Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

fungate.jpeg

123

Katika sofa jingine la watu wawili nilimwona mjomba mkubwa, Japheti Ngelela aliyekuwa anakaa Kiloleni Tabora akiwa ameketi peke yake na alikuwa kimya akionekana kuzama kwenye tafakari. Mjomba Japheti alikuwa mwanamume wa makamo, mrefu na maji ya kunde, alikuwa na ndevu nyingi zilizokizunguka kidevu chake na umbo kakamavu la kimichezo lililofanana na maumbo ya wachezaji wa ligi ya mpira wa kikapu.

Alikuwa amevaa shati zuri jeupe lenye mistari midogo ya rangi ya bluu, la mikono mirefu, brandi ya Maria Santangelo kutoka nchini Italia, tai nyekundu shingoni na suruali nyeusi.

Na kwenye sofa jingine dogo nilimwona mjomba mwingine, Mchungaji Edwin Ngelela aliyekuwa anaishi Jijini Dodoma, alikuwa ameketi kwa utulivu na mkononi alishika Biblia. Mchungaji Ngelela alikuwa amevaa suti ghali ya kijivu ya single button brandi ya Piacenza kutoka nchini Italia na shingoni alivaa kola ya kichungaji. Pia alikuwa na miwani ya macho.

Nilibaki nimewakodolea macho nikiwa nimetahayari sana. Wote walikuwa wananitazama kwa umakini kisha macho yao yaliutazama mzinga wa Konyagi nilioshika mkononi. Nilihisi kijasho chembamba kikinitoka mwilini. Nikafungua mdomo wangu kutaka kusema neno lakini maneno hayakutoka, mdomo wangu ulinidondoka kwa hofu utadhani nilikuwa nimezingirwa na wanamgambo hatari wa kundi la kigaidi la al-Shabab waliokuwa tayari kujilipua wakati wowote.

“Karibuni mezani…” niliisikia sauti ya Amanda, na nilipogeuza shingo yangu kuangalia kule ambako sauti ilikuwa inatokea nikamwona Amanda akitokea kwenye chumba cha chakula (dining room) na kuja pale sebuleni huku akiwa amepambwa na tabasamu usoni kwake. Alikuwa amevaa dela na juu yake akivaa aproni akionekana kuwa alikuwa ametoka kuandaa chakula.

“Mama, ulisema nikuandalie…” alitaka kusema lakini akasita na kusimama ghafla baada ya kuniona. Tukabaki tumetazamana kwa kitambo.

Watu wote pale sebuleni waligeuka kumtazama Amanda kisha wakayarudisha macho yao kwangu. Niliona kama vile macho yao yaliniangalia kwa kunisuta.

Nikavuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kuzishusha taratibu huku nikijipa ujasiri kisha nikaanza kupiga hatua taratibu hadi kwenye sofa alilokalia mjomba Japheti, nikaketi na kuwasalimia watu wote kwa unyenyekevu huku nikilazimisha tabasamu. Bila hiyana wote waliitikia salamu yangu lakini hawakuacha kunitazama kwa umakini.

“Jason!” mjomba Japheti aliniita kwa sauti tulivu ya chini huku akinitazama usoni kwa umakini.

“Naam!” niliitikia kilevi huku nikijitahidi kuifanya sauti yangu iwe tulivu.

“Natambua kwamba mapito unayopita ni magumu sana, lakini aina hii ya maisha uliyoamua kuishi si sawa kabisa, mjomba,” mjomba Japheti aliniambia kwa sauti tulivu huku akininyang’anya chupa ya Konyagi niliyoshika mkononi, kisha akaitazama kwa umakini na kuiweka kando.

“Umekula?” mjomba Japheti aliniuliza huku akiendelea kunikazia macho usoni kwa umakini.

“Hapana,” nilijibu huku nikiangalia chini kuyakwepa macho yake.

“Twende mezani tukale,” mjomba Japheti aliniambia huku akinishika mkono kuninyanyua.

“Hapana uncle, nipo poa,” nilimjibu huku nikikataa kuinuka.

No, unatakiwa kula, mjomba,” mjomba Japheti alizungumza huku akigeuka kumtazama Amanda ambaye alikuwa bado amesimama akinitazama kwa wasiwasi.

“Itabidi nikajimwagie kwanza maji,” niliwahi kumwambia mjomba Japheti kabla hajasema chochote huku nikiinuka ili nielekee chumbani kwangu. Muda huo kichwa changu kilikuwa na mawenge kutokana na Konyagi nilizokunywa, na nilipoanza kuondoka Mama akaniwahi.

“Jason, tukimaliza kula nitahitaji kuzungumza na wewe,” Mama alisema huku akiinuka pale kwenye sofa alipokuwa ameketi.

“Usiku huu!” nilimuuliza Mama kwa mshangao huku nikiitazama saa yangu ya mkononi.

“Ndiyo, usiku huu huu maana raha ya mchuzi uunywe ukiwa bado wa moto,” Mama alisema kwa sauti ya msisitizo.

Nilitaka kusema neno lakini nikasita na kuwatazama wajomba kwa wasiwasi kidogo kabla macho yangu sijayahamishia kwa Amanda ambaye muda wote alikuwa mtulivu mno akiwa amesimama kwa unyenyekevu.

“Sawa, Mama!” nilisema huku nikishusha pumzi kwani sikuwa na namna nyingine yoyote ya kufanya isipokuwa kukubali.

Niliingia chumbani kwangu na kuvua shati langu kisha nikalitupa kitandani, nikavua viatu na kuviweka kwenye stendi maalumu ya viatu, halafu nikavua soksi na kuzitupia kitandani na mwisho nikavua suruali na kuitupia kitandani. Nilipomaliza nikachukua shati langu nililovua na kuanza kupekua kwenye mifuko ya shati, nikatoa vimbaka vitatu na nusu vya kuchokonolea meno na kuvitupa ndani ya kapu la taka lililokuwa mle chumbani.

Kisha nilichukua suruali yangu na kuanza kukagua mifuko ya mbele kwanza kwa kutoa nje vitambaa vyake, nikatoa kitambaa laini cha kujifutia jasho na simu yangu ya mkononi na kuviweka kitandani, kisha nilitomasa mfuko wa nyuma, nikatoa pochi na kuiweka kitandani.

Kisha nikachukua taulo na kuingia bafuni ambako nilifungua bomba na kujimwagia maji, baada ya muda fulani nilitoka nikiwa nimechangamka. Sasa nilianza kujisikia mwepesi kidogo na akili yangu ilichangamka. Dakika ishirini baadaye nilitoka nikiwa nimevaa suruali nyepesi ya mazoezi na fulana na kuungana na watu wengine pale sebuleni. Niliwakuta wakiwa na vimbaka wakiondoa masalio ya chakula kwenye meno.

“Nadhani sasa una muda, naomba tukazungumzie ofisini kwako,” Mama aliniambia huku akiinuka toka kwenye sofa.

Kisha aligeuza shingo yake kumtazama Amanda aliyekuwa anatoka jikoni kuja pale sebuleni, mkononi alikuwa amebeba trei kubwa lililokuwa na sahani kadhaa zenye matunda aina ya ndizi, vipande vya nanasi, embe na vipande vya matikiti maji vilivyokoza wekundu.

“Mama, naomba mwandalie mwenzako chakula halafu ulete kule ofisini kwake,” Mama alimwambia Amanda.

“Sawa mama,” Amanda aliitikia kwa unyenyekevu huku akilitua lile teri la matunda juu ya meza ya kioo pale sebuleni.

Sikuwa na namna nyingine ya kufanya nikaondoka huku Mama akinifuata nyuma, tukaingia kwenye ofisi yangu binafsi ambayo pia niliitumia kama maktaba. Ilikuwa ofisi nzuri yenye hadhi ikiwa na samani na vifaa vyote vya kiofisi. Tuliketi kwenye viti vya kiofisi vya ngozi halisi na hapo Mama akanikabili.

“Jason mwanangu…” Mama alisema mara baada ya kuketi huku akiitazama kwa umakini picha kubwa ya Rehema iliyotundikwa ukutani. Nami nikaitupia jicho mara moja kisha nikayarudisha macho yangu kwa Mama nikisubiri kusikia alichotaka kuniambia.

“Jason!” Mama aliniita huku akinitazama kwa umakini.

“Ndiyo, Mama,” nilisema kwa sauti iliyojaa wasiwasi.

“Hivi umejitazama kwenye kioo kuona kama kweli wewe ndiye Jason? Umeiona taswira yako?” Mama aliniuliza huku akinitazama kwa huzuni.

Sikuweza kujibu maswali yake, nilibaki kimya nikiwa nimeinamisha uso wangu na macho yangu yakitazama sakafuni. Hata hivyo nilipeleka mkono wangu wa kulia na kuzishika ndevu huku nikiwa kama mtu asiyeamini kwa kile nilichokigusa.

“Ulipozaliwa tu nilikupa jina la baba yangu nikiwa na matumaini makubwa sana juu yako, kwamba utakuwa jasiri kama babu yako. Sijajua kwa nini unachanganyikiwa kwa sababu ya mapenzi? Kwa nini unaihangaisha akili yako kufikiri juu ya mtu ambaye hujui kama bado umo akilini mwake!” Mama alilalamika kwa sauti iliyojaa uchungu uliodhihirishwa kwa machozi yaliyoanza kumtoka.

Itaendelea...
 
fungate.jpeg

124

Yalikuwa maneno mazito, lakini nilihisi akili yangu ikishindwa kuamua. Mama alipangusa machozi mashavuni mwake huku maneno mazito yakiendelea kumtoka, “Siku uliyozaliwa nilifurahi sana, nilijua nimempata mbadala wa baba yangu, kumbe nilikuwa najidanganya kwa kuweka matumaini yangu kwa mtumwa wa mapenzi! Sikutegemea kuona mapenzi yanakuchanganya, Jason… kwani wanawake wapo wangapi dunia hii mpaka uchanganyikiwe na Rehema?”

Nilishindwa kumjibu Mama, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kuangalia chini. Kikafuatia kitambo fulani cha ukimya.

“Halafu… una mpango gani na Amanda?” Mama aliniuliza na kuvunja ukimya.

“Kivipi Mama?” nilimuuliza huku mapigo ya moyo wangu yakianza kwenda kasi.

“Huoni kama ana sifa zote za kuwa mke? Mtoto wa watu anakuhangaikia sana ili uwe sawa na kupata furaha,” Mama alisema kwa huzuni huku akinitazama kwa tuo.

“Mama, kusema kweli kwa sasa sina mpango wa kuwa na mwanamke yeyote, bado namsikilizia Rehema,” nilijibu huku nikijitahidi kuyakwepa macho ya Mama kwa kutazama kando.

“Kwa nini? Unadhani utaishi maisha haya ya uhuni hadi lini?” Mama aliniuliza huku akinitazama kwa macho yasiyoamini kile alichokisikia toka kinywani mwangu.

“Hata sijui niseme nini lakini hadi sasa Rehema bado hajatoka moyoni mwangu, ninajitahidi kumtoa lakini nimeshindwa na hivyo akili yangu haijafikiria kabisa suala la kuoa mwanamke mwingine.”

“Rehema! Rehema!” Mama alisema kwa sauti tulivu. “Sina tatizo na Rehema, lakini najua kuwa baba yake hataki hata kukusikia achilia mbali kukuona! Hebu fikiria utaishi vipi na mwanamke ambaye wazazi wake hawakutaki na wameapa kutoruhusu umuoe binti yao labda mpaka wawe wamekufa?”

Nilishindwa kusema chochote kwa sababu alichokiongea Mama kilikuwa kinaniumiza sana na kuufanya moyo wangu kuwaka moto, nikabaki kimya nikiwa nimeangalia chini.

“Mbona Amanda ana sifa zote za kuwa mke na isitoshe ni mwanamke mvumilivu sana!” Mama alizungumza kwa msisitizo huku akinikazia macho yake.

“Mama…” nilitaka kusema lakini Mama akanikatisha.

“Hakuna cha Mama… naomba uyafikirie maneno yangu. Sipendi kuendelea kusikia habari za ajabu ajabu toka kwako. Tunashindwa hata kufanya shughuli zetu kisa unataka kujiua kwa sabau ya Rehema! Kwani tatizo lako nini mwanangu, au umerogwa?” Mama alizungumza kwa uchungu huku machozi yakimlengalenga.

“Mama, naelewa unachokisema lakini nahitaji muda wa kumsahamu Rehema na kuyasahau yote yaliyotokea kwenye maisha yangu kabla sijamfikiria mwanamke mwingine. Hadi sasa Rehema ndiye mwanamke anayeishi moyoni mwangu,” nilizungumza kwa sauti tulivu ili kumshawishi Mama anielewe.

Nilitamani kumwambia Mama kuwa Rehema ndiye aliyekuwa mwanamke pekee aliyeugusa moyo wangu kati ya wanawake wote niliowahi kukutana nao na ndiye aliyenionesha mapenzi ambayo sijawahi kuyapata kwa wanawake wengine, na kwamba sikuwahi kufurahia mapenzi kwa namna Rehema alivyokuwa akinionesha. Lakini sikuthubutu kutamka maneno hayo mbele ya Mama.

Mama alitaka kusema neno lakini nikamwona akisita baada ya kusikia mlango wa ofisi yangu ukigongwa taratibu kisha ukafunguliwa. Na hapo Amanda akaingia taratibu akiwa amebeba trei kubwa lililosheheni mapochopocho. Kulikuwa na wali, samaki wa kupakwa, bakuli la maharagwe, saladi, sahani ya matunda, jagi la kunawia, jagi la maji baridi ya kunywa na bilauri.

Aliviweka mezani na kuchukua jagi la maji ya kunawa ili kuninawisha mikono. Nilitaka kukataa lakini nilipomwona Mama akinitazama usoni kwa namna ya kunisisitiza nisimuumize Amanda ikabidi nikubali. Amanda alininawisha mikono huku akinitazama usoni kwa kuvizia vizia.

Kisha alifumba macho akakiombea chakula na alipomaliza alinipakulia wali kidogo kwenye sahani, akaniwekea mchuzi wa samaki na kumwagia juu yake maharage kwa wingi, kisha aliweka saladi nyingi na kunisogezea huku akinikaribisha kwa unyenyekevu. Wakati hayo yakifanyika Mama alikuwa ananitazama usoni kwa umakini sana, alionekana kuwa na donge moyoni.

Amanda alipotaka kuondoka Mama alimfanyia ishara ya kuketi, Amanda akaketi kwenye kiti kwa utulivu huku akinitupia jicho la wizi wakati nikianza kula taratibu, kwa kujilazimisha. Ukimya mzito ulitawala ndani ya ofisi, hakuna aliyeongea na kilichokuwa kikisikika muda huo ni mgongano wa kijiko na vyombo mezani, nilikuwa nimepoa sana kama niliyeshikwa na baridi kali baada ya kunyeshewa na mvua ya barafu.

“Binti yangu, subiri mwenzio akimaliza kula utaondoa vyombo, mimi nipo sebuleni,” Mama alimwambia Amanda huku akiinuka na kutoka akituacha peke yetu mle ofisini.

Nilijua kuwa huo ulikuwa ujanja wa Mama kuniacha na Amanda akitumai kuwa kitendo cha kuwa karibu na mwanamke huyo huenda kingesaidia kunirudisha katika hali ya kawaida. Niliendelea kula taratibu huku kichwa changu kikiwa kimejawa na mawazo, hata hivyo, kama kawaida ya mapishi ya Amanda kile chakula kilikuwa chakula kitamu sana.

“Mbona kama hukifurahii chakula?” Amanda aliniuliza kwa wasiwasi huku akiniangalia usoni na kuuvunja ukimya uliotawala mle ndani.

“Nakifurahia… ni chakula kitamu sana,” nilimwambia Amanda huku nikiachia tabasamu. Amanda akatabasamu pia huku akishusha pumzi za ahueni.

“Kwani wazee wamekuja saa ngapi?” nilimuuliza Amanda.

Amanda alifikiria kidogo kama ambaye hakuwa ameelewa mantiki ya swali langu kisha kama aliyekumbuka kitu akashusha pumzi. “Ilikuwa saa tisa alasiri hivi maana Mama alinipigia simu muda huo akiniomba nije kwani tayari yupo hapa nyumbani.”

“Kwani huwa mna mawasiliano ya karibu?” nilimuuliza Amanda huku nikimtulizia macho.

“Mawasiliano na nani?” Amanda aliuliza akionekana kutoelewa kusudi la swali langu.

“Na Mama yangu! Huwa mnawasiliana?” niliongea kwa sauti tulivu nikiwa bado nimemtulizia macho yangu usoni kwake.

Amanda alitaka kusema neno lakini akasita kidogo na kuangalia chini kuyakwepa macho yangu, alionekana kama alikuwa na jambo ila hakupenda kuniambia. Nililigundua hilo lakini sikutaka kumuuliza zaidi.

“Kuna chochote ulichoongea na Mama juu yangu?” nilimuuliza kwa namna nyingine huku nikiendelea kumkazia macho.

“Kama nini?” Amanda aliniuliza huku akinua uso wake kunitazama usoni kwa umakini.

“Chochote tu… au Mama hajakwambia chochote kuhusu mimi?” niliuliza tena huku nikiendelea kumkazia macho Amanda.

Amanda alikaa kimya tena akionekana kufikiria kisha akatingisha kichwa chake taratibu huku akibetua midomo. Muda huo huo mlango wa ofisini kwangu ukagongwa taratibu.

“Pita!” nilisema kwa sauti tulivu.

Mlango ulifunguliwa na Eddy akachungulia na kutuona, aliachia tabasamu na kuingia ndani kisha alisimama huku akituangalia kwa tabasamu na kumfanya Amanda ainamishe sura yake kutazama chini.

* * *

Itaendelea...
 
fungate.jpeg

125

Wewe ni Shupavu


Saa 4:15 usiku…

Sebule ilikuwa imetulia, kila mmoja wetu alikuwa kimya akitafakari. Ni sauti ya chini kidogo ya muziki laini wa kuabudu uliokuwa unarushwa kutoka kwenye redio kubwa pale sebuleni ndiyo iliyosikika.

Pale sebuleni tulikuwa tumebakia watu wanne; mimi, Mama, mjomba Japheti na Mchungaji Ngelela. Hii ilikuwa baada ya Eddy, mkewe Emmy na Amanda kuondoka.

Muda huo sikuwa najisikia vizuri, mwili wangu ulikuwa unatetemeka na nilihisi akili yangu haifanyi kazi sawa sawa. Ubaridi fulani wa aina yake ulikuwa unanitambaa mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakienda mbio isivyo kawaida! Ili kichwa changu kikae sawa nilitamani ninywe Konyagi au Whisky lakini niliogopa kufanya hivyo kutokana na uwepo wa wale wazee. Sikutaka kuwavunjia heshima.

Mawazo mengi juu ya Rehema yalikuwa yananisumbua sana kichwani kwangu na kunifanya nihisi hatia ikinikaba kooni, nilijitahidi sana kumsahau Rehema bila mafanikio na sikujua hali ile ingeendelea hadi lini!

Mara nikaanza kusikia sauti fulani ikinisemesha na kuishilia akilini mwangu. Nilihisi ni mimi pekee niliyekuwa nikiisikia sauti ile na ilikuwa sauti tulivu sana ya kirafiki lakini iliyokuwa ikinionya. Sauti hii haikuwa ngeni kabisa masikioni kwangu, na wala haikuwa mara yangu ya kwanza kuisikia sauti hiyo.

Tangu nilipoanza kuisikia kwa mara ya kwanza sikuweza kutambua kama ilikuwa ya mwanamume au ya mwanamke na ilikuwa inapenya vyema masikioni mwangu hadi kwenye ubongo, ikaujaza ganzi mwili wangu wote. Wakati hali hiyo ikinitokea nilianza kuyasikia maneno ya Mama yakijirudia akilini mwangu; “…Kwani tatizo lako nini mwanangu, au umerogwa?

Kisha nilianza kuhisi kichwa changu kikizunguka, akili yangu ikishindwa kufanya kazi sawa sawa na muda huo huo nikishindwa kuwaza lolote. Niligwaya na hofu ya chini chini ilianza kunitambaa mwilini mwangu na kusababisha maungo yangu yazizime huku nikihisi joto kali sana likitambaa kwenye mishipa yangu ya damu na kusambaa mwilini kama vile nilikuwa ndani ya tanuru la kuokea mikate.

Mikono yangu ilikuwa inatetemeka kama niliyepatwa na ugonjwa mbaya wa kiherehere cha moyo kutokana na wasiwasi mkubwa au upungufu wa damu. Niliwatazama wajomba pamoja na Mama kwa wasiwasi huku nikitamani kupiga kelele lakini nilishindwa, nyuso za wazee zilionesha wazi kuwa walikuwepo hapo kwa ajili ya kikao kizito sana.

Licha ya kwamba wajomba wote wawili walinipenda sana na walikuwa watu wacheshi na wenye kuheshimu hisia za mtu mwingine, hasa Mchungaji Ngelela aliyekuwa amejaaliwa busara ya hali ya juu na mwenye ufahamu mkubwa wa masuala mbalimbali ya kijamii, kisaikolojia na kiimani, lakini nilishindwa kuzuia wasiwasi wangu na kuanza kuwaogopa.

Nilikuwa nimetahayari sana na kichwa changu nilikiinamisha chini kwa wasiwasi. Baada ya kile kitambo kifupi cha ukimya pale sebuleni huku wale wazee wakinitazamana kwa umakini, mjomba Japheti alijiweka vizuri kisha akakohoa kidogo ili kurekebisha sauti yake.

“Jason, najua umechoka na saa hizi ungependa kupumzika lakini kama ujuavyo safari yetu kuja hapa ni kutokana na matatizo yaliyokupata…” mjomba Japheti alisema huku akishusha pumzi. “Tumeona ni vyema tuzungumze usiku huu kwa sababu jambo kama hili halipaswi kusubiri kesho.”

Niliwaangalia wale wazee kwa umakini hasa mjomba Japheti aliyekuwa anaongea. Na hapo nikamwona Mchungaji Ngelela akijiweka vizuri kwenye kiti. Muda huo nilihisi kuchanganyikiwa zaidi na jasho lilikuwa linanitoka.

“Kabla ya yote, naombeni tufumbe macho na tumwombe Mungu atusimamie kwenye kikao hiki ili busara itawale kikao,” Mchungaji Ngelela alisema huku akianza kufumba macho yake.

Wote tulifumba macho, Mchungaji Ngelela alianza kuomba na muda huo huo nilianza kujishangaa sana baada ya kuanza kuhisi fundo la hasira likinikaba kooni, hata sikujua hasira hiyo ilitoka wapi. Ilimchukua Mchungaji Ngelela takriban dakika tano kuomba na baadaye alipomaliza kila mtu akaitikia “Amen” isipokuwa mimi.

Katika muda wote wa maombi hasira ilikuwa imenitawala na mikono yangu ilikuwa inatetemeka, nilianza kuingiwa na wasiwasi kuwa kama nisingekuwa makini ningeweza kuharibu kila kitu. Mjomba Japheti alinishtukia baada ya kuiona mikono yangu ikitetemeka.

“Jason, uko sawa?” mjomba Japheti aliniuliza huku akiushika mkono wangu mmoja na kuutazama kwa umakini.

Sikumjibu bali akili yangu ilikuwa inafanya kazi haraka, nilitakiwa kufanya kitu fulani haraka sana ili niondokane na tatizo hilo lililonisababishia hasira, hofu na msongo wa mawazo. Sikujiuliza mara mbili na wala sikutaka kulaza damu, niliwataka radhi wale wazee na kuinuka haraka kisha nikaelekea kwenye ukumbi uliojengwa kwa mfano wa kaunta ya baa, nilikuwa bado nimejawa na hasira moyoni.

Sikuujali mshangao wa wazee kwa jinsi walivyokuwa wananiangalia kwani hali yangu haikuwa shwari kabisa, nilikuwa nahisi hasira hasa na sikujua kwa nini hasira hizo zilinijia ghafla kiasi hicho!

Nilipoingia katika ukumbi wa baa nikafungua shelfu mojawapo pale ukutani kisha nikatoa chupa kubwa ya Grant’s Whisky na kuiangalia kwa uchungu, kwa mikono inayotetemeka nikaifungua na kuigugumia pombe iliyokuwemo kwenye chupa kama maji huku nikisisimkwa mwili. Wakati ile pombe ikiwa inashuka tumboni mwangu nilikuwa nayasikilizia mapigo ya moyo wangu jinsi yalivyokuwa yananienda mbio mithili ya mgonjwa mwenye shinikizo la juu la damu.

Kichwa changu kilikuwa kinazunguka na ndani yake kulijitokeza mseto wa hofu, chuki na huzuni ambavyo kwa pamoja vilianza kunitambaa taratibu mwilini. Baada ya dakika tatu nilihisi pombe ikianza kuirubuni akili yangu na taratibu nikianza kuzisahau hasira zangu na kuchangamka. Mikono iliacha kutetemeka.

“Nahitaji matibabu ya ugonjwa wangu ulioletwa na maumivu makali ya kiakili. Maumivu yanayotokana na ukweli wa kuachwa na mtu muhimu sana katika maisha yangu…” niliwaza huku nikigugumia tena funda jingine kubwa la pombe.

“Hakika sitarudi nyuma… nimeteseka sana kwa maumivu makali kama ya mwendesha pikipiki ambaye muda mfupi alionekana akiendesha kwa furaha na mbwembwe nyingi, lakini dakika chache baadaye akajikuta yu wodini akiwa kavunjika miguu yake yote kutokana na ajali…” nilizidi kuwaza, sikuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kuwaza tu.

Kisha nikawachungulia wazee pale sebuleni, walikuwa wameketi kwa utulivu mkubwa wakionesha kunisubiri, hata hivyo Mama alionekana mwenye wasiwasi mkubwa. Nilishusha pumzi huku nikijiuliza hali ile ya maumivu makali ya moyo ingeendelea kunitesa hadi lini!

“Nimekuwa na maumivu kama yalivyo maumivu makali ya kiakili ya mtu ambaye jana alionekana mwenye afya njema lakini leo anagundulika kuwa ana saratani… lakini naamini kila kitu kina tiba yake hata kama ni ya mionzi, na kila kitu kina ufumbuzi wake… mfano, kifo humliwaza marehemu ingawa huwaacha wafiwa wakiwa katika majonzi makubwa…”

“Jason!” sauti ya Mama ilinishtua kutoka kwenye mawazo, niligeuka kuangalia upande ilikotokea sauti hiyo, nikamwona Mama akiwa amesimama huku akinitazama kwa wasiwasi uliochanganyika na huzuni.

Niliigugumia tena ile pombe kama maji na kuimaliza pombe yote iliyokuwemo kwenye ile chupa kisha nikaanza kupiga hatua kurudi pale sebuleni huku Mama akinifuata nyuma, niliwakuta wajomba wakiwa wameketi kwa utulivu, wote walikuwa wananitazama kwa umakini wakati nafika na kuketi kwenye sofa. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya huku wazee wakiangaliana na hapo nikaona wakipeana ishara fulani.

Itaendelea...
 
fungate.jpeg

126

“Sasa mjomba, tunaomba utuambie kinachoendelea hapa maana taarifa tulizozipata zimetutatanisha kidogo!” mjomba Japheti aliniambia baada ya kutulia huku akinitazama usoni kwa umakini.

Nilimtazama mjomba Japheti kwa kitambo huku nikiwa sijui niseme nini kisha macho yangu nikayahamishia kwa Mama na mwisho nikamalizia kwa Mchungaji Ngelela na kushusha pumzi.

“Je, ni kweli ulitaka kujiua?” mjomba Japheti aliuliza tena baada ya kuniona nipo kimya.

“Ndiyo,” nilijibu pasipo shaka yoyote, pombe ilikuwa inafanya kazi yake vyema kichwani.

“Kwa nini?” mjomba Japheti aliuliza huku akiendelea kunitazama kwa wasiwasi.

“Kwa kuwa sikuona namna nyingine ya kufanya…” nilijibu kwa kujiamini na kuwafanya wazee watazamane kwa mshangao mkubwa kisha waliyarudisha macho yao kwangu.

“Hivi u mzima kweli wewe, au una wazimu?” Mama aliniuliza kwa sauti ya upole akiwa haamini kile alichokisikia toka kwenye kinywa changu.

“Mungu apishe mbali, sina wazimu, sijapagawa na wala sina kichaa. Sijui kama mnajua napitia maumivu makali kiasi gani!” nilisisitiza huku machozi yakianza kunilengalenga machoni. Pombe ilizidi kufanya kazi yake na akili yangu ilinituma kuangua kilio.

Niliwaona wazee wakiangaliana huku wakiwa hawaamini kama ni mimi niliyekuwa nikiyasema maneno hayo. Walionekana kuchanganyikiwa.

“Hapana, kutakuwa na shida, huyu si mwanangu Jason ninayemjua! Lazima kutakuwa na shida kwenye ufahamu wake, na huu ulevi aliouanza si wa starehe hata kidogo, kichwa chake hakiko sawa kabisa, sijui nani aliyemloga mwanangu!” Mama alisema kwa huzuni huku akitokwa na machozi.

“Jason, unadhani kujiua ndiyo suluhisho la kumaliza maumivu makali unayopitia?” Mchungaji Ngelela aliniuliza kwa sauti tulivu huku akinitazama kwa umakini.

Nilimtazama Mchungaji Ngelela kwa kitambo kama niliyekuwa nafikiria jibu na kujikuta nikiduwaa huku nikishindwa kujua nijibu nini.

“Kifo!” hatimaye nilisema nikilitamka neno hilo kwa sauti ya chini baada ya kitambo kifupi cha kukaa kimya kisha nilishusha pumzi. “Sielewi lakini ninachojua, kifo humliwaza marehemu…”

Wazee walizidi kunikazia macho kwa mshangao mkubwa zaidi kisha waliangaliana wenyewe kwa wenyewe. Nikamwona Mchungaji Ngelela akishusha pumzi ndefu na kubetua kichwa chake.

“Je, unadhani kifo kama tiba ya matatizo ndiyo njia mwafaka katika kupata ufumbuzi? Na unaelewa kuwa watu wote shupavu hupenda kupambana zaidi na zaidi hadi wanaposhinda?” Mchungaji Ngelela aliniuliza kwa sauti tulivu huku akiwa ameyatulia macho yake kwa umakini zaidi kwenye uso wangu.

Nilibaki kimya huku nikiwa nimegwaya sana, niliinamisha uso wangu kutazama chini nikiwa sina cha kusema, machozi yalikuwa yananitoka, si kwa sababu ya maneno aliyokuwa akiyasema Mchungaji Ngelela bali kwa sababu ya pombe ambayo ilinishawishi kulia.

“Jason, wewe ni shupavu kama alivyokuwa wajina wako. Baba yetu mzee Jason Ngelela alikuwa mtu shupavu sana… usikubali shetani akukatishe tamaa, unatakiwa kupambana hadi mwisho,” Mchungaji Ngelela alisema kwa msisitizo huku akiwa amekunja ngumi kuonesha alama ya ushindi. Kisha aliyapeleka macho yake kutazama moja ya picha za Rehema zilizokuwa ukutani.

“Hebu niambie… huyo ukutani ndiye mke wako mtarajiwa?” Mchungaji Ngelela aliniuliza huku akionesha kwa kidole picha moja ya Rehema.

Niliinua macho yangu kutazama ukutani zilipo picha za Rehema kisha nikaitikia kwa kubetua kichwa.

“Sijawahi kukutana na binti huyu lakini naamini anastahili kabisa kuwa mkeo. Anazo sifa zote za kuwa mke… lakini naona kama wewe hustahili kuwa mumewe kwa kuwa humaanishi kile unachokisema!” Mchungaji Ngelela aliniambia kwa sauti ya upole.

“Namaanisha mjomba, ni yeye pekee nimpendaye,” nilijaribu kujitetea.

“Hapana, unaonesha kabisa hauko serious,” Mchungaji Ngelela alisisitiza huku akinikazia macho kisha akaitazama tena ile picha ya Rehema.

“Niko serious kabisa mjomba,” nami nilisisitiza huku machozi yakinitoka.

“Mtu ambaye yuko serious hupambana kuhakikisha anakitia kwenye himaya yake kitu anachokitaka, tena kwa gharama yoyote ile. Je, unadhani kulewa au kutaka kujiua kutakusaidia kumrudisha huyo mkeo mtarajiwa kwenye himaya yako?” Mchungaji Ngelela aliniuliza huku akinikazia macho.

Nilikaa kimya huku nikiyatafakari maneno ya Mchungaji Ngelela lakini nilihisi akili yangu ikigoma kufanya kazi. Pombe nilizokunywa zilinifanya nihisi ule mseto wa hofu, chuki na huzuni ukiujaza moyo wangu na kunitambaa mwilini, machozi mengi yalianza kunitoka na kutiririka kwenye mashavu yangu. Nilitaka kusema neno lakini mdomo wangu ulikuwa mzito sana kufunguka na maneno yalikuwa hayatoki. Nikaanza kulia kilio cha kwikwi.

Mjomba Japheti alinishika bega akaanza kunipapasa katika hali ya kunifariji, jinsi alivyokuwa akinifariji ndivyo alivyozidisha uchungu moyoni mwangu na kilio changu kikazidi, nililia sana huku nikihisi donge la uchungu likinikaba kooni. Kila nilipotaka kuongea mdomo wangu ulikuwa mzito sana na maneno hayakuweza kutoka.

Muda wote Mama alikuwa ananitazama kwa huzuni huku akijitahidi kuyazuia machozi yake yaliyokuwa yanamlengalenga.

Muda ulizidi kusonga na mimi nilikuwa nalia kwa uchungu pasipo kukoma, nikamwona Mchungaji Ngelela akiinuka na kuanza kuimba; “Tazama wewe ni Bwana Mungu wa wote wenye mwili, je kuna neno gumu lolote usiloliweza… Je, kuna neno, kuna neno, kuna neno usiloliweza, je kuna neno gumu lolote usiloliweza…”

Wakati Mchungaji Ngelela akiimba wimbo huo niliwaona Mama na mjomba Japheti pia wakiungana naye kuimba wimbo huo kwa hisia. Iliwachukua takriban dakika tatu wakiimba kisha Mchungaji Ngelela akaanza kuongea lugha ambayo sikuielewa kabisa, wenyewe walisema ni kunena kwa lugha.

Wakati akinena kwa lugha alinifuata pale nilipoketi huku nikiendelea kulia kilio cha kwikwi na kunishika kichwa, akaanza kuomba na kadiri alivyozidi kuomba huku akiwa amenishika kichwa changu nilihisi kupatwa na kizunguzungu na fundo la mchanganyiko wa hasira na hatia likinikaba kooni. Ilifikia hatua nikahisi pumzi zikinipaa, nikaanza kushindwa kupumua vizuri.

Nilitamani kufungua mdomo wangu ili niwaambie wanyamaze kwani walikuwa wananipigia kelele lakini mdomo wangu ulizidi kuwa mzito sana na sauti iligoma kabisa kutoka. Moyo wangu ulianza kuunguruma sana kama uliokuwa ukipambana na kazi isiyo ya kiasi chake, macho yangu nayo taratibu yalianza kupoteza nguvu ya kuona. Na hatimaye shughuli mbalimbali za mwili wangu zilianza kusitisha utendaji wake.

Akili yangu ilianza kushindwa kufanya kazi na sasa nikaanza kujiona nikitumbukia kwenye shimo lenye kiza kisha nguvu zikaanza kuniishia na mwili wangu ukalegea huku mapigo yangu ya moyo nayo yakidorora… kuanzia hapo sikuelewa nini kiliendelea.

Nilipokuja kushtuka nilijiona nikiwa nimelala chali sakafuni huku nikiwa kifua wazi, sikuweza kufahamu nililala pale kwa muda gani nikiwa sijitambui. Wajomba na Mama walikuwa wamenizunguka huku wakiendelea kuimba.

Walipogundua kuwa nimerudiwa na fahamu zangu walininyanyua toka pale sakafuni nilipolala huku wakimshukuru Mungu kisha wajomba walinikokota taratibu kunipeleka chumbani kwangu ambako walinilaza kitandani, kisha wakatoka na kurudi sebuleni. Kwa mbali niliwasikia wakianza tena kuimba wimbo wa kumshukuru Mungu…

* * *

Itaendelea...
 
fungate.jpeg

127

Saa 9:15 usiku…

Sikuweza kufahamu ni wakati gani usingizi mzito ulinichukua lakini baada ya kuzinduka toka usingizini niliisikia sauti ya mtu kutokea sebuleni, alikuwa anaomba huku maneno yake yakiambatana na kilio. Niliyatega vizuri masikio yangu kusikiliza kwa umakini na nikagundua alikuwa Mchungaji Ngelela, alikuwa anaomba, tena alikuwa anaomba kwa uchungu sana.

Niliamka nikafikicha macho, kisha nikaelekea maliwato na kujisaidia haja ndogo na kurudi kukaa kitandani huku nikisikiliza kwa umakini. Nilimsikia akiendelea kuomba, tena kwa mzigo hasa. Kuna wakati nilimsikia akiongea maneno ambayo sikuwa nayaelewa kabisa, alikuwa ananena kwa lugha.

Niliitupia jicho saa yangu na kugundua kuwa ilikuwa imetimia saa tisa na robo usiku, nikashusha pumzi huku nikishangaa sana. Mchungaji Ngelela aliendelea kuomba na mimi nikawa nimekaa kimya kitandani nasikiliza.

Kuna muda alitulia kidogo kisha akaanza kuimba; “Wewe ni Mungu mkuu, waweza yote, hakuna Mungu kama wewe… Wewe ni Mungu, unaweza, unaweza, unaweza Yesu, unaweza unaweza Yesu…”

Aliimba kwa kitambo fulani kisha akaanza kuomba tena huku akinena kwa lugha. Muda huo nilihisi machozi yananitoka ila sikujua kwa nini nilitokwa na machozi. Nilipoiangalia tena saa yangu nikagundua kuwa ilikuwa inaelekea kuwa saa kumi na robo. Mchungaji Ngelela alikuwa bado anasali!

Niliendelea kukaa pale kitandani nikimsikiliza. Alianza tena kuimba na baada ya muda akaanza tena kuomba. Dah! Nilijikuta nikichoka kabisa! Mchungaji Ngelela alikuwa ameniacha hoi kabisa na hakuonekana kunyamaza, hakuonekana kutulia, aliendelea kuomba pasipo kuchoka! Nilipoiangalia tena saa yangu nikaona muda umesonga zaidi, ilikuwa inaelekea kuwa saa kumi na mbili asubuhi!

* * *


Zilipita siku tatu huku hali yangu ikizidi kuwa mbaya, ilikuwa ngumu sana kuukubali ukweli na nilizidi kuelemewa na msongo wa mawazo, na hivyo muda mwingi nilikuwa nimelewa. Kuna wakati nilijifungia chumbani nikipitisha siku bila kuzungumza neno lolote na muda wote kumbukumbu juu ya Rehema zilipita akili kwangu, tena zilipita kwa kasi sana na kuzidi kunivuruga.

Mchungaji Ngelela alifunga kula kwa siku tatu huku akiomba na aliamini kuwa, Mungu kupitia manabii wake anasema; “abishaye hodi kwa dhati atafunguliwa”.

Mama alianza kukata tamaa, alijua mwanawe ndiyo nimekwisha changanyikiwa na hakuona tena njia nyingine ya kufanya isipokuwa kumwachia Mungu tu, kwani ndiye hupanga kila kitu. Hata hivyo, nilijua kuwa Mama asingekubali kirahisi kuwa ameshindwa kuniokoa mwanawe, na siku mbili baadaye alimleta mwanasaikolojia chumbani kwangu ili angalau asaidie kunirejesha katika hali ya kawaida, lakini juhudi zao ziligonga mwamba!

Jambo moja tu ambalo Mama hakuthubutu kulifanya, nalo ni kuwatafuta waganga wa kienyeji. Hakuthubutu kuwafikiria kwa sababu ya imani yake ambayo haikumpa nafasi kufanya kazi na watu hao, licha ya kudhani kuwa nilikuwa nimerogwa. Hakuthubutu kabisa kuwapa nafasi waganga kwa sababu aliamini kuwa uchawi na uganga ni ushirikina, na ushirikina haukuwa na nafasi katika maisha yake.

Mchungaji Ngelela aliendelea kuomba kwa siku saba mfululizo lakini bado sikuweza kubadilika. Mama alishauri tuondoke na kwenda Tabora ili nikapumzishe akili yangu, pengine ningeweza kuyasahau masaibu yaliyonipata. Nilikataa.

Mama alinihurumia sana mwanawe lakini hakuwa na namna nyingine ya kufanya ila kuzidi kuniombea kwa Mungu.

* * *

Itaendelea...
 
fungate.jpeg

128

Mshtuko Mkubwa.


Saa 3:30 usiku…

POMBE kali aina ya K Vant ilikuwa inashuka taratibu tumboni mwangu na kutengeneza starehe ya aina yake. Bado akili yangu ilikuwa haijatulia na iliendelea kusumbuka katika kutaka kujikwamua kwenye tatizo la ulevi. Muda huo nilikuwa nimeketi kwenye meza moja ya pembeni kabisa kwenye mandhari safi na tulivu kabisa ya bustani katika baa ya Kahama Tulivu Garden.

Kulikuwa na wahudumu wa kike warembo waliokuwa wakihudumia wateja wachache waliokuwa katika bustani hiyo wameketi kwenye meza nzuri za mbao ya mti wa jacaranda na viti vifupi vyenye foronya laini.

Nilipiga tena funda kubwa la pombe kuupoza mtima wangu huku nikiyatembeza macho yangu kuangalia mle ukumbini. Niliitazama saa yangu ya mkononi kisha nikapiga funda jingine la kinywaji.

Zilikuwa zimepita wiki mbili tangu nilipopata ugeni wa wajomba na Mama nyumbani kwangu, pamoja na jitihada walizozifanya bado niliendelea kusumbuliwa na jinamizi la ulevi, na sasa maisha yangu yalitegemea pombe, bila kulewa hali yangu ilikuwa mbaya na nisingeweza kulala.

Nilikuwa nimeamua kuishi maisha ya kutegemea pombe ili kujisahaulisha kuhusu Rehema, nilianza kufanya jitihada ili Rehema atoke kwenye mawazo yangu na niweze kuendelea na maisha yangu ya kawaida. Nilikuwa nimepungua sana na nilionekana kituko mbele ya watu walionifahamu.

Nywele zangu zilikuwa ndefu zisizo na matunzo, zilikuwa zimetimkatimka kana kwamba sikujua kama kulikuwa na chanuo duniani kwa ajili ya kuchania nywele ndefu, au kana kwamba sikujua kwamba kuna saluni na mkasi kwa ajili ya kunyoa nywele.

Sasa nilikuwa siendi sehemu zenye mkusanyiko mkubwa wa watu na badala yake nilikwenda mahala ambako ni patulivu sana, kwenye watu wachache, sehemu ambayo nilipata wasaa japo muda mfupi wa kuyasahau maisha yangu ya nyuma.

Kahama Tulivu Garden ilikuwa moja ya sehemu pekee nilizodhani zingenisaidia sana kuyasahau masaibu yangu kwani sehemu hiyo ilikuwa na utulivu wa hali ya juu sana kama lilivyokuwa jina lake. Ilikuwa sehemu ambayo inapendwa sana na wageni toka sehemu mbalimbali kutokana na utulivu wake na mandhari ya kuvutia mno.

Niliifahamu vyema sehemu hii na ndiyo maana nilichagua kwenda hapo kwa sababu ilikuwa sehemu pekee niliyoamini ingesaidia sana kunisahaulisha na zahma iliyonikumba japo kwa kipindi fulani. Katika bustani hiyo tulivu kulikuwa na sura nyingi za wageni na ukimya ulikuwa umetawala. Ni sauti ya muziki laini wa ala ndiyo iliyokuwa inasikika. Hakika sehemu hii iliniliwaza kidogo na hata mimi nilipafurahia mno.

Saida Mhando, mhudumu aliyekuwa ananihudumia alifika nilipokuwa nimeketi na kwa adabu akaangalia kama kinywaji changu kilikuwa kimekwisha, kisha aliniuliza kama ningependa aongeze kinywaji kingine. Nilimwambia ningemwita kama ningehitaji chupa nyingine ya K Vant, muda huo nilianza kuhisi furaha. Sikujua kwa nini nilijihisi furaha kwa muda ule niliokuwa pale.

Saida alikuwa msichana mzuri na mrembo sana na alivalia sketi nyeusi fupi iliyoishia juu ya magoti na ilikuwa imenasa vyema kwenye kiuno chake chembamba kilichoshikilia mzigo mkubwa wa makalio yake imara yaliyoimarisha vizuri minofu ya mapaja yake yaliyotuna kama chura.

Wakati akiondoka pale alitembea kwa madaha huku akiuteka umakini wangu, nilimsindikiza kwa macho mara macho yangu yakaachana na yule mhudumu na kutua kwa mwanadada mmoja aliyekuwa ameketi meza moja ya pembeni kabisa. Nilipomwona tu nikampa alama zote na kukiri kuwa alikuwa mrembo sana huku nikimpa Mungu heko yake kwa kazi nzuri ya uumbaji.

Alikuwa mrefu, alikuwa mweupe kiasi na mwenye haiba nzuri ya kuvutia. Nywele zake zilikuwa ndefu nyeusi na laini na macho yake malegevu. Alivaa suruali ya dengrizi ya rangi ya bluu mpauko iliyolichora vyema umbile lake refu maridhawa lenye tumbo dogo, nyonga pana na kiuno chembamba kilichoshikilia mzigo mkubwa wa makalio na minofu ya mapaja yake yaliyonona vyema.

Juu alivaa blauzi nyeusi ya mikono mirefu yenye miraba myeupe, blauzi hiyo iliyaficha matiti yake madogo yaliyotishia kuitoboa, na miguuni alikuwa amevaa viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio. Mkononi alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe na juu ya meza yake kulikuwa na mkoba mzuri wa ngozi ya pundamilia ambao ulimgharimu fedha nyingi kuununua. Alikuwa anakunywa maji.

Katika kumwangalia kuna jambo moja lilinishtua sana, yule mwanadada alikuwa anafanana sana na Rehema, kwa sura, umbo na hata kimo. Tofauti yao ilikuwa ndogo sana hasa kwenye rangi ya ngozi. Rehema hakuwa mweupe wala mweusi bali alikuwa na rangi ya maji ya kunde lakini mwanadada huyo alikuwa na weupe kidogo.

Nilihisi labda nilikuwa namwangalia kwa macho ya kilevi, nikayafikicha macho yangu ili niweze kumwona vizuri. Nilipoyatupa tena macho yangu kwenye ile meza kwa mara nyingine, sikuyaamini macho yangu, meza ilikuwa tupu na hakukuwa na mtu wala kitu chochote juu ya meza!

Nilitulia kidogo na kufikiria huku nikiwa siamini, nilihisi labda nilikuwa nimezidiwa na pombe. “Haiwezekani, nimemwona kabisa amekaa hapo sasa hivi, iweje asiwepo tena? Au ni jini?” nilijiuliza mwenyewe pasipo kupata jibu. “Hapana nimeshalewa…”

Nilimwita Saida ili nilipe bili na kisha niondoke zangu nikapumzike nyumbani maana sikutaka kuendelea kushuhudia mauzauza, Saida alibetua kichwa chake akanipa ishara kuwa angekuja muda si mrefu, na muda huo huo nikashtuliwa na sauti ya mtu iliyotokea nyuma yangu.

“Nakuona muda wote upo kimya sana na huna kampani, hujisikii upweke?” mwanamume mmoja aliyefika na kuketi kwenye meza yangu aliniuliza kwa Kiswahili cha lafudhi ya Kikongo.

Yule mwanamume alikuwa mrefu na mwembamba, alivaa joho la kitambaa cha bazee lililodariziwa vizuri shingoni kwa nyuzi za dhahabu na kofia ya kufuma iliyozihifadhi nywele zake ndefu za rasta kichwani alizozizungusha na kuzifunga. Alikuwa na ndevu nyingi zilizokizunguka kidevu chake na alivaa miwani ya macho. Katika vidole viwili vya mkono wake wa kushoto alikuwa amevaa pete mbili za madini ya dhahabu na rubi. Mkononi alikuwa ameshika sigara aina ya Dunhill na bilauri ya mvinyo mwekundu.

Kwa tathmini yangu ya haraka haraka nilihitimisha kuwa mwanamume yule alikuwa mtu mwenye kipato cha kueleweka. Nilimtazama kwa udadisi na hapo nikagundua kuwa alionekana kuwa mtu wa starehe kwa sana.

“Hapana, nilihitaji utulivu kidogo,” niliongea kwa sauti tulivu kisha nikaendelea. “Lafudhi yako inaonesha kuwa wewe si Mtanzania!”

“Mimi ni Mkongomani lakini maskani yangu kwa sasa yapo jijini Paris nchini Ufaransa,” yule mwanamume aliniambia kwa utulivu huku akivuta funda la kinywaji chake.

“Na hapa Kahama umekuja kikazi au matembezi?” nilimuuliza yule mwanamume huku nikimsaili kwa macho.

“Hapana! Nipo hapa kwa mapumziko mafupi baada ya shughuli nzito za utafutaji, nawapenda sana Watanzania, ni watu wakarimu mno!” yule mwanamume aliongea huku akiangua kicheko hafifu, alikuwa ananitazama kwa umakini na hapo nikapata nafasi ya kumwangalia vizuri.

Alikuwa mwanamume wa makamo ambaye alikadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka arobaini na arobaini na tano. Alikuwa mrefu wa futi sita na ushee, mweupe kiasi na shababi kweli kweli mwenye mwili uliojengeka kwa misuli. Macho yake yalikuwa makubwa na makali.

Nilitaka kumuuliza kwa nini alichagua kuja Kahama badala ya miji mingine lakini nikakatishwa na sauti ya Saida aliyekuja na kusimama mbele yangu akiwa ameshika chupa nyingine ya K Vant.

Itaendelea...
 
fungate.jpeg

129

“Sihitaji tena pombe, nimekuita ili nikulipe bili yako, nahitaji kwenda kupumzika,” nilimwambia Saida huku nikiiangalia ile chupa ya K Vant.

“Bili yako imeshalipwa tayari, na hii chupa nimeagizwa nikuletee, amekununulia dada mmoja alikuwa amekaa pale,” Saida aliniambia huku akigeuka kunionesha kwenye ile meza aliyokuwa ameketi yule mwanamke anayefanana na Rehema aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Alikuwa amekaa kwenye meza ile muda si mrefu,” Saida alisema kwa msisitizo.

“Yukoje huyo dada?” niliuliza kwa utulivu huku nikimtazama Saida machoni katika namna ya kutaka kupata uhakika wa jibu ambalo lingemtoka mdomoni.

“Alikuwa amevaa blauzi nyeusi ya mikono mirefu yenye miraba myeupe na suruali ya dengrizi,” Saida alisema huku akiachia tabasamu maridhawa.

“Unamfahamu vizuri huyo dada?” nilimuuliza Saida kwa shauku huku nikiendelea kumtazama machoni.

“Sifahamu anaitwa nani ila si mara ya kwanza kumwona hapa Tulivu. Hata jana alikuja na alikaa meza ile pale,” Saida alisema huku akinionesha meza moja ya pembeni.

“Usije ukawa umekosea, una uhakika alikwambia uniletee mimi?” niliuliza huku wasiwasi ukianza kunitawala.

“Ndiyo. Alitaja hadi jina lako, au kuna Jason mwingine hapa?” Saida alisema kwa msisitizo akionekana kuwa na uhakika.

Kauli ya Saida ilinishtua kidogo, nilimtupia jicho yule mwanamume Mkongomani nikamwona akinitazama kwa namna ambayo sikuweza kuelewa tafsiri yake. Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani na kwa sekunde kadhaa nilibaki nimeganda kama sanamu nikimtazama Saida huku nikiwa sijui nichukue uamuzi gani iwapo niichukue ile chupa ya K Vant au niikatae.

Koo langu lilikauka ghafla kwa hofu na mapigo ya moyo wangu yalianza kunienda mbio huku baridi nyepesi ikisafiri katika maungo yangu. Kwa kweli moyo wangu ulipoteza kabisa utulivu ingawa sikutaka kuruhusu hali ile ionekane usoni kwangu.

Nilianza kujiuliza maswali mengi kuhusu yule mwanamke, kwa nini hakutaka kujitokeza kwangu? Hata hivyo, nilipiga moyo konde na kujipa ujasiri ingawaje kwa namna fulani nilianza kujionya juu ya kuwa makini. Niliipokea ile chupa ya K Vant na kuiweka juu ya meza. Saida akaondoka huku akiniachia maswali kibao kichwani.

Niliitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilikuwa inaelekea kutimia saa nne na nusu usiku. Nikamuaga yule mwanamume Mkongomani na kuondoka zangu.

* * *



Saa 7:00 usiku…

Hata sikujua nilikuwa naelekea wapi lakini akili yangu ilinituma kusonga mbele zaidi, nilipiga hatua huku nikitembea kwa mwendo wa haraka na kukatiza barabara kisha nikawa nakifuata kichochoro kimoja. Mara nikajikuta navutiwa kumtazama msichana mmoja aliyekuwa amesimama peke yake kwenye jengo moja, alionekana kama aliyekuwa anasubiria kitu.

Alikuwa msichana mrefu na maji ya kunde mwenye haiba nzuri ya kuvutia. Alikuwa na nywele ndefu nyeusi na alivaa suti nzuri ya kike ya rangi ya maruni iliyompendeza sana na kulipendezesha umbo lake refu maridhawa, alikuwa na nyonga pana na kiuno chembamba kilichoshikilia mzigo mkubwa wa makalio na minofu ya mapaja yake yaliyonona vyema.

Nikiwa na hakika kuwa alikuwa hafahamu chochote kuwa nilikuwa namtazama nilisimama na kumtazama kwa udadisi na muda huo nilianza kuhisi hisia za upweke zikinitawala, sikujiuliza mara mbili nikaanza kupiga hatua kumfuata kwa mwendo wa haraka huku uso wangu ukianza kutengeneza tabasamu la kirafiki.

Msichana yule akawahi kugeuka na kunitazama kabla sijamfikia na hapo macho yetu yakakutana na kunifanya nipunguze mwendo wangu.

“Rehema!” niliita kwa mshangao.

“Jason!” Rehema aliniita kwa sauti ya upole iliyojaa mahaba makubwa huku akiachia tabasamu.

Kisha alinikimbilia na kunikumbatia kwa nguvu, tukakutana mwili kwa mwili na kukumbatiana kwa nguvu huku kila mmoja wetu akishindwa kujizuia kutoa machozi. Rehema alijigandamiza kwenye mwili wangu kama aliyetamani kuunganisha mwili wake na wangu, kwa kweli alikuwa kama mama aliyekuwa amempoteza mwanawe wa pekee na sasa amempata.

Kisha aliipitisha mikono yake nyuma ya shingo yangu na kusababisha chuchu za matiti yake kukitekenya kifua changu na kufanya joto kali la mwili wake linipe faraja ya aina yake. Nilipomtazama Rehema machoni nikayaona machozi ya furaha yakianza kumtoka. Alionekana ana afya njema kabisa ingawa alikuwa amepungua kidogo.

Kwa kiganja changu taratibu nikamfuta machozi lakini ilionekana kwamba tendo lile halikuwa na umuhimu wowote kwake kwani haraka aliuondoa mkono wangu machoni mwake kisha akanivuta karibu na hapo ndimi zetu zikakutana.

Tukapeana mabusu motomoto tukiwa bado tumekumbatiana kwa nguvu zenye hisia nzito huku nikipeleka mikono yangu kuyatomasa makalio yake laini yaliyoshiba minofu. Nilijikuta nasahau kuhusu safari yangu na kusahau kuwa eneo lile tulilokuwepo halikuwa sahihi kwa kile kilichokuwa kinaendelea baina yetu, ni kama tuliokuwa tumedungwa sindano za ganzi ya aibu, tukidhihirisha ule usemi usemao “mapenzi ni upofu”.

“Rehema, nilijua sitakuona tena,” nilimwambia Rehema huku nikimtazama machoni, wakati huo macho yangu yalikuwa yamejaa machozi.

“Jason…” Rehema aliniita kwa sauti ya chini huku akiwa amekunja sura yake.

“Naam Rehema…”

“Ulikuwa wapi, mbona hukuja hospitali kuniona?” Rehema aliniuliza huku akijitahidi kudhibiti donge la hasira kooni mwake.

“Naomba unisamehe mpenzi ila sikufanya makusudi,” Nilimsihi kwa utulivu huku usoni nikiumba tabasamu la kirafiki.

“Hebu niambie, ulikuwa wapi siku zote hizi?” Rehema hakutaka kunisikiliza, aliniuliza huku akiwa amekasirika.

“Naomba tutafute sehemu nzuri tukae halafu nikuelezee,” Nilinong’ona huku nikimkumbatia.

Itaendelea...
 
fungate.jpeg

130

So you have refused to obey my commands?” (Kwa hiyo umekataa kutii maagizo yangu?) sauti nzito ya mtu ilisikika kando yetu.

Tuliachiana mara moja na kugeuka kuangalia kule sauti ilikotokea, tukamwona mzee Benard Mpogoro, baba wa Rehema akiwa anatuangalia kwa hasira. Mkononi alikuwa ameshika bastola aina ya FNX 45 Tactical na alikuwa ameielekeza kwangu. Nilitamani ardhi ipasuke ili nizame ndani yake.

“Baba!” Rehema aliita kwa mshangao huku akimkodolea macho baba yake.

Mzee Mpogoro hakutaka kumsikiliza Rehema, alichofanya ni kuvuta ndimi ya bastola na kuielekeza kwenye kichwa changu, nikafumba macho yangu huku nikiomba Mungu aninusuru. Mara ukasikika mlio mkubwa wa risasi ulioambatana na mwanga mkali.

Nikaanguka chini huku nikihisi moyo wangu ulikuwa umepoteza mapigo yake…

_____

Nilikurupuka kutoka usingizini huku nikitweta, moyo wangu ulikuwa unagonga kwa nguvu na kasi mfano wa saa kubwa ya Jamatini na jasho lilikuwa linanitoka. Nilipojitazama vizuri nikagundua kuwa nilikuwa nimelala kitandani chumbani kwangu.

Niliitupia jicho saa yangu na kugundua kuwa ilikuwa imetimia saa saba ya usiku. Nilianza kuwaza kuhusu ile ndoto niliyoota na maana yake lakini sikuweza kupata jibu, niliposikiliza kwa makini nikagundua kuwa mvua ilikuwa inanyesha huko nje, mvua iliyoambatana na radi.

Na hapo nikaelewa kuwa ule mlio mkubwa wa risasi ulioambatana na mwanga mkali niliousikia ndotoni ilikuwa ni radi. Nilijikunyata nikijaribu kulala usingizi lakini usingizi ulionekana kunipaa, kwani ndoto niliyoota ilinitatanisha sana na kunifanya nisipate tena usingizi.

Nilijaribu kuwaza na kuwazua, nikajiuliza maswali mengi pasipo kupata majibu, nikaanza kuhisi naanza kupata wazimu. Nilipiga miayo na kujinyoosha kisha nikaelekea maliwato, niliporudi kitandani nikafumba macho yangu nikijaribu kuyasahau yote na kuutafuta usingizi lakini sikuupata.

Baada ya kitambo kirefu cha mahangaiko pale kitandani hatimaye ilitimu saa kumi na mbili alfajiri. Nilijiinua kutoka pale kitandani na kujinyoosha huku nikipiga miayo ya uchovu, niliketi kitako huku nikiendelea kutafakari. Bado sikupata majibu, nikashusha pumzi za ndani kwa ndani na kujitoa pale kitandani taratibu, nikatembea kwa kuyumbayumba mithili ya mlevi na kuelekea sebuleni.

Nilifika pale sebuleni na kusimama huku nikiyazungusha macho yangu kuitazama sebule yangu, mara macho yangu yakatua kwenye chupa ya K Vant iliyokuwa juu ya meza. Nikakumbuka kuwa nilinunuliwa na yule mwanadada aliyefanana sana na Rehema niliyemwona pale Tulivu Garden. Nikainua uso wangu kuitazama picha kubwa ya Rehema iliyotundikwa ukutani.

Muda huo huo mvua ilikatika na kuliachia jua lenye kupunga la asubuhi lichomoze. Nikaanza kuwasikia ndege wa kila aina wakilia kwa namna ya kuisifia asubuhi ile na kuifanya kuwa njema, ingawa kwangu haikuwa njema kabisa.

Nililifuata dirisha na kufunua pazia, nikachungulia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha na kuwaona ndege wakiruka huku na kule huku wakiisifia asubuhi ile, tena walionekana ni wenye furaha kubwa.

Niliwasikiliza wale ndege kwa muda, nikajaribu kubashiri maana ya zile nyimbo nzuri walizokuwa wakiimba, nikajitahidi kuyasikia maneno katika nyimbo hizo na kubaini kuwa yalibeba ujumbe mzuri sana japo kwangu ulikuwa wa kusikitisha, nikaguna.

“Mmh! Labda wao wameumbwa kuwa wenye furaha daima,” nilijiambia baada ya kuwasikiliza wale ndege kwa umakini wakiimba kwa namna yake.

“Kama ni hivyo, basi mimi ni binadamu mpweke sana katika dunia hii na wala sina mfano! Lakini ndege nao hupatwa na majanga kama vile kukosa nafaka, kuharibiwa kwa viota na makinda yao, na mengineyo mengi ikiwemo kuwindwa na binadamu… wao pia wanayo matatizo, tena makubwa lakini hawakati tamaa, bali hutafuta njia madhubuti ya kutatua matatizo yao. Kwa nini mimi nishindwe? Kwani mimi nimemkosea nini Mungu?” niliwaza huku donge la uchungu likinikaba kooni.

Nilianza kuzidiwa na mawazo kupita kiasi kitendo kilichonifanya nihisi kuchanganyikiwa zaidi. Sikutaka kuendelea kujiumiza na mawazo, niliichukua ile chupa ya K Vant na kuifungua kisha nikaigugumia kama maji pombe yote iliyokuwemo ndani ya chupa.

* * *

Endelea kufuatilia...
 
View attachment 2184687
66

“Kama hakuna tatizo mbona huongei? Naona umenywea ghafla au eneo hili linakuboa?” Rehema aliniuliza tena huku akiniangalia kwa umakini.

“Wala hapajaniboa, na-enjoy chakula kitamu ingawa hawakufikii, mpenzi wangu,” nilijibu Rehema huku nikiachia tabasamu.

“Haya bwana,” Rehema aliongea kwa sauti tulivu iliyobeba uchovu. Lakini sikuona tashwishwi yoyote usoni kwake.

Muda huo nilijifanya kuzungusha macho yangu kuyatazama mandhari ya ukumbi ule lakini lengo langu lilikuwa kumwangalia Amanda. Katika uchunguzi wangu macho yangu yalianza kutua kwenye ile meza ya jirani iliyokuwa na wale akina dada wawili warembo na mwanamume mmoja, rafiki zake Rehema.

Hapo hayakukaa sana, niliyapeleka moja kwa moja kwenye meza aliyoketi Amanda na mwanamume wake, nikamwona akiinamisha kichwa chake chini kama aliyeona kitu kwenye miguu yake, aliangalia chini kwa kitambo kisha aliinua uso wake taratibu kwa madaha kana kwamba alikuwa anaigiza filamu, mara macho yetu yakakutana. Kwa nukta kadhaa macho yetu yalitulia yakitizamana kisha Amanda aliyahamisha macho yake na kutazama kando.

Muda huo huo nikamwona akiyashusha macho yake kuitazama simu yake ya mkononi ambayo ilikuwa inatoa mwanga na hapo nikatambua kuwa ilikuwa inaita. Aliitazama ile simu kwa kitambo akionekana kama aliyekuwa akijishauri jambo, akabana taya zake na kumnong’oneza jambo yule mwanamume aliyekuwa naye kisha akainuka na kusogea kando, sehemu isiyo na kelele za muziki na kuipokea kisha akaipeleka moja kwa moja sikioni.

Alionekana kuwa mtulivu sana alipokuwa akiongea na simu na muda wote alikuwa ananitupia jicho la wizi. Baada ya mazungumzo ya takriban dakika tatu huku sura yake ikibadilika kisha alikata simu na kuonekana akishusha pumzi kisha akarudi pale kwenye meza.

Nilihisi kuwepo jambo maana nilimwona akiongea jambo na yule mwanamume aliyekaa naye kisha akachukua chupa ya bia iliyokuwa juu ya meza na kuimiminia bia yote iliyokuwemo katika bilauri huku akinitupia jicho la wizi, kisha alinyanyua na kuigida bia yote na kuikita ile bilauri juu ya meza. Kisha alitupia tena jicho la wizi akionekana mwenye wasiwasi kabla hajanyanyua mkono wake kuitazama saa yake ya mkononi.

Niliendelea kumchora tu nikajisahau kuwa Rehema alikuwa ameketi pembeni yangu na alikuwa akiniangalia kwa umakini kila nilichokifanya. Amanda alinong’ona tena jambo kwa yule mwanamume aliyekuwa naye na kunyanyuka huku akinitupia jicho la wizi. Macho yetu yakagongana. Amanda akajifanya kutazama tazama huku na kule mle ukumbini kama aliyekuwa akitafuta kitu kisha nikamwona akiondoka haraka eneo lile, akaelekea kwenye vyumba vya maliwato.

Sikutaka kusubiri maana nilikuwa nahisi kuchanganyikiwa kadiri muda ulivyosonga, nikamwomba Rehema anielekeze vilipo vyumba vya maliwato, bila ajizi akanielekeza. Nilisimama nikaelekea huko na nilipomtupia jicho la wizi yule mwanamume aliyekuwa ameketi na Amanda nikagundua kuwa alikuwa akiniangalia kwa mashaka, lakini sikumjali. Nilisonga na hatimaye nikajikuta nipo mahala ambako kulikuwa na ukumbi mpana uliokuwa na picha mbili za kuchorwa zilielekeza vyoo vya wanawake upande wa kushoto na vyoo vya wanaume upande wa kulia.

Nikasimama katika eneo ambalo ningeweza kumwona kila aliyetoka katika vyoo vya wanawake nikiwa na nia ya kumsubiri Amanda ili nimbane hadi anieleze ukweli kuhusu yule mwanamume aliyekuwa naye na kwa nini alikuja Ushirombo bila kuniambia.

Mara nikamwona Amanda akitokea kwenye vyumba vya maliwato ya wanawake na aliponiona alishtuka sana akataka kurudi chooni lakini akasita, jasho lilikuwa linamtiririka na alikuwa na wasiwasi mwingi. Alijongea taratibu mahala nilipokuwa nimesimama huku akilazimisha tabasamu, alijifanya kutokuwa na shaka yoyote. Niliendelea kumwangalia kwa umakini nikiwa nimekunja uso wangu.

Aliponifikia tu nikamkamata kwa nguvu na kumvutia kwenye vyoo vya wanaume, na hapo tukajikuta tumetokea kwenye ukumbi mpana na msafi wa vyoo uliokuwa na masinki kadhaa ya kunawia mikono na kando kulikuwa na sehemu za kujisaidia haja ndogo. Niliyazungusha haraka macho yangu kutazama eneo lile huku nikiwa makini, sikumwona mtu yeyote zaidi yetu, nikaiona milango kadhaa ya vyumba vya maliwato. Sikusubiri, nikamshika mkono Amanda na kumpeleka kwenye chumba kimojawapo pasipo mtu mwingine kutuona.

Ni kama mwili wa Amanda ulikuwa umeingiwa na ganzi, hakuweza kunigomea wala kuzungumza chochote bali alifuata kila nilichomtaka kufanya na muda wote alikuwa ananiangalia kwa wasiwasi mkubwa huku jasho likimtoka. Tulipoingia mle chooni nikambana kwenye ukuta huku nikimkabili. Tukabaki tumetazamana.

Macho yake legevu yalinitazama kwa wasiwasi kama mtu ambaye alikuwa akijutia kosa fulani alilolifanya. Hisia zangu zilianza kuwa taabani na macho yangu yakaanza kufanya ziara ya kushtukiza kifuani pake na hapo kupitia kivazi chake nikaziona chuchu zake laini zilivyosimama kwa utulivu juu ya milima miwili kama zilizokuwa zikinidhihaki.

Macho yangu yakatambaa kuuangalia mwili wake na yalishuka hadi kiunoni na hapo nikaiona nyonga yake laini yenye mifupa miteke iliyopakana na mzigo imara wa makalio yaliyotuama vema. Wakati nikiwa katika hali ile ya mduwao mara nikakumbuka kuwa nilimfuata kule chooni kwa ajili ya kumuhoji na si kufanya mapenzi.

“Unafanya nini hapa Ushirombo?” nilimuuliza kwa hasira huku nikimkazia macho.

“Na wewe unafanya nini, kwani hapa ndo Tabora?” Amanda akaniuliza huku akikunja sura yake.

“Kwa hiyo tunashindana, siyo? Mimi nikifanya hivi na wewe unafanya vile?” nilimuuliza kwa hamaki huku nikimkazia macho, akabaki kimya akiwa ameinamisha uso wake. “Nitakutandika makofi sasa hivi.”

Amanda alibaki kimya akiniangalia kwa woga, alikuwa anapumua kwa shida na niliweza kuona jinsi mapigo ya moyo wake yalivyokuwa yakienda kasi isivyo kawaida.

“Niambie, yule mwanamume ni nani?” nilimuuliza kwa hasira lakini Amanda akaendela kubaki kimya huku akionekana kupumua kwa shida.

“Nakuuliza, yule mwanamume ni nani?” nililirudia tena swali langu.

“Naomba unisamehe mpenzi wangu,” Amanda alinisihi kwa sauti ya kunong’ona.

“Nikusamehe kwa lipi, naomba kwanza uniambie yule ni nani?” niliuliza kwa ukali huku nikimminya kwa nguvu pale ukutani. Amanda akaanza kutetemeka kwa hofu.

“Yule nii… nii… Jason naomba unisamehe, tutazungumza…” Amanda alitaka kusema lakini akaonekana kusita sana na kuinamisha uso wake chini. Alishindwa kuvumilia na sasa machozi yalikuwa yanamtoka.

Nilimtazama nikaona asingeweza kunijibu, na sikuwa na muda wa kuendelea kubembelezana kwani sikutaka kabisa Rehema ashtukie jambo lile baada ya kuona nimechukua muda mrefu kule chooni. Niliinua mkono wa kulia nikataka kumzaba kofi usoni, nikamwona akijikunja kwa hofu huku akitoa yowe hafifu la woga.

“Nakuuliza kwa mara ya mwisho, yule ni…” kabla sijamaliza Amanda alianza kulia na haraka akaipitisha mikono yake nyuma ya shingo yangu na kunikumbatia kwa nguvu kitendo kilichofanya chuchu za matiti yake kukitekenya kifua changu, nikahisi joto kali la mwili wake likitambaa kwa kasi mwilini kwangu na kufanya nijisikie faraja ya aina yake.

Ingawa nilikuwa nimekasirika sana lakini mbele ya Amanda nilijikuta nimekuwa kama mbwa muoga mbele ya chatu mwenye njaa kali. Bila kujua, kwa kiganja changu taratibu nikaanza kumfuta machozi lakini aliuondoa mkono wangu machoni mwake kisha akanisogezea mdomo wake kisha akaanza kuniporomoshea mabusu mfululizo mdomoni na hapo ndimi zetu zikakutana.

Kabla sijajua nini nifanye nikajikuta nikiishiwa nguvu na hapo tukaanza kubadilishana ndimi na kuufanya mwili wangu kusisimka kwa raha. Nilichoweza kusikia baada ya pale ilikuwa ni sauti nyepesi ya pumzi yake iliyokuwa ikipenya kwa fujo kwenye matundu ya pua yake. Nilitaka kuleta pingamizi lakini sikufanikiwa kwani sikuwa na ujasiri wa kupingana na hisia zangu.

Mikono yangu ikaanza kutambaa taratibu kwenye mwili wa Amanda huku kila mmoja akionekana kuwa na hamu na mwenzake japo mazingira hayakuruhusu. Nikaanza kulipandisha gauni lake juu haraka nikiwa nimedhamiria kumaliza mchezo humo humo chooni.

Mara nikahisi mlango mkubwa wa kuingilia maliwato ukifunguliwa na kisha nyayo za mtu au watu ziliingia na kusimama, kumbe hata Amanda alikuwa amezisikia lakini akazipuuzia. Mikono yangu ikaendelea kutambaa, kwa tahadhari, katika mwili wa Amanda na kumfanya azidi kulegea. Mara nikahisi kuwa zile nyayo za mtu zikija hadi pale kwenye mlango wa choo tulichokuwemo.

Kabla sijajua nifanye nini nikahisi mtu huyo akigusa kitasa cha mlango wa choo tulichopo na kukinyonga huku akiusukuma mlango kwa pupa, ukafunguka na hapo tukakatisha zoezi letu baada ya kumwona mwanamume akisimama pale mlangoni.

Niligeuka haraka kumwangalia kwa umakini nikiwa nimekasirishwa sana na kitendo chake cha kuvamia starehe za watu wengine lakini nilipomwona nikajikuta nikinywea. Alikuwa ni yule mwanamume aliyekuwa na Amanda, na alisimama akituangalia katika hali ya kutoamini kile alichokiona.

Amanda alishtuka sana, alimwangalia mara moja kisha akayarudisha macho yake kwangu kabla hajainamisha uso wake chini akionekana kutetemeka huku akiliweka vizuri gauni lake. Mapigo ya moyo wangu yakaanza kunienda mbio, si kwa sababu ya kumwogopa yule mwanamume ila kwa sababu ya ukweli kwamba kama yule mwanamume angeleta matata habari zingemfikia Rehema, na sikupenda kumuudhi.

“Amanda!” yule mwanamume alimaka kwa mshangao. “Nooo! Nooo…” alipiga kelele na taratibu nikamwona akilegea kabla hajaanguka na kupiga kichwa chake sakafuni, akapoteza fahamu. Amanda akachanganyikiwa.

Nami nilipatwa mshtuko mkubwa sana. Hata hivyo, akili yangu ilikuwa inafanya kazi haraka haraka sana.

“Sikia Amanda, nataka kesho urudi Kahama na mambo yote tutakwenda kuyamaliza huko, mchana nikukute umeshafika, sawa?” nilimwambia Amanda, akabetua kichwa chake kukubali na hapo nikatoka nje haraka nikimwacha ametaharuki asijue la kufanya.

Nilimkuta Rehema akiwa ameketi kitini kwa utulivu kama nilivyomwacha, niliketi kando yake huku nikilazimisha tabasamu ingawa uso wangu haukuweza kuficha wasiwasi niliokuwa nao, sikujua nini kingefuata baada ya yule mwanamume kuzinduka. Rehema alikuwa ananiangalia kwa umakini lakini aliendelea kuwa mtulivu sana. Sikujua alikuwa ananiwazia nini.

“Tuondoke, nimeshachoka kukaa hapa,” nilimwambia Rehema huku nikizungusha kichwa changu kuangalia upande ule wa kuelekea maliwato.

“Vipi, kuna tatizo lolote?” Rehema aliniuliza kwa sauti tulivu huku akiendelea kuniangalia kwa umakini sana.

“Hakuna tatizo, nimechoka tu kukaa hapa, nahitaji tukapumzike. Au kuna ubaya?” nilimuuliza huku nikiendelea kutabasamu. Hata hivyo moyoni nilikuwa na wasiwasi mkubwa nikiogopa kuumbuka.

Okay, as you wish!” Rehema alisema na kumwita mhudumu kisha akalipia kile chakula na vinywaji. Tukainuka na kutoka nje huku akimpigia simu dereva wa teksi iliyotuleta akimtaka atufuate.

* * *

Itaendelea...
Sio bure ni kweli umerogwa Jason
 
fungate.jpeg

131

Mwekezaji


Saa 11:45 jioni…

JIONI ya siku hiyo nilikwenda tena Kahama Tulivu Garden kisha nikaagiza Konyagi kubwa na kuanza kuinywa kwa tuo huku kichwa changu kikikabiliwa na mawazo lukuki juu ya Rehema, mwanamke ambaye sikujua kama nilikuwa bado moyoni mwake na kama alijua kuwa nilikuwa bado nampenda kupindukia.

Nikiwa naendelea kunywa taratibu huku mawazo juu ya Rehema yakiendelea kutawala kichwa changu nikashuhudia chupa nyingine ya Konyagi ikiletwa mezani kwangu na Saida.

“Nimeagizwa tena nikuletee Konyagi na yule dada pa…” Saida aliniambia huku akigeuza shingo yake kunionesha kwenye meza moja aliyodai ameketi dada aliyemwagiza kuniletea Konyagi, lakini akasita baada ya kuona ile meza ikiwa tupu!

“Alikuwa amekaa pale sasa hivi!” Saida alisema kwa mshangao.

“Dada yupi?” nilimuuliza huku nikimtazama kwa umakini.

“Yule mdada wa jana aliyekununulia K Vant, alikuwa kwenye ile meza… labda atakuwa ameenda msalani,” Saida alisema huku akionesha wasiwasi kidogo.

“Dah, sasa haya ni mauzauza! Kama mtu mwenyewe haonekani nami siwezi kuipokea mpaka aje mwenyewe…” nilimwambia Saida kwa msisitizo huku nikianza kuingiwa na wasiwasi.

Wakati nasema hayo nilimwona Saida akiduwaa kidogo huku akiwa anaangalia kando, alionekana kutaka kusema neno lakini akasita, na kabla sijamuuliza chochote nikashtuliwa na sauti tamu na nzuri ya mwanamke, “Habari yako, kaka?”

Niligeuza shingo yangu kutazama ilikotokea ile sauti tamu na macho yangu yakatia nanga kwenye umbo zuri la mwanadada aliyeonekana kuwa mchangamfu sana, alikuwa amesimama huku akiniangalia kwa tabasamu. Nilimtambua mara moja kuwa ni yule mwanadada aliyekuwa anafanana sana na Rehema ambaye nilimwona siku iliyotangulia.

Alikuwa amevaa suruali nyeusi ya dengrizi, blauzi ya pinki ya mikono mirefu na kofia aina ya kapelo ya rangi ya pinki. Nguo zake zilimbana kiasi na kulichora vyema umbo lake zuri lenye kiuno chembamba kilichoshikilia minofu laini ya mapaja yake. Shingoni alivaa kidani kilichozama katikati ya matiti yake yaliyosimama kama mkuki wa Kimasai. Miguuni alivaa buti ngumu za ngozi na begani alining’iniza mkoba mzuri wa rangi nyeusi.

“Nzuri dada, habari yako!” nilimjibu huku nikimtazama kwa umakini zaidi. Kwa kiasi fulani alionekana kufanana sana na Rehema, na hata umri wao haukupishana sana.

“Habari yangu nzuri, sijui naruhusiwa kuketi hapa?” yule mwanadada aliniuliza huku akinitulizia macho usoni.

“Hakuna shida, unaweza kuketi,” nilijibu kwa sauti tulivu, na hapo akavuta kiti na kuketi.

“Sahamani mdogo wangu, naomba niletee kinywaji changu nimekiacha pale katika meza niliyokuwa nimekaa,” yule mwanadada alimwambia Saida ambaye muda wote alikuwa ameduwaa akitushangaa. Saida akaondoka haraka kuelekea kwenye ile meza.

“Sahamani kaka kama nimekusumbua, tangu juzi nakuona unakuja hapa na muda wote uko mwenyewe tu, nikaona leo nisogee pengine tupeane kampani. Sahamani kama nitakuwa nimekukwaza,” yule mwanadada alisema na kunifanya nitabasamu kutokana na ustaarabu aliouonesha kwangu.

“Bila samahani, dada yangu,” nilimwambia huku nikimtazama kwa umakini.

“Nashukuru sana… hakika wewe ni mtu muungwana sana,” yule mwanadada alisema huku akikaa vizuri pale kwenye kiti. Muda huo huo Saida alifika na kumkabidhi yule mwanadada chupa kubwa ya maji na bilauri.

Nilishangaa nikajiuliza kuja kwake pale Kahama Tulivu Garden ni kwa ajili ya kunywa maji tu? Nilitegemea labda angekuwa anakunywa bia au aina nyingine ya pombe kali! Nikajikuta napatwa na shauku ya kutaka kumfahamu zaidi yule mwanadada. Alimimina maji katika bilauri halafu akayanywa yote, kisha akanitazama huku akiachia tabasamu.

“Naitwa Olivia Mkuro, nina uhakika wewe ni Jason Sizya,” alisema yule mwanadada huku akiendelea kutabasamu.

Yeah! Ila sijajua umelifahamu vipi jina langu?” niliitikia na kumuuliza huku nikimtulizia macho.

“Nimelifahamu kwa kuwa nililijikuta nikitamani sana kukufahamu baada ya kugundua kuwa umefanana sana na ex-boyfriend wangu,” Olivia alisema huku akiendelea kutabasamu na kunifanya nimwangalie kwa umakini zaidi kwa sababu hata tabasamu lake lilirandana sana na lile la Rehema.

“Ex-boyfriend wako! Huenda ndiye mimi, hebu niangalie vizuri!” nilimwambia Olivia kwa utani huku nikiachia tabasamu lililoishia kwenye kicheko hafifu.

“Hapana, yeye haishi Tanzania. Ila mnafanana kwa kiasi kikubwa sana,” Olivia alisema huku akiniangalia kwa namna ya kunisaili.

“Kwa sasa anaishi wapi?” nilimuuliza kwa shauku.

“Nadhani bado yupo Botswana ingawa sitaki hata kujua habari zake,” Olivia alisema huku akionekana mwenye aibu.

“Kwa nini sasa hutaki kujua habari zake wakati unaonekana bado unampenda? Na ilikuaje mkaachana?” nilimuuliza kwa udadisi.

“Kuna mambo fulani tu yalitokea kati yetu ambayo sipendi hata kuyakumbuka… nadhani hatukuumbwa kuishi pamoja,” Olivia alisema huku akiangalia chini kuyakwepa macho yangu jambo lililonifanya nihisi kuwa huenda alikuwa ametendwa, na hivyo nikapatwa na shauku ya kutaka kujua zaidi.

“Ooh! Pole sana,” nilisema huku nikiyatuliza macho yangu kwenye uso wake kumtazama kwa umakini.

“Usijali…” Olivia alisema huku akijiweka vizuri pale kwenye kiti.

“Lakini hata wewe umefanana sana na mchumba wangu…” nilimwambia Olivia huku nami nikijiweka vizuri kwenye kiti changu.

“Ah, kumbe una mchumba?” Olivia aliniuliza huku akionesha mshangao mkubwa.

“Ndiyo, ila kwa sasa hatupo sawa, na tupo mbalimbali,” nilisema kwa huzuni lakini kwa sauti tulivu huku nikijitahidi kuzuia donge la huzuni lililoanza kunikaba kooni. “Kuna mambo fulani yametokea kati yetu na yananifanya nikaribie kupatwa na wendawazimu…”

“Duh! Pole sana. Usiniambie kuwa uwepo wangu hapa unakukumbusha machungu!” Olivia aliniuliza huku akinikazia macho.

“Hapana. Ila jana nilipokuona nilipatwa na mshtuko mkubwa! Sikuyaamini macho yangu kwa jinsi mnavyofanana kwa kiasi kikubwa,” nilimwambia Olivia huku nikianza kuhisi faraja fulani ndani yangu kutokana na uwepo wake.

What a coincidence! Ex-boyfriend wangu anafanana na wewe, girlfriend wako anafanana na mimi, na kila mmoja wetu kuna mambo yametokea kati yake na mwenzi wake!” Olivia alisema kwa mshangao mkubwa huku akiniangalia kwa umakini. Kisha akaniuliza, “Wewe ni mkaazi wa hapa hapa Kahama?”

“Ndiyo, na wewe mwenzangu mkaazi wa wapi?” nilimuuliza Olivia huku nikiyatafakari maneno yake kwa kina.

“Kwa sasa makazi yangu yapo jijini Gaborone nchini Botswana japokuwa wazazi wangu wanaishi Kilosa, Morogoro. Hapa Kahama nimekuja kuangalia fursa za uwekezaji… huu mji ni mzuri na unakua kwa kasi na pia ni business hub ya ukanda huu,” Olivia alisema na kushusha pumzi. “Na hapa Tulivu Garden nimependa tu kuja kwa ajili ya kupata hewa safi na kutuliza kichwa.”

“Oh, kumbe wewe ni mfanyabiashara?” nilimuuliza Olivia kwa shauku.

“Ndiyo. Ninataka kuwekeza kwenye biashara ambayo tayari soko lake ni la uhakika na linanisubiri mimi tu,” Olivia alinijibu huku uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu.

Endelea...
 
fungate.jpeg

132

“Ni biashara gani hiyo? Huenda ukani-inspire na mimi kuifanya!” nilizidi kumuuliza kwa shauku na kumfanya atabasamu.

“Nataka kujenga kiwanda cha kutengeneza biskuti ambazo zitatokana na viazi vitamu, najua huku vinalimwa kwa wingi sana… ingawa wenyewe wanavichezea tu kwa kutengeneza michembe na matoborwa,” Olivia alisema huku akinitazama kwa utulivu mkubwa.

“Biskuti za viazi vitamu sijawahi kuziona!” nilimwambia Olivia huku sura yangu ikishindwa kuuficha mshangao wangu.

“Basi utaziona mara tu uzalishaji utakapoanza,” Olivia aliniambia huku akijimiminia maji kwenye bilauri na kuyanywa yote.

I see! Kwa hiyo umefikia wapi katika uwekezaji wako?” nilimuuliza Olivia huku nikiendelea kushangaa kisha nikaziangalia chupa za Konyagi mezani kwangu huku hamu ya pombe ikianza kuniisha.

“Suala bado lipo kwenye mchakato, kwa sasa naandaa mpango mkakati na eneo maalumu la mradi na vikikamilika tu nitaanza kushughulikia vibali serikalini,” Olivia aliniambia kwa kujiamini.

“Unatarajia kiwanda kiwe wapi?” nilimuuliza.

“Kitakuwa hapa hapa Kahama, bado wataalamu wangu wanafanya tathmini juu ya eneo lipi litafaa zaidi kwa kiwanda na ofisi,” Olivia aliniambia.

“Nimefurahi sana kusikia hivyo, Olivia. Unajua hata mimi kuna kipindi huwa nawaza kuachana na kazi ya kuajiriwa na kuwa mjasiriamali lakini nachelea kufanya hivyo kwa kuwa kichwa changu kina mambo mengi mno,” nilimwambia Olivia.

“Ni kweli kabisa Jason. Ujasiriamali unahitaji sana commitment na focus katika jambo husika. Mimi sikuwa na wazo la kuwa mfanyabiashara na wala sikuwahi kuota kwamba iko siku nitawekeza katika biashara kubwa au kumiliki viwanda. Kitaaluma mimi ni daktari wa afya ya akili lakini kwa sasa nimeachana na shughuli za udaktari na kujikita zaidi katika uwekezaji…”

Really?” nilimuuliza Olivia huku nikimtazama kwa mshangao mkubwa, sikuamini kama mrembo huyo angeweza kuwa na taaluma ya udaktari, tena daktari wa afya ya akili!

Yeah! Ni mwaka juzi tu nilikutana na mtu aliyenivutia sana na kunishawishi kuwa mjasiriamali alipogundua kuwa nina uwezo mkubwa wa kubuni miradi. Kwa kuwa nilihitaji kuyabadili maisha yangu nikaichukulia hiyo kama fursa. Huwezi kuamini kwa miaka miwili tu tayari nimeshapiga hatua kubwa na namshukuru Mungu, mpaka sasa ni nimeshakuwa mmoja kati ya wajasiriamali wa kati wenye mafanikio makubwa nchini Botswana,” Olivia alisema na kuzidi kuniongezea udadisi juu yake.

“Una bahati sana. Umewezaje kufanikiwa katika jambo ambalo hukuwahi kuota?” nilimuuliza huku nikionesha mshangao.

“Nimefanikiwa kwa sababu ya kujituma sana kwani nilihitaji kufanya kitu ambacho kingenifanya niyasahu maisha yangu ya nyuma na kuanza maisha mapya. Hii ndiyo sababu iliyonifanya nijitume mno,” Olivia alisema na kunifanya nizidi kupatwa na mshawasha wa kutaka kujua mengi zaidi kuhusu maisha yake ya nyuma.

“Nafurahi kwa jinsi ulivyojituma na ukafanikiwa. Ila ninachofurahi zaidi ni jitihada zako za kuyasahu maisha ya nyuma kama ulivyosema. Kwani yalikuwaje na kwa nini ulitaka kuyabadili?” nilizidi kumdadisi Olivia huku nikimtazama usoni kwa umakini nikijaribu kuyasoma mawazo yake.

Olivia hakujibu bali aliniangalia moja kwa moja machoni kwa kitambo kifupi kisha akaachia tabasamu laini lakini lililoonekana kuficha kitu ndani yake.

“Ulitaka kusahau kitu gani? Si vibaya kufahamu kwa sababu hata mimi ninapita katika mapito makubwa na ninahitaji kuyabadili maisha yangu na kuyasahau maisha yangu yaliyopita,” nilimuuliza tena Olivia huku nikijaribu kujieleza katika namna ya kumtoa wasiwasi.

Olivia alinitazama tena kwa kitambo fulani kama aliyekuwa anatafuta jibu kisha aliachia kicheko hafifu huku akijiweka sawa kwenye kiti chake, akatoa leso laini na kujifuta macho kisha akanitazama tena.

“Unajua… katika maisha tunapitia mambo mengi sana na kuna nyakati mambo hayo yanatusababisha tuyachukie maisha au tuichukie dunia na watu waliomo ndani yake na hata kufikiria kujiua. Kuna nyakati vile vile tunaamua kuyabadili maisha yetu na kuamua kuwa wapya tena kutokana na maisha tuliyoishi huko nyuma…” Olivia alisema kwa namna ambayo ilinifanya nianza kuyafikiria maisha yangu na yote niliyopitia.

“Kwa sasa mimi ni mtu mwenye furaha na amani katika maisha yangu tofauti na nilivyoishi huko nyuma. Ila kilichonifanya kuamua kubadili maisha yangu ni jambo binafsi. Nasikitika kwamba siwezi kuliweka wazi,” Olivia aliniambia huku akiyakwepa macho yangu na kuangalia kando.

Nilianza kuhisi kuwa mimi na Olivia tulikuwa na mengi sana yaliyofanana, kumbukumbu za maisha yangu ziliendelea kupita akilini mwangu na kunifanya nikae kimya ghafla. Nilihisi Olivia aliligundua hilo.

“Jason, uko sawa?” Olivia aliniuliza huku akinitazama kwa udadisi usoni.

“Usijali, nipo sawa,” nilimwambia lakini nilihisi kuwa sauti yangu ilinisaliti.

“Unaonekana kama umezama katika mawazo ghafla,” Olivia alisema huku akiendelea kunitulizia macho usoni.

“Ah, nilikuwa nafikiria namna ulivyofanikiwa kuyabadili maisha yako… ni kweli kuna mambo yanatutokea katika maisha na mengine yanatulazimu kuachana kabisa na maisha yetu ya nyuma na kuishi maisha mapya, mimi pia natamani kuyabadili maisha yangu kama wewe,” nilimwambia Olivia huku nikilazimisha tabasamu na kumfanya acheke kwa sauti.

Niligundua kuwa Olivia alikuwa mwanamke wa aina yake ambaye kila mwanamume asingetaka kumkosa, alijaaliwa uzuri na pia alikuwa mcheshi sana. Kwa muda mchache tu niliokaa naye nilijisikia faraja sana na alikuwa amefanikiwa kunifanya niyasahau masaibu yangu. Pia nilitambua kwamba mbali na mafanikio yake hakuwa na silika ya kujivuna au kujiona bora zaidi kuliko wengine kama ilivyokuwa kwa wasichana wengine wenye vipato. Nilijikuta naanza navutiwa naye sana.

“Naona unaniangalia sana usoni. Kuna tatizo lolote au huniamini?” Olivia aliniuliza baada ya kugundua kwamba muda wote nilikuwa namwangalia usoni na sikuishiwa hamu ya kuitazama sura yake, nilihisi kama nipo na Rehema.

“Kama nilivyokwambia kwamba unafanana sana na mtu ninayempenda, na pia nyote wawili ni wacheshi sana na waongeaji wazuri, imenibidi nikuangalie tena na tena usoni ili nithibitishe kwamba wewe si yeye. Na kuna wakati nahisi labda wewe ni malaika mwenye sura na umbo kama la Rehema uliyetumwa kuja kuyabadili maisha yangu baada ya mateso yote niliyopitia,” nilimwambia Olivia na kumfanya acheke kwa sauti.

“Kwa nini unahisi kuwa mimi ni malaika, Jason?” Olivia aliniuliza huku akinikazia macho.

“Hata sielewi… ila hisia zangu zinaniambia kuwa wewe ni malaika mwokozi wangu maana kwa muda huu mfupi tuliokaa pamoja hapa tayari najiona mtu mpya! Najisikia huru na mwenye furaha kupita kiasi. Nimeweza kuyasahau matatizo yangu yote niliyonayo na hata sina tena hamu ya kuendelea kunywa pombe. Ninajiona kama vile ninaishi katika dunia isiyokuwa na matatizo ya aina yoyote!” nilijikuta nimeongea maneno mengi pasipo hata kutarajia.

Olivia aliangua kicheko na kunifanya na mimi pia nicheke. Alicheka hadi machozi yakamtoka, nikamwona akichukua kitambaa na kujifuta machozi.

“Haki ya Mungu Jason umenifurahisha sana leo. Sijawahi kukutana na mtu aliyenifurahisha kama wewe leo. Eti unajiona kama vile unaishi katika dunia isiyokuwa na matatizo ya aina yoyote! You’re too funny!” Olivia alisema huku akiendelea kucheka.

It’s true! I wish I’d be this happy everyday,” (Ni kweli! Natamani ningekuwa na furaha kama hii siku zote) nilimwambia Olivia huku nikicheka. Olivia aliendelea kucheka.

Endelea...
 
fungate.jpeg

133

I hope tutaendelea kukutana zaidi na zaidi,” niliongeza.

“Usijali, bado nina wiki nzima ya kuwepo hapa Kahama, naamini tutaendelea kukutana na kufurahi zaidi. Kwa kweli leo nimefurahi sana na nimeipenda kampani yako. Nashukuru sana kukufahamu… you’re such a wonderful guy,” Olivia alisema na kunifanya nitabasamu.

“Hata mimi nafurahi sana kukufahamu Olivia. Sikutegemea kama siku ya leo ningeweza kufurahi namna hii!” nilisema huku nikiendelea kutabasamu.

By the way, hujanieleza ni mambo gani yamekutokea katika maisha yako?” Olivia aliniuliza kwa sauti ya upole huku akinitazama kwa wasiwasi.

Nilimtazama Olivia kwa kitambo pasipo kusema chochote, ndani yangu kulikuwa na sauti mbili zilizokinzana; sauti moja ilikuwa ikinizuia kumweleza Olivia ukweli maana sikupaswa kumwamini kirahisi namna ile. Lakini sauti nyingine ilinitaka nimweleze ukweli wote kwa kuwa angeweza kuwa msaada wangu katika kujikwamua toka maisha ya nyuma na kuishi maisha mapya. Nikajikuta nikiwa njia panda.

Muda wote Olivia alikuwa ananitazama kwa umakini usoni kama aliyekuwa akiyasoma mawazo yangu, kisha akaachia tabasamu laini.

“Jason, ni kitu gani kimekutokea kwenye maisha yako? Tafadhali naomba uniambie, nitakusaidia,” Olivia alisema kwa msisitizo huku akiwa amenikazia macho.

“Ni hadithi ndefu sana na nisingependa kuongelea masuala hayo kwa sasa,” nilimwambia Olivia kisha nikashusha pumzi.

Come on, Jason, we are friends now hata kama tumeonana leo kwa mara ya kwanza. Naomba uniamini, na kama usiponieleza leo utanieleza lini?” Olivia alisema kwa kumaanisha.

“Sawa, kwa vile umesisitiza kutaka kujua ukweli, basi nitakueleza,” nilimwambia Olivia huku nikihisi kuwepo na nguvu fulani isiyo ya kawaida kati yetu.

Sikutaka tena kujiuliza mara mbili, nilianza kumsimulia mkasa wangu wote wa uhusiano wangu na Rehema, jinsi nilivyokutana na Jamila na baadaye Asia na mazingira ya vifo vyao, na mwisho kile kilichotokea kwa Rehema hadi muda huo akiwa kitandani hospitali akipigania uhai wake. Kisha nilimweleza jinsi nilivyojikuta nikikata tamaa ya kuishi na kutaka kujiua kwa risasi, nikaokolewa na hatimaye kutumbukia kwenye maisha ya ulevi wa kupindukia nikidhani labda ingenisaidia kuyasahau matatizo yangu.

Wakati nikimsimulia Olivia kuhusu mkasa wangu kuna wakati nilijikuta nashindwa kujizuia na kutokwa na machozi kitendo kilichomfanya Olivia naye atokwe na machozi mara kwa mara. Nilipomaliza kusimulia, ile hali ya furaha iliyokuwa imetawala mwanzo ilikuwa imeondoka kabisa na sasa simanzi ilitawala. Kisha kitambo kirefu cha ukimya kikapita huku Olivia akinipapasa mgongoni katika namna ya kunifariji.

“Samahani sana Olivia kwa hali ilivyobadilika ghafla, nimeshindwa kabisa kuvumilia. Nahisi maumivu makali sana moyoni mwangu,” nilimwambia Olivia kwa uchungu mkubwa huku nikishusha pumzi ndefu.

It’s okay, Jason. Kila kitu kitakuwa sawa… utakuwa sawa tu,” Olivia aliniambia huku akinisugua sugua kwa namna ya mahaba.

“Sidhani. Sijui kama unajua napitia maumivu makali kiasi gani!” nilimjibu Olivia huku nikitingisha kichwa changu taratibu.

Olivia alinitazama kwa umakini pasipo kusema neno, na hapo kikapita kitambo kingine cha ukimya.

“Nimekuelewa… now let’s not talk about it. Nisingependa tuiharibu furaha yetu, tumekuja hapa kwa ajili ya kufurahia na kupoteza mawazo, si kuongeza mawazo,” Olivia aliniambia huku akiachia tabasamu kabambe kisha alibadilisha mada na kuanza kunieleza fursa nyingi zilizopo nchini Botswana.

Taratibu furaha ilianza kurudi tena, tuliongea mambo mengi na kucheka kwa furaha sana. Kwa mara nyingine tena niliyasahau matatizo yangu na kujikuta nikiwa na furaha iliyopitiliza. Nilijikuta nikiwa na hisia za furaha ya ajabu sana, hisia kama hiyo ilikuwa inanipata nilipokuwa na Rehema peke yake.

Kwa kweli siku yangu ilionekana kuisha vizuri sana. Nilisahau kabisa kama muda mfupi uliokuwa umepita nilikuwa nimezama katika dimbwi la mawazo. Kwa kweli Olivia alikuwa na uwezo wa ajabu sana wa kunisahaulisha machungu yote yaliyonisibu, japo kwa saa chache.

Tukiwa katikati ya maongezi yetu nikamwona Olivia akinyanyua mkono wake wa kushoto kuangalia saa yake kisha akaonekana kushtuka.

“Inakaribia saa sita za usiku! Nikiendelea kukaa hapa na wewe tunaweza kukesha hadi asubuhi…” Olivia alisema kwa sauti ya chini iliyoonesha wazi kuwa alitamani sana kuendelea kukaa nami.

“Kwa kweli sipati neno la kukushukuru kwa jinsi ulivyoifanya siku yangu ya leo kuwa yenye furaha. Nashukuru sana Olivia,” nilimwambia Olivia huku nikiinuka toka kwenye kiti changu.

“Usijali, nadhani mimi na wewe tumeumbwa toka kwenye udongo mmoja, ndiyo maana hata nafsi zetu zimeendana sana,” Olivia aliniambia huku naye akiinuka.

“Leo nimejisikia faraja kubwa sana kupata kampani yako, hakika mwanamume atakayekuoa atakuwa na bahati kubwa mno,” nilimwambia Olivia na kumfanya acheke.

“Sifikirii kuwa na mwanamume, ninayafurahia maisha yangu bila hata mwanaume,” Olivia aliniambia huku akiendelea kucheka.

“Na vipi kuhusu kuwa na watoto?” nilimuuliza huku nikimtazama usoni. Nikamwona akisita kujibu na kukaa kimya kwa kitambo.

“Kuhusu watoto…” Olivia aliongea kisha akaonekana kusita na kunitazama kwa tabasamu lililoficha hisia za uchungu.

“Ndiyo. Pia hufikirii kuwa na watoto?” nilikazia huku nikiendelea kumtulizia macho usoni.

“Napenda sana watoto, na ningependa kuwa na watoto wawili…” Olivia alisema huku akianza kupiga hatua za taratibu kuondoka.

“Na utawapataje bila kuwa na mume?” nilizidi kumbana kwa maswali huku tukianza kutembea kueleka nje.

Can we please talk of something else?” (Samahani tunaweza kuongea mambo mengine?) Olivia alisema akionesha wazi kulikwepa swali langu.

Nilimtazama kwa umakini nikahisi kuwa maongezi hayo yalikuwa yanamkubusha jambo ambalo hakupenda kulikumbuka, na hivyo nikaheshimu uamuzi wake na kubadilisha mada.

“Kwani hapa Kahama umefikia wapi?” nilimuuliza Olivia.

“Nimefikia Hotel Latitude. Na wewe unaishi maeneo gani?” Olivia aliniuliza.

“Kwa sasa ninaishi Mwime,” nilimwambia wakati tukizidi kupiga hatua kuelekea nje, Olivia akiwa pembeni yangu. Muda huo nilikuwa nahisi msisimko wa ajabu. Niliendelea kumshukuru kwa kampani yake na jinsi alivyoifanya siku yangu kuwa yenye furaha.

Nilimsindikiza hadi kwenye eneo la maegesho ya magari, tukalikuta gari la Olivia aina ya Range Rover Vogue la rangi ya maruni.

“Nilisahau kukuuliza, una usafiri? Kama huna nikupeleke nyumbani kwako kisha nitaelekea hotelini kwangu,” Olivia aliniuliza kabla hajafungua mlango wa gari lake.

“Nashukuru, usijali sana kuhusu mimi, hapa Kahama ni alwatan, nina watu wengi wa kunipeleka nyumbani,” nilimjibu Olivia kwa namna ya kumtoa hofu.

Olivia alibonyeza kitufe kwenye ufunguo wa gari lake na kufungua mlango wa gari, akaingia na kuliwasha. Nilibaki nimesimama palepale hadi alipoligeuza na kuliweka tayari kwa kuondoka. Kisha akashusha kioo na kunipungia mkono.

Tukaagana na Olivia akafunga kioo chake na kuliondoa gari taratibu. Nililisindikiza lile gari kwa macho wakati likiondoka hadi lilipopotea kabisa kwenye macho yangu.

Kisha nilielekea sehemu zilipokuwa zimeegeshwa teksi, upande wa pili wa barabara na kuingia kwenye teksi moja ambayo dereva wake alikuwa mtu mzima, mrefu na mnene kiasi mwenye sura ya ucheshi muda wote, alikuwa amevaa kofia aina ya baragashia, shati la mistari ya pundamilia, suruali ya kijivu na makubazi meusi ya ngozi miguuni, nikamtaka anipeleke nyumbani kwangu Mwime.

* * *

Endelea...
 
fungate.jpeg

134

Surprise!


Saa 11:00 alfajiri…

ADHANA zote mbili za alfajiri nilizisikia nikiwa bado nahangaika kitandani, tangu ile adhana ya kwanza ambapo mwadhini alikuwa anasema “Swala ni bora kuliko kulala”, na hata ile ya pili iliyotolewa kuwajulisha Waislamu kuwa wakati umefika ili wahudhurie kuswali.

Tangu nilipoachana na Olivia kule Tulivu Garden na kurudi nyumbani sikuweza kupata usingizi, usiku kucha nilikuwa nahangaika kitandani kwangu kujaribu kutafuta usingizi bila mafanikio. Usiku kucha mawazo juu ya Olivia yalikuwa yananijia kichwani.

Kumbukumbu juu ya maongezi yetu ilikuwa inazunguka kichwani kwangu na maneno matamu ya Olivia yalikuwa yanajirudia kichwani kama filamu na kunifanya muda wote sura yangu ipambwe na tabasamu. Maneno yake yalizunguka akilini kwangu kwa kasi ya ajabu sana na kunifanya nishindwe hata kulala. Kulikuwa na nguvu ya ajabu iliyotenda kazi ndani yangu ambayo ilikuwa inaniendesha, na si akili zangu, hata nilipojaribu kuvumilia ilikataa.

Hiyo ndiyo wazungu huita ‘love at first sight’, yaani kuonana siku moja tu tayari nilianza kuhisi kuwa Olivia aliniteka akili yangu kiasi hicho! Sikuwa na shaka kabisa na hisia zangu na niliamini moyo wangu usingeweza kunidanganya kwamba Olivia alishaniingia moyoni mwangu.

She’s such an amazing woman!” nilisema kwa sauti ndogo huku nikiinuka toka pale kitandani na kuketi. Muda huo nilikuwa nahisi njaa kali na tumbo lilikuwa linaunguruma. Pia mwili ulikuwa umechoka sana kwa sababu ya kukosa usingizi.

Niliinuka na kuelekea maliwatoni kujimwagia maji ili nipunguze kwanza uchovu kabla ya kuandaa stafustahi. Ilinichukua dakika chache tu kuoga na kujifuta maji kisha nikavaa bukta ndefu nyeusi ya kadeti iliyofika hadi magotini na fulana nyekundu. Kisha nilielekea kwenye jokofu nikalifungua na kutazama ndani, nikaona kichana kimoja cha ndizi mbivu, matufaa mawili na embe moja tu. Hakukuwa na kingine cha kuweza kula.

Sikuwa na hamu ya pombe kabisa kama ilivyokuwa mwanzo japo ndani ya nyumba yangu kulikuwa na chupa kadhaa za pombe kali ikiwemo ile aliyoninunulia Olivia siku iliyotangulia. Nilichukua tufaa moja nikalitafuna kisha nikakumbuka kufua nguo zangu chafu zilizojaa kwenye tenga la nguo chafu. Nikazikusanya na kuzitumbukiza kwenye mashine ya kufulia na kuchukua ndizi mbivu, nikawa natafuna wakati nikisubiri zile nguo zikichakatwa na mashine.

Baada ya muda nikazitoa na kuzianika kwenye kamba kisha nikachukua raba yangu nyekundu aina ya Nike na kutoka, nikachukua boda boda na kumwambia dereva anipeleke Chattle Restaurant kwa ajili ya kutia uzito tumboni hususan kupata mchemsho wa kuku wa kienyeji na matoke. Kwa mara ya kwanza tangu nipatwe na mikasa nilihisi njaa na nilihitaji kula chakula nilichokipenda.

Hata wakati nilipokuwa nakula bado sura ya Olivia ilikuwa ikinijia akilini kwangu na kuniweka katika fikara nzito! Niliona saa kumi ilikuwa inachelewa ili nikaonane tena na Olivia, nilijilaumu kwa kutochukua namba yake ya simu kwani ningeweza kumpigia simu ili nisikie japo sauti yake tamu yenye kuburudisha.

Baada ya kifungua kinywa nilielekea saluni, nikanyoa vizuri nywele zangu na ndevu zangu nilizinyoa katika mtindo wa circle beard au kama wengi walivyozoea kuita “O”. Sasa nilikuwa katika mwonekano mpya kabisa nikiwa tayari kwa ajili ya kukutana na Olivia. Nilipoangalia saa yangu nikagundua kuwa ilikuwa inaelekea kuwa saa 5:30 asubuhi.

Nilisimama mbele ya kioo cha saluni kwa kitambo kidogo nikijitazama bila akili yangu kuwepo pale kwani mawazo juu ya Olivia yalikuwa yameanza kupita upya kichwani mwangu na wakati huo nilianza kuhisi kupungukiwa na kitu moyoni fulani mwangu.

Sikujua ni kwa nini nilitokea kumpenda sana Olivia hata baada ya mkasa wa kuhuzunisha ulionipata. Huenda mfanano wake na Rehema ulisababisha nijikute nikimpenda, maana kila nilipozikumbuka nyakati za furaha nilizokuwa nazo na Rehema nilijihisi mpweke sana na nilianza kuchanganyikiwa, lakini sasa alitokea mbadala wa Rehema na kuanza kuchukua nafasi yake moyoni mwangu.

Lo! Kwa kweli hisia juu ya Olivia zilianza kunitafuna moyoni na sasa nilikuwa saluni nimesimama mbele ya kioo, badala ya kujitazama nilikuwa namfikiria yeye. Roho iliniuma sana nilipokumbuka kuwa Olivia hakuwa mpenzi wangu na sikuwa na uhakika kama ni kweli hakuwa na mpenzi kama alivyodai. Kwa kweli nilihisi upungufu wa kitu fulani katika nafsi yangu.

Kisha nilitoka nikavuka barabara na kuanza kutembea kandokando nikiufuata uelekeo wa barabara iliyoelekea nyumbani kwa shangazi wa Asia. Baada ya mwendo mfupi wa miguu nikawa nimefika kwenye maegesho ya teksi na pale nilikuta teksi tatu zilizoegeshwa, hivyo niliiendea teksi moja iliyokuwa imejitenga kidogo na eneo lile. Dereva wa teksi ile alinipokea kwa bahasha zote na kunifungulia mlango.

“Nipeleke Mwime,” nilimwambia yule dereva huku nikiketi siti ya nyuma.

“Sawa bosi,” yule dereva alisema huku akiingia na kuliwasha gari lake, kisha taratibu ile teksi ikaanza kuyaacha maegesho yale na kuingia barabarani, tukaingia upande wa kulia na muda mfupi baadaye tukauacha mtaa mmoja na kuingia mwingine tukiendelea na safari yetu.

Wakati safari ikiendelea mawazo yangu yote yalikuwa juu ya Olivia. Kitu fulani kuhusu mapenzi na mwanamke huyo kilikuwa kimeanza kujengeka ndani ya moyo wangu kiasi kwamba nilianza kuhisi kuichukia dunia endapo nisingempata Olivia.

Nikiwa katika lindi la mawazo niliinamisha kichwa changu na kushusha pumzi taratibu nikijaribu kuipumzisha akili yangu huku nikijihisi mgonjwa wa mawazo, akili yangu ilikuwa mbioni kuchoka. Nikainua macho yangu na kumtazama dereva wa ile teksi nikiwa kama sanamu huku taratibu nikilamba midono yangu.

“Tayari tumeshafika Mwime,” yule dereva wa teksi aliniambia kama mtu anioneaye huruma. Nilimtazama yule dereva huku nikiachia tabasamu kisha nikashusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Tayari tumeshafika Mwime, sijui nikushushe wapi?” yule dereva aliniuliza kwa sauti iliyojaa huruma.

Niliangalia nje nikayaona mazingira ya Mwime na kugundua kuwa tulikuwa tumesimama kwenye kijiwe cha bodaboda jirani na nyumbani kwangu. Nikamshukuru yule dereva na kumlipa fedha yake kisha nikashuka na kupiga hatua kuelekea kwenye nyumba yangu.

Nilipoingia sebuleni nilijipweteka juu ya sofa na kuitazama saa yangu ya mkononi, ilikuwa imetimia saa 6:25 mchana. Dah! nilikuwa bado nina takriban saa nne kabla ya kuonana na Olivia. Nilianza kuuona muda ukininyima raha kwani ulikuwa ukinyiririka taratibu sana, kwa madaha na maringo kama kinyonga. Olivia ndiye aliyekuwa mchawi wa huo ‘muda’. Alikuwa na mamlaka ya kuuamuru uwe duma mwenye kasi ama uendelee kuwa kinyonga.

Mawazo yalipita kichwani kwangu na moyo ulianza kunienda mbio kama mtu mwenye ugonjwa wa kihelehele. Nilijiuliza iwapo hali ile ilikuwa ni matokeo ya kutaka kuonana na Olivia, je, ingekuwaje pindi ningekutana naye? Nilianza kujiuliza, alikuwa na nini huyu Olivia hadi kunifanya kuanza kuteketea ndani kwa ndani kwa moto wa mapenzi yake?

Kilichonishangaza zaidi ni kwamba hali kama hiyo haikutofautiana kabisa na hali iliyowahi kunikuta wakati nilipokuwa nikimfukuzia Rehema. kama ilivyokuwa kwa Rehema, hata huyu Olivia alikuwa na kila kitu ambacho wasichana wengine wengi walikikosa.

Ili kupunguza mawazo niliamua kuwasha runinga, nikaanza kutazama filamu ya The American President iliyosimulia kuhusu maisha ya siasa na mapenzi ya Rais wa Marekani, Andrew Shepherd ‘aliyemzimia’ sana mwanadada Sydney mara tu walipoonana kwa mara ya kwanza na hatimaye wakaangukia kwenye mapenzi jambo lililosababisha mashambulizi kutoka kwa mpinzani wake mkuu kisiasa, Seneta Bob Rumson.

Endelea...
 
fungate.jpeg

135

Filamu hiyo ya dakika 113 iliyoandikwa na Aaron Sorkin na kuongozwa na Rob Reiner ilifanikiwa kuniteka akili yangu kwani ilielezea juu ya joto la kisiasa, mahaba mazito na mchanganyiko wa visa na mikasa katika namna ya ucheshi… ukweli Rais Shepherd alikuwa amenasa kwenye mtego wa mahaba na hakuweza kutoka!

Nikiwa bado naifuatilia stori hiyo tamu ya mapenzi kwenye filamu hiyo mara nikashtushwa na sauti ya kengele ya geti iliyoanza kuita kwa fujo. Nikawasha runinga ndogo ya kuona aliyeko getini huku nikiwaza mgongaji angekuwa nani, na hapo akili yangu ikafikiria huenda angekuwa Amanda, hata hivyo sikutamani awe yeye.

Nikatamani sana kama angekuwa Olivia lakini nikajiambia kuwa asingeweza kuwa yeye kwani hakupafahamu nyumbani kwangu, isitoshe tulikuwa tumekubaliana kukutana jioni ya siku hiyo. Runinga ile ilipowaka ikamwonesha mtu aliyesimama nje ya uzio wa nyumba yangu akiangalia sehemu ya kengere ambako kulikuwa na kamera ya ulinzi iliyochukua sura ya mtu aliyesimama hapo.

Nikiwa makini kutazama runinga nikashtuka sana kuiona sura ya Olivia akiwa amesimama nje ya geti! Sikuamini macho yangu. Niliyapikicha nikihisi yalikuwa yananidanganya na kutazama tena kwenye ile runinga, ni kweli alikuwa Olivia na alikuwa amesimama mbele ya geti kwa utulivu.

Kwa nukta kadhaa moyo wangu uliyasahahu mapigo yake na yalipoanza tena nilivuta pumzi ndefu kisha nikazishusha taratibu huku nikimtazama kwa makini kwenye ile runinga, nilianza kujiuliza aliwezaje kupafahamu nyumbani kwangu wakati sikuwa nimemwelekeza? Lakini sikuwa na jibu.

Nikiwa bado natafakari sauti ya kengele ya getini ikanishtua kutoka kwenye mawazo yangu, nilipotazama nikamwona Olivia akionekana kukata tamaa na alipotaka kuondoka nikawahi kubonyeza kitufe cha kuongelea.

“Usiondoke nakuja,” nilisema kwa sauti tulivu na hapo nikamwona Olivia akigeuka kuangalia kwenye ile kamera ya ulinzi pale getini na kuachia tabasamu.

Nikatoka hadi getini na kufungua geti dogo na kuchungulia nje na hapo pua zangu zililakiwa na harufu nzuri ya manukato yenye kuhamasisha ngono huku macho yangu yakitia nanga kwenye umbo zuri la Olivia. Yeye alikuwa amesimama akinitazama kwa utulivu huku akitabasamu kabla ya tabasamu lake halijageuka kicheko cha kirafiki. Loh! Alizidi kunichanganya akili yangu kwani alikuwa amependeza isivyo kawaida.

Alikuwa amevaa suti nzuri ya kike ya rangi ya maruni, blauzi ya bluu ya mikono mirefu na viatu vya maruni vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio. Nguo zake zilikuwa zimemkaa vizuri na kulichora vyema umbo lake zuri na shingoni alivaa kidani ambacho sikuweza kukitazama vizuri kwa vile taswira ya matiti yake ilianza kuzivuruga hisia zangu. Mkononi alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe na alikuwa amebeba pochi nzuri nyekundu.

Olivia alijaribu kuzuga kwa kuitazama simu yake ya mkononi huku akipambana na aibu ya kiutu uzima aliponiona nimeduwaa nikimtazama. Nilipoangalia kando ya geti nikaliona gari lake la kifahari aina ya Range Rover Vogue.

“Karibu ndani, Olivia,” nilimkaribisha Olivia huku sura yangu ikipambwa na tabasamu kabambe.

“Ahsante,” Olivia alinijibu na kurudi kwenye gari lake.

Sikusubiri, nikachukua remote ya kufungulia geti na kubofya kitufe cha ‘OPEN’ na hapo geti likaanza kufunguka taratibu, kisha Olivia akaliingiza gari lake ndani ya uzio wa nyumba na kupita kwenye barabara nzuri iliyotengenezwa kwa vitofali vidogo vilivyovutia katikati ya bustani nzuri ya maua ya kupendeza na kisha akaliegesha kwenye sehemu maalumu ya maegesho ya magari, na wakati huo geti lilikuwa linajifunga lenyewe taratibu.

Muda huo akili yangu ilikuwa bado inachemka kwa maswali lukuki, swali kuu lilikuwa juu ya Olivia, aliwezaje kupafahamu nyumbani kwangu?

“Habari za toka jana?” nilimuuliza Olivia baada ya kushuka kwenye gari huku nikitabasamu na kumsogelea.

“Habari nzuri Jason. Sijui wewe?” Olivia alijibu kwa sauti tulivu huku akiniangalia kwa umakini.

“Nipo poa kabisa,” nilimwambia, nikamwona akitabasamu.

“Na kweli, nakuona uko poa kabisa, umekumbuka hata kunyoa nywele na ndevu!” Olivia alisema kwa utani huku akiachia kicheko hafifu na kunifanya nipeleke mkono wangu kichwani kugusa kichwa changu.

“Hakika umependeza sana. Ulipaswa kuwa mwanamitindo wa mavazi, you look so handsome,” Olivia aliniambia huku akiniangalia kwa umakini.

“Ahsante,” nilijibu huku nikimshika mkono kwa mahaba na kumkokota taratibu kuelekea sebuleni huku nikimuuliza, “Do you mind?”

Nilidhani labda Olivia angekataa au kushtushwa na kitendo changu cha kumshika mkono lakini badala yake kitendo hicho kilimfurahisha sana kwani aliachia tabasamu pana usoni kwake. Tulipoingia sebuleni nilimwona akiyazungusha macho yake kuyatazama mandhari ya sebule yangu na kuziona picha za Rehema, akaonesha kushtuka kidogo na kugeuza shingo yake kuniangalia kwa tabasamu.

You have a nice house!” (Una nyumba nzuri!) Oliva alisema huku akitabasamu.

Thanks,” nilijibu huku nami nikitabasamu.

Kisha nilimketisha taratibu kwenye sofa utadhani malkia, nami nikaketi kando yake huku nikimwangalia kwa umakini, swali la alipajuaje nyumbani kwangu lilikuwa bado linanitesha. Olivia alinitazama kwa jicho la wizi, nilihisi kuwa alikwisha yasoma mawazo yangu.

“Naona umeshangaa sana kuniona nyumbani kwako?” Olivia aliniambia huku akiniangalia usoni kwa umakini.

“Kidogo… kwani nani aliyekuelekeza nyumbani kwangu?” nilimuuliza Olivia huku nikionesha mshangao.

“Kama niliweza kulifahamu jina lako ningeshindwaje kufahamu mahali unapoishi? Sikutaka tu kukwambia kuwa napafahamu nyumbani kwako kwa kuwa nilitaka kukufanyia surprise,” Olivia alisema huku akiangua kicheko.

“Na kweli, leo umeni-surprise sana!” nilisema huku nikishusha pumzi ndefu.

Are you living alone?” (Unaishi peke yako?) Olivia aliniuliza huku akizungusha tena macho yake pale sebuleni.

I’m all alone…” (Nipo peke yangu) nilisema huku nikitabasamu.

“Peke yako kwenye jumba kubwa kama hili!” Olivia aliuliza kwa mshangao huku akiwa bado anayatazama mandhari ya sebule na kuongeza, “No servant to serve you?” (Hakuna hata mfanyakazi?)

I don't like servants,” (Sipendi wafanyakazi) nilijibu kwa sauti tulivu huku nikiendelea kutabasamu.

I guess whoever Rehema she is, she is sure a lucky girl!” (Naamini huyo Rehema, kwa vyovyote ni msichana mwenye bahati sana) Olivia alisema kwa sauti iliyojaa wivu huku akiitazama picha kubwa ya Rehema iliyotundikwa ukutani.

Nilimtazama kwa umakini usoni, nikaona macho yake yalikuwa yakimaanisha. Sikuwa na shaka na hisia zangu kuwa Olivia alionesha kunipenda, niliamini hivyo na niliamini kuwa hisia zangu zisingeweza kunidanganya kwamba kama nilivyonasa kwenye penzi lake basi hata Olivia alikuwa amenasa kwenye mapenzi. Nilijikuta nikipatwa na furaha ya ghafla.

“Kuhusu Rehema nilikueleza kila kitu jana, nimeshakataliwa na wazazi wake na hivyo sina changu. Nashukuru ujio wako umenifanya kuwa mtu mpya. Sasa najisikia huru na mwenye furaha kupita kiasi. Kwa hiyo naomba tusizungumze habari za watu wengine,” nilisema kwa sauti tulivu huku nikimkazia macho Olivia.

“Sawa,” Olivia alijibu huku akinitazama kwa macho yaliyokuwa yanafikisha ujumbe fulani.

Endelea...
 
Back
Top Bottom