Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #241
154
Wewe ni lulu ya pekee…
Saa 5:00 usiku.
ULIKUWA usiku wa aina yake, usiku ambao nilihisi kama vile niko peponi. Hisia zangu zilikuwa zitendewa vyema kwa faraja kubwa iliyopenya hadi kwenye mishipa ya damu. Nje ya chumba tulichokuwemo mbalamwezi ilikuwa ikiangaza na kuifanya dunia ing’ae kwa nuru safi na adhimu ya mbalamwezi. Chumba chetu kilikuwa na mwanga hafifu uliotoka kwenye taa mbili za rangi ya bluu.
Kilikuwa chumba kizuri cha kifahari, taa mbili za rangi ya bluu zilikuwa zinatoa mwanga hafifu wenye mg’ao na kufanya nusu ya chumba kile kuwa kizani. Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kitanda kikubwa cha samadari cha futi sita kwa sita, cha mbao ngumu za mninga na chenye droo mbili kila upande, na juu ya zile droo kulikuwa na zile taa mbili za rangi ya bluu.
Mbele ya kitanda kulikuwa na seti nzuri ya runinga pana ya inchi 52 na chini ya runinga hiyo kulikuwa na meza nzuri nyeusi ya kioo. Upande wa kushoto wa chumba, kwenye kona, kulikuwa na jokofu la vinywaji na hatua chache kutoka kwenye jokofu hilo kulikuwa na dirisha pana la kioo lililofunikwa kwa pazia zito na refu lenye nakshi za mchoro wa hifadhi ya taifa ya Serengeti uliodariziwa vizuri.
Upande mwingine wa chumba kulikuwa na kabati la ukutani la nguo na pembeni ya kabati kulikuwa na makochi mawili ya sofa na meza ndogo ya kioo. Kando ya sofa moja kulikuwa na meza fupi ya mbao iliyokuwa na simu ya mezani na kitabu kikubwa cha njano chenye orodha ya majina ya watu na kampuni zilizotumia huduma ya simu hiyo ya mezani.
Kwenye kona hiyo ya chumba upande wa kulia kulikuwa na mlango wa kuelekea kwenye chumba kidogo cha maliwato na bafu. Ukutani kulikuwa na picha kadhaa kubwa za michoro zilizotundikwa zikiwaonesha wanyama wa porini waliochorwa kwa ustadi wa hali ya juu. Picha zote ziliwekwa ndani ya fremu nzuri za kioo.
Mimi na mwanamke niliyempenda kuliko wanawake wote duniani, Rehema, tulikuwa tumejilaza kitandani. Rehema alikuwa amekilaza kichwa chake kifuani kwangu. Mguu wake mmoja ulikuwa katikati ya mapaja yangu huku mkono wake mmoja akiwa ameuzungusha shingoni kwangu na alikuwa anahema taratibu kwa sauti hafifu ya uchovu. Alikuwa ametulia mikononi mwangu na mimi nilikuwa nimemkumbatia kwa mahaba mazito.
Nilifumba macho yangu nikamshukuru Mungu kwa mara nyingine tena kwa zawadi hii aliyoniletea ya mwanamke mzuri pengine kupita wote duniani. Moyoni nilikuwa namsifu muumba kwa jinsi alivyolifinyanga umbo la Rehema kwa ufundi wa hali ya juu. Nilijihisi kama siko tena katika dunia hii iliyojaa kero na karaha za kila aina bali niko katika ulimwengu mwingine kabisa, ulimwengu wenye utulivu na mahaba mazito, ulimwengu usiokuwa na kero wala husuda za wanadamu.
Nilikuwa na kila sababu ya kufurahia kuwa na Rehema kwa sababu niliamini sasa ulikuwa wakati mwafaka wa kuwa na familia kwani umri nao ulikuwa unakwenda, aina ya maisha ya ubachela niliyokuwa nayaishi hayakupaswa kuwa sehemu ya maisha yangu tena. Mimi mwenyewe nilikwisha choshwa na maisha hayo.
Baada ya mateso makubwa niliyokuwa nimeyapata wakati Rehema alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi kisha akaibuka mwanadada Olivia akijifanya mwekezaji na kisha nikaungana tena na Rehema kabla hatujawekeana ahadi ya kuwa pamoja katika shida na raha, sasa niliamini nimepata kitulizo cha moyo wangu. Rehema alikuwa kila kitu kwangu. Nilimpenda kuliko maelezo.
Mkono wangu mmoja ulikuwa unaichezea shingo laini ya Rehema. Ngozi ya mwanamke huyo ilikuwa laini kama sufu, nikapatwa na hisia kwamba huenda sikuwa nikiigusa ngozi ya binadamu wa kawaida. Nilihisi kuwa pengine nilikuwa naigusa ngozi ya malaika kwa jinsi ilivyokuwa laini na ya kung’aa hata katika mwangaza huu hafifu uliokuwemo chumbani kwetu.
Ilikuwa ni siku ya Jumapili, siku ya kwanza kabisa ya fungate ndani ya hoteli maarufu ya Singita Grumeti Reserves iliyopo kwenye hifadhi ya taifa ya Serengeti baada ya harusi yetu iliyoacha gumzo katika Mji wa Kahama, tukipeana ahadi mahususi ya kulizatiti pendo thabiti litakalovumilia raha na shida zote za ulimwengu kama chuma cha pua. Tukikubaliana kujenga pendo ambalo tungehakikisha halipwayi wala kupauka na kutiliana sahihi hati za mkataba wa milele usioweza kuvunjwa kwa kupwa na kujaa kwa bahari.
Kama ambavyo wazee wa zamani walisema; “Kawia ufike”, nami nilikuwa nimepigania kummiliki mrembo maridadi mwenye kila aina ya sifa ya uzuri, nikamtia mikononi mwangu na sasa tulitaraji kuishi maisha ya mume na mke.
Wazo la kwenda Serengeti lilikuja kama utani siku tatu tu kabla ya harusi yetu, mwanzoni tulikuwa tumepanga kwenda visiwa vya Mauritius kabla Rehema hajaja na wazo jingine.
“Hivi kwa nini tusitafakari upya wapi twende fungate?” Rehema alitoa wazo wakati tukiandikiana ujumbe kwa njia ya WhatsApp.
“Samahani mpenzi, wewe unafikiri twende wapi kwa ajili ya fungate yetu?” nilimuuliza nikaona ameweka ‘emoji’ za kushangaa kisha aliandika; “Unanirudishia swali, Jason!”
“Basi kama hupapendi Mauritius unaonaje twende Johannesburg, London, Paris au New York… sema wapi? Popote upendapo dear tutakwenda na hii ni zawadi ya pendo langu kwako…” nilimwandikia Rehema.
“Tuna haja gani ya kwenda nchi ya ugeni?” Rehema aliniandikia kisha akaendelea, “Kwa nini tusiende kwenye hifadhi ya taifa ya Serengeti na ikiwezekana tufike hadi bonde la Ngorongoro?”
“Wazo zuri sana, mpenzi…” nilimjibu Rehema. “Tutapata nafasi ya kuona wanyama na kupumzika vile vile. Leo leo nafanya mpango ili baada tu ya harusi yetu twende huko, wiki mbili zitatosha…”
Hivyo ndivyo tulivyojikuta tupo ndani ya Singita Grumeti Reserves katika hifadhi ya taifa ya Serengeti, hoteli ambayo sifa zake kwa nyakati tofauti ziliwavuta watu mashuhuri duniani wakiwemo marais wa Marekani wa 42 Bill Clinton na wa 43 na George W. Bush, kufikia kwenye hoteli hiyo.
Tulipanga kukaa Singita Grumeti Reserves kwa wiki mbili na kutembelea vivutio mbalimbali katika hifadhi ya taifa ya Serengeti kujionea idadi kubwa ya wanyamapori na uhamisho wa kila mwaka wa zaidi ya milioni moja ya nyumbu wanaovuka mto Mara na baadaye twende bonde la Ngorongoro.
Kwa dakika kadhaa macho yangu yalikuwa wazi kabisa yakikodolea dari ya chumba hicho tulichokuwemo. Kisha niliuvunja ukimya wa muda.
“Rehema Benard Mpogoro!” nililiita jina lake kwa ukamilifu kwa sauti tulivu na kumfanya Rehema ainue kichwa chake na kunitazama kwa udadisi.
“Abee!” Rehema aliitika huku akinitazama machoni kwa udadisi.
“You are my wife now… u mke wangu sasa,” nilimwambia kwa Kiingereza na kisha kurudia kwa Kiswahili.
Rehema alicheka kidogo na kusema kwa sauti yake laini sana iliyoyafanya maungo yangu yasisimke, “Ndiyo, na wewe ni mume wangu sasa.”
“Kabisa! Am totally yours,” nilisema huku nikizishika shika nywele zake.
“Jason Sizya!” Rehema naye aliniita jina langu kwa ukamilifu huku akiendelea kunitazama usoni.
“Unasemaje malkia wangu?” nilisema huku nikimtazama machoni.
“Do you really love me, Jason? Unanipenda kweli? Nataka kuondoa shaka iliyo moyoni mwangu,” Rehema aliniuliza maswali mfululizo huku akiendelea kunitazama machoni.
Maswali yake yaliufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu. Nilimtazama kwa nukta kadhaa kisha nikashusha pumzi ndefu na kuminya midomo yangu.
“Shaka gani, Rehema?” nilimuuliza kwa sauti tulivu huku nikihisi hali fulani ya woga ikinitambaa mwilini kwangu. Ni kama aliyekuwa akiyasoma mawazo yangu, Rehema aliachia tabasamu.
“Unafahamu ninakupenda kiasi gani?” badala ya kujibu swali langu aliniuliza swali jingine huku akiwa bado amenikazia macho.
Nikatabasamu kidogo na kushusha pumzi za ahueni.
“Rehema, malkia wangu, nafahamu kwamba unanipenda sana, sioni kitu cha kulinganisha na upendo wako kwangu. Ni upendo ambao hauwezi kupimwa wala kulinganishwa na kitu chochote kile,” nilisema kwa sauti ya chini ya mahaba.
“Nashukuru kama unalifahamu hilo. Napenda kuongezea kwamba nakupenda kupita hata ninavyojipenda mimi mwenyewe. Nameamua kukabidhi moyo na mwili wangu uvilinde na kuvichunga kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Wewe ndiyo kila kitu kwangu,” Rehema alisema kwa hisia kubwa.
Nikamkumbatia kwa nguvu zaidi na kumbusu katika paji la uso wake.
“Wewe ni lulu ya pekee na ya thamani kubwa katika maisha yangu. Nakosa hata neno la kukwambia ni namna gani nakupenda zaidi ya unavyoweza kufikiri. Naahidi kuwa siku zote nitakulinda, kukuheshimu na kukuthamini…” nilimwambia Rehema huku nikimtazama usoni, nikayaona machozi ya furaha yakimtoka na kukilowesha kifua changu.
* * *
Endelea kufuatilia...