Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Acha kabisa...penzi la Brazil bado liko kichwani kwakedogo anashindwa kuzuia mihemko yake
Asante nduguNapenda utunzi wako, big up sana
Sorry deadear. Am back nowElton wangu uko wapi leo,nimeshakumiss huku
asante kwakuja dearSorry deadear. Am back now
Mwama amepata dhahama mbaya sana, bila shaka atatoboa tuDYLAN
Story by Elton Tonny
Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA NNE
★★★★★★★★★★★★★★★
Dylan aliendelea kudondoka kuelekea chini kwa kasi, huku mwili wake ukizunguka-zunguka ovyo ovyo sana. Alikuwa akijaribu kuishika kamba ya kuvutia parachuti ili lifunguke kutoka kwenye begi, ambalo bado lilikuwa mgongoni kwake, lakini akawa anashindwa kuipata kutokana na upepo kuirusha huku na huku. Alianza kuona kuwa alikaribia chini zaidi sasa, na kwa ustadi akajikunja na kujiviringisha angani hapo ili aweze kuuweka mwili wake sawa, kisha akafanikiwa kuishika kamba hiyo na kuivuta kwa nguvu.
Parachuti lilifunguka, lakini kutokana na kasi yake lilipofunguka, ilifanya mwili wa Dylan urudi juu kidogo kwa kushtukiza, hivyo kasi yake ya kudondoka ikapungua, lakini tatizo lingine likatokea. Kwa kuwa hakuwa ameifunga mikanda ya begi kifuani, ilifanya mikono ya begi iteleze kutoka mabegani kwake na hivyo begi hilo kumtoka mgongoni! Alikuwa amekaribia chini sana, na baada ya begi kumtoka, akaanza kuanguka huku anapiga kelele za hofu.
Mwili wake ulidondokea kwenye kamba nene iliyokuwa ya kivuko/daraja refu la kamba, ambalo lilikuwa juu katikati ya miamba miwili mikubwa ya bwawa pana sana la maji yenye kina kirefu. Baada ya kujigonga hapo, akaanza kuangukia chini huko na kudumbukia ndani ya bwawa kwa nguvu sana, na mwili wake ulipokuwa unazama chini, kichwa chake kikajigonga kwa nguvu kwenye jiwe kubwa ndani ya maji hayo.
Upande wa helicopter, rubani alijitahidi sana kurudisha chombo hicho kwenye utaratibu mzuri, lakini jitihada zake zikaendelea tu kugonga mwamba. Helicopter iliendelea kuzunguka na kwenda ovyo ovyo, na kwa dakika kadhaa baadae, ikaishiwa nguvu yote na kuanza kuelekea chini kwa kasi sana; hapo ikiwa imevuka mikoa michache toka ilipoanza kuleta shida. Kwa kusikitisha sana, iliangukia sehemu ya mbali ambayo ilikuwa na mlima, na yote ikalipuka.
★★★
Huzuni, simanzi na majonzi vilitawala familia nzima ya Dylan baada ya kuwa wamepata taarifa kuhusu ajali iliyompata kijana huyo. Walisafiri haraka kuelekea mkoa ambao helicopter iliangukia, na baada ya kufika huko, waliweza kuonyeshwa miili mitatu ambayo ilikuwa imeungua sana na kuwa myeusi yenye kutisha. Gilbert alikumbuka kuwa, Dylan alipanda helicopter pamoja na mwanaume mwingine wa kampuni yao, hivyo ukijumuisha na rubani bila shaka walikuwa watatu. Kwa hiyo kwa haraka wote wakajua kwamba Dylan pia alikuwa amepoteza maisha kwenye ajali hiyo. Walilia sana.
Camila pamoja na mchumba wake walikuwepo pia, naye alimwombolezea mpwa wake kwa uchungu mwingi sana moyoni, ukitegemea hawakuwa wameachana kimtazamo mzuri.
Walifanya msiba baada ya siku chache, kukiwa na ndugu na marafiki wa karibu waliofika kuwafariji. Aliyepoteza matumaini kabisa alikuwa ni Jaquelin. Hakula vizuri, hakuongea, angelia mara kwa mara na kuanza kupiga-piga vitu walipokuwa nyumbani, na hakutoka nyumbani kwa siku nyingi. Muda mwingi angelala tu kitandani akiwa anaangalia picha za Dylan huku analia kwa huzuni, na mambo yote haya yalimvunja sana Gilbert.
Fetty aliumia sana. Alihisi ni kama mikosi kwake isingeisha kamwe. Dylan alikuwa ni kitu kizuri sana kuwahi kuingia kwenye maisha yake. Kuna msemo wa kwamba mtu huwa hatambui umuhimu wa kitu alichonacho mpaka anapokuja kukipoteza, naye Fetty alihisi ni kama msemo huo ulimfaa yeye kwa sababu ijapokuwa nafasi ilikuwepo kabisa ya kuwa pamoja na Dylan kimahusiano, hakupiga hatua hiyo. Hivyo alijilaumu kuwa alikuwa akichezea muda tu wakati angekuwa ameshamwambia mapema kuwa alimpenda. Kutokea hapo, mwanadada huyu hakuwa na furaha tena moyoni, kwa kuwa kitu kilichompatia furaha kilikuwa kimepotea.
Camila alirudi Brazil na mchumba wake baada ya miezi mitatu. Hawakuwa wamepanga kukaa muda mrefu hivyo, lakini baada ya mambo hayo yasiyotazamiwa kutokea, Camila alihitaji kuwa na ndugu zake karibu zaidi. Lakini kwa kuwa walihitaji kuendelea na kazi, ilibidi warudi Brazil sasa; Camila akimuahidi Jaquelin kuwa angeendelea kuwasiliana naye kila siku.
Kufikia wakati huu, Gilbert alikuwa anaendelea kujitahidi kuweka mambo sawa kwenye kampuni, kwa kuwa baada ya Dylan "kufa," mipango mingi iliyokuwa ikiendeshwa naye iliharibika. Ijapokuwa Gilbert alijitahidi sana kuongoza mambo vyema, vizuizi vya kimakusudi kutoka kwa watu waliotaka aporomoke vilimrudisha nyuma; na wakati huu ilikuwa ni kama anapoteza mwelekeo kwa kuhisi yuko mwenyewe. Jaquelin alianza tena kwenda kwenye kampuni, lakini akili yake haikukazia fikra kabisa kazi, bali ni mwili wake tu ndiyo ulikuwa pale.
Maisha ya wawili hao yaliendelea kuwa yenye misukosuko zaidi kadiri siku zilivyoendelea kwenda, na haikuonekana kama wangeweza kupata ahueni tena.
★★★
Dylan anafumbua macho yake taratibu, akiwa anahisi kama ametoka kwenye usingizi mzito. Anatazama sehemu aliyopo na kutambua ni chumba fulani. Anapojaribu kugeuza shingo, anahisi maumivu yanayofanya akunje sura yake kwa hisia za kuumia. Kichwa chake kinamuuma sana, naye haelewi kwa nini iko hivyo.
Kisha anasikia sauti pembeni yake ikisema, "...ameamka... nyie... ameamka..." naye anatambua sauti hii ni ya mvulana mdogo, lakini hawezi kumwona kwa kuwa hawezi kuigeuzia shingo yake upande huo.
"Emmy, kamwite dokta..."
Anasikia sauti hiyo nyingine ikisema hivyo. Hii ni ya mwanaume mtu mzima, lakini hatambui ni nani. Kisha hapo hapo mwanaume fulani anasogea karibu na uso wake na kuanza kumwangalia-angalia usoni mwake. Hamtambui hata kidogo, kisha anakuja mwanaume mwingine na kuanza kumkagua usoni; analimulika jicho lake kwa tochi ndogo, anatumia kifaa cha kusikilizia mapigo ya moyo kusikiliza ya kwake, kisha anamuuliza Dylan anahisije mwilini.
Dylan akaanza kuzungusha macho huku na huku bila kutoa jibu lolote. Mwanaume huyo, daktari, akaanza kuongea na yule mwanaume mwingine pembeni. Alikuwa anamwambia kwamba mgonjwa anaonekana kuwa na shida kwenye ubongo, hivyo angehitaji kupelekwa hospitali kubwa zaidi. Dylan akamsikia mwanaume huyo mwingine akimwambia daktari kuwa hana pesa ya kumgharamia na kumpeleka kwenye hospitali kubwa, kwa kuwa alimpata tu akiwa kwenye hali mbaya, hivyo akamsaidia na kumleta hapo kwenye zahanati hii.
Mwanaume huyo akamuuliza daktari shida ya mgonjwa kwenye ubongo ni nini, naye daktari akasema atahitaji kumfanya mgonjwa aongee ili aweze kuwa na uhakika zaidi, ndipo atoe jibu. Dylan alisikia vizuri walichokuwa wanasema, lakini HAKUELEWA kilichokuwa kinaendelea. Daktari akamsogelea tena, kisha akanyanyua vidole viwili mbele ya uso wa Dylan huku anamwangalia kwa makini.
"Hii ni ngapi?" daktari akauliza.
Dylan akaukazia macho mkono wa daktari, kisha akasema, "Mbili."
Daktari akafurahi kuona ameweza kuongea na kutoa jibu kwa usahihi, kisha akamwangalia macho tena kwa kuyavuta-vuta.
"Unaitwa nani?" daktari akamuuliza tena huku anamwangalia.
Dylan akafungua mdomo ili ajibu, lakini akabaki ameachama bila kutoa neno lolote. Akaanza kupeleka macho huku na huku, akionekana kutafuta jibu. Daktari akarudia tena kumuuliza jina lake ni nani, lakini Dylan akawa amekunja tu uso huku anaonyesha kutangatanga kiakili. Daktari akamtuliza kwa kumwambia asijilazimishe maana kichwa kingeanza kumuuma, kisha akamgeukia yule mwanaume aliyemsaidia Dylan.
"Inaonekana atakuwa amepoteza kumbukumbu," daktari akamwambia.
"Mh! Sasa itakuwaje?" mwanaume huyo akauliza.
"Tumchukue tumpeleke nyumbani," akajibu mvulana yule mdogo.
Mwanaume huyo akamwangalia Dylan kwa wasiwasi.
"Sasa dokta, ikiwa anaweza kukumbuka namba mbili, anashindwaje kukumbuka jina lake?" akamuuliza.
"Aam... kumbukumbu ni pana. Na mara nyingi kwenye visa vya kupoteza kumbukumbu, watu husahau hasa mambo mengi kuhusu maisha waliyoishi, lakini vitu vichache walivyofundishwa mara nyingi hubaki kwenye ubongo. Ndiyo maana unaona hajasahau kiswahili," daktari akaeleza.
"Ee ndiyo baba. Ndo' maana unaona anaweza kuongea, la sivyo asingesema chochote," akasema binti ya mwanaume huyo, aliyeitwa Emilia.
"Hahah... angekuwa kama litoto anafanya bhabhabha..." akasema mvulana yule, na wote wakacheka kidogo (isipokuwa Dylan).
"Nini kinaendelea? Nimefikaje hapa? Kwa nini sikumbuki vitu?" Dylan akauliza kwa wasiwasi.
Daktari akamsogelea na kusema, "Pole sana. Inaonekana ulipatwa na ajali, na sasa... ukaangukia vibaya jiwe kubwa na kukipiga kichwa chako kwa nguvu. Kwa hiyo sehemu kubwa ya ubongo wako iliyotunza kumbukumbu imevurugika," daktari akaelezea.
"Ajali? Jiwe? Mbona sikumbuki?" akasema Dylan kwa huzuni.
"Usijali. Tatizo hili litaisha baada ya muda fulani kupita. Atahitaji dawa za kusaidia maumivu ya mishipa ya shingo, nitakuandikia," daktari akamwambia mwanaume yule.
Kisha daktari akaondoka kwenda kwa wagonjwa wengine, akiwaacha wote hapo.
"Sasa baba, kama amepoteza kumbukumbu atarudije kwao?" Emilia akamuuuliza baba yake kwa sauti ya chini.
"Nitamsaidia kutafuta alikotokea. Nafikiri kuna watu eneo hili wanaomfahamu," akajibu.
Dylan alikuwa anaangalia huku na huku kwa wasiwasi, akijaribu kuvuta picha ya mambo mengi, lakini anashindwa kukumbuka. Mwanaume huyo akamsogelea na kuketi kitandani akimwangalia, naye Dylan akamwangalia pia.
"Hujambo? Naitwa Baraka, mimi ndiyo nilikusaidia na kukuleta hapa," mwanaume huyo akasema.
"Asante. Nini kilinipata?" Dylan akauliza kwa hisia.
"Sijui kwa kweli. Nilikuwa kwenye mtumbwi na mwenzangu, tukijaribu kuvua dagaa wachache bwawani. Nikakuona ukiwa chini ya maji kwa sababu ya... shati lako jeupe, kwa hiyo tukakutoa, na ulikuwa umepoteza fahamu. Kichwa chako kilikuwa kimevimba kwa nyuma huku damu zinakutoka, kwa hiyo tukakuwahisha hapa kwa sababu bado ulikuwa hai..." Baraka akaelezea.
Dylan akanyanyua mkono wake na kujishika kichwani. Akatambua alikuwa amefungwa bendeji kuzungukia kichwa chake, kisha akafumba macho kwa huzuni.
"Haukumbuki kitu chochote kabisa?" akauliza Emilia.
Dylan akafumbua macho na kumtazama Emilia. Aliweza kumwona akiwa amesimama pembeni kidogo, huku akiwa ameikunjia mikono yake kifuani.
"Kuna vitu najua. Najua wewe ni msichana... najua hiki ni kitanda... najua hapa tuko hospitali...aam, zahanati..." Dylan akasema.
Baraka akatabasamu kwa kutambua kuwa Dylan alikuwa mwerevu.
"Lakini vitu vingi vya maisha yangu sivijui... aah... ni hisia mbaya sana," akasema Dylan.
Wote walimwonea huruma sana.
"Usihofu. Kama dokta alivyosema, usijilazimishe... itarudi yenyewe. Jipe tu muda," Baraka akamtia moyo.
Dylan akashusha pumzi taratibu, kisha akauliza, "Nimekuwa hapa kwa muda gani?"
"Siku...6. Tokea tulivyokutoa kwenye maji," Baraka akajibu.
"Haionekani kwamba nilikuwa humo muda mrefu?" Dylan akauliza.
"Hapana. Inaonekana ulidumbukia siku hiyo hiyo tuliyokutoa, la sivyo tungekuta umekufa," Baraka akamwambia.
Dylan akatulia kidogo.
"Hawa ni wanangu. Huyu ni Emilia, na huyu mdogo ni Steven," Baraka akawatambulisha wanae kwa Dylan.
Dylan akatabasamu kidogo, na watoto wa Baraka wakatabasamu pia kirafiki.
Waliendelea kukaa na Dylan kwa muda fulani, kisha wakaondoka na kumwacha chini ya uangalizi wa wauguzi.
★★★
"Hivi kweli baba Leila... unawezaje kufanya uamuzi huo?"
"Kwa hiyo unataka nimwache tu kijana wa watu?" akajibu Baraka.
"Ina maana hana familia? Waje wamchukue! Wewe unataka kutuletea hapa mtu ambaye hatumfahamu hata kidogo. Unajua vipi tabia zake? Je kama ni jambazi?"
"Mama Leila, usiwe hivyo. Yule kijana anahitaji msaada. Hana pa kwenda kwa sababu hakumbuki maisha yake. Siwezi kumwacha tu mpaka nimsaidie arudi kwao..."
"Lakini si kuna watu maalumu wa kumtafutia? Kwa nini wewe? Umemmwokoa asizame, umempeleka zahanati, umemtolea hela ya matibabu ambayo tungetumia hapa nyumbani, inatosha. Sasa sa'hivi unataka tena kumleta hapa ili iweje? Aagh..."
Haya yalikuwa ni maongezi kati ya Baraka na mke wake. Ilikuwa imepita wiki moja sasa tokea Dylan alipoamka, na daktari alisema yuko vizuri kimwili kuweza kutoka zahanati hapo. Lakini shida ilikuwa kwamba Dylan hakukumbuka vitu, kwa hiyo hangekuwa na pa kwenda. Baraka alikuwa ametumia muda huo wa wiki kuulizia sehemu za maeneo yao ikiwa kuna kisa cha mtu kupotea, lakini hakupata mtu aliyeonekana kufahamu upotevu wa Dylan.
Baadhi ya watu waliofahamiana na Baraka walikuwa wameenda pamoja naye zahanati ili kumwona Dylan, lakini wote hawakumtambua hata kidogo. Sasa kijana huyo angetakiwa kuondoka zahanatini kesho, na Baraka alikuwa anafikiria kumpa hifadhi nyumbani kwake wakati wakiendelea kutafuta watu ambao wangemfahamu. Jambo hill lilikuwa limemkera sana mke wake, ambaye aliona ingekuwa kuongeza mzigo tu kwenye maisha yao ikiwa wangemleta Dylan hapo.
"Mimi ndiye nitakayewajibika kwa ajili yake. Wewe niamini mimi," Baraka akamwambia.
"Maisha yetu kama unavyojua ndiyo hivyo... hayaeleweki. Wewe kuanza kujifanya msamaria mwema kutaongeza tu..."
"Aagh mama Leila! Nimeshasema anahitaji msaada, na nitamwajibikia mimi. Hebu acha basi kulalamika... agh!" Baraka akamwambia akiwa ameudhika.
"Sawa, utajua mwenyewe," mke wake akamwambia kwa kukerwa.
Akatoka hapo kwenye kochi walilokuwa wameketi na kuelekea chumbani akiwa amekasirika. Baraka akabaki sebuleni akitafakari mambo kwa makini, bila kujua kwamba binti yake mkubwa, Leila, alikuwa akiwasikiliza kutokea pembeni akiwa amejibanza.
Baraka alikuwa na familia yenye mke mmoja na watoto watatu. Binti yake wa kwanza ndiye aliyeitwa Leila, na alikuwa na umri wa miaka 22. Binti yake wa pili aliitwa Emilia, naye alikuwa mwenye miaka 18. Mwana wake wa tatu aliitwa Steven, naye alikuwa na umri wa miaka 11. Jina la mke wake lilikuwa Shani, lakini alizoea kuitwa mama Leila na wengi.
Baraka alikuwa mwanaume mstaarabu sana. Alikuwa ana ujuzi wa masuala ya makarai; alitengeneza majiko ya vyuma, mageti, nguzo za chuma, na alirekebisha mambo mengi yaliyohusisha vyuma. Hii ndiyo iliyokuwa kazi yake tokea zamani sana ambayo ilimpatia kipato kidogo kwa ajili ya kutegemeza familia yake. Eneo waliloishi lilikuwa mbali kutokea na sehemu aliyofanyia kazi, ambayo ilikuwa kama soko dogo la biashara ambako watu wengi walifanya kazi zao.
Mke wake, Shani, alikuwa mwanamke mwenye kujiamini na mkali kiasi. Mara nyingi ungekuta akiwafokea-fokea watoto wake kwa vitu vidogo vidogo tu, nao walikuwa wameshamzoea. Alikuwa anafanya kazi ya upishi, yeye kama maman'tilie, kwenye mgahawa wake mdogo eneo la soko lile la biashara. Alikuwa mwenye mwili mnene kiasi, lakini haukuwa na manyama mengi, bali uliofanya umbo lake lionekane vyema kwa kutokeza kalio lake kubwa vizuri kwa nyuma. Alipenda sana kuvaa nguo za kujiachia na kujiremba; ili kufanya aonekane kama binti mdogo bado!
Leila, binti mkubwa wa Baraka, alikuwa mwanamke mwenye kujiamini, mkaidi, na mwongeaji sana. Alikuwa amemaliza kidato cha nne miaka kadhaa nyuma na kwenda kwenye chuo cha ufundi, lakini akaachana na masuala ya shule ili akazie fikira biashara. Kwa kukosa kutengeneza mazingira mazuri ya biashara, alianza kufanya kazi kama muhudumu kwenye mgahawa fulani, tofauti na wa mama yake, na aliendelea kuwa hapo kwa miezi kadhaa. Leila alikuwa mwenye umbo zuri, nene kidogo lakini lililojikata kike sana, na hips na kalio lake vilitokeza vyema. Alikuwa na uso mzuri, naye alipenda kusuka rasta za kuchanganya rangi, na nguo nyingi alizopendelea kuvaa zilikuwa ni dera.
Emilia, binti wa pili, alikuwa msichana mstaarabu, mpole na mwenye akili sana. Wakati huu alikuwa kidato cha nne, akikaribia kumaliza masomo ya sekondari. Alikuwa mzuri pia kisura na kitabia, huku umbo lake lililonona pia likiwatamanisha wanaume wengi, ambao walikuwa wamejaribu sana kupita hapo ila binti akawagomea. Alikuwa anajiheshimu, na alipatana vizuri sana na baba yake.
Kisha kuna dogo Steven, ambaye ni mwana, na mtoto wa mwisho wa Baraka na Shani. Alikuwa mvulana mjanja, mtundu, mwongeaji, na mwerevu pia. Alikuwa darasa la 6 wakati huu, na alisoma kwa bidii pia ili afanikiwe kuingia darasa la 7 mwaka ujao.
Hiyo ndiyo ilikuwa familia ya bwana Baraka. Alikuwa amejenga nyumba ya kawaida yenye vyumba vinne ndani; kimoja kama sebule, kimoja cha kulala yeye na mke wake, kimoja cha kulala Leila na Emilia, na kingine cha kulala Steven. Walikuwa na jengo lingine dogo kwa nje ambalo lilitumiwa kama jikoni, na choo na bafu vilikuwa nje pia.
Walikuwa na shamba kwenye eneo hilo hilo ambalo walipanda mazao fulani waliyotumia kama chakula na kufanyia biashara kwenye kazi ya Shani. Nyumba za majirani wengi hapo zilikuwa kwa umbali fulani kutoka kwa moja na nyenzake, hivyo hawakubanana hata kidogo. Ilikuwa ni eneo kwenye mwinuko mkubwa sana, ambao ulikuwa na bwawa kubwa sehemu za mbele, lililotenganisha mwamba wa eneo hilo na mwamba mwingine kufikia upande wa pili wa mtaa huo; ambao ndiyo ulikuwa wenye eneo la biashara.
Katikati ya bwawa hilo, kutokea kwenye kingo za miamba hiyo, lilijengwa daraja refu la kamba na shaba ngumu kama kivuko kufika upande mwingine, lakini kivuko/daraja hili lilikuwa limeharibika katikati kwa muda mrefu sasa, na halikuwa limetengenezwa. Wenyeji wa upande huu wa eneo hili waliloishi familia ya Baraka walikuwa wameshajaribu kuomba msaada kutoka kwa diwani wao, lakini kwa sababu fulani hakuwa ametoa msaada na kuwapuuzia tu.
Ni daraja hili ndiyo ambalo Dylan aliangukia juu ya kamba yake ya kulishikilia siku ile aliporushwa nje kutoka kwenye helicopter, na wakati amedumbukia bwawani, Baraka alikuwa pamoja na rafiki yake kwenye mtumbwi wakitafuta dagaa kwa ajili ya chakula, ndiyo akaweza kumtoa baada ya kumwona kwenye maji.
Baada ya muda fulani, Baraka pia akaelekea chumbani ili kupumzika, baada ya kuwa amekorofishana na mke wake kuhusu kumleta Dylan hapo kwao. Ilikuwa ni usiku, hivyo walijua watoto walikuwa wamelala, pasipo kujua Leila alikuwa anasikiliza maongezi yao.
★★★
Asubuhi ilipofika, Baraka alielekea zahanati ili kumfata Dylan. Dylan angeweza kutembea vizuri, lakini kwa uangalifu sana ili asitie kichwa chake mtikiso ambao ungemuumiza, kwa kuwa alikuwa na kidonda kikubwa bado kichwani kilichofanya sehemu kubwa ya kichwa chake kufunikwa kwa bendeji. Baraka alimtoa huko na kumpeleka kwake, wakitembea mwendo mrefu sana.
Alimkaribisha vyema kwake, kisha akamwekea maji ya kunywa, na baadae ya kuoga. Akamwelekeza chumba ambacho angetumia, nacho kilikuwa kile alicholalia Steven. Kwa kuwa Baraka alikuwa na godoro la ziada, alimwambia Dylan kuwa angelala chini, kwa sababu hakukuwa na kitanda, na kitanda cha Steven kilikuwa kidogo. Dylan akasema hakuna shida, na kwamba anapenda kulala chini. Baraka akabaki anamwangalia kwa makini.
"Umejuaje kwamba unapenda kulala chini?" akamuuuliza.
Dylan akamtazama Baraka, akiwa hajatambua kwamba alisema kitu fulani kuhusu utu wake bila kukaza sana fikra.
"Amm... sijui. Ahah... hiyo ni ishara nzuri, siyo?" Dylan akasema kwa shauku kiasi.
Baraka akatabasamu na kusema, "Ndiyo. Pole kwa pole... kumbukumbu yako itarudi."
Dylan akamshukuru sana Baraka kwa msaada wake wote aliompatia.
Baada ya hapo alienda kuoga, kisha akarejea na kupata chakula. Baraka alikuwa amempatia baadhi ya nguo zake ili awe anavaa, naye alimwelezea Dylan kuhusu watu wa familia yake, na baadae kijana akapata kuwatambua vizuri baada ya kuwa wamerudi. Emilia na Steven walimwonyesha Dylan roho ya ukarimu kwa kumkaribisha vizuri, lakini Shani pamoja na Leila hawakuonyesha upendezi wowote kumwelekea Dylan. Ijapokuwa alitambua kwamba siyo wote wangempokea vyema, alijitahidi kuwa mtaratibu na mwelewa; akitumaini kuweza kukumbuka maisha yake ya zamani haraka ili asiwabane tena.
"Kaka haitatosha baba. Tumtungie jina," akasema Steven wakati wote wakiwa wameketi sebuleni pamoja usiku.
"Ahahah... tumtungie jina gani sasa?" akauliza Baraka.
"Lolote tu. Kumwita kaka haifai kwa sababu siyo kaka yao," akasema Shani kwa njia yenye kuvunja moyo.
Leila alikuwa bize ku-chat tu, nao wengine walitambua Shani alisema hivyo kwa nia mbaya.
"Achague Steven. Ungependa uniiteje?" Dylan akasema.
"Mmmm... jina gani, jina gani, jina ganiii.... Tumwite ISHENGOMA!" akasema Steven kwa uhakika.
Wote wakacheka, huku Dylan akishangaa jina hilo.
"Ishwegwama?" Dylan akauliza.
"Ahahahah... kwa nini unataka tumwite hivyo?" Emilia akamuuuliza Steven.
"Jina la kibabe. Kama yule Ishengoma mvuta bangi kule sokoni," akasema Steven, na wote wakacheka.
"Ahah... kumbe nafanana naye?" Dylan akauliza.
"Hamna, wewe mzuri. Yeye ana sura ngumu, huwa tukimwona tunakimbia. Sema ana marasi kama wewe, ndiyo maana nikaona tukuite hivyo," Steven akajibu.
"Mhm... linamfaa," akasema Leila kikejeli huku akiendelea ku-chat.
"Hamna bwana, baya. Tutafute la kizungu," akasema Emilia.
"Ili iweje?" akauliza Shani.
"Tumwite... Brian," akasema Baraka ili kumpotezea Shani.
"Mm-mm," Emilia akakataa.
"Kendrick?" akasema Baraka.
"Mm-mm."
"Sebastian?" akasema Steven.
"Mm-mm."
"Sasa we unataka lipi?" Shani akamuuuliza Emilia.
"Ishengoma," akajibu Leila, na wote wakacheka.
"Hamna bwana," Emilia akasema.
Dylan alikuwa anamwangalia Emilia huku anatabasamu.
"Basi wewe mchagulie, maana unayajua majina ya wazungu kuliko hadi wazungu," Leila akamwambia Emilia.
"Ndiyo, Emilia. Nichagulie jina," Dylan akamwambia.
Wote wakamtazama Emilia, naye akawa anamwangalia Dylan kwa makini, kama anatafakari jina ambalo litamfaa.
"Mmmm... Ethan. Tumwite Ethan," akasema Emilia.
Dylan akatabasamu.
Leila akasonya kidogo na kusema, "Me nikafikiri labda utasema Pipindopolupsykapolis."
Baraka akacheka kidogo, kisha akasema, "Ni zuri. Tutakuita Ethan mpaka utakapokumbuka jina lako."
"Na asipolikumbuka milele?" Shani akauliza.
"Haiwezekani. Saa zile alikumbuka kwamba huwa anapenda kulala chini. Atakumbuka vitu vingine tu taratibu," Baraka akasema.
"Kweli?" Steven akauliza.
"Ahahah... ndiyo," Dylan akajibu.
Akamwangalia sana Emilia huku akitabasamu, naye binti akatabasamu pia. Kisha akamshukuru kwa kumpa jina zuri, na kuanzia sasa, Dylan angeanza kufahamika kama ETHAN.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
WhatsApp +255 787 604 893
MuendelezoDYLAN [emoji666]
Story by Elton Tonny
Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
ILIPOISHIA....
"....na mbona mmerudi hivi, eeh? Nimempigia mama Conso simu akaniambia ulikuwa umeshaondoka kule mapema...ulienda wapi?" Shani akawa anamfokea Leila.
Leila akawa amekaa kimya tu akiwa ameudhika.
"Mama Leila..." Dylan akamwita.
Shani pamoja na wengine wakamtazama.
"...samahani...haikuwa makosa yake. Ni mimi ndiyo nilimchelewesha," Dylan akamtetea Leila.
Leila akamwangalia Dylan, akishangaa kwa nini kadanganya.
"Unamaanisha nini?" Shani akamuuliza kwa ukali.
"...nilikuwa nafanya zoezi nika...nikamwona. Nikamwita nikamwambia...anisubirie ili tuje wote nyumbani. Lakini nikamchelewesha sana, mpaka mvua ikaanza," Dylan akasema.
"Na mbona mmerudi bila kuvaa nguo?" Shani akauliza.
"Mvua ilitunyeshea wakati tunarudi na...Leila akawa ameumia mguu...kwa hiyo ikabidi tutafute sehemu ya kujikinga mpaka mvua ilipoisha. Alikuwa akihisi baridi sana, kwa hiyo hakuweza kuvaa nguo yake...ndiyo nikaja naye hivyo hivyo," akaeleza Dylan.
Shani akamwangalia binti yake, kisha akamtazama tena Dylan kwa mashaka.
"Baraka, mama Leila...naombeni mnisamehe sana kwa jambo hili...nitahakikisha halitokei tena," Dylan akasema kwa unyoofu.
Baraka akamshika begani huku anamtazama kwa kujali.
"Usijali Ethan. Poleni sana kwa kila kitu. Mama Leila alikuwa anawawaza sana kwa hofu maana hatukujua mko wapi. Kaa ili mle. Emilia, wapakulie," Baraka akasema.
Emilia akaenda kuwapakulia chakula.
Leila alikuwa akimwangalia Dylan (Ethan) kwa kuchanganywa sana. Alijiuliza ikiwa alifanya vile kumsaidia au kujifanya yeye ni mtu mzuri sana. Ijapokuwa bado alijawa na kiburi, hakuweza kuzizuia hisia za shukrani kumwelekea Dylan (Ethan). Sasa ni kama alianza kumwangalia kwa njia tofauti na jinsi alivyomchukulia mwanzoni.
★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA SABA
★★★★★★★★★★★★★★★
"Steven rudi ukalale, kesho shule," Shani akamwambia mwanae.
"Yaagh... kulala mapema! Yaani naombea mvua kubwa inyeshe kesho nilale mpaka jioni," Steven akaondoka huku analalamika.
Baraka akasogea karibu na mguu wa Leila ulioumia na kujaribu kuunyoosha, lakini Leila alilia kwa maumivu sana, hivyo Baraka akaacha. Emilia alikuwa ameleta vyakula alivyowapakulia kwenye sahani mbili na kuviweka mezani.
"Hamna hata dawa ya kuchua, sasa tutafanyaje?" Shani akauliza kwa kujali.
"Nisaidieni kwenda chumbani," akasema Leila.
"Kula kwanza," Baraka akasema.
"Hapana, sijisikii kula," akasema Leila.
"Chakula kimeshapakuliwa sasa, em' kula bwana," Shani akasema kwa ukali.
"Sijisikii kula, nataka kulala," Leila akasema huku machozi yanamlenga.
Baraka akatazamana machoni na Dylan, wakiambiana bila maneno kuwa Leila ana tatizo fulani bila shaka. Lakini ilibidi Dylan atulize hisia zake kwa kuwa aliwasimulia story tofauti kidogo na ukweli wenyewe. Ikabidi Baraka na Shani waanze kumsaidia Leila anyanyuke ili wampeleke chumbani, lakini akawa analia kwa maumivu aliyohisi mguuni. Shani alikuwa akimwambia ajikaze, lakini Leila aliendelea kuonyesha hangeweza kwenda kwa mtindo huo.
Ndipo Dylan akasogea karibu na kuwaomba wazazi wake ambebe mikononi ili ampeleke chumbani. Wakakubali, naye akamnyanyua taratibu na kufanya binti awe kama amelalia mikononi mwake, huku nyuso zao zikitazamana, kisha akaanza kumpeleka chumbani. Alimlaza kitandani kwa uangalifu, kisha yeye na Baraka wakaondoka humo, wakiwaacha Leila na mama yake.
"...najua wewe siyo wa kukaa na kumsubiria Ethan, labda uwe umerogwa. Niambie ukweli, mlikuwa wapi?" Shani akawa anamshawishi Leila aseme ukweli.
"Mama... naomba uniache. Sijisikii vizuri. Udadisi wako haunisaidii," Leila akamjibu akiwa amelala huku amegeukia upande mwingine.
Shani akamwangalia kwa ufupi, kisha akasonya na kusema, "Utajua mwenyewe sasa."
Akaondoka chumbani hapo baada ya Emilia kuingia. Leila aliendelea kujilaza kimya tu akitafakari matukio ya siku hiyo, na baada ya muda fulani akawa amesinzia.
Dylan alibaki na Baraka sebuleni akipata msosi. Baraka aliongea naye kuhusiana na ishu yake ya kulitengeneza daraja, naye Dylan akamwambia alikuwa anataka kuanza kesho. Baraka alimuuliza kwa mara nyingine kama kweli alikuwa anajua anachokifanya, na kijana huyu akamwambia ijapokuwa bado hakujua ni kwa nini, moyo wake ulimwambia anafahamu vizuri kile ambacho angefanya. Pia, alidokeza kuwa huenda hii ikawa njia nyingine ya kumsaidia ili arudishe kumbukumbu yake mapema.
Baada ya Dylan kumaliza kula, wote walielekea vyumbani ili kupumzika kwa ajili ya kesho.
★★★
Asubuhi kama kawaida, wote waliondoka, isipokuwa Leila na Dylan. Leila aliumwa mguu bado, hivyo hangeweza kwenda kufanya kazi. Shani alikuwa ameongea na mama Conso, mwenye mgahawa ambao Leila alifanyia kazi, akimwombea ruhusa kwa kumtaarifu kuwa Leila alipatwa na ajali ndogo. Ijapokuwa mguu wake uliuma, asubuhi hii alijitahidi kwa kuwa alitembea taratibu kwa kuchechemea. Dylan alimsaidia mara kwa mara kumpa egemeo kama angehitaji kwenda nje, na Leila alijihisi vizuri kila mara kaka huyo alipomsaidia. Hakuleta kiburi tena, ijapokuwa bado moyoni hakuwa amemzoea.
Ilipofika mida ya saa 5, Baraka alimpigia simu Leila kumuuliza mguu unaendelea vipi. Akasema bado anahisi maumivu, lakini Ethan (Dylan) anamsaidia sana. Baraka akamwambia ampe simu "Ethan" ili waongee, naye akamuuliza ikiwa alianza kazi. Dylan alimwambia kuwa bado hakuanza kwa sababu alihisi alihitajika kumwangalia Leila, lakini Baraka akamhakikishia kuwa Leila angekuwa sawa, hivyo kama angetaka kuanza kazi, aanze tu.
Baada ya Dylan kumrudishia simu Leila, alimuuliza ikiwa ingekuwa sawa akimwacha kwenda kufanya kazi fulani.
"Haina shida. Nenda tu," Leila akasema.
"Naona kama... inaweza ikatokea dharura," Dylan akasema kwa kujali.
"Usijali niko sawa. Kila kitu kipo vizuri, chakula kipo, mimi nakuwa chumbani tu, kwo' we nenda wala usiwaze," Leila akamwambia kistaarabu.
"Sawa. Wacha... ngoja niende. Ikitokea...ikitokea dharura nipigie...aagh...sina simu kweli..." Dylan akawa anababaika.
Leila akacheka kwa sauti ya chini.
Hii ndiyo mara ya kwanza Leila anacheka kutokana na kitu alichosema Dylan. Dylan akafarijika sana moyoni kuona badiliko hilo.
"Okay. Baadae," akamuaga.
"Poa," Leila akamjibu.
Kijana akaondoka na kubeba vifaa alivyohitaji kwa siku hiyo. Akafika usawa wa daraja, kukiwa hamna mtu hata mmoja eneo la hapo, naye akaanza kazi sasa. Alifanya vitu jinsi kichwa chake kilivyomwongoza, na alijitahidi kuweka umakini wa hali ya juu ili kufanya mambo kwa njia iliyo bora kabisa.
Baadae, watu fulani waliopita eneo hilo wakiwa wanatokea eneo la upande wa pili walimwona akikomaa na matengenezo, nao wakamuuliza alikuwa anafanya nini. Ndiyo hapa akawaambia alikuwa kwenye harakati za kulitengeneza daraja hilo, na baadhi yao walimwona kuwa mjinga. Wengine walifikiri ameanza kuvuta bangi kama Ishengoma, wakiangalia marasi yake na ndevu zake nyingi, hivyo wakampuuzia tu na kuendelea na mambo yao. Kwa siku hiyo, Dylan alifanikiwa kutengeneza msingi imara wa mwingilio wa daraja hilo, ulioingia chini ya ardhi sana kwa kuuunganisha na ule wa zamani.
★★★
Kila siku baada ya hapo aliendelea kwenda kwenye kivuko hicho, akiongeza vitu, akipunguza vitu, akitengeneza na kulirudisha daraja katika mwonekano wake mpya na uliofaa. Watu wengi walimwambia aache kwa kuwa anajisumbua, na haingechukua muda angekata tamaa. Shani alimvunja sana moyo kuwa hatafanikiwa, lakini Dylan hakuacha kufanya kazi hiyo.
Kadiri siku zilivyozidi kusonga, aliendelea kuwashangaza watu kwa sababu alizidi kulisogeza daraja mbele tu. Baraka angemsaidia mara kwa mara, akifurahia sana utendaji wa kijana huyu. Dylan hakuogopa hata kudondokea kule chini; alijitoa kwa moyo wake wote ili kuwasaidia watu hao.
Wenyeji wa eneo hilo walipoona Dylan amelifikisha daraja nusu ndani ya wiki mbili tu, walishangaa sana. Wengi waliomwona mwanzoni kama mjinga, wakaanza kusaidiana naye kuendeleza ujenzi. Muundo wa daraja wakati huu ulikuwa tata zaidi, kwa sababu mwanzoni vikanyagio vyake vilikuwa vya chuma nyepesi sana (kama bati) na mbao nene, lakini wakati huu Dylan aliweka ZOTE ziwe za chuma ngumu. Hivyo, watu wengi walisaidia kwa kuleta vyuma vingine vingi zaidi na vifaa mbalimbali; wakifata maelekezo yake alipowaongoza jinsi ya kuvipangilia.
Ilikuwa ni wakati wenye kusisimua wengi, kwa sababu bila kutarajia, Dylan alikuwa amewaunganisha watu wote washirikiane kufanya jambo ambalo walitegemea mpaka kupewa msaada na watu wa juu. Sasa wakawa wametambua kuwa walihitaji mkandarasi mmoja tu, tena aliyepoteza kumbukumbu, ili waweze kujenga tena matumaini yaliyokuwa yamebomoka.
Daraja likawa limekamilika ndani ya wiki tano tokea Dylan alipoanza kulitengeneza, kwa kuwa nguvu kazi ilikuwa ya mikono tu. Sasa alichokuwa akifanya ni kuhakikisha sehemu zote muhimu za kulikaza ziko imara.
★★★
Ilikuwa ni Jumamosi moja mida ya jioni watu kadhaa walipokuwa eneo hilo la daraja. Walikuwepo wanaume kwa wanawake na watoto, wakifurahia kutembea-tembea hapo huku Dylan na wenzake baadhi wakihakikisha daraja liko vizuri. Familia yote ya bwana Baraka ilikuwepo pia, na kufikia wakati huu hata Shani alikuwa amemkubali sana jamaa.
Wakati Dylan alipokuwa anaangalia sehemu fulani ya chini ya daraja hilo katikati, aliteleza na kupindukia upande wa pili kama anadondokea kuelekea chini, lakini mkono wake mmoja ukashika kamba nene ya kushikia daraja, hivyo akawa amening'inia. Wengi walishtuka na kuanza kumkimbilia, huku akijitahidi kuendelea kulishikilia kwa utulivu, maana kama angetikisika kidogo tu, mkono ungeteleza. Walifika rafiki zake wawili haraka na kuanza kumvuta, nao wakafanikiwa kumrudisha kwa juu.
Watu walimtazama kwa wasiwasi, wakimuuliza kama yuko sawa, lakini Dylan akaanza kucheka. Wote walimshangaa sana, wakishindwa kuelewa angewezaje kucheka ndani ya hali hiyo. Akanyanyua kidole gumba juu huku anacheka, kuwaonyesha kwamba yuko sawa. Wote wakaanza kucheka pia wakitambua kweli jambo hilo liliburudisha. Watu wengi walipendezwa na kufurahishwa na Dylan, na sasa akawa anaonwa kama mtu mwenye kutegemeka sana.
Uhusiano wake pamoja na Shani na Leila ulizidi kuwa wa kirafiki zaidi. Leila alipendezwa sana na Dylan na hata kumsimulia mara nyingi kwa rafiki zake. Alikuwa amemzoea zaidi sasa, hata walikuwa wanataniana kama kaka na dada wanavyofanya. Shani naye alimwonyesha Dylan heshima zaidi, akitambua kijana huyo alikuwa baraka kwao. Baraka kwa upande mwingine, alimsifia sana kijana wake huyo kwa marafiki, akiwaambia jinsi ambavyo alisaidiana naye mpaka kufanikisha mpango huo. Alijivunia sana.
Baada ya Dylan kuwa ametulia kutokana na kukaribia kuanguka, aliwatangazia watu kuwa daraja lilikuwa limekamilika. Wengi walishangilia, huku baadhi ya wanawake wengi wakimkimbilia na kumkumbatia. Walifurahi sana, na watu wote wakakubaliana kufanya sherehe ndogo kesho kwa Baraka ili kuweza kufurahia mafanikio yao.
Watu wangepita hapo mara kwa mara, wakifurahia kivuko chao kipya baada ya miaka miwili ya kusota wakizunguka kwa kutumia njia ndefu sana. Steven alimsifia sana Dylan kwa kuwa alifurahi kwamba hangewaza tena kuhusu kuamka mapema mno. Habari hizo za daraja kujengwa zilikuwa zimesambaa mpaka maeneo ya mjini zaidi, na watu kadhaa walitaka kuja hapo kujua ni nini kilichofanya mpaka daraja lilioachwa ukiwa kwa miaka miwili na zaidi, litengemae.
★★★
Asubuhi iliyofuata, Jumapili, watu kadhaa walikuwa wamefika hapo kwa bwana Baraka, wakipangilia masuala ya sherehe. Michango ilikuwa imekusanywa kwa uharaka sana, na hii ilionyesha jinsi gani watu walivyokuwa na hamu ya kusherehekea siku hii. Wanawake wengi walikuja na vyombo vyao, wakianza kuandaa mambo ya upishi. Kulikuwa na vyakula mbalimbali ambavyo vilinunuliwa na kuletwa na vijana, ambao walifanya kazi upesi kutokana na kurahisishiwa mambo kwa sababu ya daraja kutengenezwa. Wenye mifugo walileta mbuzi na ng'ombe wa kuchinja kwa ajili ya nyama, na mboga mbalimbali zikaanza kupikwa pia.
Dylan alikuwa pamoja na rafiki zake, hasa sehemu waliyounganishia sabufa kubwa na kompyuta ndogo kwa ajili ya muziki. Fred, yule rafiki yake, alikuwa ni DJ pia na alimiliki ofisi ndogo ya kubani na kuuza CD, na kuwekea watu movie na miziki. Watoto wadogo walicheza muziki pamoja, na maandalizi ya misosi yakaendelea kuwekwa sawa na wanawake. Dylan akaamua kuwaacha ili aelekee saluni kwa ajili ya kutengeneza nywele. Zilikuwa nyingi na ndefu sana wakati huu, hivyo aliona ni bora akiweka mwonekano mpya, hasa baada ya rafiki zake kumwambia mara nyingi kwamba anaonekana kama mtumwa wa wakati ujao!
Alikwenda kwenye saluni eneo la pili na kutengeneza nywele na ndevu zake kwa njia nzuri. Hakuwa amekumbuka chochote kuhusu jinsi alivyopenda kunyoa zamani, lakini alinyoa kwa mtindo kama ule alioupenda. Alizikata rasi mpaka kufikia shingoni, naye alihakikisha anazitengeneza kwa njia ambayo zile nene zingeondolewa na kubaki nyembamba kiasi. Pande za kichwa chake alizinyoa na kuacha nywele laini kidogo sana, na ndevu alizipunguza na kuacha kidogo; zikichongwa vizuri kutokea kwenye timba. Kisha, akatafuta 'rubber band' na kuzifunga rasi zake kwa nyuma ili chache zimwagikie kichwani kama mkia (ponytail) na chache za mbele akaziacha zidondokee pembeni ya uso. Alikuwa na style nzuri sana Dylan hata kama hakukumbuka mambo mengi vizuri.
Akiwa bado mbele ya kioo cha saluni, aliona jambo fulani ambalo lilivuta umakini wake. Kupitia hicho hicho kioo, aliona mwanaume fulani upande wa nje, akiwa amevalia kofia iliyofunika uso wake kiasi, na akiwa kama anamtazama sana. Ilibidi Dylan aendelee kujifanya kama anatengeneza tu mwonekano wake kwa kujiangalia kwenye kioo, lakini kwa kuibia akawa anamwangalia mwanaume huyo.
Hakumjua, na hakuwahi kumwona kabla, kwa nini alikuwa anamtazama sana? Alijiuliza bila kupata jibu. Kisha, akamwona mwanaume huyo anatoa simu yake mfukoni na kuiweka sikioni, naye akaondoka eneo hilo. Dylan hakujua afikie mkataa gani kuhusu mtu huyo; ikiwa labda alikuwa anamtazama kwa nia nzuri au mbaya, ama ikiwa yeye mwenyewe (Dylan) ali-panick tu. Kwa kuwa mwanaume huyo aliondoka eneo hilo, jamaa akaona ampotezee tu.
Baada ya kuridhishwa na mwonekano wake mpya, akatoka zake saluni na kuanza kurejea nyumbani. Watu wengi aliopishana nao walimwangalia sana kutokana na jinsi mwonekano wake mpya ulivyombadilisha. Alipofika kule kwenye sherehe, watu walimsifia sana kwamba amependeza, wengine wakishangaa jinsi mtindo wake wa nywele ulivyomfanya aonekane mdogo. Wanawake na wasichana kadhaa walivutiwa naye, na wengi walikuwa wanajishebedua sana ili aelekeze uangalifu wake kwao, lakini jamaa hakuwa na muda.
Kama ni mwanamke aliyevutiwa zaidi na sura ya Dylan wakati huu kuliko wote, basi hakuwa mwingine ila Leila. Mwanzoni alipomwona alishindwa hata kuendelea na kazi ya kupika, akibaki kumtazama tu mpaka aliposhtuliwa na sauti ya 'Leila si ukoroge hayo maharage!' Uzuri wa Dylan ni kwamba alikuwa mwanaume aliyetulia sana, hivyo mambo kama wanawake hayakumpa presha hata kidogo.
Muda wa msosi uliwadia. Watu walikula, walikunywa, na kuserebuka kupita maelezo. Ilikuwa ni kama eneo lile lote liliishiwa na nafasi kutokana na watu kuwa wengi mno. Hadi vyombo vya kuwekea chakula viliisha, hivyo ikabidi wengine wasubirie waliomaliza kula wawape sahani ili nao wapate msosi. Kutokana na wingi wa chakula, wengi walikuja kumaliza kula saa 11, ndipo muziki wa kujiachia ukaanza. Watu walicheza kwa mbwembwe sana, huku wengine wenye ustaarabu wakifurahia kuwatazama tu.
Watu walicheza sana, na kama ilivyo kawaida ya ma-DJ, Fred alibadili muziki kila mara na kuwapa ladha nyingi nzuri, na sasa akawa akiweka muziki wa nyimbo za aina ya singeli. Wanawake wengi walipenda nyimbo hizo, nao walizicheza kwa furaha sana. Leila na rafiki zake wengi walikuwa wamevaa madera, hivyo walizungusha viuno na kutikisa makalio kwa njia yenye kusisimua. Wanaume kadhaa vijana walijumuika nao kucheza, lakini kwa uangalifu ili wasiguse mke wa mtu.
Baraka na wengine walikuwa wakimshawishi Dylan aende kucheza pia, lakini kwa unyoofu alisema hakujua kucheza; hasa kwa sababu aliona haya. Huyu alikuwa Dylan aliyepoteza kumbukumbu yake, mstaarabu, na mpole. Ingekuwa ni Dylan yule wa zamani aliyekuwa mtundu sana, wote hapo wangemshangaa kwa kuwa angewaonyesha jinsi gani alivyojua mambo.
Fred alipoweka wimbo wa singeli wa msanii Rayvanny akimshirikisha Dulla Makabila, ulioitwa Miss Buza, wanawake walipiga kelele kwa shangwe nyingi. Hata wengine waliokuwa wamekaa pembeni walijiunga nao hapo ili kuonyesha upendo wao kwa wimbo huu. Ilipofika kwenye daraja la wimbo huo (bridge), sauti za juu za wanawake zilisikika zaidi, wakifatisha maneno aliyoimba msanii Rayvanny.
"....ana msitu kwapani, ndala kifuani... Kwenye daladala anapita dirishani... Ghetto anazima taa, vipele mapajani... Ana dera jipya, chupi la zamani... Ayoo yoo yoooh.. huyo Miss Buza...."
Wakaanza kusasambua sasa! (twerking)
"...mama Miss Buza..."
Wanasasambua tu!
"....jamani Miss Buza... Nampenda Miss Buza...."
Mambo haya yote yalimchangamshasana Dylan. Na pia, muda mwingi alimkazia fikra Leila, kwa kuwa mwanamke huyo alicheza huku akimtazama pia. Alifanya mambo kwa njia iliyoonyesha kwamba alimchezea Dylan, kutia ndani na wanawake kadhaa ambao walivutiwa na Dylan. Dylan alipenda sana jinsi Leila alivyoonyesha ufundi wa viuno na usasambuaji.
Baada ya usiku kuwa umeingia, wakubwa waliwasihi vijana wengi waelekee majumbani kwao, na watu baadhi wakaanza kuviondoa vitu kadha wa kadha eneo hilo. Kila mtu alihisi kuburudishwa sana, na sasa bila shaka wangetarajia mambo mengi mazuri yaendelee kutawala eneo hilo baada ya kulirekebisha daraja lao.
★★★
Mambo hayakuwa mazuri upande wa wazazi wake Dylan. Ni kama kila jambo walilofanya baada ya "kifo" cha mwanao halikufanikiwa hata kidogo.
Mr. Bernard pamoja na mtu yule aliyekuwa anashirikiana naye ili kumwangusha Gilbert, walifanikiwa kwa kiwango kikubwa kumharibia sifa yake nzuri kwenye kampuni na kumwondoa kwenye uongozi; tena kwenye kampuni aliyoijenga na kuikuza mwenyewe! Mambo waliyoyafanya watu hawa sanasana ilikuwa ni kusambaza porojo za uwongo kuhusu kifo cha Dylan, kuharibu baadhi ya mipango mingi ya Gilbert, na hasa kuporomosha utendaji kwa kuiba vifaa vingi ambavyo Gilbert alitumia pesa nyingi kuviweka hapo; lengo lao likiwa kukwamisha miradi ya kampuni.
Hivyo, mapato yalishuka kwa kiwango kikubwa, na wafanyakazi wengi walilalamika kutolipwa jinsi walivyostahili. Kwa hiyo washiriki wa bodi ya kampuni, wakiwa na nguvu kubwa ya usemi hapo kutokana na kushikilia hisa za juu zaidi, walimwondoa Gilbert kwenye nafasi ya uraisi wa kampuni na kumweka Mr. Bernard, ambaye alitumia hila nyingi kuwashawishi washiriki hao wafikie uamuzi huo bila Gilbert kujua.
Ilifikia hatua mpaka ikawabidi Gilbert na Jaquelin kuondoka kwenye nyumba yao kwa kuwa waliimudu kupitia pesa zao ambazo ziliunganishwa (linked) na kampuni moja kwa moja; kwa sababu kampuni ilikuwa yao. Lakini sikuzote watu wenye nia mbaya hufanya kila wanachoweza ili kuwaporomosha wengine, na watu hao walifanikiwa kwa hilo. Ikawabidi wazazi hao wa Dylan wahamie kwenye ile nyumba ambayo Gilbert alimpa Dylan, kwa kuwa ilikuwa chini ya jina la mwanao, ambaye aliweka kila jambo lililomhusu kwa kibinafsi sana na siyo kutegemea kampuni.
Jaquelin alikutana na watu wengi aliowafahamu ili wamsaidie kuweza kutatua tatizo lao, hasa wanasheria, lakini kila sehemu ikawa ni kutokufanikiwa tu. Gilbert alitaifishwa kampuni ndani ya muda mfupi sana, na roho ilimuuma mno. Hawakuwa na njia nyingine tena ya kulazimisha mambo, hivyo wakageukia mradi mwingine ambao ungewasaidia kwa wakati huo, yaani mgahawa wa Dylan, Dy-Foods.
Wakati ule alipoondoka na kupatwa na ajali, Dylan alikuwa ameuacha mgahawa wake chini ya uangalizi wa msimamizi wake aliyemwajiri kipindi kile, aliyeitwa Tony, na alikuwa amekwishampatia maelekezo ya kumwajiri Fetty kama msimamizi msaidizi (assistant manager). Kufikia wakati huu, mgahawa huu uliendelea kuingiza pesa nzuri tu, na hata idadi ya waajiriwa iliongezeka. Fetty alikuwa hapo pia kama msimamizi msaidizi, akiwa ameiacha kazi yake ya zamani miezi michache nyuma.
Kwa muda huo wote waliofikiria kwamba Dylan alikuwa amekufa, Gilbert, kabla hajaondolewa kwenye kampuni, alikuwa akiwasiliana na Tony ili kujua maendeleo ya mgahawa huo, na aliongoza mambo bila Jaquelin kujua kwa sababu yeye hakuujali. Lakini wakati huu mambo yalibadilika, naye Jaquelin akawa tayari kujihusisha nao na kusaidia kuupanua zaidi, huku wenzi hao wa ndoa wakijitahidi kutafuta suluhisho la tatizo lao bila kupata matokeo mazuri.....
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
WhatsApp +255 787 604 893