Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

View attachment 2200867
110

“Usiseme hivyo Asia, nakupenda na nitakupenda hadi kifo kitakapotutenganisha,” niliongea kwa utulivu huku nikiruhusu tabasamu langu kuchanua usoni.

“Unanidanganya Jason, unachofanya ni kunifariji kama mtoto. Kwa kweli nafsi yangu inajuta kukufahamu. Umeuteka moyo wangu na sasa nashindwa kabisa kukuacha.”

“Nakuhakikishia kuwa nipo tayari kwa lolote mpenzi. Wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu,” niliongea huku nikizichezea nywele zake na hapo nikaona tabasamu hafifu likichanua usoni mwake.

“Kweli mpenzi?” Asia aliniuliza huku akiniangalia machoni. Sasa tabasamu liliupamba uso wake.

“Kweli kabisa nakuhakikishia,” nilimhakikishia.

“Lakini tuna tofauti kubwa, mimi ni Muislamu na wewe ni Mkristo, sasa tutaoana vipi?” Asia alisema. Nikafikiria kidogo.

“Vyovyote utakavyopenda wewe, ikiwa Kiserikali, Kikristo na hata Kiislamu pia… niko tayari kubadili dini kwa ajili yako!” nilisema kwa kumaanisha. Hata hivyo bado kauli yake kuwa alikuwa na kasoro kubwa iliyomfanya asiwe tayari kulala na mimi ilizidi kuniumiza kichwa, nikaona nimalize utata.

“Asia, sasa naomba uniambie ukweli… kwa nini hauko tayari kulala na mimi?”

Asia alionesha kushituka na uso wake ulionesha maumivu kiasi fulani. Tabasamu lililokuwa limetawala likayeyuka ghafla. Alibaki akiniangalia kwa kitambo kirefu akionekana kujishauri. akijaribu kutabasamu, alitaka kuendelea lakini hakufanya hivyo. Ilimchukua muda kujikusanya pamoja ili aweze kunieleza yaliyomsibu.

“Kwa kweli hata sijui nianzie wapi kukueleza… lakini kwa kifupi ni kwamba, nimekuwa nikiishi na Virusi vya Ukimwi kwa muda mrefu baada ya kuambukizwa na wazazi wangu…” Asia alisema sauti ya unyonge.

Habari ile ilikuwa kama pigo la kisu ambalo lilipenya mwilini na kuujeruhi moyo wangu. Nilishtuka sana na moyo wangu ulipiga mshindo mkubwa kama uliotaka kupasuka kwa mshtuko. Masikio yangu hayakuamini kile ambacho yalikuwa yakikisikia na ubongo wangu uligoma kabisa kukubaliana na kile nilichokisikia toka katika kinywa na Asia.

Jambo hilo lilikuwa kubwa mno na nilishindwa kulibeba kabisa. Nililiona jahazi la mapenzi yetu likienda mrama na mimi kama nahodha nilikuwa sina uwezo wa kulinusuru toka katika gharika lile kubwa.

“Jason, Wazazi wangu walishindwa kufuata taratibu za kiafya hasa ukizingatia kuwa kipindi kile bado wanasayansi walikuwa hawajagundua mbinu mbadala za kumfanya mtoto asipate maambuikizi ya ukimwi. Nilizaliwa nikiwa na virus vya ukimwi, na mama yangu kabla ya kufa alinikanya kuwa ni heri nife peke yangu kuliko kuua yeyote asiyekuwa na hatia ndiyo maana pamoja na kuwa nakupenda sana lakini nimekuwa nikisita kulala na wewe…” Asia alisema huku akiniangalia usoni.

Nilivuta pumzi ndefu kisha nikazishusha taratibu. Jasho jepesi lilikuwa likinitoka mwilini na mapigo yangu ya moyo yalikwenda kasi sana. Hata hivyo nilijikuta nikimhurumia sana Asia.

“Nakupenda sana Asia, nakupenda kutoka ndani ya moyo wangu japo umeniambia unaishi na virusi vya ukimwi, lakini tambua si mwisho wa maisha yako. Bado kuna mambo mengi ambayo tunaweza kufanya bila kuathiri maisha yetu,” nilimwambia Asia kwa sauti tulivu lakini iliyobeba huzuni kubwa ndani yake. Machozi yalikuwa yananilengalenga machoni.

“Lakini kwa tatizo langu sina hadhi ya kulala kitanda kimoja na wewe…” Asia alisema kwa huzuni, nikamkatisha.

“Hapana, usiseme hivyo. Ungekuwa huna thamani kwangu nisingekuwa na wewe muda huu. Ni kwa sababu una thamani ndiyo maana unaona niko na wewe…” nilimwambia Asia kwa sauti tulivu.

“Unachokifanya sasa ni kunipa moyo tu. Hilo tu basi! Si zaidi ya hivyo,” Asia alisema kwa huzuni.

“Nikuombe kitu?” nilimuuliza huku nikimtazama moja kwa moja machoni.

“Ndiyo.”

“Naomba uniruhusu nikuoe, najua kuwa tukifuata ushauri wa kitaalamu tutaishi vizuri kama…”

“Jason!” nilikatishwa na sauti kali ya Jamila iliyotushtua sote, mimi na Asia, wakati tukiwa bado tumekumbatiana pale kwenye sofa tukipeana faraja.

Nikainua kichwa na ghafla nikakutana na kitu ambacho sikukitarajia kabisa. Jamila alikuwa amesimama mlangoni na alikuwa akitusogelea taratibu na kisha akasimama hatua kadhaa toka mahala tulipokuwa tumeketi kwenye sofa. Mkononi kwake alikuwa ameshika bastola. Sikujua aliitoa wapi na alikuwa amefika hapo muda gani.

“Jamila!” niliita kwa mshangao.

Asia naye alimwona na kunitazama, tukatazamana pasipo kusema chochote. Muda huo Jamila alikuwa anatetemeka kwa hasira.

Jamila please… huhitaji kufanya hivyo tunaweza kuzungumza…” Asia alisema kwa sauti ya kutetemeka.

Shut up! Nakuheshimu sana Asia na usitake nikufanyie kitu ambacho hutakisahau… tena usinieleze upumbavu wako wowote la sivyo nitaanza na wewe,” Jamila alisema kwa ukali kisha akaikoki bastola yake na kuielekeza kwa Asia.

“Jamila hebu acha utani na silaha za moto,” nilisema kwa sauti tulivu katika namna ya kumsihi Jamila. Hata hivyo macho yake hayakuonesha masihara hata kidogo.

“Nakujua vizuri Jamila, najua wewe si muuaji na huwezi kuniua, tafadhali weka bastola chini,” niliendelea kumsihi Jamila.

“Unanijua vizuri eh? Kwa taarifa yako huujui upande wangu wa pili… sasa leo nitakuonesha mimi ni nani!” Jamila alisema kwa hasira huku akiihamishia bastola yake kwangu, midomo ilikuwa inamtetemeka kwa hasira.

“Jamila tafadhali naomba upunguze hasira unaweza kufanya kitendo ambacho utakijutia maishani mwako. Tafadhali punguza hasira na uiweke chini bastola yako tuongee…” nilijitahidi kumsihi Jamila.

“Hakuna tena kitu cha kuongea mimi na wewe Jason. Umekwisha nionesha wazi kwamba mimi na wewe tumefikia mwisho bila hata kujali kama nimebeba mtoto wako tumboni. Hakuna kitu tunachoweza tukaongea tena. It’s over Jason… it’s over!” Jamila aliongea huku machozi yakimtoka, ni wazi alikuwa ameumia sana moyoni.

“Una roho ya kikatili sana Jason, pamoja na kujiweka wazi kwako bado umeamua kunigeuka na kunitupa kama takataka! Nimeumia sana kiasi ambacho sikutegemea. Maisha yangu yote niliyakabidhi kwako na sioni kama kuna sababu ya kuendelea kuishi hapa duniani bila ya kuwa na wewe…” Jamila alisema huku machozi yakiendelea kumtiririka.

Sasa aliishika vyema bastola yake na kuielekeza kwenye kichwa changu huku kidole cha shahada kikielekea kwenye triga tayari kufyatua risasi.

“Jamila tafadhali acha utani, hiyo ni silaha za moto,” Asia alimwambia Jamila huku akipiga hatua za taratibu kumkaribia.

Stop! Unaona nafanya utani we malaya? Unaona kama nawatania eh?” Jamila alisema kwa ukali na mara akaielekeza bastola kwa Asia na mlipuko mkubwa ukasikika. Wote tukaanguka na kulala sakafuni. Baada ya nukta kadhaa nikafumbua macho yangu taratibu, pembeni yangu alilala Asia na damu nyingi zikimtoka.

“Shetani mkubwa wewe! How could you do this?” nilijikuta nikifoka kwa ghadhabu.

“Usihofu Jason. Hata wewe utamfuata malaya wako muda si mrefu,” Jamila alisema huku akiachia tabasamu la kifedhuli. Ni wazi alikuwa amechanganyikiwa maana alianza kucheka pasipo sababu. Kisha akanyamaza na kunitazama kwa macho makali yaliyojaa chuki huku akiukaza mkono wake kuielekeza bastola yake kwangu.

Hapo akili yangu ilianza kufanya kazi haraka. Nilimtazama kwa umakini machoni nikijaribu kuyasoma mawazo yake. Kufumba na kufumbua nikajinyanyua toka pale sakafuni na kumrukia lakini kabla sijamfikia nikashtukia kitu fulani cha moto mkali kikipenya kifuani kwangu na kunitupa sakafuni kwa kishindo kikubwa.

Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka, nilianza kutetemeka kama niliyekumbwa na ugonjwa mbaya wa degedege. Maumivu makali yalinitawala katika kifua changu, nikajishika kwenye kifua na kugundua kulikuwa na damu zikinitoka, ikanibidi niukaze mkono wangu ili kuzuia damu nyingi isiendelea kuvuja katika sehemu ambayo risasi ilipita.

Jamila alinitazama kwa hofu, akawa kama aliyerudiwa na fahamu zake, akaanza kuweweseka huku akiwa haamini kwa tukio alilolifanya. Aliitupa bastola yake sakafuni na kunisogelea, akapiga magoti na kunikumbatia huku akiangalia kifuani kwangu kisha akaanza kulia kwa uchungu.

“Jason, nilikuwa nakutania! Tafadhali usiniache…” Jamila alisema huku akilia kwa uchungu, alionekana kuchanganyikiwa sana kwa kitendo alichokifanya. “I’m sorry Jason! Please forgive me!”

Mara mlango wa sebuleni kwangu ukapigwa kumbo na hapo nikasikia sauti ya vishindo vya watu waliokuwa wakija mbio pale sebuleni, niliinua uso wangu kuangalia nikaona watu watatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja aliyewafuata kwa nyuma. Niliweza kumtambua yule mwanamke, alikuwa mchumba wangu Rehema na alivaa gauni zuri la kitenge na kilemba kichwani.

Oh My God! We binti umemuua Jason? Kwa nini umemuua Jason?” niliisika kwa mbali sauti ya Rehema akipiga ukelele.

Muda huo huo nikamwona Jamila akiniachia haraka na kuinuka huku akiwa ametahayari.

Taratibu nikahisi nguvu zikiniishia huku mwili ukizizima kwa kukosa uwezo wa kufumbua macho na hapo nikajikuta nikiwa katika hali nzito ambayo sikuwahi kuipata katika maisha yangu ikiutawala moyo wangu. Na mara giza zito likaanza kutanda kwenye mboni zangu za macho na mwili wangu ukilegea, mapigo yangu ya moyo nayo yakaanza kudorora, mwishowe nikahisi roho yangu ikifika njia panda.

“Wewe simama na usijaribu kupiga hata hatua moja! Wewee, hebu mkamate!” kwa mbali nikasikia sauti ya mwanamume ikisema kwa ukali.

“Jason! Jasoon! Jasoooon amkaaa!” kwa mbali sana niliisikia sauti ya Rehema akiniita huku akilia.

Nilitaka kuinuka lakini badala yake nikaanza kujiona nikitumbukia kwenye shimo refu sana lilikokuwa na kiza. Nilijaribu kupiga kelele za kuomba msaada lakini nilihisi sauti yangu haikuweza kutoka bali niliisikia akilini mwangu…

* * *

Mambo yanazidi kunoga. Endelea kuufuatilia mkasa huu wa kusisimua...
Huyo Jason Sizya ni kiboko aisee.Hongera mkuu kwa kutuburudisha wasomaji wako.
 
View attachment 2163558
10

Hata hivyo, kuna nyakati ambazo nilikuwa najiuliza kama hawa wanawake ni viumbe dhaifu kupita vyote duniani ama walikuwa viumbe majasiri kulikoni vyote? Kila nilivyofikiria uchungu wanaoupitia katika kutubeba kwenye matumbo yao na kisha kutuzaa katika hali ya uchungu mkubwa, basi nilipiga goti na kuwavulia kofia ya heshima ingawa kulikuwa na mengine lukuki ambayo kila nilipoyafikiria nilijikuta kichwa kikiniuma sana.

Pamoja na kufikiria hivyo bado tabia ya kuwabadili wasichana kama nguo sikuiacha na ilinifanya nigombane na kaka yangu Eddy mara kwa mara, kwani yeye aliamini kuwa mwanamke alistahili kupewa heshima yake kama ilivyokuwa kwa mwanamume.

Mara nyingi Eddy aliniasa kwa kuniambia kuwa “mwanamke unayemchezea leo, ndiye atakayeolewa na mwanamume mwenzako kesho! Je, unajua mke utakayemuoa anafanywa nini leo na mwanamume mwenzako?”

Neno ambalo halikukauka mdomoni mwa Eddy kila mara aliposikia nina uhusiano na mwanamke mwingine lilikuwa ni “Jason, tafadhali usipende kuchezea hisia za mwanamke.” Alipenda kunikumbusha kuhusu tukio la kuhuzunisha la kifo cha mwanadada Belinda Mwikongi, aliyekuwa binti wa Diwani wa Kata ya Gongoni katika Manispaa ya Tabora, mzee Albert Mwikongi.

Belinda alikuwa msichana aliyetokea kunipenda sana na siku zote aliamini kuwa ningemuoa baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kama ambavyo nilikuwa nimemuahidi, kumbe moyoni kwangu sikuwa na mpango wowote wa kumuoa bali nilipanga kumchezea tu.

Kilichomfanya Belinda anipende sana na kuniamini zaidi ni kwa sababu mimi ndiye ‘nilimwondolea utoto’ wake baada ya kumlaghai sana na kisha kumwingiza katika dunia ya wakubwa. Hiyo ilikuwa ni baada ya kufanya mtihani wake wa mwisho wa kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Uyui hapo Tabora.

Wakati nakutana na Belinda alikuwa na umri wa miaka 18 na alikuwa bado hajamjua mwanamume. Nilipomuuliza kwa nini alikuwa amejitunza hadi wakati huo aliniambia kuwa mtu pekee ambaye alipaswa kuchukua zawadi hiyo ni mume wake pekee na asingeweza kumwamini mtu mwingine yeyote hata mimi japo alikuwa ametokea kunipenda.

Kiukweli nilitumia kila njia hadi kumnasa Belinda na kumwingiza kwenye himaya yangu. Belinda hakuwa mtu wa wanaume kabisa na hakujua chochote kuhusu ulimwengu wa mapenzi. Kilichonisaidia kumnasa ni kwamba nilikuwa mchezaji mzuri sana wa mpira wa kikapu, mchezo ambao Belinda alikuwa anapenda sana kuuangalia.

Hapo ndipo ukawa mwanzo wa uhusiano kati yetu, uhusiano ambao mwanzoni ulianza kwa sharti kwamba tusingekuwa tunakutana faragha mpaka pale ambapo tungeingia kwenye ndoa, hasa kwa kuwa nilikuwa nimeahidi kumuoa pindi tu akishamaliza masomo yake.

Hata hivyo, kutokutana faragha lilikuwa sharti gumu sana kwangu lakini nililipokea kwa shingo upande kwa sababu nilijua tu kuwa ingetokea siku angefanya kosa kwa kuingia kwenye kumi na nane zangu. Siku moja tu alipojisahau nami nikautumia mwanya huo huo kumfunga goli la kiufundi, na hapo ndipo pazia la mapenzi yetu lilipofunguka rasmi.

Wakati matokeo ya mtihani wake yakiwa ndiyo kwanza yametoka ndipo alipogundua uwepo wa mabadiliko mengi katika mwili wake ikiwemo kutapika na kutoona siku zake za kila mwezi. Aligundua hilo baada ya kuona imepita miezi miwili na hali yake ya kimwili ikianza kubadilika.

Baada ya kugundua jambo hilo alinitumia ujumbe mfupi kwenye simu yangu ya mkononi kunieleza kuhusu mabadiliko katika mwili wake na kwamba mama yake alikuwa ameanza kumshtukia na hivyo alikuwa ana mpango wa kumpeleka hospitali kupimwa ujauzito. Kiukweli jambo lile lilinishtua sana, na hivyo nikawa natafuta namna ya kujinasua kwa kuwa sikuwa tayari kuingia kwenye majukumu ya kutunza familia.

Kesho yake alinipigia simu lakini sikupokea akaamua kunifuata nyumbani na kunikuta nikiwa na msichana mwingine aliyeitwa Rahma, na hapo nikaamua kumkana jambo lililomuumiza sana. alilia sana lakini bado nilishikilia msimamo wangu ule ule ya kwamba simjui, na wala sikujali. Hata hivyo, japokuwa sikuamini kuwa duniani kulikuwa na mapenzi ya kweli lakini ukweli ulibaki kuwa Belinda alikuwa ananipenda kikweli kweli!

Pamoja na kumkana kwamba sikumjua lakini chozi lake liliniumiza sana na kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilihisi hatia ikinikaba moyoni mwangu. Hata hivyo, sikutaka kuonesha kama nilikuwa nimeumizwa wakati nilipokuwa mbele ya Rahma, msichana ambaye siku hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kukutana naye.

Siku iliyofuata kaka yangu Eddy alinipigia simu na nilipopokea tu nikashtushwa na sauti yake ya huzuni, akanipa taarifa za kuhuzunisha kwamba Belinda alikuwa amekufa baada ya kunywa sumu. Na kwamba alikuwa ameacha barua fupi iliyokutwa kando ya maiti yake, chumbani kwake ikielezea kuwa “aliamua kujiua kwa sababu asingeweza kuishi huku akimshuhudia mwanamume ampendaye akimsaliti na wanawake wengine…” hata hivyo, katika barua hiyo hakuwa ametaja jina la mwanamume huyo.

Taarifa ile ilinichanganya sana na kifo cha Belinda kiliniumiza sana nikiamini kuwa mimi ndiye niliyesababisha mauti yake. Hata hivyo, sikuwa na namna nyingine yoyote ya kufanya kwani maji yalikwisha mwagika na yasingeweza tena kuzoleka. Ilibidi nimsahau na maisha mengine yaendelee.

Eddy alitarajia kuwa kifo cha Belinda kingekuwa funzo kwangu lakini haikuwa hivyo, ni kama niliyekuwa na pepo la ngono, niliendelea na maisha ya ‘kula ujana’ na walimbwende wa kila rika, kila umbo, kila rangi na kadhalika kila nilipopata nafasi ya kufanya hivyo. Niliamini kuwa maisha yangu yasingeweza kuwa ya furaha kama nisingeiridhisha nafsi yangu ilivyotaka.

Nilikula ujana kwa kubanjuka na warembo mbalimbali nikiamini kuwa huo ndiyo ulikuwa muda wangu sahihi wa kuyafurahia maisha yangu maana kuna wakati ungefika nisingeweza tena kubanjuka nao, hata mwanamuziki Samba Mapangala aliwahi kuimba kuwa “Vunja mifupa kama bado una meno…

______

Itaendelea...
Duh! Belinda akafa kirahisi tu maskini🥲[emoji25]
 
narudi buzwagi.jpeg


111


Pole Sana Kaka!


Saa 4:00 asubuhi…

MACHO yangu yalifunguka, nikajikuta nikiwa nimelala kitandani ndani ya chumba kikubwa kilichoonekana kama chumba maalumu cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu kikiwa na vitanda viwili maalumu kwa wagonjwa na mitambo ya kisasa ya tiba yenye kumsaidia mgonjwa kupumua na mingine ya kusoma mapigo ya moyo jinsi yanavyoendelea.

Niligundua kuwa muda huo nilikuwa nimelala kitandani kama mfu nikiwa nimefunikwa kwa shuka safi la rangi ya samawati na nilivalishwa mashine maalumu ya kunisaidia kupumua huku skrini kubwa ya ukutani ikionesha mwenendo wa mapigo ya moyo wangu. Mwili wangu ulikuwa umezingirwa na nyaya mbalimbali zilizounganishwa na kompyuta kubwa.

Nikiwa nimetulia kama mfu nilianza kuyazungusha macho yangu na kuiona meza ndogo upande wangu wa kulia na juu ya ile meza kulikuwa na trei ndogo ya chuma iliyokuwa na vifaa muhimu vya tiba kama mikasi, bandeji, plasta, dawa ya kukaushia vidonda, mabomba ya sindano, glovu na kadhalika. Baadhi ya vile vifaa vilikuwa vimefunguliwa na kuachwa wazi kitendo kilichoashiria kuwa tayari vilikuwa vimekwisha tumika.

Kando kidogo ya kile kitanda kulikuwa na stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyokuwa imetundikiwa chupa ya damu, na mrija wake ulishuka hadi kwenye mkono wangu wa kulia na mwishoni kulikuwa na sindano iliyochomekwa kwenye mkono wangu na kupeleka damu kwenye mshipa wangu wa damu. Niliiangalia ile chupa ya damu kwa umakini na kushikwa na mshangao mkubwa nisijue nilifikaje pale hospitali!

Nilihisi maumivu mwilini, nilijaribu kukumbuka kilichonitokea lakini sikuweza kukumbuka chochote. Niliyatega vema masikio yangu kwa makini huku nikijaribu kutafakari kuwa pale nilikuwa wapi. Sikusikia sauti ya kitu chochote na utulivu ndani ya chumba kile ulikuwa ni wa hali ya juu kiasi kwamba nilianza tena kuingiwa na hofu. Nilipogeuza shingo yangu kutazama upande mwingine wa kile chumba macho yangu yalikutana na macho ya Mama yangu aliyekuwa amekaa kwenye kiti, mwisho wa kile kitanda.

Mama alikuwa amevaa vazi maalumu mfano wa joho, la rangi ya samawati, kofia maalumu na barakoa iliyofunika mdomo wake na pua. Alipogundua nimefungua macho yangu akaanza kuliita jina langu kwa sauti tulivu iliyobeba huzuni. “Jason!”

“Naam!” nilimuitikia Mama kwa sauti ya chini.

“Unajisikiaje mwanangu?” Mama aliniuliza kwa sauti tulivu iliyojaa huzuni. Macho yake yalikuwa yanalengwalengwa na machozi.

“Hata sijui… ila nahisi kizunguzungu na mwili umedhoofu sana,” nilimwambia kwa sauti tulivu huku nikimtazama kwa umakini.

“Mungu atakusaidia utapona… ulipoteza damu nyingi mwilini ila daktari amesema ukimaliza hii chupa ya tatu utapata ahueni,” Mama alisema huku akishusha pumzi, na muda huohuo akafanya ishara ya msalaba kasha akainua mikono yake juu kumshukuru Mungu.

Dah! kumbe nilikuwa nimeongezewa chupa tatu za damu! Nilihisi koo langu likinikauka ghafla, nikataka kunyanyuka lakini nikashindwa na hapo nikamwona Mama akiinuka haraka na kunirudisha chini taratibu. Kwa kufanya vile nikagundua kulikuwa na bandeji iliyofungwa kwenye kifua changu upande wa kushoto. Nikajaribu kujiuliza tena nini kilikuwa kimenikuta?

Mara kumbukumbu zikanikumbusha kuwa dakika za mwisho nilikuwa nimekaa kwenye sofa sebuleni kwangu kisha Jamila akaingia na kuninyooshea bastola. Picha ya Jamila akiwa amesima mbele yangu huku ameshika bastola ikanijia kichwani… hapana sikuwa peke yangu, bali tulikuwa wawili… ndiyo nilikuwa na Asia. Kisha… mmh… kuanzia hapo sikuelewa kitu kilichoendelea hadi nikawa pale na Mama akiwa pembeni yangu.

“Mama, nimefikaje hapa?”

“Ni hadithi ndefu kidogo mwanangu, ila kwa sasa pumzika, nitakusimulia kila kitu ukipata nafuu,” Mama alinijibu huku akiangalia pembeni kuyakwepa macho yangu. Nikagundua kuwa alikuwa anatokwa na machozi lakini akawahi kuyafuta ili nisigundue kama alikuwa akilia.

“Kwani nimeletwa hapa tangu lini?” nilimuuliza tena Mama huku nikimwangalia kwa umakini.

“Leo umetimiza siku ya sita tangu uletwe hapa,” Mama alinijibu huku akirudi kwenye kiti chake na kuketi.

Nilishangaa sana, inamaana nilipoteza fahamu kwa siku sita! Hata hivyo jambo hilo halikuwa la muhimu sana kwangu. Jambo lililokuwa la muhimu ni kwamba nilikuwa bado nipo hai. Nilipiga moyo konde na kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuniweka hai hadi wakati huo nikiamini alikuwa ametenda muujiza wake.

Nilitaka kumuuliza Mama swali lakini simu yake ikaanza kuita, akaitazama kwa muda kisha akaipokea. “Hello... Ndiyo ameamka.” Mama aliongea huku akinitupia jicho, kisha alionekana kusikiliza kwa makini na kubetua kichwa.

“Kwa kweli tumshukuru sana Mungu…” akasema na kusikiliza kidogo kisha akakata simu huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Baba yako alikuwa anaulizia hali yako, kesho atafika hapa,” Mama aliniambia kisha akanisogelea na kubusu katika paji la uso wangu.

Mara nikahisi mlango wa kile chumba ukifunguliwa, nilipotupa macho yangu nikamwona daktari akiingia, alikuwa mwanamume mrefu aliyekuwa na umri uliokaribia miaka hamsini, maji ya kunde na misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu. Alikuwa amevaa suruali ya kadeti, shati jeusi na juu yake alivaa koti refu jeupe la kidaktari, shingoni kwake alining’iniza kifaa cha kupimia mapigo ya moyo na alivaa miwani mikubwa iliyoyahifadhi macho yake makubwa. Mkononi alikuwa ameshika faili.

Alipoingia alimsalimia Mama kisha akanitupia jicho mara moja tu na kusimama kando ya kitanda changu karibu na ule mlingoti wa chupa ya damu, akaiangalia kwa makini ile chupa ya damu, aliangalia jinsi matone ya damu yalivyokuwa yakidondoka kutoka kwenye chupa na kuingia kwenye mrija uliopeleka damu kwenye mshipa wangu wa damu. Kisha alitazama saa yake ya mkononi na kushika kigurudumu kidogo kilichokuwa chini ya chupa kwenye mrija uliopeleka damu mwilini na kukirekebisha kidogo.

Aliporidhika akaisogelea ile skrini kubwa ya ukutani na kusoma mwenendo wa mapigo ya moyo wangu kisha akalifungua lile faili alilokuja nalo na kuandika maelezo fulani. Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kugeukia Mama.

“Naona sasa hali yake imeimarika, leo tutamhamishia chumba cha wagonjwa wa kawaida,” yule daktari alimwambia Mama huku akitabasamu. Kisha alinigeukia huku akiwa bado anatabasamu, akanivua ile mashine maalumu ya kunisaidia kupumua. “Pole sana.”

“Asante, dokta…” nilisema kwa sauti ya chini.

Daktari alibetua kichwa chake huku tabasamu likiendelea kuonekana usoni kisha alimtaka radhi Mama na kuanza kuondoka.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

112

“Dokta…” Mama alimuwahi yule daktari wakati akijiandaa kufungua mlango ili atoke, akainuka kumfuata kisha wakatoka nje ya kile chumba.

Alichukua muda mrefu sana na aliporudi mle ndani alikuwa mkimya sana, niligundua kuwa alikuwa akiyakwepa macho yangu. Sikutaka kumuuliza chochote kwa kuwa nilijua kuwa mambo mengine yote ningekuja kuyafahamu baadaye.

Baadaye jioni ya siku hiyo nilitolewa toka katika kile chumba maalumu cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu na kuhamishiwa katika chumba kingine cha wagonjwa wa kawaida, ilikuwa ni wodi maalumu ya VIP.

Siku hiyo watu wengi wakiwemo wafanyakazi wenzangu walifika kunitembelea pale hospitali na kunijulia hali huku wakinitakia uponaji wa haraka. Mmoja wa watu waliofika kuniona alikuwa Amanda ambaye muda wote alionekana mwenye majonzi. Amanda aliambatana na dada yake, Mariam na shemeji yake Swedi Mabushi. Pia Eddy na mkewe Emmy pia walifika kunijulia hali.

Ilipita wiki moja tangu nihamishiwe katika kile chumba cha wagonjwa wa kawaida na hali yangu iliendelea kuimarika siku hadi siku, na sasa nilifahamishwa kuwa baada ya shambulio lile nilikimbizwa hospitali na kufanyiwa upasuaji wa dharura wa kuondoa risasi kifuani. Upasuaji huo ulichukua saa sita hadi kukamilika kwani aliyenipiga risasi alilenga kuupiga moyo lakini kwa bahati nzuri risasi ilipita pembeni kidogo ya moyo na hivyo kujeruhi baadhi ya mshipa.

Katika kipindi chote cha wiki nilimwona Amanda akifika pale hospitali mara kwa mara na alikuwa akishinda pale na akisaidiana na Mama na shemeji Emmy kunihudumia. Amanda alikuwa amepungua kidogo na hakuonekana kuwa na furaha, sikujua kwa nini!

Hata hivyo, kuna jambo lilikuwa linaniumiza sana kichwa changu kwani tangu nilipopata nafuu na kuhamishiwa katika chumba kile nilikuwa natembelewa na watu wengi kila siku lakini katika watu wote walionitembelea kulikuwa na watu wawili muhimu sana ambao sikuwaona kabisa. Ni Rehema pamoja na Asia.

“Kwa muda mrefu sasa sijamwona Rehema, yuko wapi? Au hafahamu kama ninaumwa na nimelazwa hospitali?” siku moja nilimuuliza Mama lakini alionekana kulikwepa swali langu, na hata nilipomuuliza Eddy pia hakuwa tayari kunijibu.

Kitu kingine kilichonishangaza ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyekuwa tayari kunieleza chochote kuhusiana na Rehema au Asia, na wala sikujua habari zozote kumhusu Jamila. Sikujua kwa nini Rehema hakutaka kuja hospitali kuniona hata kama nilikuwa nimemuudhi. Niliamini kuwa Rehema hakuwa mtu wa kuweka kinyongo moyoni mwake. Sasa kwa nini hakutaka kufika hospitali kuniona?

Pia nilitamani sana kujua Asia alikuwa anaendeleaje kwa sababu kwa mujibu wa kumbukumbu zangu, Jamila alimpiga risasi Asia muda mfupi kabla hajanipiga mimi.

“Hivi Asia anaendeleaje? Yuko wapi? Na vipi kuhusu Jamila? Je, kakamatwa au alifanikiwa kutoroka?” nilijiuliza maswali ambayo sikuwa na majibu yake, na hakuna mtu yeyote aliyekuwa tayari kuyajibu maswali yangu.

“Ngoja nitamuuliza shemeji Emmy, lazima ataniambia” nilijiambia mwenyewe.

Hadi muda huo bado nilikuwa siamini kama Jamila angeweza kufanya kitendo cha kinyama kama kile. Niliamini kuwa ingenichukua muda mrefu sana kuisahau ile siku. Mpaka muda huo nilikuwa naona ulikuwa ni muujiza mkubwa ambao Mungu alikuwa amenitendea kuwa hai. Nilikuwa nimekiona kifo changu na nilihisi tayari nilikuwa nimekufa baada ya risasi kupenya mwilini mwangu. Hilo lilikuwa tukio baya kabisa kuwahi kunitokea.

Niliuma meno yangu kwa hasira na mara picha ya Asia akiwa amelala pembeni yangu huku damu nyingi zikimtoka ikanijia. Nikakumbuka nilimwona Jamila akiwa amechanganyikiwa sana akipiga magoti na kunikumbatia huku akilia kwa uchungu baada ya kunipiga risasi.

Machozi yalianza kunitoka nilipolikumbuka lile tukio la Jamila kutupiga risasi mimi na Asia, iliniumiza sana kugundua kuwa mtu ambaye hakuwa na hatia na nilitokea kumpenda alipigwa risasi kwa ajili yangu, ukweli hakustahili kabisa kuumizwa. Kama ni kisasi bora Jamila angenimaliza mimi na si kumpiga risasi Asia.

“Jamila… sitakusamehe kabisa kwa ulichonifanyia,” nilijiapiza moyoni kwangu huku nikijifuta machozi. Kisha nikakumbuka kuwa mlango wa sebuleni kwangu ulipigwa kumbo na watu watatu waliingia, wanaume wawili na mwanamke mmoja. “Rehema!” nilijikuta nikilitaja jina hilo kwa sauti ya kunong’ona.

“Oh Rehema, najua nimekukosea sana lakini kwa nini umeshindwa hata kuja kunijulia hali?” niliwaza na hapo machozi yakazidi kunitoka.

* * *

Saa 6:00 mchana…

WIKI ya pili ilikuwa imepita na hali yangu ilikuwa imeimarika sana, niliweza kufanya mazoezi madogo madogo ya kutembea, na hivyo nikaruhusiwa kutoka hospitali na kurudi nyumbani. Ndugu zangu kadhaa walikuwepo hospitali pamoja na Amanda wakati nikiruhusiwa kurejea nyumbani. Lakini Baba alikuwa amekwisha ondoka kurudi Tabora ili kuendelea na majukumu mengine.

Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na hadi wakati huo bado nilikuwa na maswali mengi kichwani kwangu ambayo sikuwa nimeyapatia majibu. Nilikuwa nikiwaangalia Mama na Eddy kwa macho yaliyojaribu kuuliza mambo mengi lakini walikuwa wakikwepa kujibu, na nilishangaa kuona kuwa wala hawakutaka mtu mwingine yeyote kuwa karibu nami kwa hofu angeweza kuniambia kitu ambacho hawakutaka nikifahamu. Muda wote Mama alinitaka nivute subira na muda si mrefu ningefahamu kila kitu, hasa baada ya kufika nyumbani.

Nilikuwa katika wakati mgumu sana wa kujiuliza maswali ambayo sikuwa na majibu yake huku Mama na Kaka Eddy wakiendelea kuyakwepa maswali yangu. Mimi, Mama, kaka Eddy na mkewe Emmy tuliingia kwenye gari la Eddy huku jamaa wengine wakiingia kwenye gari maalumu lililoletwa toka ofisini, na safari ya kurudi nyumbani ikaanza.

Niliamua kubaki kimya tu nikiwatazama Mama na Eddy kwa kuibia bila kusema lolote, wote walikuwa kimya kabisa hadi tulipofika nyumbani katika zile nyumba za mameneja wa Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi katika eneo la Mbulu. Mama na kaka yangu Eddy hawakutaka nirudi kule kwenye nyumba yangu ya Mwime kwa kuwa walidhani nyumba hiyo ingerudisha kumbukumbu zangu na kuniumiza zaidi.

Tulipofika nyumbani sikutaka kuendelea kuumiza kichwa changu kwa maswali yasiyo na majibu, sasa niliazimia kuufahamu ukweli, kwa njia yoyote ile hata kama walikuwa hawataki kuniambia. Ndipo nilipopewa taarifa zilizonifanya nihisi ubaridi mwepesi ukinitambaa mwilini mwangu na mwili wangu kuzizima kwa hofu huku nikiishiwa nguvu.

Ilikuwa ni taarifa mbaya sana ambayo sikuitarajia kabisa, taarifa kuhusiana na vifo vya Asia na Jamila. Eddy alinieleza ukweli kwamba Asia alikufa palepale katika tukio na Jamila alifanikiwa kutoroka lakini akajiua baadaye kwa sumu. Hii ilikuwa ni taarifa mbaya sana kwangu, nilihisi nilikuwa na hatia kubwa sana kwa vifo vya wasichana wale. Pia niliambiwa kuwa Rehema alikuwa amepatwa na kiharusi, aliangua na kupooza mwili baada ya kushuhudia tukio lile, na hadi muda huo hali yake ilikuwa mbaya sana.

Akili yangu iligoma kabisa kuipokea taarifa ile nikihisi huenda ile ilikuwa ndoto tu kama ndoto zingine na mara tu ningeamka kutoka usingizini na kukuta kila kitu kikiwa shwari kabisa. Hata hivyo, hisia zangu zilinitanabaisha kuwa ile haikuwa ndoto bali ni kitu halisi kilikuwa kimetokea. Iliniumiza kupita kiasi.

Sikujua kilichoendelea baada ya pale kwani niliishiwa nguvu, moyo wangu ukashikwa na mfadhaiko, mikono yangu ilikuwa inatetemeka na jasho jingi lilianza kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu. Macho yangu nayo yalianza kupoteza nguvu ya kuona na hatimaye shughuli mbalimbali za mwili wangu nazo nikazihisi kuwa zilikuwa mbioni kusitisha utendaji wake.

Baada ya hapo sikuweza kukumbuka nini kiliendelea hadi nilipokuja kurudiwa na fahamu nikajikuta nikiwa nimelala kitandani chumbani kwangu huku macho yangu yakiwa yamejawa na machozi, daktari alikuwa amesimama kando yangu akinipima mapigo ya moyo wangu. Mama na kaka Eddy walikuwa wamesimama kando wakiniangalia kwa huzuni.

Nilikuwa nimefungwa mashine ndogo ya kupimia shinikizo la damu na mapigo ya moyo kwenye mkono wangu wa kulia na yule daktari alikuwa akipampu kitufe fulani cheusi cha plastiki huku presha (pressure gauge) ikipanda juu. Niliyafumba macho yangu huku nikibana pumzi kutokana na ile mashine kubana kwenye mkono wangu na kusababisha maumivu kidogo.

Kisha yule daktari alianza kulegeza taratibu kifungo fulani kidogo kilichokuwa pembeni, mara nikasikika sauti ya ‘hisssiii’ huku pressure gauge ikishuka taratibu.

“Kwa sasa presha yake iko vizuri, ana 120 juu ya 70 na moyo wake unapiga mara 72 kwa dakika,” yule daktari aliwaambia Mama na kaka Eddy huku akifungasha vifaa vyake kisha akaniangalia na kugundua kuwa nilikuwa nimeamka.

“Pole sana kaka!” yule daktari aliniambia kwa sauti ya upole huku akiachia tabasamu la kirafiki. Kisha yule daktari alichukua sindano na kuijaza dawa fulani ambayo sikuijua kisha akanichoma na kuwataka jamaa zangu waniache nipumzike.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

113

Kaa Mbali na Binti Yangu.


Saa 5:30 asubuhi…

ILIKUWA imepita wiki moja tangu niliporejea pale nyumbani toka hospitali, ilikuwa siku ya Jumamosi, Mama na kaka Eddy walinipeleka hadi nyumbani kwa Bi Aisha, shangazi yake Asia, kisha tukaondoka na Bi Aisha hadi katika kaburi la Asia.

Asia alikuwa amezikwa kwenye makaburi ya familia, alizikwa kando ya kaburi la Mama yake. Sikuamini baada ya kusimama mbele ya kaburi jipya la Asia. Ni kweli Asia alikuwa amezikwa hapo. Haikuwa ndoto, ni kweli ilitokea kuwa Asia alikuwa amekufa baada ya kupigwa risasi na Jamila. Nilishindwa kujizuia, nikaanza kulia kwa uchungu, nililia sana siku hiyo.

Mama, Eddy na Bi Aisha walisimama kando wakiniangalia kwa majonzi, hakuna aliyethubutu kuninyamazisha kwa kuwa hata wao walishindwa kustahimili baada ya kuniona nikilia kwa uchungu, wao pia walianza kutokwa na machozi.

“Oh Asia… sikutegema kama yangetokea haya yaliyotokea. Sikufikiria kabisa kama kukutana kwetu safarini kungetufikisha hapa tulipofika na kusababisha mauti yako. Bado siamini kama umekufa. It’s hard to believe…” nilisema kwa uchungu huku machozi yakiendelea kunitoka na kutiririka katika mashavu yangu. Sura ya Asia akitabasamu mbele yangu ikanijia akili kwangu na kuniumiza sana.

“Nisamehe sana Asia, hukustahili kufanyiwa haya uliyofanyiwa,” nilisema kwa sauti ya kunong’ona nikiwa nimefumba macho yangu na kuuma meno kwa uchungu.

“Upumzike pema peponi Asia… kamwe sitakusahau mpenzi!” nilisema kwa huzuni kisha nikainamisha kichwa changu mbele ya kaburi lake kama ishara ya kutoa heshima zangu za mwisho. Sikuweza kuendelea kusimama pale, nikaamua kuondoka taratibu kwa huzuni, mikono yangu ikiwa nyuma. Mama, Eddy na Bi Aisha walinifuata taratibu nyuma bila kusema neno.

* * *



Saa 3:50 asubuhi…

Siku iliyofuata, siku ya Jumapili ilinikuta katika mji wa Masumbwe nikiwa nimesimama mbele ya kaburi jipya la Jamila nikilitazama kwa huzuni. Japo mwanzoni nilikuwa nimepata upinzani mkubwa sana kutoka kwa Selemani ambaye hakutaka kabisa kuniona nikifika pale nyumbani kwao, lakini kwa hekima ya Mama yake na shangazi yake, Bi Aisha, hatimaye nikaruhusiwa kuliona kaburi la Jamila. Siku hiyo pia nilikuwa nimeongozana na Mama na kaka Eddy ambao walikuwa bega kwa bega na mimi.

Muda wote machozi yalikuwa yakinitoka pasipo kukoma. Ni kweli Jamila alikuwa amejiua kwa sumu na kuzikwa kwenye makaburi ya familia. Mkononi nilikuwa nimeshika barua yake niliyopewa na shangazi yake. Barua hiyo alikuwa ameiandika kabla hajajiua akiomba nikabidhiwe endapo ningekuwa nimepona.

Barua ile ilikuwa imekutwa kando ya mwili wake chumbani kwake na ilikuwa na ujumbe ulionisikitisha sana na kunifanya nizidi kuhisi hatia ikinikaba kooni, nikaanza kupumua kwa shida.

Barua yenyewe iliandikwa hivi:

Mpenzi Jason,

Natumaini kuwa u mzima na umepata nafasi ya kuisoma barua yangu, nakuomba unisamehe sana kwa yote yaliyotokea na wala usisikitike kusikia kuwa nimekufa, ninastahili kufa baada ya yale niliyoyafanya. Niliumia sana baada ya kugundua kuwa sina tena nafasi moyoni mwako kitu ambacho nilishindwa kujizuia kudhibiti hasira yangu. Kumbuka maisha yangu yote niliyakabidhi kwako na sioni kama kuna sababu ya kuendelea kuishi hapa duniani bila ya kuwa na wewe, mwanamume ninayekupenda kuliko maelezo.

Nimeamua kujiua baada ya kuona furaha ya maisha yangu imebebwa na uhai wangu. Kaka yangu Selemani na Mama hawataki kabisa kusikia chochote kuhusiana na kuheshimu hisia zangu kwa kuniacha nijichagulie mwenyewe yule nimpendaye, hawataki kunisikiliza zaidi ya kuniwekea vikwazo kwa kunizungushia ukuta nishindwe kuvuka kuelekea katika daraja la mapenzi yenye furaha na utulivu katika moyo wangu!

Mwisho wa yote nimegundua njia ya kupita peke yangu ni njia ya kifo. Ninastahili kufa na ninaomba kifo changu kiwe kumbukumbu yako milele kuwa nilikupenda sana.

Ninayaandika haya huku chupa ya sumu ikiwa pembeni yangu, nakufa leo lakini nimewaomba ndugu zangu wasikuchukie kabisa kwani ni mimi niliyekuchagua, ni mimi nilikushawishi japo wewe hukutaka kugombana na kaka Selemani.

Buriani Jason, mpenzi wa moyo wangu…


_____

“Nimekusamehe Jamila… hata mimi nilikupenda sana ingawa sikuwa tayari kuona ukigombana na ndugu zako kwa kumwacha mwanamume waliyekuchagulia kwa ajili yangu. Ninaumia sana ninapokumbuka nyakati zile za furaha tulizokuwa nazo, ni Mungu pekee ndiye anayefahamu maumivu ninayoyapata wakati huu. Sifurahii kifo chako lakini ukweli utasimama pale pale kwamba ni mimi ninayestahili kukuomba msamaha kwa kuwa ndiye chanzo cha haya yote, na hili ni fundisho kwa wanaume wengine. Wewe umeimaliza safari yako lakini mimi bado nina safari ndefu na ngumu katika kuyarudisha mapenzi yangu kwa Rehema lakini niko tayari kwa lolote lile litakalotokea kwa sababu Rehema ndiye mwanamke pekee ambaye ninaamini amezaliwa kwa ajili yangu…” nilisema kwa sauti ya chini kisha nikainamisha kichwa changu mbele ya kaburi la Jamila kama ishara ya kutoa heshima zangu za mwisho.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

114

Saa 11:30 jioni…

Siku hiyo hiyo ya Jumapili nilifika nyumbani kwa Dk. Camilla Mpogoro, dada wa Rehema, nikiwa nimeongozana na Eddy na Swedi. Safari hii Mama hakutaka kuongozana nasi bali alibaki nyumbani. Tulimkuta Dk. Mpogoro na mumewe na walitupokea vizuri ingawa Dk. Camilla hakuonesha ule uchangamfu aliokuwa nao siku zote, na baada ya kuniona alishindwa kujizuia na kutokwa na machozi.

Ni hapo nilipopata taarifa zilizozidi kuninyong’onyesha kabisa, nilitamani nami ninywe sumu nijiue kwani sikuona kama nilistahili kuendelea kuvuta pumzi huku nikiwa mwenye hatia.

Taarifa nilizopata pale ni kwamba hali ya Rehema ilikuwa mbaya sana kwani alikuwa amepooza kabisa na mwili wake haukuweza hata kutikisika, macho yake yalifumba na hakuweza hata kufumbua jicho, na ilibidi baba yao mzee Benard Mpogoro aje kwa ndege ndogo ya kukodi na kumchukua, akapelekwa Muhimbili ambako haikusaidia na hivyo akapelekwa nchini India kwa matibabu na huduma zaidi.

Nilishindwa kujizuia kutokana na taarifa ile, nikajikuta nikitokwa na machozi muda wote. Sikupata neno ambalo lingeweza kuelezea uchungu niliokuwa nao kwa wakati ule. Ilikuwa ni kama filamu ya kusikitisha na ilikuwa vigumu sana kuamini kilichotokea.

Baada ya taarifa ile Dk. Mpogoro alinipa barua ambayo ilikuwa imeandikwa na baba yao akiagiza kwamba nipewe. Niliipokea huku nikiitazama ile bahasha kwa wasiwasi, sikutaka kuifungua pale. Na baada ya maongezi mafupi tuliaga na kuondoka, na tulipofika tu nyumbani niliharakisha nikaifungua ile barua, iliandikwa:

Ndugu Jason,

Pamoja na yote yaliyotokea, nakuombea kwa Mungu upone haraka na uendelee na majukumu yako. Nakuomba samahani kwa kuwa nimeshindwa kuja hospitali kukujulia hali kwa sababu nimekuta hali ya binti yangu Rehema ni mbaya sana, amepooza mwili baada ya kushuhudia kile kilichotokea nyumbani kwako, na inaonesha wazi kuna mambo yaliyokuwa yanaendelea chini kwa chini yanayonifanya nisifahamu lengo lako kwa binti yangu ni nini hasa!

Japokuwa hatujui mlikutana vipi na wapi na ni kwa kiasi gani mnapendana lakini kuna maamuzi ambayo sisi wazazi wake tumeamua kuyachukua, kwanza tumeamua kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi. Jambo la pili ambalo najua linaweza kuwa gumu kwako lakini hatunabudi kulifanya, nakuomba achana kabisa na binti yangu Rehema. Tumegundua kwamba umekuwa ukimuumiza sana kihisia na hutaki kubadilika, kumbuka wewe ndiye chanzo cha binti yetu kupatwa na matatizo haya.

Sitaki tena kusikia masuala ya mahusiano kati yako na Rehema na kama unataka kuendelea na uhusiano na binti yangu itabidi usubiri kwanza nife lakini kama bado nipo hai sitaruhusu kamwe. Naomba usinielewe vibaya Jason, nakupenda kwa sababu wewe ni kijana mchapakazi, jasiri, msomi makini na mwenye nidhamu lakini hufai kuwa na binti yangu.

Najua hili ni jambo ambalo hukulitegemea na linaweza kukuumiza sana lakini kuna nyakati katika maisha lazima tufanye maamuzi magumu. Sisi wazazi tumefanya maamuzi hayo kwa faida yako na ya binti yetu.

Nasisitiza tena: kaa mbali na binti yangu.

Meja Jenerali Benard Mpogolo…


_____

Nilipomaliza kuisoma barua hiyo nilihisi kama mwili wangu ulikuwa umepigwa na shoti kali ya umeme. Nilihisi ubaridi mkali ukinitambaa mwilini na mwili ukifa ganzi. Barua ile ilikuwa na maneno mazito sana na ambayo katu sikutegemea kuyasikia katika wakati ule ambao nilihitaji sana kupata faraja. Nilihisi kuadhibiwa na dunia.

Kulikuwa na maumivu makali sana ndani ya moyo wangu, maumivu ambayo hayakuelezeka. Ilikuwa ni zaidi ya maumivu. Niliwaza sana kuhusiana na mustakabali mzima wa maisha yangu bila Rehema; niliwaza nilikotoka, niliko na kule nilikokuwa nikienda, nikajiona ni mtu mwenye mkosi mkubwa au laana. Nilijikuta nikilia sana. Eddy na Swedi walijitahidi sana kuniliwaza.

“Eddy, najua nimekosea sana lakini sistahili kuadhibiwa na dunia kiasi hiki! Kwa nini?” nilisema kwa uchungu huku nikitokwa na machozi.

“Jason, jikaze wewe ni mwanamume… kumbuka kila jambo hutokea kwa sababu maalumu, hivyo mtegemee Mungu pekee, yeye atakushindia. Be strong my brother,” Eddy aliniambia huku akinipiga piga taratibu mgongoni.

I’m hurt, brother. Kwa nini yule mzee anifanyie hivi?” nilisema kwa uchungu mkubwa.

Calm down. Huna sababu ya kuumia sana, kumbuka akipangacho Mungu binadamu hawezi kukipangua… kama Rehema ndiye mwanamke uliyeandikiwa kuwa naye basi siku moja utakuwa naye. Kumbuka mlikotoka, kumbuka kakuvumilia kwa mengi! Mapenzi yana nguvu kuliko kitu chochote kile, mapenzi yana uwezo hata wa kuusambaratisha mlima. Kama ni kweli wewe na Rehema mnapendana siku moja mtakuwa pamoja, niamini ndugu yangu,” Eddy aliniambia na kauli yake ikaungwa mkono na Swedi.

Sikwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kukubaliana na matokeo, kwani hata kama ningefanya nini tayari ilikwisha tokea, nisingeweza kuurudisha wakati nyuma. Sasa nilikuwa nimekosa mwana na maji ya moto. Asia na Jamila walikuwa wamekufa, na sasa Rehema alikuwa kitandani akipigania uhai wake huku baba yake akinitaka nikae mbali na binti yake!

Sikuwa na mtu wa kumtupia lawama kwani yote hayo yalisababishwa na tamaa yangu, tamaa ya kutamani kila kilichofichwa ndani ya andawea ya kila msichana mrembo aliyepita mbele yangu.

Nilihisi kuchanganyikiwa sana nikiwaza kuwa kila sehemu ambako ningepita macho ya watu yangekuwa yakinitazama kwa kunisuta; wapo ambao wangekuwa na hasira juu yangu, wapo ambao wangenitazama kwa dharau na baadhi wangenitazama kwa huzuni. Kwa kweli sikujua nifanye nini!

Sasa nilianza kutamani ardhi ipasuke ili nijifiche ndani yake kukwepa macho ya jamii. Nikajikuta nikipata wazo la kunywa sumu ili nami niondoke hapa duniani.

Huu ni mwisho wa Msimu wa Pili kwenye mfululizo wa Harakati za Jason Sizya. Usikose Msimu wa Tatu hapa hapa katika mkasa uitwao “Fungate”.
 
View attachment 2205708
114

Saa 11:30 jioni…

Siku hiyo hiyo ya Jumapili nilifika nyumbani kwa Dk. Camilla Mpogoro, dada wa Rehema, nikiwa nimeongozana na Eddy na Swedi. Safari hii Mama hakutaka kuongozana nasi bali alibaki nyumbani. Tulimkuta Dk. Mpogoro na mumewe na walitupokea vizuri ingawa Dk. Camilla hakuonesha ule uchangamfu aliokuwa nao siku zote, na baada ya kuniona alishindwa kujizuia na kutokwa na machozi.

Ni hapo nilipopata taarifa zilizozidi kuninyong’onyesha kabisa, nilitamani nami ninywe sumu nijiue kwani sikuona kama nilistahili kuendelea kuvuta pumzi huku nikiwa mwenye hatia.

Taarifa nilizopata pale ni kwamba hali ya Rehema ilikuwa mbaya sana kwani alikuwa amepooza kabisa na mwili wake haukuweza hata kutikisika, macho yake yalifumba na hakuweza hata kufumbua jicho, na ilibidi baba yao mzee Benard Mpogoro aje kwa ndege ndogo ya kukodi na kumchukua, akapelekwa Muhimbili ambako haikusaidia na hivyo akapelekwa nchini India kwa matibabu na huduma zaidi.

Nilishindwa kujizuia kutokana na taarifa ile, nikajikuta nikitokwa na machozi muda wote. Sikupata neno ambalo lingeweza kuelezea uchungu niliokuwa nao kwa wakati ule. Ilikuwa ni kama filamu ya kusikitisha na ilikuwa vigumu sana kuamini kilichotokea.

Baada ya taarifa ile Dk. Mpogoro alinipa barua ambayo ilikuwa imeandikwa na baba yao akiagiza kwamba nipewe. Niliipokea huku nikiitazama ile bahasha kwa wasiwasi, sikutaka kuifungua pale. Na baada ya maongezi mafupi tuliaga na kuondoka, na tulipofika tu nyumbani niliharakisha nikaifungua ile barua, iliandikwa:

Ndugu Jason,

Pamoja na yote yaliyotokea, nakuombea kwa Mungu upone haraka na uendelee na majukumu yako. Nakuomba samahani kwa kuwa nimeshindwa kuja hospitali kukujulia hali kwa sababu nimekuta hali ya binti yangu Rehema ni mbaya sana, amepooza mwili baada ya kushuhudia kile kilichotokea nyumbani kwako, na inaonesha wazi kuna mambo yaliyokuwa yanaendelea chini kwa chini yanayonifanya nisifahamu lengo lako kwa binti yangu ni nini hasa!

Japokuwa hatujui mlikutana vipi na wapi na ni kwa kiasi gani mnapendana lakini kuna maamuzi ambayo sisi wazazi wake tumeamua kuyachukua, kwanza tumeamua kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi. Jambo la pili ambalo najua linaweza kuwa gumu kwako lakini hatunabudi kulifanya, nakuomba achana kabisa na binti yangu Rehema. Tumegundua kwamba umekuwa ukimuumiza sana kihisia na hutaki kubadilika, kumbuka wewe ndiye chanzo cha binti yetu kupatwa na matatizo haya.

Sitaki tena kusikia masuala ya mahusiano kati yako na Rehema na kama unataka kuendelea na uhusiano na binti yangu itabidi usubiri kwanza nife lakini kama bado nipo hai sitaruhusu kamwe. Naomba usinielewe vibaya Jason, nakupenda kwa sababu wewe ni kijana mchapakazi, jasiri, msomi makini na mwenye nidhamu lakini hufai kuwa na binti yangu.

Najua hili ni jambo ambalo hukulitegemea na linaweza kukuumiza sana lakini kuna nyakati katika maisha lazima tufanye maamuzi magumu. Sisi wazazi tumefanya maamuzi hayo kwa faida yako na ya binti yetu.

Nasisitiza tena: kaa mbali na binti yangu.

Meja Jenerali Benard Mpogolo…


_____

Nilipomaliza kuisoma barua hiyo nilihisi kama mwili wangu ulikuwa umepigwa na shoti kali ya umeme. Nilihisi ubaridi mkali ukinitambaa mwilini na mwili ukifa ganzi. Barua ile ilikuwa na maneno mazito sana na ambayo katu sikutegemea kuyasikia katika wakati ule ambao nilihitaji sana kupata faraja. Nilihisi kuadhibiwa na dunia.

Kulikuwa na maumivu makali sana ndani ya moyo wangu, maumivu ambayo hayakuelezeka. Ilikuwa ni zaidi ya maumivu. Niliwaza sana kuhusiana na mustakabali mzima wa maisha yangu bila Rehema; niliwaza nilikotoka, niliko na kule nilikokuwa nikienda, nikajiona ni mtu mwenye mkosi mkubwa au laana. Nilijikuta nikilia sana. Eddy na Swedi walijitahidi sana kuniliwaza.

“Eddy, najua nimekosea sana lakini sistahili kuadhibiwa na dunia kiasi hiki! Kwa nini?” nilisema kwa uchungu huku nikitokwa na machozi.

“Jason, jikaze wewe ni mwanamume… kumbuka kila jambo hutokea kwa sababu maalumu, hivyo mtegemee Mungu pekee, yeye atakushindia. Be strong my brother,” Eddy aliniambia huku akinipiga piga taratibu mgongoni.

I’m hurt, brother. Kwa nini yule mzee anifanyie hivi?” nilisema kwa uchungu mkubwa.

Calm down. Huna sababu ya kuumia sana, kumbuka akipangacho Mungu binadamu hawezi kukipangua… kama Rehema ndiye mwanamke uliyeandikiwa kuwa naye basi siku moja utakuwa naye. Kumbuka mlikotoka, kumbuka kakuvumilia kwa mengi! Mapenzi yana nguvu kuliko kitu chochote kile, mapenzi yana uwezo hata wa kuusambaratisha mlima. Kama ni kweli wewe na Rehema mnapendana siku moja mtakuwa pamoja, niamini ndugu yangu,” Eddy aliniambia na kauli yake ikaungwa mkono na Swedi.

Sikwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kukubaliana na matokeo, kwani hata kama ningefanya nini tayari ilikwisha tokea, nisingeweza kuurudisha wakati nyuma. Sasa nilikuwa nimekosa mwana na maji ya moto. Asia na Jamila walikuwa wamekufa, na sasa Rehema alikuwa kitandani akipigania uhai wake huku baba yake akinitaka nikae mbali na binti yake!

Sikuwa na mtu wa kumtupia lawama kwani yote hayo yalisababishwa na tamaa yangu, tamaa ya kutamani kila kilichofichwa ndani ya andawea ya kila msichana mrembo aliyepita mbele yangu.

Nilihisi kuchanganyikiwa sana nikiwaza kuwa kila sehemu ambako ningepita macho ya watu yangekuwa yakinitazama kwa kunisuta; wapo ambao wangekuwa na hasira juu yangu, wapo ambao wangenitazama kwa dharau na baadhi wangenitazama kwa huzuni. Kwa kweli sikujua nifanye nini!

Sasa nilianza kutamani ardhi ipasuke ili nijifiche ndani yake kukwepa macho ya jamii. Nikajikuta nikipata wazo la kunywa sumu ili nami niondoke hapa duniani.

Huu ni mwisho wa Msimu wa Pili kwenye mfululizo wa Harakati za Jason Sizya. Usikose Msimu wa Tatu hapa hapa katika mkasa uitwao “Fungate”.
Pamoja sana aseeeee daaaaaaaaaaah
 
Stori nzuri ila kusifia mavitu ndio inaboa.... screen kubwa mara handsome...nikisoma stori ya mhusika huwa natengeneza muonekano wake mimi mwenyewe bila kusaidiwa na muandishi.....yote kwa yote tunashukuru kwa stori.
 
Stori nzuri ila kusifia mavitu ndio inaboa.... screen kubwa mara handsome...nikisoma stori ya mhusika huwa natengeneza muonekano wake mimi mwenyewe bila kusaidiwa na muandishi.....yote kwa yote tunashukuru kwa stori.
Ndugu mwandishi bishop,nakukubali sana brother,tunasoma bure bila kulipia,watu kama hawa wasikukatishe tamaa,nimesoma simulizi zako zote brother,hii ndio staili yako,na ninzuri,shukran sana brother
 
Back
Top Bottom