201
Saa 9:15 alasiri…
Nililiondoa gari, tukaingia barabarani tayari kwa safari ya kurudi Dodoma. Safari hii ndani ya gari aliongezeka mtu mwingine, Almasi, ambaye aliketi kiti cha mbele huku Grace na Rehema wakikaa viti vya nyuma.
Kabla hatujaianza rasmi safari yetu ya kurudi Dodoma nililiingiza kwanza gari katika kituo cha mafuta. Mafuta yakajazwa. Kisha nikaingia kwenye
super market ya hapo hapo kwenye kituo cha mafuta, nikanunua maji, vitu vya kutafuna, soda za
take away na
Energy kadhaa. Pia sikusahau kuchukua Savanna tatu.
“Nipeni saa tatu tu tutakuwa Dodoma,” niliwaambia huku nikifunga mkanda.
“Ila angalia tu tusije tukaishia
mortuary,” Grace alisema kwa utani.
“Wewe wifi jamani… maneno gani hayo lakini?” Rehema aling’aka huku uso wake ukionesha wasiwasi mkubwa.
Nililiondoa gari na kuliingiza barabarani. Mwendo wangu ulikuwa wa kasi ila wa uhakika na nilikuwa makini, bado sikuwa najali hata kidogo kuhusu askari wa usalama barabarani kwa kuwa nilikuwa nimetenga fedha kwa ajili yao.
Nikafanya kosa, tulipokuwa tunavuka Dumila tukielekea Dodoma, nje kidogo ya Dumila tuliwakuta askari watatu wa usalama barabarani, mmoja wao alijaribu kutusimamisha, nikamvuka bila kusimama. Hao tukaendelea na safari yetu huku nikijiona mshindi.
Tulipokuwa tukiingia Gairo ilikuwa imetimia saa 11:25 jioni, haraka nikapunguza mwendo wa gari baada ya kukiona kizuizi cha barabarani na kisha askari wawili wakajitokeza mbele yetu na kusimama katikati ya ile barabara huku wakituonesha ishara kwa mkono kuwa tusimame. Nilipowatazama vizuri nikaona kuwa mikono yao ilikuwa imekamata vyema bunduki aina ya
SMG.
“Msala huo…” Almasi alisema huku akionekana mwenye wasiwasi.
Wakati nikipunguza zaidi mwendo na kujiandaa kusimama mara nikawaona askari wengine wawili wakijitokeza na kujongea katikati ya ile barabara kisha wakasimama nyuma ya kizuizi kilichokuwa katikati ya ile barabara.
Nililisimamisha gari letu kando kando ya barabara
, nikawatazama vizuri wale askari huku roho yangu ikinidunda kwa nguvu. Sikushuka, niliamua kubaki ndani ya gari kisha nikashusha kioo cha dirishani kwangu huku nikijiandaa kutengeneza tabasamu la kirafiki pindi askari mmoja akinifikia.
“Unatoka wapi na unaelekea wapi?” askari mmoja ambaye alikuwa na cheo cha Koplo aliniuliza baada ya kunifikia huku akiwa amenikazia macho usoni.
“Natoka Kilosa naelekea Dodoma… Vipi kuna tatizo lolote?” nilimuuliza yule askari kwa kujiamini huku nami nikimkazia macho.
“Kwa nini hujasimama uliposimishwa huko Dumila?” aliniuliza huku akiendelea kunikazia macho yake pasipo kupepesa.
“Sijaona kama tulisimamishwa mahali. Kama ningesimamishwa kwa nini nisisimame?” nilisema kwa sauti tulivu huku nikimtazama yule askari usoni.
Wakati huo huo askari mwingine aliyekuwa na cheo cha Inspekta, akiwa na nyota mbili mabegani, alilifikia gari letu na kuzunguka akielekea upande wa nyuma wa gari huku akiwa analichunguza kwa jicho la hadhari.
“Nipe leseni yako ya udereva,” yule Koplo aliniambia kwa sauti kali ya kuamuru huku akiendelea kunikazia macho yake.
Nikatoa leseni yangu na kumpa huku nani nikimkazia macho bila kupepesa. Aliipokea ile leseni na kuanza kuikagua. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita wakati yule askari akiendelea kuikagua ile leseni na wakati akifanya hivyo yule askari mwingine mwenye cheo cha Inspekta aliyekuwa amezunguka upande wa nyuma akawa anakuja mbele kwenye mlango wangu.
“Umebeba nini ndani ya gari yako?” yule Koplo aliniuliza tena kwa ukali akiwa bado kaishikilia mkononi leseni yangu.
Nilimtazama kwa umakini huku donge la hasira likianza kunikaba kooni maana niliona kuwa alikuwa anatuchelewesha kuendelea na safari yetu pasipo sababu za maana. Nilitafakari kidogo nikitafuta jibu la kumpa lakini kabla sijamjibu, yule Inspekta akanifikia na kunitazama kwa umakini usoni.
“Hey, Jason!” yule Inspekta alisema huku akiachia tabasamu pana usoni kwake.
Nilimtazama vizuri usoni na kumtambua. Aliitwa Ibrahim Ubwa, mtoto wa Mwalimu Musa Ubwa. Mimi na Ibrahim tuliishi mtaa mmoja huko Manispaa ya Tabora na tulikuwa marafiki wakubwa wakati tukisoma darasa moja kuanzia la kwanza hadi darasa la saba katika Shule ya Msingi Gongoni.
“Ooh, Inspekta Ubwa!
Long time no see!” niliitikia huku nami nikiachia tabasamu pana usoni kwangu.
“Habari za siku, ndugu yangu,” Inspekta Ubwa alinisalimia kwa bashasha.
“Nzuri…” niliitikia huku nikitaka kumwambia aturuhusu kwani tulikuwa katika haraka za kumfuatilia mtu.
“Pole sana na matatizo… Mama aliniambia kilichokupata, na nilipompigia simu Eddy naye akanithibitishia! Pole sana mkuu,” Inspekta Ubwa alisema kwa huzuni.
“Ndo hivyo, yote ni mipango ya Mungu,” nilisema na kushusha pumzi.
“Daah… niliposikia sikuamini kabisa!” Inspekta Ubwa alisema na kuwatazama watu wengine niliokuwa nao ndani ya gari kisha akawasalimia, “Habari zenu jamani!”
“Nzuri,” waliitikia kwa pamoja.
“Enhe! Na huku mnatoka wapi tena?” Inspekta Ubwa aliniuliza huku akinitazama machoni.
“Kuna mtu tulimfuata Kilosa lakini bahati mbaya tumepishana naye, ameelekea Dodoma,” nilimwambia Inspekta Ubwa.
“Ooh!” Inspekta Ubwa alisema na kushusha pumzi.
Wakati huo yule Koplo alikuwa akitutazama mimi na Inspekta Ubwa kwa zamu na sasa alionekana kunywea, huenda ni baada ya kuona kuwa mtu aliyekuwa anataka kumkagua alikuwa anafahamiana na bosi wake. Sasa hakuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kunirudishia ile leseni yangu. Niliipokea na kushukuru.
Inspekta Ubwa akaturuhusu tuondoke na kuwapa ishara askari wengine waliokuwa wamesimama kwenye kile kizuizi kuondoa kile kizuizi. Askari hao walitii amri na kuondoa kile kizuizi cha barabarani, wakaturuhusu kupita.
“Tutafutane basi, namba yangu ni ile ile,” Inspekta Ubwa aliniambia na kutuashiria kuwa tunaweza kuondoka.
“N’takutafuta, ngoja kwanza nimalize haya mambo,” nilimwambia Inspekta Ubwa huku nikiachia tabasamu la kirafiki na kuwapungia mkono wale askari katika namna ya kuwaaga kisha nikatia moto gari na kuliondoka kutoka eneo lile nikiwaacha wale askari wakilisindikiza kwa macho.
Muda huo ilikuwa imetimia saa 11:45 jioni. Tulikuwa tumetumia takriban dakika ishirini katika kizuizi hicho cha barabarani.
Wakati tukiondoka nikakumbuka jambo, nilimwambia Almasi ajaribu kuipiga namba ya Zainabu, lakini bado ilikuwa haipatikani. Nikapata wazo la kumpigia simu mjomba, Mchungaji Ngelela na kumweleza kila kitu kisha tukakubaliana kuwa afuatilie katika kituo cha mabasi cha Nanenane, jijini Dodoma, pengine angeweza kumpata Zainabu.
Kisha nilimwomba Almasi amtumie mjomba picha ya Zainabu, kwa njia ya
WhatsApp. Almasi alifanya hivyo.
Endelea...