye matatizo mbali mbali.Nashukuru Mungu kwa kunipa moyo huu wa kuguswa na matatizo ya watu.Laiti kama ningekuwa na uwezo wa kuweza kuyatafutia ufumbuzi matatizo yao,lakini uwezo wangu ni mdogo na bado una mipaka na ndiyo maana nafikiria kuwa na taasisi yangu mwenyewe ya kuwasaidia watu kama Marina na wengine wenye matatizo mbali mbali makubwa.” Akawaza Innocent wakati akielekea ofisini kwa Latoya
“kwa sasa najiona ni mwenye furaha kusikia kwamba Sabrina amepata kazi ambayo itamuwezesha kujitegemea yeye mwenyewe.Sabrina ni mlemavu wa ngozi na hakuwa akipewa thamani yoyote na familia yangu,alitengwa na kubaguliwa kwa kitu kimoja tu ulemavu wa ngozi yake..Leo hii amesoma na amepata kazi ya kufanya na muda si mrefu ataanza maisha yake mwenyewe.Haya ni mafanikio.Grace naye ni msichana ambaye amepitia magumu mengi na ambaye alikwisha kata tamaa ya maisha kwa kuamini kwamba ni muathirika wa ukimwi,kwa sasa anaendelea na mafunzo ya upishi na nina uhakika kwamba baada ya kumaliza mafunzo yake atapata kazi au atajiajiri yeye mwenyewe.Haya ni mafanikio makubwa sana ambayo ninaweza kujivunia.Nimeweza kuyabadili maisha ya wasichana hawa.Nimewasaidia kuzitimiza ndoto zao walizokwisha poteza matumaini ya kuzitimiza tena.Wasichana hawa ni wachache lakini katika jamii wapo wengi zaidi ya hawa wawili,ambao hawana mtu wa kumsemea shida zao.Kwa sasa natakiwa kuelekeza nguvu kwa Marina.Ni lazima niokoe maisha ya Marina na kumsaida kuzitimia ndoto zake vile vile.Baada ya hapo ndipo nitafikiria namna ya kuweza kuanzisha taasisi yangu mwenyewe itakayokuwa ikiwasaidia watu wenye matatizo mbali mbali makubwa katika jamii” Innocent alikuwa na mawazo mengi.Kitendo cha baba yake mzee Benard kumtamkia maneno makali namna ile kilimuumiza sana moyo.
Hatimaye akawasili katika jengo zilimo ofisi za taasisi binafsi inayoendeshwa na mwanadada Latoya. Aliposhuka garini akapanda lifti ya jengo lile hadi ghorofa ya tisa ambamo ndimo zilimokuwa ofisi za taasisi hiyo.Mtu wa kwanza kumtambua Inno alikuwa ni Sabrina.
“kaka Innocent karibu sana” Sabrina akamkaribisha Inno kwa furaha huku akitabasamu
“Hii ndiyo ofisi yetu kaka Innocent karibu sana.” Sabrina akasema huku akimtambulisha Inno kwa wafanyakazi waliokuwa pale ofisini.Innocent hakuificha furaha yake.Kwa muda huu mfupi aliowasili hapa kila mmoja alionekana kuufurahia ucheshi na uchangamfu wa Innocent. Baada ya maongezi na utani wa hapa na pale kama kawaida yake ,Sabrina akamchukua Inno na kumpeleka katika ofisi ya Latoya.
“Dada huyu ndiye Innocent,amekuja kukuona kwa ajili ya lile suala nililokueleza” Sabrina akamtambulisha Innocent kwa Latoya.Kwa sekunde kadhaa walibaki wanatazamana halafu Latoya akasema
“Karibu sana Innocent,nafurahi kukufahamu” Latoya akasema huku akisimama na kumpa mkono
“Hata mimi nafurahi sana kukufahamu “ Innocent akajibu huku akihisi kama vile macho yake yalikuwa yakimdanganya kwa msichana aliyekuwa mbele yake.
TUKUTANE SEHEMU IJAYO……