Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #181
123
Katika sofa jingine la watu wawili nilimwona mjomba mkubwa, Japheti Ngelela aliyekuwa anakaa Kiloleni Tabora akiwa ameketi peke yake na alikuwa kimya akionekana kuzama kwenye tafakari. Mjomba Japheti alikuwa mwanamume wa makamo, mrefu na maji ya kunde, alikuwa na ndevu nyingi zilizokizunguka kidevu chake na umbo kakamavu la kimichezo lililofanana na maumbo ya wachezaji wa ligi ya mpira wa kikapu.
Alikuwa amevaa shati zuri jeupe lenye mistari midogo ya rangi ya bluu, la mikono mirefu, brandi ya Maria Santangelo kutoka nchini Italia, tai nyekundu shingoni na suruali nyeusi.
Na kwenye sofa jingine dogo nilimwona mjomba mwingine, Mchungaji Edwin Ngelela aliyekuwa anaishi Jijini Dodoma, alikuwa ameketi kwa utulivu na mkononi alishika Biblia. Mchungaji Ngelela alikuwa amevaa suti ghali ya kijivu ya single button brandi ya Piacenza kutoka nchini Italia na shingoni alivaa kola ya kichungaji. Pia alikuwa na miwani ya macho.
Nilibaki nimewakodolea macho nikiwa nimetahayari sana. Wote walikuwa wananitazama kwa umakini kisha macho yao yaliutazama mzinga wa Konyagi nilioshika mkononi. Nilihisi kijasho chembamba kikinitoka mwilini. Nikafungua mdomo wangu kutaka kusema neno lakini maneno hayakutoka, mdomo wangu ulinidondoka kwa hofu utadhani nilikuwa nimezingirwa na wanamgambo hatari wa kundi la kigaidi la al-Shabab waliokuwa tayari kujilipua wakati wowote.
“Karibuni mezani…” niliisikia sauti ya Amanda, na nilipogeuza shingo yangu kuangalia kule ambako sauti ilikuwa inatokea nikamwona Amanda akitokea kwenye chumba cha chakula (dining room) na kuja pale sebuleni huku akiwa amepambwa na tabasamu usoni kwake. Alikuwa amevaa dela na juu yake akivaa aproni akionekana kuwa alikuwa ametoka kuandaa chakula.
“Mama, ulisema nikuandalie…” alitaka kusema lakini akasita na kusimama ghafla baada ya kuniona. Tukabaki tumetazamana kwa kitambo.
Watu wote pale sebuleni waligeuka kumtazama Amanda kisha wakayarudisha macho yao kwangu. Niliona kama vile macho yao yaliniangalia kwa kunisuta.
Nikavuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kuzishusha taratibu huku nikijipa ujasiri kisha nikaanza kupiga hatua taratibu hadi kwenye sofa alilokalia mjomba Japheti, nikaketi na kuwasalimia watu wote kwa unyenyekevu huku nikilazimisha tabasamu. Bila hiyana wote waliitikia salamu yangu lakini hawakuacha kunitazama kwa umakini.
“Jason!” mjomba Japheti aliniita kwa sauti tulivu ya chini huku akinitazama usoni kwa umakini.
“Naam!” niliitikia kilevi huku nikijitahidi kuifanya sauti yangu iwe tulivu.
“Natambua kwamba mapito unayopita ni magumu sana, lakini aina hii ya maisha uliyoamua kuishi si sawa kabisa, mjomba,” mjomba Japheti aliniambia kwa sauti tulivu huku akininyang’anya chupa ya Konyagi niliyoshika mkononi, kisha akaitazama kwa umakini na kuiweka kando.
“Umekula?” mjomba Japheti aliniuliza huku akiendelea kunikazia macho usoni kwa umakini.
“Hapana,” nilijibu huku nikiangalia chini kuyakwepa macho yake.
“Twende mezani tukale,” mjomba Japheti aliniambia huku akinishika mkono kuninyanyua.
“Hapana uncle, nipo poa,” nilimjibu huku nikikataa kuinuka.
“No, unatakiwa kula, mjomba,” mjomba Japheti alizungumza huku akigeuka kumtazama Amanda ambaye alikuwa bado amesimama akinitazama kwa wasiwasi.
“Itabidi nikajimwagie kwanza maji,” niliwahi kumwambia mjomba Japheti kabla hajasema chochote huku nikiinuka ili nielekee chumbani kwangu. Muda huo kichwa changu kilikuwa na mawenge kutokana na Konyagi nilizokunywa, na nilipoanza kuondoka Mama akaniwahi.
“Jason, tukimaliza kula nitahitaji kuzungumza na wewe,” Mama alisema huku akiinuka pale kwenye sofa alipokuwa ameketi.
“Usiku huu!” nilimuuliza Mama kwa mshangao huku nikiitazama saa yangu ya mkononi.
“Ndiyo, usiku huu huu maana raha ya mchuzi uunywe ukiwa bado wa moto,” Mama alisema kwa sauti ya msisitizo.
Nilitaka kusema neno lakini nikasita na kuwatazama wajomba kwa wasiwasi kidogo kabla macho yangu sijayahamishia kwa Amanda ambaye muda wote alikuwa mtulivu mno akiwa amesimama kwa unyenyekevu.
“Sawa, Mama!” nilisema huku nikishusha pumzi kwani sikuwa na namna nyingine yoyote ya kufanya isipokuwa kukubali.
Niliingia chumbani kwangu na kuvua shati langu kisha nikalitupa kitandani, nikavua viatu na kuviweka kwenye stendi maalumu ya viatu, halafu nikavua soksi na kuzitupia kitandani na mwisho nikavua suruali na kuitupia kitandani. Nilipomaliza nikachukua shati langu nililovua na kuanza kupekua kwenye mifuko ya shati, nikatoa vimbaka vitatu na nusu vya kuchokonolea meno na kuvitupa ndani ya kapu la taka lililokuwa mle chumbani.
Kisha nilichukua suruali yangu na kuanza kukagua mifuko ya mbele kwanza kwa kutoa nje vitambaa vyake, nikatoa kitambaa laini cha kujifutia jasho na simu yangu ya mkononi na kuviweka kitandani, kisha nilitomasa mfuko wa nyuma, nikatoa pochi na kuiweka kitandani.
Kisha nikachukua taulo na kuingia bafuni ambako nilifungua bomba na kujimwagia maji, baada ya muda fulani nilitoka nikiwa nimechangamka. Sasa nilianza kujisikia mwepesi kidogo na akili yangu ilichangamka. Dakika ishirini baadaye nilitoka nikiwa nimevaa suruali nyepesi ya mazoezi na fulana na kuungana na watu wengine pale sebuleni. Niliwakuta wakiwa na vimbaka wakiondoa masalio ya chakula kwenye meno.
“Nadhani sasa una muda, naomba tukazungumzie ofisini kwako,” Mama aliniambia huku akiinuka toka kwenye sofa.
Kisha aligeuza shingo yake kumtazama Amanda aliyekuwa anatoka jikoni kuja pale sebuleni, mkononi alikuwa amebeba trei kubwa lililokuwa na sahani kadhaa zenye matunda aina ya ndizi, vipande vya nanasi, embe na vipande vya matikiti maji vilivyokoza wekundu.
“Mama, naomba mwandalie mwenzako chakula halafu ulete kule ofisini kwake,” Mama alimwambia Amanda.
“Sawa mama,” Amanda aliitikia kwa unyenyekevu huku akilitua lile teri la matunda juu ya meza ya kioo pale sebuleni.
Sikuwa na namna nyingine ya kufanya nikaondoka huku Mama akinifuata nyuma, tukaingia kwenye ofisi yangu binafsi ambayo pia niliitumia kama maktaba. Ilikuwa ofisi nzuri yenye hadhi ikiwa na samani na vifaa vyote vya kiofisi. Tuliketi kwenye viti vya kiofisi vya ngozi halisi na hapo Mama akanikabili.
“Jason mwanangu…” Mama alisema mara baada ya kuketi huku akiitazama kwa umakini picha kubwa ya Rehema iliyotundikwa ukutani. Nami nikaitupia jicho mara moja kisha nikayarudisha macho yangu kwa Mama nikisubiri kusikia alichotaka kuniambia.
“Jason!” Mama aliniita huku akinitazama kwa umakini.
“Ndiyo, Mama,” nilisema kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
“Hivi umejitazama kwenye kioo kuona kama kweli wewe ndiye Jason? Umeiona taswira yako?” Mama aliniuliza huku akinitazama kwa huzuni.
Sikuweza kujibu maswali yake, nilibaki kimya nikiwa nimeinamisha uso wangu na macho yangu yakitazama sakafuni. Hata hivyo nilipeleka mkono wangu wa kulia na kuzishika ndevu huku nikiwa kama mtu asiyeamini kwa kile nilichokigusa.
“Ulipozaliwa tu nilikupa jina la baba yangu nikiwa na matumaini makubwa sana juu yako, kwamba utakuwa jasiri kama babu yako. Sijajua kwa nini unachanganyikiwa kwa sababu ya mapenzi? Kwa nini unaihangaisha akili yako kufikiri juu ya mtu ambaye hujui kama bado umo akilini mwake!” Mama alilalamika kwa sauti iliyojaa uchungu uliodhihirishwa kwa machozi yaliyoanza kumtoka.
Itaendelea...